Mbinu Mahususi za Kumpata Mke, Mume mwema!

NI Jumatatu nyingine Mungu ametujaalia pumzi ya kuendelea kuishi. Tunakutana kwenye eneo letu la kujidai, eneo la kupeana darasa la uhusiano. Tujifunze mambo mbalimbali ya uhusiano maana bila kujifunza wakati mwingine ni rahisi kuangukia kwenye ‘midomo ya mamba’.

 

Mapenzi ya sasa ni kizungumkuti. Usipokuwa makini unaweza kujikuta kila siku unaambulia maumivu maana watu wenye mapenzi ya kweli hawapo au hawana muda wa kuishi kwenye uhusiano sahihi. Wanataka kurukaruka na njia. Wanaorukaruka na njia huwa wanakuwa na yao vichwani.

 

Kuna wengine wanakuwa na watu wao wa maana pembeni. Yaani mwanaume au mwanamke anakuwa na wewe ukiamini ni mtu sahihi kumbe mwenzako ana mtu mwingine tofauti anayemuhusudu. Anaye anayemheshimu na kumpa thamani yote ya kuwa mke au mumewe mtarajiwa.

 

Anakuficha, anakutumia kwa matumizi yake binafsi anayoyajua kichwani halafu mwisho wa siku anakuacha kwenye mataa.

 

Ndiyo maana nasema kwenye dunia hii iliyojaa kila aina ya utapeli ni vyema sana ukajifunza mbinu au njia sahihi za kupita ili uweze kumpata mwenza wa maisha. Mume au mke mwema anatengenezwa, kuwa tayari kumtengeneza usidhani utampata tu kama ajali.

 

Ndugu zangu, hakuna mbinu sahihi sana ya kufanya katika suala la kumtafuta mwenza wa maisha kama kumuomba Mungu.

 

Mungu pekee ndiye anayeweza kukupa mwenza sawasawa na mahitaji yako. Macho yetu haya huwa yanatudanganya sana. Vijana wa sasa wanachanganyikiwa na maumbo, sura na vitu vingine na kusahau kabisa hili suala la mwenza wa maisha linahitaji jicho la tofauti katika kuchagua.

 

Kwa nguvu na akili zetu hatuwezi, utaishia kukutana na watu wa ajabu maishani. Mtangulize Mungu katika safari yako ya kumsaka mwenza wa maisha. Mwambie Mungu kwamba macho yako pekee hayatoshi kuona mtu sahihi. Yeye mwenyewe akuoneshe mtu ambaye ataishi nawe miaka yako yote ya hapa duniani.

 

Usiwe mtu wa kukurupuka mtu anapotokea maishani mwako. Jipe muda wa kumjua vizuri, inasaidia angalau kuweza kumjua tabia zake. Ishi kwenye misingi ya dini. Kama wewe ni Muislam au Mkristo au dini nyingine yoyote inayomuabudu Mungu, basi muombe yeye akuoneshe. Kaa kwenye mstari wa imani, jiheshimu. Unapaswa kuishi kwa hofu ya Mungu miaka yako yote. Usikengeuke kutokana na tamaa, fuata maadili ya Kitanzania. Achana na mambo ya kuiga ya kuishi kama mhunimhuni.

 

Vaa vizuri na upendeze, wapende na uwaheshimu watu wote. Usimdharau mtu kwani wanadamu wote ni sawa. Kila mwanadamu ameumbwa na Mungu hivyo huna sababu ya kumheshimu fulani kwa sababu ana fedha na kumdharau fulani kwa sababu hana kitu. Utangulize utu katika maisha yako.

 

Mpende Mungu na uwapende watu wanaokuzunguka. Ukiishi kwenye misingi hiyo huku ukimuomba Mungu akuoeshe, hakika Mwenyezi Mungu atasikia maombi yako. Yeye ni mwenye huruma, vuta subira maana hachelewi wala hawahi. Atakupa mtu sahihi kwa wakati na atakapokuja wewe mwenyewe utaona kweli ndiye.

 

Ukizingatia mafundisho haya, hakika utaishi vizuri na hata ikitokea umeingia kwenye ndoa na kukatokea kutoelewana kwa hapa na pale, kamwe hutatetereka. Bado utasimama na Mungu, utamuomba akupe jibu la tatizo husika na utafanikiwa. Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii. Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

Makala na Erick Evarist

DIAMOND Alivyopanda STEJINI Wasafi FESTIVAL, TABORA Yazizima!

The post Mbinu Mahususi za Kumpata Mke, Mume mwema! appeared first on Global Publishers.


USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.