Simulizi: Je haya ni mapenzi sehemu ya tisa (9)
Akamfata karibu, kisha akachukua mkasi
uliokuwepo kwenye meza ya Sabrina na kuikata
ile kamba.
Sabrina akapigwa na butwaa kwani kilikuwa ni kitendo cha gafla kwa mama yake kuikata ile kamba.
Alitamani apige makelele kwa kulia kwani aliona mambo yake yote yakiharibika, hakutegemea kama mama yake angefanya vile alivyofanya.
Sabrina alikaa chini huku machozi yakimtoka
"Yani unalia sababu ya hii kamba Sabrina? Mbona unaniletea mambo ya ajabu wewe mtoto jamani!"
Sabrina alikuwa kimya kabisa huku machozi yakimtoka, ila Joy hakujua ni kwanini mtoto wake alikuwa akitokwa na machozi kiasi kile, hakujua kama ile kamba ilikuwa na maana kubwa sana kwenye kiuno cha mwanae.
"Sabrina, hivi wewe mtoto una kichaa au ni kitu gani jamani? Unajua sikuelewi! Yani sikuelewi kabisa. Eti unalia na kulia sababu ya huo uchafu nilioukata, mtoto mwehu kweli wewe"
Joy akatoka chumbani kwa mwanae na kwenda kuendelea na kazi zake zingine.
Sakina alipoona muda unapita tu bila ya Sabrina kutokezea, akaamua kwenda kumfata mwenyewe.
Na alipofika alikaribishwa na Joy, wakasalimiana na kumuulizia Sabrina.
"Asubuhi yote hii Sabrina wa nini?"
"Kuna mahali nilipanga nae kwenda ila sijamuona hadi sasa"
"Wewe si ndio msiri wake! Nenda huko chumbani kwake ukamuangalie anavyolia lia"
Sakina akashangaa kumuona Joy akiongea kwa jazba kiasi kile, akajua kwa vyovyote vile lazima kuna kitu Joy amekijua kuhusu Sabrina.
Akaongoza moja kwa moja mpaka kwenye chumba cha Sabrina, alimkuta kajifunga khanga huku amejiinamia na machozi kumtoka.
"Nini tatizo Sabrina mdogo wangu jamani?"
Sabrina akamuonyesha Sakina ile kamba pale chini na kumfanya Sakina nae ashtuke kisha akamuuliza kuwa imekuwaje.
"Mama kaikata na mkasi"
"Ameionaje?"
Sabrina akamuelekeza Sakina ilivyokuwa
"Nilijua tu kuwa mama yako akijua itakuwa balaa kama hivi, yani mamako kaongeza tatizo juu ya tatizo hata sijui itakuwaje jamani!"
"Nisaidie dada, nitafanyaje mimi jamani!"
"Basi ngoja tufanye kitu, najua wewe haupo sawa kwasasa. Hivyobasi ngoja mimi niende mahali kuulizia vizuri kuwa tufanyaje kisha nitakwambia kila kitu mdogo wangu. Punguza mawazo, mimi nipo kukusaidia Sabrina"
"Basi nitashukuru dada"
Sakina akampooza pale Sabrina kisha akamuaga na kuondoka.
Kufika nje, akamuaga na Joy ili aende zake
"Nenda mama, ya kiunoni nimeikata. Nenda ukamletee ya shingoni sasa ili niione vizuri na nitaichoma moto"
Sakina alimuangalia tu Joy kwani alielewa wazi kama akiamua kubishana nae basi atabishana nae hadi siku ya pili.
Akamuaga tena na kuondoka.
John baada ya kusikia mkasa alioufanya mpenzi wake kwa Sabrina akajihisi vibaya na kuamua kumpigia simu Sabrina ili aweze kumuomba msamaha.
Ila ile simu iliita tu bilawake na ndiomana hakutaka kuwasiliana nae tena bila kujua kwamba Sabrina alikuwa na matatizo mengine yaliyomsumbua akili yake tayari.
Sabrina hakujisikia vizuri kabisa siku ya leo, kila alipofikiria masharti ya ile kamba ya kiunoni iliyokatwa hakujua itakuwaje. Hakujua mama yake atapatwa na janga gani baada ya kumkata ile kamba.
Alijihisi vibaya na moyo kumuuma sana kwa mawazo.
Aliisikia simu yake ikiita ila hakujisikia kuzungumza na mtu yeyote wala kumjibu ujumbe mtu yeyote kwahiyo alikuwa akiitazama tu simu yake wakati inaita.
Joy alikaa na kujifikiria sana, alihisi kuwa mwanae ana mapepo na ndiomana amekuwa akifanya mambo ya ajabu.
Akaamua kumpigia simu mchungaji wao na kumueleza matatizo ya mtoto wake.
"Nimekuelewa mama James, nadhani jioni nitafika hapo na nitapenda kuzungumza na huyo binti yako"
"Hakuna tatizo mchungaji, utamkuta tu hapa nyumbani"
"Ila kuna huduma nafanya, kwahiyo itakuwa ni jioni sana"
"Hakuna tatizo, cha muhimu ni ufike tu"
Joy akaona itakuwa afadhari kwa binti yake kuzungumza na huyo mtumishi wa Mungu, kwakuwa matendo yake yalimdhihirishia wazi kuwa mwanae ana mapepo kwani yale mambo ya kujifunga kamba za kichawi kiunoni hayakuwa ya kawaida.
"Yani mtoto wangu ni wa ajabu huyu mmh! Maombi kwake mwiko, yeye na ushirikina tu hata sijui kajifunzia wapi!"
Joy alikuwa akijilalamisha mwenyewe tu bila ya muafaka wa anachokilalamikia kwa muda huo.
Sabrina akaona kujifungia ndani ni kuzidi kujipa mawazo tu, kwahiyo akaona ni vyema hata atoke na kutembea tembea kidogo ili kupoteza mawazo mpaka pale Sakina atakaporudi.
Alitoka na kumuaga mama yake kuwa anaenda kutembea tembea kidogo
"Umepata nguvu ya kuzurulia sasa eeeh!"
"Sio hivyo mama"
"Nini sasa?"
"Siendi mbali mama, nafika hapo kwa rafiki yangu Sia tu"
"Haya wee nenda tu, naona leo hata wakina Sia wamekumbukwa ila uwahi kurudi tu"
"Sawa mama"
Sabrina akaondoka na kwenda kwa huyo rafiki yake.
Alipofika alimkuta rafiki yake na kufurahi sana, walikaa na kuongea mambo mengi sana.
"Sabrina, hivi yule kaka yangu Japhet unamjua?"
"Ndio namjua, kafanyaje kwani?"
"Jamani Sabrina, kaka yangu anakupenda yule yani kafa kaoza kwako"
"Mmh Sia ya kweli hayo!"
"Mie nitakudanganyaje wewe shoga yangu jamani! Kaka yangu anakupenda, tena anakupenda sana Sabrina"
Sabrina alijikuta akitabasamu kwa furaha kwani alikuwa na tatizo kubwa moja, yani yeye akisikia kuwa anapendwa alijihisi kama kupagawa wakati zamani alikuwa hataki hata kusikia kuhusu mapenzi ila siku hizi akiambiwa anapendwa basi anajihisi kama ni malkia pekee kwenye dunia.
Kwahiyo swala la Sia kumwambia kuwa anapendwa na kaka yake lilimfanya asahau matatizo yake kwa muda na kujisikia vizuri,
"Nimpe namba zako? Maana aliniomba mawasiliano yako ili akwambie mwenyewe"
"Mpe tu namba zangu, hakuna tatizo"
"Mmh Sabrina! Je na wewe utampenda?"
"Sijui"
Na kuanza kucheka, Sia akapata jibu kuwa lazima Sabrina nae atakuwa anampenda kaka yake huyo ila tu hakuweza kusema.
Wakaongea mengi sana, na mwisho wa siku Sabrina akaaga na kuanza safari ya kurudi kwao.
Akiwa njiani kuelekea nyumbani kwao, alipita karibu na mti wa mbuyu.
Mti ule ulikuwa umefungwa kwa pembeni kitambaa chekundu na cheusi, halafu chini yake kulikuwa na kiwembe kimoja na yai ambalo lilikuwa limechorwa chorwa kwa maandishi mekundu.
Sabrina akaogopa sana kupita na kuanza kurudi nyuma nyuma, alipofanikiwa kufika nyuma akaanza kukimbia kwa uoga kwani hakutegemea ile hali kwakweli, hakutegemea kukutana na vitu vya aina ile pale njiani.
Alipofika mbele alisimama na kuhema sana, mara akapita mmama mmoja ambaye hakuwahi kumuona yani ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kumuona.
Yule mmama akamwambia Sabrina,
"Kilichokukimbiza ni nini wakati wewe ni jasiri!"
Sabrina akamuangalia huyu mmama bila ya kumjibu kitu chochote na kuendelea na safari yake, ila yule mmama akamuita Sabrina kwa nguvu
"Wee Sabrina!"
Sabrina akaogopa kuona huyu mama kamuita kiasi hicho, inamaana anamjua. Na kama anamjua basi anamjuaje!
Sabrina akasita kugeuka na kuendelea kutembea kwa nguvu, akaisikia sauti ya yule mmama ikisema
"Unajifanya kiburi eeh!! Utaona sasa"
Sabrina akaogopa sana na kumfanya aanze kukimbia ili aweze kupotea kwenye eneo hilo aliloona kuwa linampa maajabu tu.
Akakimbia sana na kutokea katika mitaa ya kwao, moja kwa moja alirudi nyumbani kwao na kumkuta mama yake akiwa ametulia tu
"Leo umewahi kurudi kweli!"
"Ndio mama, nimekuwa mtoto mzuri"
"Haya, mmbea mwenzio katoka hapa sasa hivi anakutafuta"
"Nani huyo mama?"
"Nani mwingine zaidi ya Sakina! Kasema uende kwake haraka uwezavyo"
Basi Sabrina alivyoambiwa hivyo hakutaka kupoteza muda na kugeuka ili aende ila kabla hajaondoka mama yake akamwambia
"Na nilijua tu baada ya ujumbe huo hutotoka hata kuingia ndani na kunywa maji tu, basi uwahi kurudi sababu kuna mtu wa muhimu sana anakuja leo kuzungumza na wewe"
"Sawa mama"
Sabrina alimuitikia mama yake ila bado alikuwa na kinyongo kikubwa sana dhidi yake kutokana na ile kamba ambayo aliikata siku hiyo na kumfanya akose raha ya maisha kwa siku nzima.
Alipofika kwa Sakina, alimkuta nyumbani kwake kama kawaida.
Na moja kwa moja Sakina alianza kumuelezea Sabrina aliyoenda kuyakuta huko alipotoka
"Mwenzangu Sabrina kuna makubwa"
"Niambie dada, si unajua nina matatizo! Sasa unaponiambia hivyo unazidi kunitisha jamani"
"Yani ile kamba haikutakiwa kukatwa na mtu yoyote yule, kwavile mama yako kaikata basi kuna majanga yatampata"
"Mmh majanga gani hayo?"
"Tena kuna mawili, anaweza akapona au asipone kabisa na kama atapona basi kunatatizo litajitokeza kwani anaweza akapararaizi"
Hii habari ilimuumiza sana Sabrina, alijihisi atanywea sasa
"Sasa nitafanyaje dada katika kumnusuru mama yangu?"
"Mmh hata mi mwenyewe sielewi ila..."
Kabla hajaendelea, simu ya Sakina ikaita na kumfanya apokee simu ile na kukatisha yale maongezi huku Sabrina akiwa na hamu ya kujua kitu kwani ile ila ya Sakina ilimfanya ahisi kuwa kuna njia ya wao kukomboka na yale majanga.
Sakina alipomaliza kuongea na ile simu, akamuangalia Sabrina kwa makini sana na kumuuliza swali moja tu
"Ulikuwa wapi leo?"
"Nilikuwa kwa rafiki yangu Sia"
"Ni kitu gani kimekutokea?"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Huku akimuangalia Sabrina kwa makini sana na kumfanya aanze kuingiwa na uoga huku akimuelezea yaliyomtokea wakati anatoka kuonana na Sia.
"Kwahiyo huyo mama aliyekuita hukuweza kumsikiliza?"
"Hata kama ungekuwa wewe dada usingeweza, alikuwa akiniita kwa ukari sana na kuniambia maneno ya kejeli"
"Sasa kwa taarifa yako tu ni kuwa yule mmama ndio alikuwa mtu pekee wa kukusaidia wewe na hilo tatizo lako"
Sabrina akashtuka na kushangaa kuwa mtoa msaada gani anakuwa mkali kiasi kile!
"Mmmh dada, mbona leo unanipa maajabu zaidi?"
"Sio maajabu ila wewe umeshindwa kupata msaada kwa ujinga wako mwenyewe. Kwanini hukutaka kumsikiliza?"
"Basi tena dada, hakuna la kufanya nimeshakosea tayari"
"Kwahiyo kirahisi tu hivyo unaitikia kuwa huna la kufanya kwavile umeshakosea tayari! Hivi unajua matatizo vizuri wewe Sabrina? Angalia jinsi ya kumuokoa mama yako, maana hapa muathirika sio wewe tu bali na mama yako pia"
Sabrina alihisi kichwa chake kuvurugika kwani hakujua ni vipi anapata msaada ikiwa wazi huyo mmama alimkimbia, alijua ni wale washirikina waliokuwa wakimsumbua.
Wakaongea mengi sana na Sakina ila hawakupata muafaka wa jambo lolote lile zaidi ya kuongea tu.
Sabrina alitulia kimya akitafakari cha kufanya na hali ya mama yake pia.
Simu ya Sabrina ikaita, na akaipokea kwa unyonge sana kwani alishakuwa na mawazo tayari
"Japhet naongea hapa"
"Aaah! Mambo vipi?"
"Poa tu, je tunaweza kuonana muda huu?"
Sabrina akajifikiria kidogo kumjibu, kisha akakubali kuonana nae na kupanga pa kukutana na huyo Japhet, kisha akakata simu.
Akamuangalia Sakina na kumuaga
"Unaenda wapi sasa Sabrina?"
"Kuna mahali nataka kwenda nikatulize akili yangu"
"Ila kwa ushauri wangu mie ni bora uka...."
Kabla hajamaliza, simu ya Sabrina iliita tena, naye akapokea
"Francis anaongea hapa"
Akajua moja kwa moja kuwa anataka kumpa hali ya Fredy tu,
"Eeh niambie"
"Nipo hapa kwenu naomba uje haraka"
Halafu akakata ile simu, Sabrina akamuangalia Sakina na kumwambia
"Huyu mwanaume ana wazimu nini? Eti uje haraka, halafu anipe nini! Ngoja nikaonane na huyo Japhet kwanza"
"Ila si yupo kwenu huyo!"
"Ndio yupo nyumbani"
"Basi nakuomba uende nyumbani kwenu kwanza kwani kuna kitu nahisi kuwa hakipo sawa huko"
Sabrina akajiona kama yupo njiapanda, na kuamua kurudi kwao huku akiwa amenuna kabisa.
Alipofika kwao, alimkuta Francis akiwa nje ya nyumba yao, naye alipomuona tu akamkimbilia Sabrina na kumwambia
"Siielewi hali ya mama yako"
Sabrina hakutaka kusikiliza zaidi na kukimbilia ndani kwao ambapo alimkuta mama yake amekaa huku ametambaliza miguu yake na kurudia rudia maneno
"Kamba, kamba, kamba, kamba...."
Sabrina alishtuka kwani mama yake alikuwa kamavile mtu aliyewehuka na alipomuona tu Sabrina, akaacha kusema na kuanguka chini huku akitapatapa.
Sabrina alishtuka kwani mama yake alikuwa
kamavile mtu aliyewehuka na alipomuona tu
Sabrina, akaacha kusema na kuanguka chini huku
akitapatapa.
Sabrina akashtuka zaidi na uoga kumjaa, akaanza kupiga makelele na yeye ili aweze kupata msaada zaidi ila mwisho wa siku akagundua kuwa kelele zake hazisaidii kitu kwani atajaza watu bure tu.
Akaona njiabora ni kwenda kwa yule mmama wa njiani aliyemkimbia ili akamuombe msaada kwani hakujielewa kitu.
Akamuangalia Francis na kumuomba abakie pale na mama yake ili yeye akachukue msaada
"Sabrina, sasa utaondokaje na kumuacha mama yako katika hali kama hii?"
"Ningoje tu Francis, acha niende kwani nimfataye ndio uzima wa mama yangu"
Kisha akatoka nje na kujaribu kukimbia ili aweze kuwahi lile eneo ambalo alikutana na yule mmama.
Sabrina alikuwa anahema sana na giza nalo lilishaanza kuingia ila Sabrina hakuacha kukimbilia eneo la tukio ili aweze kuwahi.
Alipofika lile eneo, akauona ule mbuyu ila hakuona vitambaa vile alivyoviona jana yake.
Akajihisi kuchanganyikiwa, akakaa chini ya ule mbuyu huku akili yake ikikosa muelekeo.
Akiwa amejiinamia vile, akapita mtu mmoja na kumshika kichwa Sabrina, kisha Sabrina akainua kichwa na kumuangalia mtu huyo ni nani.
Alikutana na mzee wa makamo aliyekuwa amevaa nguo ndefu mpaka chini aina ya kanzu na kikofia kidogo kichwani.
Yule mzee akamuuliza "Unafanya nini hapo na giza hili binti?"
"Kuna kitu nangoja"
"Unangoja nini? Mashetani au?"
"Kuna mtu namngoja"
"Unamngoja mtu chini ya mbuyu binti yangu? Hivi unajua kama mibuyu ni nyumba za majini?"
Sabrina akashtuka sana kusikia ni nyumba za majini na kuanza kuogopa.
Yule mzee akamwambia tena Sabrina,
"Mtumainie mwenyezi Mungu, hayo mambo ya kukaa chini ya mibuyu hayatakusaidia"
Kisha yule mzee akaondoka na kumfanya Sabrina ainuke kwenye eneo lile alilokuwa amekaa.
Sabrina akaanza kuondoka taratibu huku akiangalia lile eneo labda apate kumuona tena yule mmama ili aweze kupata msaada.
Akafika mbele na kusimama huku macho yake yakiwa katika eneo lile la mbuyu na akiamini kuwa yule mmama atatokea kumpa msaada.
Wakati amesimama vile, ni kweli yule mmama akatokea ila alikuwa amekasirika sana, lakini Sabrina alishukuru huku akiamini kuwa mama yake atakuwa mzima.
Sabrina akaanza kumfata yule mmama, ila yule mmama alianza kuongea kwa hasira sana,
"Mmeniudhi sana nyumbani kwenu nyie"
Sabrina alimuangalia tu yule mmama kwani hakuelewa ni kitu gani kingendelea
"Nakwambia kwenu mmeniudhi sana, rudi nyumbani kwenu na ukawazuie yote wanayoyafanya"
"Kwani ni nini?"
"Tena uwazuie uwezavyo lasivyo mimi nammaliza mama yako"
Sabrina akaogopa sana kwani hakujua ni kitu gani kinaendelea nyumbani kwao.
Akiwa bado amesimama kwa kusitasita, yule mmama akampazia sauti
"Nammaliza mama yako, nenda wee mwanakwenda"
Ile kauli ya nammaliza mama yako ikamtisha zaidi Sabrina na kumfanya Sabrina apige magoti kwa yule mmama na kuanza kumuomba kuwa asimdhuru mama yake
"Hivi wewe mtoto una akili kweli? Watakaomdhuru mama yako ni hao waliopo nyumbani kwenu, nenda ukawazuie ili mama yako nimuachie lasivyo nammaliza leo leo"
Sabrina aliwaza kuwa ni watu gani hao wanaozuia uponyaji wa mama yake na kuamua kuanza kukimbilia maeneo ya nyumbani kwao ili akawawahi watu hao na kuwazuia ila hakujua kuwa ni watu wa aina gani.
Wakati Sabrina ameondoka kwaajili ya kumfata yule mmama kule kwenye mbuyu, huku nyumbani kwao alifika yule mchungaji ambaye alipigiwa simu asubuhi ili aweze kuja kuongea na Sabrina.
Na muda huo, Francis nae alikuwa amempigia simu mchungaji aliyekuwa anamfahamu na kuomba afike eneo hilo. Kwahiyo wale wachungaji walijikuta wamefika wote wawili kwa muda mmoja, na kwavile hali ya Joy ilikuwa mbaya waliamua kuingia kwenye maombi moja kwa moja na kuanza kukemea roho ya mapepo wakati huo Joy alikuwa hajitambui kabisa, kwani alikuwa akitapatata tu huku na kule.
Ila kadri walivyokuwa wakiomba ilionyesha Joy akipatwa na unafuu fulani.
Sabrina alipofika nyumbani kwao aliwakuta wale wachungaji wakiendelea kufanya maombi, moja kwa moja alienda kati yao na kuanza kuwazuia
"Muacheni mama yangu, hakuna anayehitaji maombi hapa"
Ila wale wachungaji waligundua wazi kuwa Sabrina anaendeshwa na mapepo kwahiyo sio akili yake inayomfanya awazuie na kufanya wazidi kufanya maombi.
Francis alibaki kushangaa kuwa kwanini Sabrina amekuwa vile na kumfata pale alipokuwa akiwazuia wale wachungaji, ila Sabrina hakuelewa wala kusikia na kumfanya apatwe na wazo lingine la kwenda kumuita yule mmama tena.
Sabrina akatoka pale kama chizi kwani alikuwa akikimbia na kumfanya Francis atake kumkimbiza ili aweze kumrudisha lakini wale wachungaji walimzuia Francis na kumwambia
"Mwache tu atarudi, Mungu ni mwaminifu"
Francis alimuacha Sabrina huku roho ikimuuma sana.
Ila wale wachungaji waliendelea na maombi ya kumuombea Joy.
Sabrina alipokaribia kufika alipokuwa anakimbilia, aliona giza zito sana yani giza ambalo huwezi hata kuona chochote kile na kumfanya aanze kuogopa.
Kisha akasikia sauti ikimkaripia kwa nguvu,
"Toka Sabrina tokaaaaaa.... Na kamwe hutokuja kupata mtoto kamwe katika maisha yako, na kila mwanaume utakayelala nae lazima afe na wewe upate kesi ya mauaji. Tokaaa Sabrinaaa....!"
Ile sauti ya mwisho ikagongana na mwangwi na kumfanya Sabrina aogope zaidi.
Ila alipiga magoti eneo lile huku machozi yakimtoka kamavile anaomba kupunguziwa ile adhabu kwani ilikuwa ni kubwa sana.
Ile sauti ikasema tena,
"Na mama yako lazima nimmalize na ba......"
Kabla hajamalizia kusema, mara ukimya ukatanda na gafla ilisikika ile sauti ikipiga ukelele wa nguvu,
"Aaaaaaaaaaaaaahhhhh.........!!!!!"
Na ikakatika gafla na kumfanya Sabrina ashtuke pale alipopiga
magoti na kuanza kuangaza macho yake ambapo yalikutana na mwanga mkali wa ajabu na kumfanya ashindwe kustahimili kuuangalia kwani alihisi ule mwanga ukimchoma choma.
Sabrina alipata nguvu ya ajabu na kuanza kukimbia huku akielekea kwao, ila kila alipokimbia ule mwanga ulizidi kumfata.
Alipofika kwao alikuwa anahema sana na moja kwa moja akaanguka mlangoni na kuzimia.
Wakambeba na kumuingiza ndani kwani hali yake haikuwa sawa, na muda huo mama yake alikuwa mzima kabisa huku akisimulia aliyokuwa akiyaona wakati ule aliokuwa akitapatapa.
Francis alikuwepo muda wote akisikiliza yaliyojiri ila walimshukuru sana Mungu kwa kuwasaidia kwa hilo na kwa kuweza kumponya mama huyo.
Ingawa muda ulikuwa umekwenda ila hakutamani kuondoka na kumuacha Sabrina akiwa amezimia vile.
Wale wachungaji walimuhakikishia kuwa hapatakuwa na tatizo lolote kwani Mungu amewakomboa tayari.
"Hapana, mi nitakuwa nao hapa hadi kesho ili niendelee kuona hali zao kwani hapa walipo wapo wenyewe"
Basi wakakubaliana na Francis kisha wale wachungaji wakaaga na kuondoka na kuahidi kuendelea kufanya maombi hata watakapokuwa makwao.
Francis alisaidiana na Joy kumkokota Sabrina na kumpeleka chumbani kwake ili akapumzike kwani wameambiwa kuwa ataamka mwenyewe tu muda ukifika kwahiyo wasiwe na wasiwasi.
Kisha Francis akaenda kulala sebleni.
Kulipokucha, Sabrina aliamka akiwa amechoka sana hata asielewe kilichokuwa kimetokea.
Alijiona akiwa na uchovu mwili mzima, hivyobasi akaenda kuoga na huko ndipo alipokumbuka swala la kamba yake ya kiunoni na kumfanya ajiulize maswali,
"Kamba yangu iko wapi? Inamaana imeyeyuka au ni kitu gani?"
Ni wazi Sabrina alijihisi kusahau kila kitu kilichomtokea.
Alipotoka kuoga, alienda na kukaa kitandani kwake huku akitafakari na kukosa jibu.
Akavaa na kwenda sebleni kwao, alishangaa kumuona Francis pale kwao na kumuuliza kwa mshangao,
"Francis, asubuhi yote hii unafanya nini hapa kwetu?"
"Khee, Sabrina kwanza niambie unaendeleaje?"
"Naendelea vizuri, kwani nilikuwa naumwa?"
Mama yake nae akatoka ndani na kumfanya Francis aage kwani usiku ulishapita na tayari palishakucha.
"Mama, mimi naenda ila kama kutatokea tatizo lolote msisite kunipigia simu na badae nitakuja kuwatembelea tena"
"Asante sana mwanangu, umetusaidia sana hapa. Mungu akubariki"
Kisha akaaga na kuondoka, na kumfanya Sabrina azidi kupatwa na maswali kuwa ukaribu wa hivyo wa Francis na mama yake umetoka wapi? Ila hakuwa na kumbukumbu kabisa kwa yaliyotokea siku ya jana.
Katika akili yake alijua wa kumpa majibu yote ni Sakina tu, hivyo akataka kwenda kwa Sakina.
Mama yake alikuwa akiingia chumbani kwake na kwake na kumwambia Sabrina,
"Nisubiri hapo mwanangu nikupe ushuhuda"
Kisha akaingia chumbani ila Sabrina hakutaka kujua hizo khabari za ushuhuda, kwani alichotaka kujua kwa wakati huo ni juu ya kamba yake ya kiunoni kuwa imekwenda wapi.
Pale pale aliinuka na kufanya safari ya kwenda nyumbani kawa Sakina.
Alimkuta Sakina akiwa amelala kwenye kochi ndani kwake, tena alionekana kuwa ni mtu aliyechoka sana.
Kisha Sabrina akamuamsha Sakina na kumfanya ashtuke sana kutoka kwenye ule usingizi.
"Utaniua kwa presha Sabrina, mambo gani hayo ya kushtuana kiasi hicho?"
"Sio hivyo dada ila nimepatwa na maajabu"
"Maajabu gani hayo?"
"Ile kamba yangu ya kiunoni imeyeyuka"
"Imeyeyuka! Kivipi?"
"Leo nimeamka asubuhi sijaikuta kwenye kiuno changu"
"Hebu acha uwehu Sabrina, wakati ile kamba jana ulikatwa na mama yako"
Sabrina akashtuka sana na kumfanya Sakina amkumbushe jinsi ilivyokuwa na kumfanya Sabrina akumbuke kila tukio ambalo lilitokea siku ya jana na kumfanya atetemeke,
"Hivi nilikuwa ni mimi au ni nani?"
"Mbona sikuelewi Sabrina?"
Ilikuwa ngumu kwa Sakina kumuelewa Sabrina kwavile matukio mengine hakujua kama yalitokea.
Sabrina aliinuka na kumwambia Sakina,
"Ngoja nikamuulize mama vizuri kama atakuwa na kumbukumbu na kuweza kunieleza"
"Hebu ningoje twende wote"
Sakina nae aliinuka akiwa na hamu ya kujua kwani hakumuelewa Sabrina hata kidogo.
Walimkuta Joy akiwa ametulia huku akisikiliza nyimbo tu.
"Yani hapa mtoto kweli sina, sikuamini kama nikitoka ndani sitakukuta mwanangu!"
"Nisamehe mama, ila kuna mambo ambayo yalinichanganya ndiomana"
Kisha akasalimiana na Sakina huku Sakina akiwa na hamu ya kujua kuwa ni mambo gani yalitokea.
Joy aliamua kuwapa ushuhuda wake juu ya mambo ambayo yalimtokea kwa siku ya jana.
"Unajua kile kitendo cha mimi kuona kamba kwenye kiuno cha mwanangu kilinisikitisha sana na ndiomana nilipatwa na hasira na kuikata, ninachoshukuru ni kuwa baada ya tukio hilo nikapata wazo la kuwapigia simu watu wa Mungu"
Sabrina akdakia kabla hata mama yake hajamaliza,
"Na ndio hapo ulipoharibu mama"
"Sijaharibu chochote, hujui tu ni jinsi gani wameifanya kazi kubwa hapa sababu ya hayo mashetani yako."
Hapo Sakina na Sabrina walitulia kumsikiliza ataongea vitu gani, Sabrina akashangaa kuona mama yake akimsimulia mambo aliyokuwa akikumbana nayo kule kwenye mbuyu, kumbe mama yake alikuwa akiyaona yote wakati ameanguka na kutapatapa,
"Ile kamba ilikuwa inakupa mwanangu uwezo wa kuwaona wachawi na kumbe ilitaka pia uwe mchawi, kule kwenye mbuyu ambako ulikimbia mara ya kwanza, walitaka wakupe uchawi ila machale yakakucheza mwanzoni na kukimbia. Ila uliponikuta mimi nikihangaika ndipo ujinga wa kwenda kumsujudia pepo ulipokupata mwanangu na kusahau kuwa Mungu ndio kila kitu"
Joy pia akasimulia jinsi Francis alivyomsimulia kwa hali aliyomkuta nayo na jinsi alivyowasiliana na yule mchungaji mwingine.
Sabrina akamuuliza mama yake,
"Inamaana Francis anajua kila kitu?"
"Ndio anajua, na yeye amesaidia kumuita mchungaji"
"Mmmh huyo Francis bibi yake ni mkubwa wa wachawi, eti leo ndio amekuitia mchungaji mama mmh!"
"Hata kama bibi yake ni mchawi wa kuzimu, kumbuka yeye yupo tofauti"
Kwa upande mwingine Sabrina alijisikia vibaya kwani akiyafikiria mambo aliyoyafanya jana na kuambiwa kuwa Francis alikuwepo alijionea aibu sana na kuhisi kamavile Francis atakuwa akimfikiria vibaya.
Joy alifanya kazi ya ziada ya kumtaka Sabrina na Sakina wamtumainie Mungu kwani aliona wazi kuwa wanaamini ushirikina zaidi ya Mungu.
"Mungu amekuokoa mwanangu, unatakiwa uanze kufanya ibada sasa"
Sabrina alikubaliana na mama yake nusu nusu kwani kwa fikra zake alihisi kuwa yale mambo yatajirudia tu.
Inaendeleeeaaa
No comments: