MAMBO HAYA NI SUMU KATIKA PENZI LAKO
UKIACHILIA mbali pesa, mapenzi huwa yana nafasi kubwa kwenye dunia tunayoishi. Si maskini wala si tajiri, wote kwa pamoja wanahitaji mapenzi kutoka kwa wanaowapenda ili dunia iende sawa kwa upande wao. Na ndiyo sababu hata mimi hapa ninaandika kuhusu mapenzi kwa sababu yananigusa hata mimi na hata wewe unayesoma hapa sasa. Kuna mambo mengi ambayo ni sumu kwenye mapenzi na wakati mwingine hata kusababisha wanandoa au wapenzi kuachana;
UONGO
Hakuna kitu kibaya kama uongo kwenye mapenzi. Uongo wa aina yoyote ile si sumu kali kwa wanaopendana kwa dhati kwa sababu hupunguza mapenzi na uaminifu kwa kiasi kikubwa mno miongoni mwa wanaopendana, hasa kama mmojawapo akigundua kuwa mwenzi wake ni muongo.
USIRI
Miongoni mwa mambo hatari pia kwenye uhusiano wa kimapenzi ni pamoja na hili la usiri wa kupitiliza. Kama una vitu moyoni na upo kwenye mapenzi bora kabisa si vizuri kuvificha na hasa vile vinavyohusiana na mapenzi yenu moja kwa moja. Ni kweli kuna vingine huwezi kumwambia kwa sababu havina uhusiano wa moja kwa moja na mapenzi yenu ila kuna vingine ni lazima avijue ili kutoleta ugomvi au matatizo kati yenu hapo baadaye.
USALITI
Kamwe usimuumize moyo akupendaye kwa dhati. Usimfanye ajutie penzi lako. Usimfanye anung’unike kwa mabaya unayomtendea. Unaweza kuona ni ujanja, lakini ipo siku utahitaji mapenzi ya kweli kwa mwingine na hutayapata. Laana ya mapenzi ipo na ni mbaya mno. Ukimuumiza mtu, ipo siku na wewe utaumia tu. Mapenzi ya kweli yanawezekana ukiamua na si kwa ‘ku-cheat’.
DHARAU
Hii pia huchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza mapenzi kama siyo kuyamaliza kabisa. Unapokuwa kwenye uhusiano, jitahidi kumpenda mtu wako bila kumuonesha dharau yeye au hata marafiki zake au ndugu zake au hata wengineo. Hakuna mtu anayependa mtu mwenye dharau hata awe nani.
UROPOKAJI
Hakuna kitu kinachoweza kumfanya mwenza wako kukukimbia au hata kukosa uaminifu na wewe kama akigundua kama wewe ni mropokaji na huna ‘kifua’ hasa kwa yale mambo ambayo ni ya chumbani na hayakutakiwa kutoka nje. Hakuna mtu anayependa siri zake kutoka hadharani na huwa inaumiza sana kwenye mapenzi kumpa mtu siri zako, halafu yeye anaenda kusimulia.
TAMAA
Tamaa ni kitu kingine ambacho hufanya uhusiano kukosa nguvu au kuvurugika kabisa. Kama mpo kwenye mapenzi na mmeamua kupendana kwa shida na raha, basi haitakiwi mmoja wenu kuwa na tamaa na kukosa uvumilivu hata kwa yale mambo yanayoweza kuzuilika.
KUKOSA MSIMAMO
Hili huwakuta wengi kwenye mapenzi ya siku hizi. Nadhani ni hali halisi ya dunia ya sasa inachangia pia pamoja na teknolojia tuliyonayo ya kutuwezesha kufanya yale tunayoyaona kwenye mitandao na vyombo mbalimbali vya habari.
KUTOJALI
Kwa kiasi kikubwa hili linaumiza mno na kusababisha kushuka kwa thamani ya mapenzi. Kama kweli unampenda mpenzi wako, basi msaidie anapopata matatizo na umjali na kumchukulia kama mpenzi wako na mtu wako wa karibu na siyo kukimbia majukumu.
UBAHILI
Huna sababu ya kuwa na pesa na mpenzi wako akawa anapata taabu kama vile humuoni. Sijasema utoe pesa hata kwa mambo yasiyo na msingi, lakini ‘at least’ utimize majukumu yako kwa mpenzi wako kila unapohitajika.
No comments: