UKIFANYA HIVI UNAJIWEKA KWENYE MAZINGIRA YA AMANI KIMAPENZI

 KUNA baadhi ya watu hawaamini kama inawezekana kuwa na uhusiano wa furaha na amani. Katika tathmini ambayo imefanywa na wataalamu mbalimbali kuhusiana na suala la imani ya watu kuwa katika mahusiano ya furaha inaonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 hawaamini furaha na amani katika mahusiano.

Wengi wanaona mapenzi ni kama njia ya utumwa  ya kuridhishana tu kimwili, kusaidiana masuala ya kiuchumi na yenye furaha ya kufikirika tu ila si suala linaloweza kumpa mtu amani na thamani stahili.

Wengi wanasema hivyo kwa sababu kadhaa. Wapo waliobadili zaidi ya wapenzi watatu kwa kutafuta furaha na bado wakaikosa.

Wapo walioonesha kupendwa  sana mwanzoni kisha baadaye kila kitu kikayeyuka. Kwa sababu hii wengi wanajiambia kupitia hisia zao za ndani kuwa furaha katika mahusiano ni hadithi tamu kuisoma ila isiyokuwa na uhalisia wowote.

 Na wewe msomaji wa makala hii ni miongoni mwa wanaoamini katika fikra hizo? Fikra za kuwa mahusiano ya mapenzi  si lolote ila ni eneo tu la kuteseka kuliko kupata furaha ya nafsi?

 Mbali na imani hiyo ya watu wengi ila tathimini inaonesha kuwa kila mhusika katika uhusiano anaweza kuwa na amani stahili kama tu atajua majukumu yake na kuyatekeleza vizuri.

Tathmini inaonesha kuwa wote walio katika mahusiano ya amani, raha na burudani ni wale wanaojitolea kwa kila kitu kwa wenzao huku wale wanaoteseka ni wale wanaosubiri mema kutoka kwa wenzao.

Iko hivi. Hakuna mahusiano duniani yatakayokuwa na raha kama wahusika ‘wanasikiliziana’ katika kuyajenga. Yaani mwanaume anaangalia mwanamke anamfanyia nini ili naye afanye. Mwanamke pia anaangalia mwanaume wake anamfanyia nini ili naye amfanyie. Ni kama wanaviziana hivi.

 Kama mmoja leo akimtumia ‘sms’ mwenzake, naye kesho atatuma. Kama mmoja akimpigia simu mwenzake na isipokelewe na yeye baadaye anafanya hivyo pia. Ujinga huu umeharibu ladha katika mahusiano mengi.

 Funguo ya mahusino ya amani ni kumpa mwenzako raha bila kujali yeye anakufanyia nini. Kitaalamu imethibitika kuwa binadamu anaathiriwa zaidi na mambo unayomfanyia.

Kwa maana nyingine ni kuwa unapomfanyia mwenzako ujinga, dharau, ama dhihaka hiyo inakuwa si njia ya kumfanya yeye akufanyie mema. Badala yake, atafadhaika( disappointed), ataumia na kulipiza. Binadamu kaumbwa hivi.

 Ushahidi wa haya ni mahusiano yaliokosa amani. Mengi ya mahusiano hayo huwa hivi,  mmoja alimfanyia mwenzie ujinga na mwenzake, pia akaona dawa ya moto ni mto. Matokeo yake kibanda chao cha mahusiano leo kinafuka moshi.

 Kama unahitaji amani na raha ya kweli katika uhusiano wako, kuwa mtoa raha( pleasure giver), kuwa mtoa furaha na pia usiwe na jicho la haraka la kuona makosa ya mwenzako na badala yake ona mazuri yake.

Kwa kuangalia zaidi mazuri yake itakufanya umuone mwenzako wa thamani na hadhi hivyo kupata sababu ya kumtendea wema.

Kila binadamu ana kiwango fulani cha hali ya kurudisha kila analotendewa( retaliating amount). Ndiyo maana hata mtaani wengi wanaosalimiana ni wale wanaosalimiana kila siku.

Ni ngumu sana kumkuta mtu akikusalimia hata kama kila siku muanzaji huwa ni yeye. Ili kuwapo na umoja bora baina yenu mmoja lazima amuanze mwenzake katika salamu kisha mwingine atajisi( feel) anapaswa kuanza kukusalimia ama kukufanyia jema lolote

Kwa ajili ya amani na raha ya uhusiano wako, fanya mazuri kwa mwenzako. Kufanya mazuri kwa mwenzako hata kama unafanyiwa ubaya si kwa kuwa mhusika kakuweza sana, si kwa sababu yeye ni mzuri ama tajiri sana ila ni kwa ajili ya kuleta amani na uimara wa mahusiano yenu.

 Uhusiano makini unajengwa na unyenyekevu. Sasa unyenyekevu utaonekana vipi kama kila mmoja anajiona zaidi ya mwenzake?

 Ili uimara wa mapenzi uwapo ni lazima mmoja baina yenu ajione mnyonge kiasi na kukubali kujifanya mjinga kwa muda. Yote haya unafanya kwa ajili ya amani ya baadaye ama kesho.

 Kila jambo zuri linahitaji hali ya kujitolea na mbinu. Bila mbinu kila siku utakuwa ukibadili wapenzi. Na mbinu makini ya kuchochea upendo na raha katika mahusiano yako ni kumfanyia mwenzako mema bila kuangalia yeye anakufanyia nini.

Instagram: g.masenga

Mwandishi wa makala haya ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia ( Psychoanalyst)

 @@@@





USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.