Kuna Madhara ya Kumpenda Mtu Sana!
UKIPATA bahati ya kuzungumza na watu wengi juu ya suala la kumpenda mtu sana, ile penda ya kupitiliza, kila mmoja atakupa mtazamo wake.
Kuna ambao watakwambia ni vizuri kufanya hivyo. Lakini pia kuna ambao watakwambia si vizuri sana.
Wale wanaokwambia ni vizuri, wanaweza kuwa na hoja kwa kushibisha maneno yao kwamba kama unampenda mtu, halafu naye akakupenda hivyo, mtaishi kwenye ulimwengu wenu. Ulimwengu wa kupendana asikwambie mtu ni mzuri, ni raha tupu na hakuna karaha. Maisha hapo lazima uyaone mazuri, kama ni kunenepa, basi utanenepa.
Wenye mtazamo huu wanaweza kuwa na hoja, lakini je, itakuwaje ukawa unampenda mtu kupita kiasi halafu yeye asiwe na upendo kama wako kwako? Andika maumivu! Ukimpenda mtu kupitiliza anaweza kukunyanyasa, hususan anapogundua kwamba unampenda sana.
Kuna wengine watakwambia ili uweze kuwa na amani ya moyo muda wote, ni vizuri ukawa na akiba ya kupenda. Kwamba mpende mtu kwa kiasi fulani ili hata ikitokea mambo yakaharibika, huwezi kuwa kwenye maumivu makali.
Hawa nao wanakuwa na hoja kwa sababu kupenda kwa kiasi kutakufanya uwe huru pale mtu atakapokwambia kwamba hakutaki tena, nenda zako. Utapiga moyo konde, utaumia kidogo, lakini utaendelea na safari.
Hii ina faida kwani kwa kipindi hiki, watu hawaaminiki. Wapo watu wanakuja kwenye maisha yako kwa majaribio. Wao hawana mpango kabisa wa kuwa na wewe, bali wanakuja tu kwa ajili ya kupita. Ukimpenda mtu wa aina hiyo unategemea nini?
Kesho na keshokutwa ataondoka na kukuacha wewe kwenye mataa. Bahati mbaya sana watu wa aina hii ni wajanja sana, wanakuja wakiwa wameficha kabisa sura zao mbaya. Wameficha kabisa sura zao za upande wa pili ambazo ukija kuziona utajuta kuwafahamu.
Ulimuona mtu mstaarabu, mtu mwenye hofu ya Mungu, kumbe wapi bwana. Ni tapeli mkubwa wa mapenzi, ameshawaacha watu wengi kabla yako. Hayupo ‘serious’ na maisha ya uhusiano. Hatambui wala hajali thamani ya mtu kumpenda.
Yeye anachukulia poa tu masuala ya uhusiano. Uwepo leo ni sawa na usipokuwepo yeye hajali, maisha yanaendelea na wala hana hata muda wa dakika tano wa kukuwaza wewe ambaye uliingia naye kwenye uhusiano.
Watu wa aina hii ni hatari, ndiyo maana tunapaswa kuwa makini kwenye kitu kinachoitwa KUPENDA. Wenye hatua za awali hususan urafiki na uchumba, hakuna sababu ya kumpenda sana mwanaume au mwanamke uliyenaye.
Mpe ushirikiano wa kuonesha unamjali na kumthamini, lakini unashauriwa usipagawe sana kwenye uhusiano. Muda wa kufanya hivyo upo. Kama unataka kupagawa, utapagawa sana mtakapofikia hatua ya ndoa. Hapo penda sana hadi uchanganyikiwe.
Simaanishi kwamba kwenye hatua za awali usimpende mtu, hapana, mpende, lakini uwe na kiasi. Ni kipindi ambacho mnazidi kufahamiana, mnazidi kujuana baadhi ya tabia hivyo nawe uwe na kiasi pia katika kuruhusu moyo wako kuchanganyikiwa na huyo mtu.
Itafika wakati mambo yenyewe yatakaa kwenye mstari. Utakuwa huru kumpenda sana maana ni wako wa kufa na kuzikana. Hakuna mwingine zaidi yako, sasa kwa nini usimpende. Mmeshatengeneza ‘bondi’ ya maisha, ninyi ni mke na mume, basi hapo una uhuru sasa wa kumpenda kupitiliza.
No comments: