Simulizi: Je Haya Ni Mapenzi? sehemu ya 44
Dorry aliamua kumsindikiza kwani aliamini kuwa kuna mengi bado hajaongea na Jeff.
Na wakiwa njiani akamueleza jinsi alivyokuwa akipigiwa simu na kupewa maelekezo ya kumsaidia Sabrina.
"Kwakweli hadi mama yako alinihisi uongo ila nilipigiwa simu na namba ngeni na sauti ilikuwa kama yako ila ya upole sana. Cha kushangaza namba hiyo hatukuiona tena kwenye simu"
"Pole Dorry ila hata mie hiyo khabari inanishangaza jamani, maana mambo kama hayo nimezoea kuyaona kwenye filamu na kusoma kwenye vitabu vya hadithi mmh! Inamaana umepigiwa simu na jini au ni kitu gani hicho?"
"Hata mimi sielewi hadi leo, kuna siku hata nilipigiza simu chini ila mama yako aliiokota ikiwa nzima kabisa. Mambo ya ajabu haya, si umemuona mama anachechemea yani alipata ajali kwa mambo haya haya"
Jeff alizidi kushangaa tu hiyo taarifa kwani hakuwa na wazo lolote juu ya majini, kwahiyo aliona kuwa ni taarifa ya ajabu kwake.
Pia akamueleza kuhusu swala la yeye kutoa makaratasi na jinsi mama yake alivyoambiwa kuwa ile nyumba yao ina majini kwani ndio yaliyotoa yale makaratasi.
"Mwambie mama yako awe makini sana na waganga, ni waongo na wamekula hela zake bure tu"
Ila Jeff alicheka kwa hii taarifa ya sasa kuwa karatasi zilitolewa na Dorry ila mama yake akaambiwa ni jini.
Wakaongea mengi na Dorry akamuahidi kumpelekea kile kitabu chake alichokichukua katika harakati za kukimbiza ile barua.
Wakaagana hapo na Jeff kurudi nyumbani kwao.
Sam alitulia nyumbani kwake siku ya leo huku akitafakari baadhi ya mambo.
Alikuwa akitafakari kuwa Sabrina akirudisha kumbukumbu zake itakuwaje.
"Mungu asaidie ili Sabrina aendelee na upendo ule ule aliokuwa nao mwanzoni juu yangu. Hata kama kazaa na wanaume gani huko ila bado nampenda Sabrina. Kitu kimoja tu ambacho anashindwa kunielewa ni kuwa siwezi kumuua. Nitamuuaje mwanamke ninayempenda kama yeye? Sielewi hata kwa Neema ilikuwaje, Mungu naomba nisamehe"
Simu yake ikaita na mpigaji alikuwa ni Sia ambapo alikuwa akimsalimia Sam.
"Mmh ila usije leo, nitakwambia ni lini uje"
"Sawa"
Ila Sia alisononeka kwa jibu hili kutoka kwa Sam kwani alipenda akubaliwe ombi lake kwa siku hiyo.
Jeff alirudi nyumbani kwao na ilikuwa ni jioni tayari ila leo aliamua kumueleza mama yake vitu kidogo kumuhusu Dorry,
"Yani siku zote hizo niko nae hapa kumbe alikuwa akinidanganya jamani!"
"Msamehe bure mama, shida ndio zilimfanya atende haya ila kaniomba sana nimuombee msamaha kwako. Tafadhari mama msamehe"
"Kale katoto ni kapumbavu sana, yani kunidanganya mtu mzima kama mimi kweli na akili zangu timamu!"
"Mama, usilaumu sana. Kila kitu hutokea kwasababu fulani mama yangu, si unaona alisaidia kwa matatizo ya mamdogo Sabrina. Kwahiyo tusilalamike tu, tuangalie na upande wa pili"
"Hata kama, ila mi ameniudhi sana"
Kisha Jeff akamuelezea mama yake kuhusu kitu kinachomsumbua Dorry na pia jinsi mama yake alivyodanganywa na mganga.
"Kheee yani yule mganga alinidanganya jamani loh! Yani anavyojaza watu kiasi kile sikutegemea kama anaweza kuwa mganga wa uongo jamani"
Sakina akatafakari na kuona kuwa ni wazi ameshaliwa pesa zake nyingi sana na mganga huyo.
"Sikutegemea kama yule mganga alinidanganya kiasi hicho"
Jeff alimwacha mama yake pale akijisikitikia kisha yeye akaenda chumbani kwake kutuliza akili yake.
Sakina pale sebleni akajikuta akikumbuka maneno ya yule mganga wa pili na kuhisi kuwa huenda yana ukweli ndani yake kwani alishamwambia amchunguze sana Dorry, akakumbuka na alivyoambiwa kuhusu Sabrina.
Akakumbuka mara ya mwisho mganga alipowakaribisha alipoenda na Sabrina.
"Mmh! Kwanini alimuita Sabrina kuwa mkwe wangu? Mbona naona mambo yanarandana na kule hospitali? Ila bado hainiingii akilini kabisa, yani Jeff alale na Sabrina? Hapana hapana nakataa"
Kwa kipindi hiki Sakina alijiona wazi kuto kujielewa kabisa na alikuwa akijiuliza vitu na kujijibu mwenyewe.
Alishindwa kuamini wala kuelewa chochote.
Jeff alikuwa akitafakari namna atakavyoweza kuzungumza na Sabrina kwani aliona wazi kwa pale kwakina Sabrina itakuwa ngumu ila je ni sehemu gani ataweza kuzungumza nae.
Wakati akiwaza hayo, akapigiwa simu na Dorry
"Yule mtu kanipigia simu tena Jeff"
"Kakupigia tena? Alikuwa anasemaje? Vipi umebahatika kuikariri namba yake?"
"Sijabahatika kwakeli, leo iliita na kutokea jina rafiki. Nikapokea na kusikia sauti yake. Ila kwenye simu yangu hakuna jina rafiki na hata alipokata nimepekua sijaliona"
"Mmh pole sana, unatakiwa ufanye ibada Dorry yasije yakawa makubwa bure"
"Sawa, ila kaniambia kuwa nikwambie wewe umpeleke mamako mdogo sehemu ya mwisho uliyokuwa naye kwa muda mrefu na umsomee barua yake"
Jeff akashtuka na kumuuliza Dorry,
"Je amekwambia kuwa hiyo barua inahusu nini?"
"Hapana hajaniambia"
"Haya nashukuru, nitafanyia kazi hilo swala"
Jeff akakata simu na kupumua kidogo huku akimuona huyo mtu kuwa ni nuksi sasa na kuona wazi kuwa anaweza kumuumbua muda wowote ule.
Jeff akaamua kulala sasa kwani alishatafakari vya kutosha.
Kulipokucha nyumbani kwa Neema alionekana kuwa hoi sana siku ya leo kuliko siku zote.
Aisha akajaribu kumuandalia uji ili ampe ila hakuweza kunywa, alionekana kutokwa na machozi tu.
"Jamani dada, kunywa japo kidogo jamani"
"Sitaki kufa Aisha, sitaki kufa kabla ya kutubu. Nahitaji kumwambia ukweli mtu huyu, nimemkosea sana"
"Nani huyo dada?"
"Sabrina, nahitaji kumwambia ukweli Sabrina. Nimekoma kutembea na waume za watu, tamaa imeniponza Neema mimi"
"Dada, unajua sikuelewi jamani, sikuelewi kabisa dada yangu kwani una nini leo?"
Neema akaanza kuropoka kamavile mtu aliyechanganyikiwa,
"Yule mwanaume, mwanaume yule anaota miba. Yule mwanaume ana misumali, yule mwanaume anatoa usaha, yule mwanaume ana........."
Neema akaanza kuweweseka sasa na kugeuza geuza macho.
Neema akaanza kuropoka kamavile mtu
aliyechanganyikiwa,
"Yule mwanaume, mwanaume yule anaota miba.
Yule mwanaume ana misumali, yule mwanaume
anatoa usaha, yule mwanaume ana........."
Neema akaanza kuweweseka sasa na kugeuza
geuza macho.
Aisha uoga ukamjaa na kujikuta akianza kupiga kelele ila wakati anapiga kelele alimuona Neema akiwa kimya kabisa, hofu ikazidi kumtawala Aisha kwani hakujua cha kufanya.
Akaamua kutoka nje ili kwenda kutafuta msaada, kwa bahati akakutana na Sam akiwa nae anaenda hapo kwa Neema na ndiye aliyemuuliza Aisha kuwa kulikoni.
Aisha akamueleza kuhusu kuweweseka kwa Neema.
"Kwani kuna kitu kakwambia?"
"Kitu gani? Ameanza gafla tu"
Sam akagundua kuwa pale Aisha hajui chochote kile kisha akaingia nae ndani ili na yeye apate kumuangalia Neema.
Aisha akashtuka kumuona Neema amekaa wakati alimuona akiweweseka chini na kuwa kimya kabisa.
Sam hakushtuka kwavile hakujua hali halisi ilivyo, ila tu alikuwa anamshangaa Aisha kwa kushtuka vile.
Kisha Aisha akamuuliza Neema kwa sauti iliyojaa uoga,
"Kumbe mzima dada?"
"Kheee ulijua nimekufa?"
Neema alipojibu, Aisha akamsogelea karibu sasa kwani ilikuwa rahisi kugundua kuwa Neema ni mzima kweli.
Alisogea karibu zaidi na kumpa pole, ambapo Neema alicheka na kuweka kama utani,
"Duh Israel kanibeep ila sijapiga"
Huku akicheka kanakwamba tukio lililotokea ni la kawaida kabisa.
Kitu hicho ndio kilichozidi kumshangaza zaidi Aisha.
Sam naye alikaa akiwaangalia sasa, Neema naye alimuangalia Sam na kumwambia kwa hasira
"Nini kimekuleta Sam?"
"Nimekuja kukuona Neema"
"Nenda kapatane na mkeo kwanza ndio uje"
"Napatana nae vipi na hana kumbukumbu zozote?"
Neema akajisikia vibaya kwani yeye ndio chanzo cha yote yaliyompata mke wa Sam ila hakuweza kujieleza kwani alijua wazi kuwa akijieleza basi itakuwa ngumu kwa Sam kuja kumuona mara kwa mara kwani atajua kama ni mtu aliyejitakia yale yaliyompata.
"Ila jaribu kuwa nae karibu basi"
"Najitahidi ila kwao hawataki hata kuniona kutokana na yale yaliyotokea"
Neema akafikiria kitu ila kutokana na hali yake akaona ni wazi atashindwa kulitenda lile analolifikiria.
Akamfikiria rafiki yake Rose ambaye ndio alikuwa msiri wake na kuona wazi kuwa yeye ndio angeweza kufanya lile analofikiria yeye ila aliamua kumwambia Sam aende tu kwani roho yake ilikuwa ikimuuma sana kwa kuendelea kumuona Sam mahali hapo.
Hivyo Sam akaacha kiasi cha pesa cha kuwasaidia na kuondoka.
Neema alibaki na Aisha sasa ambapo Aisha alikuwa bado akimshangaa Neema kwani tukio lililotokea kabla lilikuwa la kustaajabisha mno.
"Mbona unanishangaa sana Aisha, yani tangu umeingia hapa na Sam unanishangaa tu"
Aisha aliamua kumueleza Neema jinsi ilivyokuwa na hadi pale,
"Kiukweli niliwaza mambo mengine kabisa, kwakifupi nilichanganyikiwa dada. Yani nilichanganyikiwa sana."
Neema akafikiria kwa dakika kadhaa na kujua wazi kuwa kilichomfanya apone ni kitendo cha Sam kwenda pale kwake ambapo imekuwa jambo jema kwake na la uzima ila kupona kwake yeye kwa staili hiyo ni kuendelea kumtesa Sabrina, ni kumfanya Sabrina aendelee kuteseka na kupata ugumu zaidi.
Akakumbuka dawa, ya kuwa kuna dawa moja hajaiondoa.
Ni dawa hiyo hiyo aliyoiwaza hata wakati Sam yupo ila je anawezaje kuiondoa.
Ndio hapo alipomkumbuka Rose kwani ndio aliyekuwa anajua mipango yote kwavile walikuwa wakipanga pamoja.
Neema hakuweza kwenda kuitoa hiyo dawa ila anamuagizaje Aisha kwenda kutoa dawa hiyo? Hapo ni lazima Aisha ajue siri yake na hapo ndio pagumu kwake.
Sabrina naye siku hiyo alijihisi maumivu makali ya shingo kanakwamba alikandamizwa na majinamizi usiku.
"Mwanangu sasa hapo hali ni mbaya, yani wewe ukiacha hili unaanza kuumwa lile, tufanyaje hapa jamani"
"Sijui mama"
"Ila usijali, Mungu atakusaidia. Utapona tu mwanangu"
Wakapeana imani na mama yake.
Muda kidogo siku hiyo alifika shangazi wa Sabrina ambaye ilikuwa ni siku nyingi sana bila kuwatembelea ndugu zake hao kutokana na yale mambo yaliyotokea baina yao, na kilichompeleka pale ni kwa lengo la kumsalimia Sabrina kwani alikuwa amesikia habari za kuumwa na kila kitu ila hakwenda kuwaona.
Alipofika pale alijua mama wa Sabrina hatompokea vizuri ila alipoingia mama Sabrina ndiye aliyekuwa wa kwanza kuinuka na kumpokea kwa furaha huku akifurahia sana kufika kwake.
Shangazi wa Sabrina akafurahi kukaribishwa vile na kuwafanya wazungumze mambo mengi sana bila kugusia ule ugomvi wao kwani mama Sabrina aliamini kuwa hakuna tena cha kugombana na wifi yake huyu.
Shangazi wa Sabrina alimuhurumia sana Sabrina kwa kile kitendo cha kupoteza kumbukumbu zake kwani hata shangazi yake hakumkumbuka.
"Pole sana Sabrina ila Mungu ni mwema utapona kabisa tu."
Sabrina akatabasamu tu ila akamshangaa huyu shangazi yake kuwa na maneno mengi kiasi kile kwani alikuwa anaongea tu.
"Yani nilikuwa naota ndoto mbaya mbaya kuhusu Sabrina na kunifanya niingie kwenye maombi kwaajili yake naona naye ilibaki kidogo kupatwa na majanga. Watu ni washirikina jamani"
Wakazungumza pale namna ya kuweza kumsaidia Sabrina kutoka kwenye yale matatizo.
Mpaka jioni shangazi wa Sabrina alipoondoka bado hawakujua cha kufanya katika kumsaidia Sabrina kurudisha kumbukumbu zake.
Bado Sam alikuwa na matumaini ya kwamba Sabrina anaweza kusaidiwa na Jeff juu ya kurudisha kumbukumbu zake ila alipoona siku zinaenda bila ya Jeff kumpa jibu linaloeleweka alionekana kukata tamaa juu ya hilo na kuruhusu mawasiliano kati ya yeye na Sia kupamba moto kwani Sia hakuchoka kumtafuta Sam na lengo kubwa ni kuwa nae karibu kama wapenzi.
Neema hakuwa na wa kumsaidia katika kuitoa dawa mahali alipoweka na kuamua kujitoa ufahamu kwa kumuomba Aisha amsaidie swala lake la kwenda kuitoa ile dawa.
Ingawa aibu ilimjaa ila hakuwa na jinsi zaidi ya kumwambia Aisha kwenda kuitoa ile dawa.
"Naomba unisaidie mdogo wangu tafadhari, nakuomba sana nisaidie"
Aisha alikuwa akimuangalia tu Neema huku akimuhurumia na kumshangaa pia.
Neema akamueleza Aisha mahali alipoweka hiyo dawa.
"Kwahiyo dada uliweka hiyo dawa kwa madhumuni yapi?"
"Acha tu mdogo wangu, nilimpenda Sam na alikuwa mume wa mtu kwahiyo nikaenda kuchukua dawa kwa mganga na hapo ninapokuelekeza ni mahali ambapo niliweka dawa moja wapo ya kumvutia. Ila dawa ile ilikuwa ikimdhuru huyo mke wa Sam"
Aisha akashangaa sana,
"Kwahiyo mimi haiwezi kunidhuru?"
"Haiwezi kukudhuru wewe, hata hivyo kumbuka kuwa dawa ile ilikuwa na dawa zingine huku nyumbani ambapo kuna siku uliona nachoma choma moto kwahiyo lazima imezidiwa nguvu na haiwezi kufanya chochote. Nisaidie kuitoa, nataka hata kama nikifa basi nife kwa amani"
"Amini utapona dada"
Neema akatabasamu tu, kwani ukweli wa mambo aliujua kuwa hawezi kupona kabisa, na alimshukuru Aisha kwa moyo aliokuwa nao, kwani ilikuwa si rahisi kwa mtu kuendelea kuvumilia ile harufu iliyokuwa ikitoka kwenye mwili wake.
Kwahiyo kwake Aisha alikuwa ni mtu muhimu na wa kipekee sana.
Huku Aisha naye akiwaza mambo mengi bila ya majibu yoyote yale ingawa alikubali kile alichotumwa na Neema na kuahidi kukitelekeza.
Jeff naye alifikiria sana jinsi ya yeye kuweza kumsaidia Sabrina, na alijua wazi kuwa ni lazima akimsomea ile barua Sabrina ataelewa tu.
Muda huo akaamua kutoka pale kwao na kumuaga mama yake kuwa anaenda kwakina Sabrina ambapo mama yake akamwambia,
"Ila Jeff mwanangu, mficha maradhi kifo humuumbua"
"Jamani mama, kwani mi nimeficha kitu gani?"
"Unajua mwenyewe unachonificha ila ipo siku nitajua tu ingawa inakuwa ngumu kwa mimi kuamini hili"
Jeff akamuangalia mama yake na kuhisi kuwa kuna kitu mama yake ameanza kukihisi juu yake, ingawa kwa binafsi yake haoni tatizo kwa mama yake kutambua hilo ila tu anahofia kwa upande wa Sabrina ambaye hakutaka ijulikane sehemu yoyote ile.
Basi Sam akaondoka pale kwao na kuelekea kwakina Sabrina.
Sam alikuwa nyumbani kwake huku akiwa na mawazo sana na kumngoja mgeni ambaye ametoka kuongea nae kwenye simu, huku yeye akiendelea taratibu kunywa vinywaji vyake vyenye kilevi huku akiamini kuwa ndio vitakavyomsaidia kupunguza mawazo au kuyaondoa kabisa.
Muda kidogo aliwasili mgeni wake ambaye alikuwa ni Sia.
Sam alitabasamu kumuona na kumkaribisha.
"Nashukuru umekuja Sia, sikujua kama ungekuja tena toka siku ile kwani ilionyesha umechukizwa sana. Ingawa tulikuwa tukiwasiliana ila sikujua kama ungekuja. Nisamehe sana"
"Usijali Sam, ila hujaniambia hadi leo. Vipi yule mtu alikusaidia?"
"Anisaidie wapi? Hadi leo kimya. Yule naye mzushi tu, alifanya nikuondoe wewe huku nikiamini kuwa atakuwa na msaada kwangu ila hadi leo hajanijibu chochote yani"
"Pole, ila hutakiwi kuwa na mawazo kiasi hicho. Naomba uniangalie mimi na kunisikiliza, nakuhakikishia kwa kupitia mimi utasahau kila kitu."
Sam akatabasamu pale na kuanza kumuangalia Sia sasa.
Jeff akafika nyumbani kwakina Sabrina na kumkuta akiwa ametulia na mama yake kwani watoto walikuwa wamelala.
Jeff akawasalimia kisha kumuomba Sabrina,
"Naomba twende mahali, kuna kitu nataka kukuonyesha"
"Mmh wapi huko?"
Mama Sabrina aliuliza kwa mshangao,
"Sio sehemu mbaya bibi, na wala hatutachelewa"
"Ila si unajua kama hana kumbukumbu"
"Natambua vizuri bibi, ila nitakuwa nae makini kupita maelezo ya kawaida na kama una kikitokea chochote kibaya basi iwe mimi wa kulaumiwa"
Mama Sabrina akamuangalia Jeff na kukubali ila Sabrina alikuwa kimya kabisa kanakwamba anayezungumziwa pale si yeye.
Mama Sabrina akamtazama Sabrina na kumwambia,
"Hivi haya tunayozungumza hapa unayaelewa kweli?"
"Nawaelewa ndio"
Sabrina akainuka na kumwangalia Jeff kisha akamwambia,
"Ndio tunaenda au?"
Jeff hakutaka kusita kwani alijua wazi kuwa iwapo Sabrina akibadili maamuzi basi itakuwa ni ngumu sana kuendelea kumshawishi kwenda, kwahiyo alipokubali tu akatoka naye.
Jeff aliita gari ya kukodi kisha safari ya yeye na Sabrina kuanza kuelekea kwenye ile hoteli aliyoenda mara ya mwisho na Sabrina kabla ya yeye kwenda nje kusoma.
Walipofika hotelini wakashuka na kumfanya Sabrina amuulize Jeff kwa mshangao,
"Mbona umenileta hotelini?"
"Nimekuleta si kwa nia mbaya ila kwa lengo la kukuonyesha kitu na kuangalia kama unaweza kurudiwa na kumbukumbu zako"
Jeff akamuomba Sabrina kuwa waingie ndani ila Sabrina alionekana kusita kwa hilo mpaka pale Jeff alipombembeleza na kumuhakikishia kuwa hawezi kufanya chochote kibaya.
Waliingia ndani kwenye chumba ambacho Jeff alikodi.
Kisha akamuomba Sabrina akae kwenye kochi na yeye kukaa kitandani, halafu akatoa ile barua ili amsomee.
"Tafadhari nisikilize kwa makini ninapoisoma hii barua na wala sina nia yoyote zaidi ya kusoma hii barua"
Sabrina alitulia na kumsikiliza Jeff ambaye alianza kuisoma ile barua sasa,
"Ni usiku sana nimeamka na kuandika haya. Kwako Jeff mpenzi, najua utashtuka sana baada ya mimi kukuita mpenzi hapo juu, yote hiyo imetokana na swala moja tu nalo ni upendo unaonipatia. Umekuwa mstari wa mbele katika kunipenda mimi, ni mara nyingi sana nimekuwa nikikukatisha tamaa kwa kukufokea hata kukufukuza lakini wewe umekuwa mwanaume mvumilivu kwangu.
Kesho unasafiri Jeff ndiomana nimeamua niandike haya maana hatujui mambo yajayo, jua kwamba nakupenda sana tena sana. Kitu kinachonizuia kuwa na wewe ni aibu, aibu ya umri, aibu ya mazoea.
Jeff wewe umekuwa kama mtoto kwangu, ni nani anayeweza kukubali mahusiano ya mimi na wewe? Ni nani atakayeweza kututazama mara mbili katika familia zetu? Jibu ni hakuna, ila moyo wangu na wako ndio unaojua ni jinsi gani tunapendana. Napenda iwe siri ingawa watu husema kuwa penzi ni kikohozi kulificha huwezi.
Napenda kukiri jambo hili kwako, hakuna mapenzi niliyowahi kuyafurahia kama yako. Pia napenda ujue kuwa wewe ni mwanaume wa pekee uliyefanikiwa kuwa na mimi kimwili, najua utakuwa unajiuliza kuhusu Sam ila siri ya Sam ninayo mimi. Napenda kukwambia kwamba.........."
Jeff akakwamia hapo kwani aliona kimya kimetanda, akamtazama Sabrina pale kwenye kochi alipokaa, akamuona amefunga macho huku kichwa chake kikiangalia juu ila alikuwa akitokwa na machozi mfululizo.
Jeff akainuka na kumfata pale kwenye kiti, Sabrina alionekana kuwa na maumivu ya moyo kwani alikuwa akilia kwa uchungu.
Jeff alipojaribu kumbembeleza, Sabrina alimtazama Jeff na kumzaba kibao cha nguvu.
Jeff akainuka na kumfata pale kwenye kiti, Sabrina
alionekana kuwa na maumivu ya moyo kwani
alikuwa akilia kwa uchungu.
Jeff alipojaribu kumbembeleza, Sabrina alimtazama
Jeff na kumzaba kibao cha nguvu.
Jeff alijikuta akiwa kama ameganda huku akimtazama tu Sabrina ambapo Sabrina alimnasa tena kibao cha pili na kumuuliza kwa hasira,
"Nani kakutuma unilete huku tena Jeff? Nakuuliza wewe?"
Jeff akatabasamu kwani alijua tayari Sabrina amerudiwa na kumbukumbu zake.
Ila Sabrina alichukizwa zaidi na kile kitendo cha Jeff kutabasamu na kumfanya azidi kulia kwa hasira.
Jeff akamkumbatia sasa kama ishara ya kumbembeleza na kufurahi ile hali aliyonayo ya kurudiwa na kumbukumbu.
Jeff alimkumbatia tu ingawa Sabrina bado aliendelea kulalamika,
"Kwanini Jeff kwanini umenileta tena huku? Kwanini hutaki kuheshimu ndoa yangu?"
"Nisamehe Sabrina, sijakuleta huku kwa lengo lolote baya. Nakupenda sana na nilikuwa nataka urudiwe na kumbukumbu zako"
"Kwani nilipoteza kumbukumbu?"
"Ndio Sabrina, nisamehe kwanza na pia naomba utulie ili nikueleweshe kidogo"
Sabrina akamtazama kwa makini sasa Jeff na kumuona ana mabadiliko tofauti na alivyokuwa awali.
"Ila saivi Jeff umekuwa mkubwa. Kwani ni kitu gani kinatokea hapa? Mbona sielewi?"
Jeff aliamua kumtuliza kwanza na kumwambia kwa kifupi kuwa alipoteza kumbukumbu kwa miezi kadhaa hata yeye alikuwa hamkumbuki.
"Kweli nilikuwa sikukumbuki wewe?"
"Ndio hukunikumbuka kabisa, na siku niliporudi na kukuona ndio siku hiyo ulishikwa uchungu na kwenda kujifungua"
"Kwahiyo nimeshajifungua?"
"Ndio mtoto wa kiume na amefanana na mimi balaa"
"Hapo ndio unapoanza kunikera sasa"
Akakaa na kufikiria kidogo, akaona kama mambo yamebadilika sana hakujielewa kwa muda huo.
"Naomba nipeleke kwa Sam, tafadhari Jeff"
Jeff alimuangalia kwa kumuhurumia na hakuweza kukataa lile swala ingawa hakuona kama ni vyema kwenda nae moja kwa moja kwa Sam.
"Kwanini tusirudi kwanza nyumbani halafu kwa Sam tukaenda hata kesho?"
"Hapana Jeff, nataka kumuona Sam nahitaji sana nimuone kwanza hapa sielewi chochote. Tafadhari nipeleke kwanza kwa Sam, kuna kitu nakihitaji"
Jeff akaamua kutoka pale na Sabrina kisha kuianza safari ya kwenda kwa Sam.
Aisha naye alikubaliana na Neema kuwa siku hiyo aende mahali alipomuelekeza kuwa akaitoe ile dawa, na kama alivyokubali hakuona kama hilo ni jambo zito kiasi hicho mpaka kwa yeye kushindwa kulifanya.
Kwahiyo akawa ameondoka nyumbani kwa Neema huku akiwa na maelekezo ya kutosha.
Alienda mpaka alipoelekezwa na Neema huku wakiendelea kuwasiliana kwenye simu ili ikitokea kama atasahau basi amuulize kwenye simu na aweze kumuelekeza tena.
Aisha alifika mpaka kwenye mti ambao alihisi kuwa ndio alioelekezwa na Neema huku akiangalia uwepo wa wapita njia na kujaribu kufanya kile alichoelekezwa.
"Mmh dada Neema aliwezaje kufanya haya karibia na nyumba ya mtu kiasi hiki? Hivi kwa mfano wenyewe wakatoka na kuzunguka hapa na kunikuta nitajiteteaje mimi? Mungu nisaidie kwa hili ninaloenda kufanya."
Aisha alikaa pale chini ya mti na kukaribu kufukua fukua ili aone kwani alipomuuliza Neema alimwambia ndio hapo hapo.
Sia alikuwa ndani kwa Sam akiendelea na harakati zake za kuchekecha hisia za Sam kwani alikuwa akicheza na kukatika haswa, alipoona kuwa inachukua muda mrefu kumteka Sam akaamua kuongeza sauti ya mziki huku akitoa nguo moja moja kwenye mwili wake.
Sam alikuwa akimtazama tu Sia anavyokatika, na kweli alikuwa akijua kucheza na kwa mwanaume yeyote rijali lazima mate yamtoke kwa kucheza kule tena bila nguo.
Sam akajikuta naye akiinuka na kuungana na Sia katika kucheza huku Sia akitumia nafasi hiyo kumtoa Sam nguo moja moja katika mwili wake.
Ila alipofikia kuitoa nguo ya ndani ya Sam, ni pale Sam akamzuia na kumfanya Sia ajiulize kuwa huyu mwanaume ni vipi kwanini agomee pale? Akahisi kuwa labda manjonjo yake hayakumvutia vizuri na kumfanya atafute pozi la kumvuta zaidi Sam.
Sia hakumvua tena Sam ile nguo ya ndani ila aliendelea kunengua na kucheza kitu ambacho kilimvutia zaidi Sam.
Kwavile Sia alikuwa na makalio makubwa, akaamua kutumia makalio yake hayo kumteka Sam ambapo aliinama huku anamkatikia Sam karibia na nguo yake ya ndani huku akimshawishi afanye kile anachokitaka.
Kwavile Sam naye ni mwanaume, hakuweza kustahimili zaidi hali ile na kumpa Sia anachostahili.
Kelele nyingine leo ilimshtua yule mlinzi wa Sam pale getini ila hakuielewa vizuri kwavile ilichanganyika na sauti za mziki.
Mlinzi wa Sam alijiuliza tu pale bila ya kupata majibu kwani kwa kelele ile ilikuwa ni kama mtu amekutana na kitu cha ajabu ila ni kelele ambayo aliisikia na kukatika gafla huku sauti ya mziki ikiendelea.
Hakutaka kufatilia kwani hayamuhusu na ukizingatia pale yupo kazini.
Aisha naye pale chini ya mti alibahatika kusikia ile kelele na kumfanya ashtuke sana ila hakuelewa chochote kinachoendelea huku akijaribu kuchimba haraka harana na aweze kuwahi kuondoka pale kwenye mti.
Muda kidogo akaona watu wawili wakiwa wameongozana na wanaelekea katika ile nyumba, alikuwa ni mdada na mkaka.
Aisha akaamua kujigeresha na kuacha kuchimba ili hata kama wakimuuliza aseme kuwa alikuwa amepumzika tu ila walipita bila ya kumuuliza chochote.
Aisha alipotazama kwenye kile kishimo anachokichimba kwa kisu, akaona kitu alichoelekezwa na Neema na kukivuta kwani kilikuwa kwenye mfuko ila kilikuwa kikipumua kama mtu na kumfanya Aisha atetemeke sana huku akikiweka kwenye mkoba wake.
Jeff na Sabrina walimkuta mlinzi wa Sam kama kawaida ambaye alikuwa tu akimshangaa Sabrina na kumuuliza,
"Unaendeleaje dada?"
"Naendelea vizuri, Sam yupo?"
Mlinzi alikuwa akiitikia kwa kusitasita na kumfanya Sabrina ampite pale getini na kuanza kufata nyumba huku Jeff akiwa nyuma yake.
Sabrina alishangazwa na ule mziki mkubwa aliousikia kutoka ndani kwa Sam na kushangaa sana kwani si kawaida ya Sam kusikiliza mziki mkubwa kiasi kile.
"Yani kama disko"
Huku akiendelea kuufata mlango.
Sam alimuhurumia sana Sia ila tayari ilishatokea hapakuwa na jinsi tena zaidi ya kuvaa nguo zake na kumsitiri Sia kwa kumfunika shuka kwani alikuwa amekaa huku akilia sana yani Sia hakuamini kile kilichompata kwa siku hiyo na kumfanya ahisi kupagawa huku akiwa na maumivu makali kwenye sehemu zake za siri.
Alilia sana na hakutaka hata kumtazama Sam,
"Tafadhari Sia usimwambie mtu yeyote"
Sam alikuwa akimbembeleza Sia huku amemshika bega, ila Sia aliurusha ule mkono wa Sam pembeni na kusema kwa ukali,
"Niache shetani mkubwa wewe"
Sia alichukua blezia yake na kuvaa, alipoinuka pale alipokaa alishangaa kuona pametapakaa damu na kujigundua kuwa lazima ameumizwa kupita vile anavyofikiria.
Akachukua nguo yake ya ndani na kuvaa.
Gafla wakashtuka mlango wa sebleni ukifunguliwa ndio Sam alipogundua kuwa hakuufunga mlango ule.
Macho ya Sia yakagongana na macho ya Sabrina ambapo Sabrina alimuangalia Sia kwa mshangao kwani Sia alikuwa na nguo ya ndani tu na ile blezia aliyovaa mwanzoni.
Sabrina akamwambia Sia kwa ukali,
"Sia!! Unafanya nini kwa mume wangu?"
Kisha akamuangalia Sam na kumwambia,
"Kumbe Sam nisipokuwepo ndio huwa unanifanyia hivi?"
Sam aliona aibu na kuinamisha macho chini, Sia naye aliona aibu ukizingatia kitendo alichofanyiwa na kumuona Sabrina mbele yake haikuwa rahisi kwake, alijikuta akijifunga lile shuka kwa aibu na kutoka mule ndani bila ya kuongea chochote.
Ila alipofika mlangoni, Sabrina akamvuta Sia na kumnasa kibao,
"Malaya mkubwa wewe, kuja hapa"
Sam akaona hii itakuwa khatari ukizingatia tayari Sia ameshapata pigo kama lile, ikabidi ainuke na kumshikiria Sabrina kisha kumwambia Sia achukue vitu vyake na kuondoka.
Alitoka nje na shuka huku akilia sana hata mlinzi wa Sam alimshangaa huku akiamini kuwa Sabrina atakuwa kamfanya kitu tu kwani ishakuwa kawaida yake ya kupambana na wadada wanaotembea na Sam.
Sia alishachanganyikiwa tayari, alitoka hadi nje na kukosa muelekeo kisha akarudi na kumuomba yule mlinzi wa Sam amuitie gari za kukodi.
Aisha aliyekuwa anakaribia kuondoka pale alishangaa kumuona Sia akiwa kajifunga shuka tena akionekana kuwa amechanganyikiwa na kupoteza muelekeo, kisha akamuona akirudi tena na kuamua kumfata na kumkuta akizungumza na yule mlinzi kisha akamshtua,
"Sia"
Sia akashtuka na kugeuka, akamuona Aisha na kumfata kisha akamkumbatia huku akilia sana.
Gari ya kukodi ilipofika, wakapanda na kuondoka.
Nyumbani kwakina Sabrina, alifika na Sakina kumuulizia Jeff.
"Maana leo kaondoka mapema na kudai anakuja huku"
"Ni kweli alikuja ila ameondoka na Sabrina hata nashangaa hawajarudi hadi muda huu."
Sakina alikaa kimya kwa muda akitafakari mahali ambako Jeff na Sabrina watakuwa wameenda bila ya kupata jibu huku moyo wake ukizidi kupata hofu juu yao.
"Tafadhari Mungu isiwe hivi ninavyofikiria"
Mama Sabrina akamuuliza Sakina kwa mshangao kuwa ni kitu gani anachofikiria.
"Kwakweli mama sielewi yani sielewi kabisa"
Mtoto mdogo wa Sabrina aliamka na kuanza kulia, ikabidi mama Sabrina na Sakina waingie ndani.
Kwavile mama Sabrina alikuwa kambeba Cherry mgongoni, ikabidi Sakina amchukue yule mtoto mdogo na kumbembeleza.
"Vipi mmeshampa jina huyu mama?"
"Ndio, kapewa jina na shangazi wa Sabrina kuwa aitwe Sam"
"Sam!"
"Ndio Sam mbona umeshangaa?"
"Kwahiyo ataitwa Sam Sam?"
"Ndio, hakuna ubaya kuitwa hivyo"
Sakina alikuwa akimtazama tu huyu mtoto kwani kulikuwa na kila sababu ya kumpa yeye jina kwavile alikuwa na hisia zote kuwa yule mtoto ni wa Jeff ingawa hakuwa na hakika na hisia zake.
Ila macho yake hayakubanduka kwenye sura ya mtoto huyu ukizingatia kuwa alimfananisha moja kwa moja na mwanae Jeff.
Sabrina alikuwa na hasira sana mule ndani ukizingatia kuwa yeye hajawahi kulala na Sam, kwahiyo kitendo cha kuona mwanamke vile kilimkera sana na wala hakutilia maanani kama kuna damu mule ndani kwani aliongea kwa mfululizo kisha kutoka nje.
Jeff naye alikuwepo katika kumfatilia nyuma nyuma ili kuhakikisha kwamba hawezi kupotea.
Sabrina na Jeff walipofika pale nje ndipo walipoona ile gari ya kukodi waliyopanda wakina Sia ikiishia, Sabrina akatamani kupata gari nyingine ya haraka ili wawafatilie ila Jeff akamzuia na kumsihi warudi nyumbani.
"Tafadhari twende nyumbani, kumbuka watoto tumewaacha. Kumbuka una mtoto mdogo sana anahitaji kunyonya, tafadhari twende nyumbani"
Kisha Jeff akatafuta usafiri wa kuwarudisha.
Sabrina alikuwa akilalamika tu kwenye gari mwanzo mwisho, mpaka Jeff aliamua kumuuliza kwani aliona wazi kuwa kunauwezekano mkubwa wa Sabrina kuwa anafahamiana na yule dada.
"Kwani unamfahamu yule?"
"Namfahamu vizuri sana, alikuwa rafiki yangu hapo zamani ila alinitendea kitu cha ajabu. Alifanya niende mahabusu bila makosa, alifanya nione mji mbaya halafu leo hii ananiibia mume wangu? Mngeniacha nimfundishe adabu yule, yani leo ningemkumbushia machungu yote niliyoyapata kule mahabusu"
"Pole sana, kumbe ndio huyu alifanya uteseke kipindi kile dah pole sana"
Sabrina alikuwa akisema maneno yote mabaya dhidi ya Sia huku akikumbukia alikopitia yeye mpaka kufikia hapo.
Walifika nyumbani na kumkuta Sakina na mama yake wakiendelea na harakati za kubembeleza watoto.
Sabrina alipowaona alienda kuwakumbatia kanakwamba hakuwaona kwa muda mrefu sana na kufanya wamshangae.
Inaendeleah
No comments: