STORY: KISA MAPENZI TU SEHEMU YA: 13




*******************
Prisca akachukua simu yake na kumpigia huyo dereva ambaye atatusafirisha hiyo kesho safari yetu. Bahati nzuri akafanikiwa kumpata hewani kwa kupitia simu yake ya mkononi na kumueleza kuwa anaomba kukutana naye kwa muda huo kule nyumbani kwake Mbezi Beach kwa mazungumzo zaidi, dereva huyo ni wa familia yao na alikuwa anaishi huko maeneo ya Mikocheni nyumbani kwa wazazi wa Prisca na Eddy. Basi dereva huyo akasema ndani ya muda mfupi ujao atakuwa tayari ameshawasili Mbezi Beach nyumbani kwa Prisca na kuonana, Pia Prisca akamuomba dereva huyo wakati atakapokuwa anakuja asitumie kuja na gari yeyote ya huko nyumbàni kwao na badala yake akodishe Taxi halafu pesa yake atamlipa akishafika.  baada ya kumaliza kuongea na dereva Prisca akakata simu na kuendelea na safari ya kuelekea nyumbani kwake!
Benny mpenzi wa zamani wa Prisca akiwa yupo pamoja na Eddy ambaye ni kaka wa Prisca waliweza kufika kwa haraka mpaka nyumbani kwa Prisca na Eddy akasimamisha gari nje ya Geti kubwa la kuingilia ndani ya mjengo huo wa kifahari. "Sijui atakuwa yupo ndani na kile kibwengo chake?" Eddy alimuuliza Benny mara baada ya kusimamisha gari hapo nje. "Sidhani kama watakuwa wapo humo ndani" Benny alisema. "Kwanini unahisi kuwa hawapo ndani?" Eddy alimuuliza Benny huku akimuangalia usoni. "Ni kwa sababu Dada yako namjua vizuri sana, muda wake mwingi sio mtu wa kutulia hapa nyumbani kwake" Benny alijibu kama vile alikuwa na uhakika kwa hicho anachokisema mbele ya Eddy. Baada ya kushauriana sana hapo nje Eddy akaamua kuisogeza mbele zaidi gari na kwenda kuipaki mtaa wa Pili yake ili wasipate kuonekana na Prisca. "Hapa leo iwe au isiwe ni lazima tujue kama yule boya bado yupo mle ndani, au kaenda kufichwa sehemu nyingine tofauti" Eddy alisema na kuizima gari yake halafu yeye na Benny wakateremka na kuanza kurudi nyuma mdogomdogo (Taratibu) kuja nyumbani kwa Prisca ili waweze kufanya uchunguzi wao, kwa Bahati nzuri au mbaya kabla awajaifikia nyumba hiyo ya Prisca ghafla wakaiona gari ya Prisca kwa mbali ikisogea maeneo ya hapo. Kwa haraka Eddy pamoja na Benny wakajificha kwenye bustani kubwa ya mauwa yaliyokuwa yamepandwa nje ya ukuta wa nyumba hiyo! Prisca alipofika usawa wa getini kama kawaida lile geti lake likafunguka lenyewe kwa vile ni (Automatic) Prisca akaiingiza ndani gari yake na huku nyumà geti hilo likajifunga tena lenyewe. Huku nje sasa baada ya Prisça kuwa ameingia ndani na gari yake wakina Eddy pamoja na Benny wakajiondoa hapo kwenye mauwa walipokuwa wamejificha! "Si nilikuambia Dada yako alikuwa hayupo ndani kwa muda ule, umeona ndio anarudi sasa hivi?" Benny alimuuliza Eddy. "Yeha nimeamini Shemeji yangu, sasa tunafanyaje ndio tubishe hodi na kuingia au? maana atujajua kama amerudi na yule boya au vipi" alisema Eddy. Lakini kabla Benny naye ajasema chochote Mara ghafla ikatokea gari nyingine ndogo aina ya Taxi na kuja kusimama hapo mbele ya geti kubwa nyumbani kwa Prisca! Kama kawaida wakarudi tena kujificha kwa haraka sana kwenye Yale mauwa na kuchungulia ili wapate kumjua ni nani huyo aliyekuja na hiyo gari Taxi, kumbe alikuwa ni huyo dereva wa familia aliyekuwa na Ahadi ya kukutana na Prisca hapa nyumbani. Dereva huyo baada ya kuteremka kwenye ile Taxi akamlipa fedha yake dereva wa hiyo Taxi aliyokuja nayo hapo na halafu ile Taxi ikaweza kuondoka maeneo Yale. Baada ya hapo Jamaa yule dereva wa akina Prisca akampigia simu Prisca kumjulisha kuwa tayari ameshafika na yupo nje ya geti, punde geti dogo la waenda kwa miguu likafunguliwa na mmoja wa wale mabinti wanaofanya kazi hapa nyumbani kwa Prisca na kumkaribisha ndani dereva Huyo, baada ya kuingia ndani Prisca akamkaribisha vizuri yule dereva! "Samahani sana kwa usumbufu kaka John ni dharura ndio iliyonifanya nikuite hapa" Prisca alianza kwa kusema. "Hakuna shida Dada Prisca ni dharura gani tena hiyo?" aliuliuliza dereva John. Prisca akajiweka sawa na kumuambia: "Nimepata safari ya ghafla kesho asubuhi inabidi nisafiri mimi pamoja na rafiki yangu wa kiume kwenda huko Morogoro kumuona bibi yake" alisema Prisca. "Sawa hakuna shida boss tunaenda na kurudi hiyo kesho au tutakaa kidogo?" aliuliza dereva John. "Nafikiri kesho hiyohiyo tutarudi hatutaweza kukaa sana huko, tutamchukua na huyo bibi wa rafiki yangu na kurudi naye hapa mjini" Prisca alisema. "Basi hakuna tatizo je tutatumia gari ipi?" alihoji dereva John. "Tutaitumia ile PRADO nyeupe naona ndio inafaa zaidi kwa safari ndefu" alisema Prisca na kuongeza tena: "Lakini kwa muda huu nilikuwa naomba kwanza unipeleke SINZA HOTEL alipo huyo rafiki yangu halafu kesho asubuhi ndio utakuja kutuchukua hapo Hotelini na kuianza hiyo safari yetu" Prisca alisema. "Hakuna shida boss wangu mimi nipo tayari kabisa kuwapeleka" alisema dereva John. "Basi ngoja niende chumbani màra mojà nikajiandae" alisema Prisça na halafu akaelekea chumbani kwake huku akimuacha dereva sebuleni ameketi kwenye kochi akiangalia TV pamoja na kunywa Juice aliyoandaliwa na dada wa kazi. Huko nje napo wakina Benny pamoja na Eddy Mara baada ya dereva John kuwa ameingia ndani kwenye nyumba ya Prisca na wao wakapata kujiondoa tena kwenye Yale  mauwa walipojificha huku wakimuona John tangu alivyoshuka kwenye ile Taxi mpaka anaingia ndani ya mjengo anaoishi Prisca. "Huyu John dereva wetu wa familia amefuata nini tena hapa kwa Dada Prisca?" Eddy alijiuliza kwa sauti mpaka Benny akasikia. "Au inawezekana na yeye pia ana uhusiano naye wa kimapenzi?" Benny alimuuliza Eddy kwa sauti iliyoonyesha wivu flani hivi. "Hapana sidhani kama kuna kitu kama hicho, huyu John nahisi atakuwa amekuja hapa kwa kazi maalumu" Eddy alisema. Baada ya hapo wakatoka na kwenda kukaa mbali kidogo na nyumbani kwa Priscà ili wakajadiliane vizuri lile jambo. Mara ghafla geti kubwa likafunguka na gari nyeupe aina ya TOYOTA PRADO ikapata kutoka na kuingia barabarani huku dereva John ndie alikuwa akiendesha na Prisca akiwa ameketi pembeni yake kwenye siti ya kushoto. Kwa Bahati mbaya kabisa awakuwaona wakina Benny pamoja na Eddy pale nje! "Tufanye hàraka sana tuwafuatilie wale wanaondoka" alisema Eddy na haraka sana wakawahi kule wàlipoificha gari yao na kuanza kuifuatilia gari aliyoipanda Prisca ambayo dereva John ndie anaeiendesha kuja huku SINZA HOTEL sehemu nilipokuwepo Mimi. Mawazoni mwao Eddy pamoja na Benny walijua na Mimi nilikuwemo mle ndañi ya ile gari hivyo wakaanza kuwafuatilia kwa nyuma ili waweze kujua wanaelekea wapi. Prisca akujua kama anafuatiliwa!
****************
Mimi naye huku kwa upande wangu tangu  alipoondoka Prisca muda ule wa mchana nilibakia tu chumbani peke yangu nikiangalia TV mpaka muda wa usiku yapata majira ya 2 : 10 bado Prisca alikuwa ajarudi. "Au itakuwa ndio amenitelekeza kijanja hapa Hotelini?" nilijiuliza huku nikizunguka mle chumbani. Kwa upande fulani niliona hata kama Prisca atakuwa ametelekeza sio mbaya sana kwani ile pesa kiasi cha shilingi laki moja aliyoniachia mchana ingenitosha kabisa kuifanya nauli ya kurudi nyumbani kwetu Morogoro kwa bibi yangu. "Kwanza kama ameniacha ndio vizuri maana nitakuwa nimeepuka balaa la yule mpenzi wake wa zamani Benny aliyenionyesha bastora asubuhi" nilijisemea moyoni na kuona hiyo itakuwa ni afadhali sana kwangu kumuepuka Benny pamoja na Eddy yule kaka yake Prisca. Nikataka nijiandae kwenda bafuni kuoga halafu nikitoka kuoga nipige simu mapokezi na kuagizia chakula cha usiku Nile na mwishowe nilale ili kesho yake asubuhi niondoke zangu Morogoro, sikutaka kabisa kumpigia simu Prisca kumuuliza mbona amechelewa kuja hapa Hotelini kwangu niliona hii ni bora sana! Kabla sijaingia bafuni kuoga Mara ghafla nikasikia mlango wa humu chumbani kwenye hii Hoteli unagongwa taratibu. "Mmh nani tena huyo, au ni Prisca ndio anarudi?" nilijiuliza mwenyewe pasipo kupata jibu la kujua ni nani huyo anayegonga mlango. Ikabidi ninyanyuke  kitandani na kujiandaa kwenda kuufungua mlango huo ili niweze kumjua.

ITAENDELEA ...







USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.