Kifo Mikononi Mwangu (Sehemu ya 5)
ILIPOISHIA IJUMAA…
KUNA mtu mwingine aliyekuwa amepiga picha akiwa na msichana huyo katika pozi lililoonesha kuwa alikuwa mpenzi wake. Tukashuku kuwa huyo aliweza kuwa mpenzi wake aliyetueleza yule mjumbe ambaye alituambia kuwa alikuwa hamuoni kwa wiki tatu hivi. Tukahisi kwamba atakuwa amesafiri au wameachana.
Kwa vile polisi wenzangu walikuwa hawatambui kwamba Charles alikuwa ndugu yangu, waliamini kuwa muuaji anaweza kuwa mmoja wa watu hao. Picha zile mbili zilitolewa na kuchapwa kwenye karatasi kisha kupachikwa kwenye ubao wetu ambao hukaa kwenye matangazo yetu.
Picha hizo zilipachikwa zikiwa na maelezo kwamba watu hao wanatafutwa na polisi.
Inspekta Mwakuchasa ambaye alikuwa msaidizi wa mkuu wa kituo chetu ndiye aliyekabidhiwa faili la uchunguzi huo, mimi nikiwa mmoja wa wasaidizi wake.
SASA ENDELEA…
INSPEKTA Mwakuchasa aliniita ofisini kwake, akaniambia kwamba vile vipande vya chupa vyenye damu pamoja na ile michirizi ya damu iliyopatikana mbele ya mlango, vitapelekwa kwa mkemia mkuu ili kutambua ile damu ilikuwa ni ya nani.
Maneno yake yakanishtua kidogo.
“Afande unasema vile vipande vya chupa vitapelekwa kwa mkemia mkuu wa Serikali ili kutambua ile damu ni ya nani wakati tunajua ile damu ni ya marehemu!” Nikamwambia.
“Katika uchunguzi kila kielelezo kinatakiwa kuthibitishwa. Tusichukulie tu ni damu ya marehemu kwa sababu ipo kwenye vipande vya chupa tunavyodhani kuwa ndiyo alipigiwa marehemu.”
“Unahisi kwamba ile damu inaweza kuwa ya mtu mwingine?”
“Ninachotaka mimi ni kuwa na uthibitisho kwamba ni damu ya marehemu na uthibitisho unaotakiwa ni wa kitaalam si wa kukisia au maneno matupu.”
“Nimekuelewa afande. Kwa hiyo vitapelekwa lini kwa mkemia mkuu?”
“Nafikiri vitasafirishwa kesho kwenda Dar.”
“Kwa upande wa muuaji nina wasiwasi sana na wale watu wawili ambao picha zao tumezipachika kwenye ubao wa tangazo. Mmojawao anaweza kuwa muuaji. Kwa vile picha yake tunayo itakuwa rahisi kumkamata.”
“Usiseme kuwa itakuwa rahisi kumkamata kwa sababu picha yake tunayo. Inawezekana ameshakimbilia mji mwingine baada ya kuona ameua.”
“Afande umesahau kwamba tuna mtandao wetu wa kipolisi ambao uko nchi nzima. Picha za wahalifu zinaweza kuonekana katika vituo vyote vya polisi. Atakimbilia mji gani ambako hakuna kituo cha polisi? Labda akimbie nchi na si rahisi kufanya hivyo.”
“Mimi imani yangu ni kuwa yupo hapahapa jijini. Kwa vile alipoua hakuonekana, imani yake ni kuwa hatafahamika. Mtu anayekimbia ni yule anayehisi anatafutwa.”
“Ni kweli afande, anaweza akawa hapahapa jijini.”
“Kama ni kukamatwa, atakamatwa hapahapa.”
Pakapita kimya kifupi kabla ya inspekta huyo kuendelea kuniambia.
“Halafu kuna kitu kimoja muhimu ambacho ni lazima tukifanyie utafiti. Ilipaswa tufahamu huyu msichana anaitwa nani, anafanya kazi gani na kama alikuwa na ndugu zake wanaofahamika. Kingine ni kuchukua alama zake za vidole ili tuwe nazo.”
“Ni kweli afande. Kujua jina la marehemu na kujua alikuwa anafanya kazi gani ni muhimu.”
“Sasa chukua gari nenda Kwaminchi muone yule mjumbe akupe jina lake na akufamishe marehemu alikuwa anafanya kazi gani ili tuweke kwenye kumbukumbu zetu. Sawa?”
“Sawa afande, acha niende mara moja.”
Nikainuka na kutoka mle ofisini. Dakika chache baadaye nikawa barabarani nikiwa kwenye gari la polisi nikielekea Kwaminchi. Nilipofika katika ule mtaa, nilikwenda kwenye nyumba ya mwenyekiti wa mtaa huo.
Baada ya kufanikiwa kumuona, nilimueleza tatizo lililonipeleka kwake.
“Mimi sifahamu yule msichana anaitwa nani wala sifahamu alikuwa anafanya kazi wapi. Subiri nimpigie mjumbe wangu,” mwenyekiti akaniambia.
“Sawa, mpigie.”
Mwenyekiti huyo alimpigia simu mjumbe wake. Nikamsikia akimuuliza.
“Eti yule msichana aliyeuawa anaitwa nani?”
Mwenyekiti alisikiliza kisha akaniambia.
“Anaitwa Matilida, kabila lake ni Mmakonde.”
“Anaitwa Matilida nani?” Nikamuuliza.
Mwenyekiti akauliza tena kwenye simu.
“Anaitwa Matilida nani?”
Mwenyekiti baada ya kuambiwa aliniambia.
“Anasema hafahamu jina la baba yake.”
“Muulize alikuwa anafanya kazi wapi?”
Mwenyekiti akauliza kisha akanijibu.
“Alikuwa akifanya kazi baa.”
“Una maana alikuwa baamedi?”
“Ndivyo alivyoniambia mjumbe wangu.”
“Sasa atufahamishe ni baa gani alikokuwa akifanya kazi?”
Mwenyekiti akamuuliza mjumbe huyo kisha akanijibu.
“Baa ya Nane-Nane iliyopo Gofu.”
Ilikuwa baa maarufu. Alipoitaja tu nikaifahamu.
“Hebu muulize anawafahamu ndugu zake?”
“Eti unawafahamu ndugu zake?” Mwenyekiti akauliza kwenye simu. Akasikiliza kidogo kabla ya kunitazama.
“Anasema hawafahamu ndugu zake,” aliniambia.
“Basi inatosha. Nitakwenda kazini kwake. Ninaweza kupata mengi zaidi.”
Nikamshukuru mwenyekiti huyo na kurudi kwenye gari. Nilipoliwasha nililiendesha hadi eneo la Gofu. Dakika chache baadaye nikawa ndani ya Baa ya Nane-Nane. Kwa vile nilikuwa nimevaa sare za polisi niliwashtua wengi nilipoingia humo. Nilikwenda kaunta nikamsalimia msichana aliyekuwa akihudumia.
Msichana alipokea salamu yangu kwa wasiwasi.
“Nataka nikuulize kidogo.”
“Uliza,” akaniambia.
“Unamfahamu Matilida?”
“Matilida hajafika kazini tangu jana.”
“Yuko wapi?”
“Alituambia alikuwa hajisikii vizuri.”
Nikanyamaza kidogo na kuyapeleka macho yangu upande mwingine.
“Amefanya nini?” Msichana akaniuliza.
“Labda hamna taarifa. Huyu msichana ameuawa jana usiku.”
Nilipomwambia hivyo msichana alishtuka na kunikazia macho.
“Matilida ameuawa?”
“Ameuawa jana usiku nyumbani kwake. Maiti yake ilikutwa na majirani zake leo asubuhi na kuiarifu polisi.”
Msichana akatikisa kichwa kusikitika.
“Ameuawa na nani?”
“Haijafahamika, ndiyo tuko kwenye uchunguzi. Tulikuwa tunawatafuta ndugu zake.”
“Ndugu zake wako Dar, wengine wako Mtwara.”
“Ni nani anayewafahamu?”
“Hapa hakuna yeyote anayewafahamu ndugu zake. Alikuwa akituambia tu kwamba ndugu zake wako Dar na wengine wako kwao Mtwara.”
“Yeye ni mtu wa Kusini, siyo?”
“Ndiyo, ni mtu wa Kusini.”
“Alikuwa na bwana?”
“Alikuwa naye, lakini waliachana muda mrefu.”
“Anaitwa nani?”
“Bwana’ke anaitwa Msami halafu umefanana naye sana. Ulipotokea nilidhani ni yeye.”
“Binadamu wanaweza kufanana. Baada ya kuachana na mwanaume huyo hakuwa na mwanaume mwingine aliyewahi kuwa naye?”
“Labda wapitanjia tu.”
“Kuna mmojawapo unayemfahamu?”
Msichana alinyamaza kimya. Nikamuuliza tena.
“Kuna yeyote unayemfahamu?”
“Kuna kijana mmoja anaitwa Mdachi, ndiye aliyekuwa akionekana naye mara kwa mara.”
“Jana au juzi alionekana naye?”
“Anakuja kunywa hapa kila siku.”
“Jana alikuja?”
“Alikuja, lakini Matilida hakuwepo. Akatuuliza, sisi tukamwambia Matilida anaumwa. Sasa hatujui kama alimfuata nyumbani kwake.”
Kwa vile picha ya mtu tuliyekuwa tunamtuhumu ukiacha ile ya Charles niliingiza kwenye simu yangu, nilifungua simu na kumuonesha ile picha.
“Ni huyu hapa?” Nikamuuliza.
“Ndiye yeye Mdachi!”
Nikaona sasa kazi imekuwa nyepesi.
“Tuseme alipoondoka hapa alikwenda nyumbani kwake akagombana naye na kumuua?”
Je, nini kiliendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.
No comments: