Faida za kiafya na kiuchumi za kuwa katika mahusiano ya ndoa

Ndoa ni muunganiko wa watu wawili wenye nia ya kuishi pamoja kwa maisha yao yote. Ni muungano wenye malengo ya kujenga familia pamoja na kuiongoza kwa namna ambavyo itakuwa bora kwao kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu.

Utafiti unaonyesha kuwa kuna faida za kuwa katika ndoa kiuchumi na kiafya.
Watu walio katika ndoa huwa na afya njema na pia huwa na maendeleo zaidi kiuchumi ukilinganisha na wale ambao wanaishi peke yao.

Hali kadhalika wananafasi kubwa ya kufanya mambo makubwa zaidi ya maendeleo kuliko watu wawili ambao hawako katika ndoa.

Hii inasababishwa na mtindo wa maisha ambao wasio katika ndoa wanaishi, vitu kama ulaji mbaya,ulevi usio na mipaka na matumizi mabaya ya fedha zao.

Faida za Kiafya za Kuwa Katika Ndoa.
Kwa wastani utafiti unaonyesha watu ambao wako katika ndoa wanaishi maisha marefu yenye afya na furaha zaidi kuliko wale wasiokuwa katika uhusiano wa ndoa.

Wanaume ambao hawana uhusiano wa ndoa wanakawaida ya kula vibaya vyakula visivyo na faida kiafya, baadhi yao wanakuwa walevi na matumizi yao ya fedha yanakuwa makubwa. Kwa kuwa hawapiki nyumbani, hula sehemu za jumuia kama migahawani na katika vilabu vya pombe. Vyakula hivi havina mchanganyiko mzuri wa virutubisho vinavyohitajika katika mwili.

Wanawake wasioolewa nao ulaji wao wakati mwingi unakuwa wa kula nje japo si kama wanaume, lakini pia wanakula vibaya vyakula vyenye mafuta mengi na visivyo na virutubisho muhimu. Vyote katika hivi vinapelekea kuhatarisha afya zao lakini pia wakati mwingine maandalizi ya vyakula hivyo huwa si mazuri.

Wanawake na wanaume ambao wameachana au mwenza wao amefariki wanasongwa sana na upweke wa kihisia. Hili hupelekea kupata magonjwa yanayosababishwa na msongo wa mawazo.

Faida za Kiuchumi za Kuwa Katika Ndoa.
Kuna faida nyingi zinazotokana na watu kuwa katika ndoa ambazo huleta mafanikio kiuchumi, faida hizo ni miongoni mwa;

Matumizi Machache
Tumeona kuwa watu wasiokuwa katika ndoa hula chakula nje zaidi na kunywa vilevi, hivyo hutumia fedha zaidi kwa mambo yasiyo ya msingi hasa kwa wanaume. Wanawake hali kadharika hutumia fedha nyingi katika mavazi na vipodozi wakiwa hawako katika ndoa kuliko wale walioolewa.

Malengo ya Muda Mrefu
Mipango ya watu wasio katika ndoa huwa ni ya muda mfupi na starehe zaidi hivyo kufanya maendeleo yao kiuchumi kuwa chini. Kinyume chake ni kuwa wale ambao wako katika mahusiano hupunguza matumizi kwa kula nyumbani zaidi na kupunguza matumizi katika vitu visivyo vya muhimu kama mavazi ya fahari.

Malengo ya watu waliooana huwa ya kujenga familia na ni malengo ya muda mrefu. Badala ya kufanya starehe kupita kiasi huwekeza katika ujenzi na biashara ambazo zitaongeza kipato chao.

Kipato Kikubwa
Kipato chao pia huongezeka kwa kuweka nguvu pamoja. Kama wote ni waajiriwa basi kutakuwa na mishahara miwili mwisho wa kila mwezi badala ya mtu mmoja na hivyo uwezo wao wa kufanya mambo makubwa unaongezeka.

Watoto wanapozaliwa katika familia huongeza mahitaji ya familia na ghrama huongezeka. Kwa kuwa inasemekana kuwa “ uwezo wa binadamu kufikiri hukua kutokana na tatizo” wazazi walio katika ndoa hupata jinsi nyingine ya kuongeza kipato na hivyo kukua kiuchumi. Watafikiria miradi zaidi au hata kutafuta kazi inayowalipa zaidi.

Ni wazi kuwa kuna raha ya kuwa na mtu unayempenda katika maisha yako na kujenga naye familia. Kama ndoa yenu ina furaha ni wazi utakuwa mtu mwenye furaha; na inajulikana kuwa mtu mwenye furaha huishi maisha marefu na huwa na afya nyema.

Hali kadhalika walio katika ndoa wana wajibika zaidi kuliko wale wasio katika ndoa na huweka jitihada za ziada za kujiongezea kipato. Hivyo uchumi wa walio katika ndoa huimarika zaidi na kuwafanya waendelee kwa haraka.

Lakini ifahamike kuwa hili linawezekana tu kama ndoa yao ina furaha, ikiwa vinginevyo matokeo huwa kinyume chake.


USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.