JE NI KWELI WANAWAKE WAKIPENDA HUWA WANAKUWA WAMEPENDA KWELI??


KARIBUNI wasomaji wangu katika safu hii ya mahusiano ambayo huwajia kila siku ikilenga kufahamishana hili au lile kuhusiana na mambo ya mapenzi au ukipenda unaweza kuita mahaba.

Awali ya yote, niwashukuru wale wote ambao wamekuwa wakitumia muda na fedha zao kutuma ujumbe wenye lengo la kupongeza mada zinazotolewa katika safu hii, huku wengine wakichangia pale walipoona inafaa kufanya hivyo. Nasema asanteni sana.

Baada ya salamu hizo, tugeukie mada ya leo. Katika mada zilizopita kuhusiana na suala zima la kupenda, wasomaji wangu wamekuwa wakichangia kwa mitazamo tofauti, huku wengi wakionekana kutofautiana kwa misingi ya kijinsia.

Mathalani, katika mada zilizohusisha suala zima la usaliti katika mapenzi na dhana nzima ya kupenda, kumetokea mabishano makali kuwa kati ya wanawake na wanaume, wanawake ndio ambao wamekuwa wakiwapenda wenzao wao kwa dhati kuliko ilivyo kwa wanaume.

Lakini pia, wapo wanaume waliokuwa wakisisitiza kuwa wanawake ndio vigeugeu katika suala zima la mapenzi kwani wengi wao si waaminifu hasa pale wanapokutana na vishawishi vya fedha, magari na nyumba za kifahari, kazi nzuri na mengineyo kama hayo.

Hao wanadai kuwa hata mwanamke umwonyeshe upendo kiasi gani, akikutana na mwanamume mwenye fedha chafu atakayemhakikishia kuishi katika nyumba ya kifahari, kutembelea gari la kifahari na mengine kama hayo, lazima atamsaliti mume au mpenzi wake.

Lakini kwa wanaume, imedaiwa kuwa wao hawatabiriki, wanaweza kuonyeshwa kila aina ya upendo na wake au wapenzi wao, lakini bado wakaendelea kujihusisha kimapenzi na wasichana wengineo, hasa wale wenye mvuto wa kisura na kimaumbile.

Kwa kifupi, wanaume wamelalamikiwa na wanawake kwa tabia zao za kutoridhika na walivyonavyo, wakitamani kila wakionacho mbele yao yaani kila mwanamke anayepita mbele yao hutamani ‘kumvua nguo’.

Lakini kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, inadaiwa kuwa wanawake ndio wenye mapenzi ya kweli kiasi kwamba wanapowapenda wanaume, huwapenda kweli kweli.

Lakini pia, wapo wanaosisitiza kuwa wanaume ndio wenye mapenzi ya dhati kiasi kwamba wanapopenda hupenda kweli na si maigizo kama ilivyo kwa wanawake.

Naamini mada ya leo itakuwa imewagusa wengi hivyo nitoe nafasi kwenu wasomaji wangu kutoa maoni yenu kabla ya kuwaletea ukweli juu ya mada hii kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu wa mambo ya mahusiano. Maoni yenu nitayatoa katika toleo la Jumamosi hii.

Lakini hebu niwape kibwagizo cha mada ya leo kutoka kwake Michael Bolton, mmoja wa waimbaji mahiri wa nyimbo za kimapenzi wa Marekani aliyejizolea sifa na tuzo kede kede.

Bolton, katika wimbo wake wa When A Man Loves A Woman, anaelezea jinsi inavyokuwa pale mwanamume anapompenda mwanamke. Pata uhondo wa kibao hicho matata.
USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.