Simulizi: Je Haya Ni Mapenzi? Sehemu ya Thelathini (30)

Sabrina akataka kupiga makelele ila yule mtu akamziba mdono, kisha wakamuangusha Sabrina chini na kumwambia,
"Achana na Sam mara moja, hili si ombi bali ni amri"
Sabrina hakuweza kujibu kitu kwavile walimziba mdomo.
Yule mwingine akainuka na kuanza kuelekea chumbani kwa Sabrina huku huyu wa mwanzo akizidi kumkandamiza Sabrina kwa pale chini.

Wakati Jeff anarudi nyumbani kwa Sabrina, njiani akakutana na rafiki yake na kujikuta wakianza kupiga story,
"Kwani unakaa wapi kwa mitaa hii Jeff"
"Hata sio mbali, ni hapo tu. Twende nikuonyeshe"
Wakaongozana kuelekea nyumbani kwa Sabrina.
Walipofika, Jeff akashangaa kwani alipaona kuwa kama tofauti vile hadi rafiki yake akamuuliza,
"Mbona unapashangaa au sio hapa?"
"Ndio hapa, ila napaona kama pako tofauti"
"Mmmh! Mi napaona kuwa sawa ila kwavile wewe ndiye unayepajua hebu angalia vizuri labda kuna matatizo"
Jeff akaanza kuongeza mwendo akielekea kwenye nyumba ya Sabrina.
Alipofika, akasukuma mlango, akamuona Sabrina akiwa chini na yule jamaa juu ikionyesha wazi anataka kumbaka.
Jeff akapandwa na hasira za ajabu na kujikuta akimvuta yule jamaa kwa nyuma na kumuangusha chini, kisha mpambano ukaanza kati yao.
Yule rafiki wa Jeff alianza kumsaidia Sabrina katika kuinuka kutoka pale chini.
Katika ule mpambano wa yule jamaa na Jeff, yule jamaa alifanikiwa kumponyoka Jeff na kukimbia.
Jeff akamsogelea Sabrina aliyeonekana kuwa bado anatetemeka, ila Sabrina hakuongea kitu ila akinyoosha kidole kuelekea chumbani kwake na kumfanya Jeff ahisi kuwa lazima kuna kitu au kuna mtu.
Jeff akachukua kisu na kuelekea chumbani kwa Sabrina, na kuanza kuangaza huku na huku kama ataona mtu ila hakuona chochote kile na kumfanya aanze kupekua kwa tahadhari kwani alihisi kuwa hata kama kutakuwa na mtu basi atakuwa amejificha kwa yale makelele aliyokuwa akigombana na yule wa mwanzo.
Kumbe yule mtu alikuwa kajificha nyuma ya mlango, kwahiyo Jeff alipotangulia mbele tu basi naye akapata upenyo wa kutoka.
Alipofika sebleni wakati anataka kukimbia akakutana na yule rafiki wa Jeff na kumkata mtama na kufanya aanguke chini huku akimwita Jeff atoke ndani.
Jeff alipotoka, walianza kwa pamoja kumshambulia yule mtu kwa kumpiga huku wakitaka awaambie kuwa ametumwa na nani na amekuja kufanya nini, ila yule mtu hakusema chochote ingawaje walimpiga sana.
Wakaamua kumtoa nje ili wakamfunze adabu vizuri na huko akawaponyoka na kuwakimbia.

Jeff alirudi ndani akiwa na hasira sana kwani hakujua lengo la wale vijana lilikuwa ni nini kwa Sabrina.
Alikaa karibu na Sabrina huku akimpa pole kwa kile kilichotokea,
"Ila imekuwaje? Na wameingia vipi ndani?"
"Kwakweli nimechanganyikiwa Jeff, unajua kuchanganyikiwa wewe? Mimi nimechanganyikiwa. Wakati wanagonga nilijua ni wewe. Ile kufungua tu wakanivamia. Nashukuru hata Mungu aliyekurudisha sababu hata sielewi ningekuwa na hali gani"
"Pole sana"
Simu ya Sabrina ikaita, na mpigaji alikuwa ni Sam.
Sabrina alipokea na kuanza kumueleza Sam kitu ambacho kimemtokea kwa siku hiyo.
"Kheee, nakuja sasa hivi"
Kisha akakata simu.
Jeff alikuwa akionekana bado kujawa na hasira dhidi ya wale watu kwani uoga wake mkubwa ulikuwa ni juu ya kukidhuru kiumbe cha kwenye tumbo la Sabrina.
Aliona wazi kuwa ni majanga iwapo wangembaka Sabrina.
Muda kidogo, Sam akafika mahali pale na kwenda moja kwa moja alipo Sabrina na kumkumbatia kwa kumpa pole.
"Pole sana mke wangu jamani, pole"
"Asante, hata sielewi kwakweli"
"Kwani walikuwa wanataka nini?"
"Wamesema niachane na wewe, tena wameniambia ni amri wala sio ombi"
Sam akafikiria kidogo, kisha ukimya ukatawala na kumfanya Jeff aulize,
"Kwani kuna watu unawahisi bamdogo?"
"Hapana, na wala sina maadui kiasi hiki cha kuja kumtishia maisha Sabrina, kwakweli nashangaa."
"Kwa mtindo huu, hatutakiwi kumuacha mamdogo hapa peke yake"
"Ila nitafanya upelelezi hadi nijue ni wakina nani na wametumwa na nani"
Sabrina nae alikuwa kimya kwa muda, kisha akamwangalia Sam na kumwambia.
"Nakuomba nipeleke kwetu"
"Hilo sio tatizo Sabrina, nipo kwaajili yako"
Kisha wakainuka wote na kufunga nyumba na kuondoka.

Walipokuwa ndani ya gari, Sabrina bado alionyesha kuwa na mawazo sana, inaonyesha wazi ni jinsi gani lile tukio lilivyoichanganya akili yake.
Sam aliligundua hilo kwa Sabrina na kujitahidi kumuongelesha ili kuweza kumrudisha katika hali yake ya kawaida.
"Sabrina, harusi yetu inakaribia ungependa tuagize keki ya aina gani?"
Jeff alikuwa kimya akiwasikiliza ambapo Sabrina alimuangalia Sam na kutabasamu, kisha akamjibu,
"Iwe keki ya chocolate"
"Ukioza meno Sabrina mi simo"
Sabrina akacheka, na hiki ndicho alichokitaka Sam, kisha akaendelea kuongea nae,
"Eeh iwe na kazi ngapi?"
"Nne tu zinatosha"
"Nne tu kwani chache? Mi napenda iwe na ngazi kumi na mbili ili tukipanda tuchoke"
Sabrina akacheka tena na kumfanya Sam amuangalie Sabrina usoni na kusahau kuwa yupo barabarani anaendesha gari.
Kwa bahati mbaya akashukia akifunga breki mbele ya mtu kabisa kwahiyo ilibakia kidogo tu amgonge mtu huyo, ambaye alianza kutukana bila kituo akimtukana Sam kwa kutaka kumgonga,
"Nyie watu wenye magari mnajidai sana, kwahiyo ungenigonga ndio moyo wako ungeridhika. Unataka kunitoa kafara mimi kwa gari yako, thubutuu nimechanjiwa mimi huwa sitolewi kafara hovyo....."
Yule mtu aliongea mfululizo tena bila hata ya kumeza mate ila Sam alimuelewa na kumuomba msamaha ingawa yule mtu hakutaka ule msamaha na kuzidi kutukana,
"Na tutaona sasa kama...."
Sabrina kuona vile akaona kuwa itakuwa mzozo kwani yule mtu anaweza kujaza watu wengine eneo lile kwahiyo akamuomba Sam kuwa waondoke tu naye Sam akaondoa gari na kuondoka.

Walipofika kwa wakina Sabrina, alimkuta mama yake akiwa na wageni ndani kisha Sabrina nae akaingia na kufurahi kumuona mgeni mwenyewe kuwa ni shangazi yake.
Wakafurahiana pale na kusalimiana, kisha Sam akakaa kidogo na kuwaaga halafu yeye akaondoka na kuwaacha waendelee na mazungumzo yao.
Shangazi wa Sabrina alikuwa akimtazama tu Sabrina na lile tumbo lake kisha akamwambia,
"Ukweli humuweka mtu huru"
"Ni kweli shangazi, na ninashukuru sana kwakuwa sasa nipo huru kweli"
"Ingawa bado hujausema ukweli wote"
"Ila na wewe shangazi ni mtu wa aina gani? Mbona huwa unagundua mambo mengi?"
"Mimi ni mtu wa kawaida tu ila huwa nayasoma macho, sasa nikiyaangalia macho yako yananiambia kila kitu kuwa kuna mengine umeyaficha. Ila hakuna tatizo kwakuwa safari moja huanzisha nyingine, na taratibu ukweli utausema mwenyewe au la ukweli huo utakuumbua mwenyewe siku usiyoitarajia"
Sabrina akamtazama tu shangazi yake na kutabasamu kwani alionyesha sasa kuanza kuzoea maneno yake na kuwa kama mbuzi anayepigiwa gitaa na wakati hachezi wala nini.
"Eeh niambie shangazi, ndio umekuja kwaajili ya harusi zetu?"
"Ndio, ila hiyo sio sababu iliyonileta bali kuna jingine ambalo nimepatwa na hisia kwamba litaibuka ingawaje bado sijajua ni jambo gani"
"Nikuulize kitu shangazi?"
"Niulize tu"
"Hivi kuna siku umewahi kuota ktwa unataka kuwa mganga wa kienyeji?"
Shangazi akacheka kwani alijua wazi kuwa swali la Sabrina limeulizwa kwanini.
Ila kabla hajajibu, Jeff alikuwa amefika pale na kuwakatisha kwa maongezi kwa kumuitia nje kidogo sabrina. Kwahiyo Sabrina akainuka na kwenda kumsikiliza,
"Eeh niambie unasemaje?"
"Kwani mnafunga ndoa lini?"
"Wiki ijayo, mbona unapenda sana kuniuliza hilo swali Jeff?"
"Sababu naumia"
"Kinachokuumiza ni kitu gani?"
"Nakupenda Sabrina"
Huku akimsogelea zaidi na kutaka kumkumbatia, ila Sabrina akajikwepesha kidogo na kumwambia,
"Tafadhari Jeff, nakuomba sana usiyaweke haya mazoea kwenye kichwa chako. Mwisho wake utakuwa mbaya sana, tena kwangu na kwako. Nakuomba siri yetu ibakie kwetu, asijue mtu yeyeto. Na hayo mazoea unayotaka kuyaweka ndio yataharibu kabisa."
"Basi niambie, unanisaidiaje Sabrina?"
"Cha kukusaidia, tafuta msichana wa rika lako uwe nae. Huyo atakufanya usahau kuhusu mimi na pia angalia sana maisha yako"
"Ila maisha yangu bila wewe si kitu Sabrina, na hao wasichana kama ningewapenda basi ningekuwa nao ila kiukweli siwezi kumpenda tena msichana yeyote zaidi yako Sabrina"
Sabrina alimwangalia Jeff na kukosa cha kumjibu kabisa, kisha Jeff akaendelea kuongea,
"Nina ombi moja kwako"
"Ombi tena!! Ushafanya ni mchezo eeh!"
"Hapana, sio ombi hilo"
"Ila ni ombi gani?"
"Naomba utakapoolewa basi na mimi niishi nyumba moja na nyie"
"Je utaweza?"
"Ndio nitaweza, na nitaitunza siri yetu milele"
"Basi haina shida, nitazungumza na Sam"
Kisha Sabrina akamuacha Jeff pale nje na kuelekea ndani kwao.

Sabrina akamkuta shangazi yake ametulia kamavile alikuwa akimngoja yeye amalize maongezi yake, ila kabla Sabrina hajasema chochote kile, shangazi yake akamwambia.
"Yule mtoto inaelekea anakupenda sana Sabrina"
Sabrina akashtuka na kuuliza,
"Yupi huyo?"
"Si huyo uliyetoka kuongea nae, maskini angekuwa mkubwa angekuoa Sabrina"
Sabrina akacheka kwa kujigelesha,
"Jamani shangazi yule ni kama mwanangu"
"Kama mwanao! Basi sawa, ila mi nimemuona kuwa anakupenda sana."
Sabrina akaona jambo la muhimu ni kumbadilishia shangazi yake mada kwani alijua angeweza kufyukunyua na mengine bure.
"Eeh! Si ndio kesho tunaenda kumtolea mahali mchumba wa kaka James?"
"Ndio ni kesho, na ndiomana mimi nimekuja leo"
Wakaendelea na maongezi mengine kwa muda huo.

Sam alirudi moja kwa moja nyumbani kwake huku akifikiria watu waliokwenda kumteka Sabrina kuwa walikuwa na nia gani na nani aliwatuma.
Akili yake iliwaza watu baadhi na kuwatilia mashaka huku akijiweka kuanza kuwapeleleza kama ni wenyewe na walikuwa na lengo gani.
Wakati anafikiria, ujumbe mfupi ukaingia kwenye simu yake,
"Ingawa vijana wangu hawajafanyikiwa leo, ila najua ipo siku watafanikiwa kwani nakujua Sam hujiwezi"
Sam alichukiza na ule ujumbe na kuamua moja kwa moja kuifuta ile meseji bila hata ya kufatilia kuwa ni nani aliyemtumia.
Ila akajisemea,
"Yani hawa wataumbuka tu siku Sabrina wangu akijifungua. Sina hata ya kukaa na meseji zao"
Kisha akaendelea na mambo yake mengine.

Usiku wa siku hiyo Sabrina alilala na shangazi yake, ambaye alishtuka usiku wa manane na kumwambia Sabrina,
"Nimeota umejifungua mtoto wa kike, halafu mtoto huyo anagombaniwa na baba yake mzazi na mwanaume mwingine asiye baba yake"
Sabrina akamuangalia shangazi yake na kuona kuwa anamletea mada zake zile zile za kila siku huku moyoni mwake akiwaza,
"Nikimfatilia huyu shangazi, si muda mrefu nami nitakuwa chizi kama yeye"
Kwahiyo alichokifanya ni kumuitikia kwa kumridhisha kisha wakaendelea kulala.

Kesho yake kama ambavyo walipanga, wakajiandaa na kufunga safari kwenda huko nyumbani kwa kina Joy kwa lengo la kujitambulisha na kutoa mahari.
Aliyeongoza msafara wao alikuwa ni James ambaye ndiye muhusika mkuu.
Walifika vizuri, na kupokelewa hadi ndani.
Mama wa Sabrina akashtuka kumuona Baba wa Joy yule mchumba wa mtoto wake James.
Baba wa Joy nae akashtuka kumuona mama wa Sabrina pamoja na Sabrina kwani akili yake ikamwambia wazi kuwa James atakuwa na undugu na hiyo familia.
Shangazi wa Sabrina, akamwangalia Sabrina na kumwambia,
"Umeona, mficha maradhi kifo humuumbua"
"Una maana gani shangazi?"
"Mama yako hapo ameshachanganyikiwa"
Sabrina akageuka na kumuangalia mama yake, mara gafla mama yake akaanguka chini.


Shangazi wa Sabrina, akamwangalia Sabrina na
kumwambia,
"Umeona, mficha maradhi kifo humuumbua"
"Una maana gani shangazi?"
"Mama yako hapo ameshachanganyikiwa"
Sabrina akageuka na kumuangalia mama yake, mara
gafla mama yake akaanguka chini.
Ikabidi Sabrina amkimbilie mama yake pale chini alipoanguka.
"Vipi mama?"
Huku akimsaidia kuinuka,
"Hata sielewi, yani nimepatwa na kizunguzungu cha gafla tu"
"Pole sana"
Na wengine wakasogea huku wakimpa pole na kumwambia kuwa huenda ikawa malaria.
Baada ya muda mfupi, baba wa Joyce aliwaaga kidogo pale ndani kuwa kuna mtu anamfata kwenye kituo cha daladala, Deo akamuuliza,
"Kwanini usiagize vijana?"
"Huyo mtu ni muhimu sana anione mimi"
Ikabidi tu wamruhusu aende ambapo walikaa na kumsubiri kwa muda mrefu bila ya kupatikana hadi mkewe akapatwa na wasiwasi,
"Hata sielewi amepatwa na kitu gani jamani, simu yake haipatikani, mambo ya hapa hatujayamaliza. Hata sielewi"
Deo akaamua kutoa maamuzi kuwa watarudi siku nyingine kwavile kisingefanyika kitu wakati baba mzazi wa binti wanaetaka kumchumbia hayupo.
Ikabidi waage na kuruhusiwa tu kuondoka kwa muda huo ili kuendelea na mambo yao mengine ingawa muda tayari ulikuwa umeenda sana.

Walipofika nyumbani, James akaamua kuondoka kwani alifadhaika kwa kitendo cha baba mkwe wake kuwaacha njiapanda.
Sabrina nae hakuwa na usemi zaidi ya yeye kubakia pale kwao kwa lengo la kumuangalia mama yake kwani alihisi kuwa huenda akawa na malaria.
Muda huo shangazi yao alikuwa naye ameshaondoka.
Sabrina alikaa na kuzungumza na mama yake kidogo,
"Kwani mama, shangazi anajua nini kuhusu wewe?"
"Tena mwanangu, ngoja nikwambie kitu. Huyo shangazi yako achana na maneno yake yatakuchanganya tu. Kwanza tambua hili, huyo shangazi yako aliugua sana kipindi cha ujana wake. Baba yako hupenda kumtumia kwenye mambo kama haya sababu anampenda tu ila akili za huyo shangazi yako si njema"
Sabrina alijidadisi na akili yake na kupata jibu kuwa huenda maneno ya mama yake yana ukweli ndani yake kwani hata yeye binafsi inakuwa ngumu sana kumuelewa shangazi yake huyo.

James alipokuwa ameenda kwa mtu aliyemuita, akaanza kuambiwa maneno ambayo yalimpa mashaka na kumfanya ashindwe kurudi nyumbani kwake,
"Hivi wewe hujiulizi kwanini unafanana na yule kijana kiasi kile? Au bado unajidanganya na ile kauli kuwa duniani wawili wawili? Hujiulizi kwanini yule kijana kapewa jina linalofanana na la kwako? Mi ukweli siujui ila kuna matukio ambayo nimeyafatilia na yakafanya nigundue kitu"
James ambaye ni baba wa Joyce alitafakari bila ya majibu ya haraka, ingawa huyu mtu aliyemuita alimruhusu kuondoka ila bado James hakuondoka kwavile moyo wake ulikuwa na maswali mengi bila ya majibu.

Mama wa Sabrina alipokuwa nyumbani na mumewe, aliamua kumueleza hali halisi kiunaga ubaga ili ajue jinsi gani watasaidiana,
"Ila Joyce, si tulikubaliana kuwa kuwa James ni mtoto wangu?"
"Ndio natambua hilo Deo"
"Sasa tatizo liko wapi?"
"Hatuja mtendea haki James, hebu jaribu wewe kufikiria kuwa leo hii watoto wako wanaoana, je utajisikiaje?"
"Ila huyo James hajui kama huyu ni mtoto wake"
"Ndio hilo kosa tulilolifanya Deo"
"Sidhani kama ni kosa, hebu tuangalie maisha yetu. Watoto wafunge ndoa mambo yaendelee"
"Ila dunia haina siri Deo"
"Ungetambua hilo basi toka mwanzoni usingetaka kunificha, ila ulinificha hadi pale ulipoumbuliwa na mdogo wangu"
Joy akaona sasa maneno yatakuwa makubwa na yatavuka mipaka hivyobasi akaamua kukaa kimya ili kuepusha mumewe kukumbushia yaliyopita.

Sabrina alienda nyumbani kwa Sam na kutulia ndani huku akimsubiria, na Sam aliporudi alimkuta Sabrina akiwa ndani,
"Nasikia eti imeshindikana kumtolea mahari dada yangu"
"Ndio imeshindikana sababu ya mjomba wako. Kaondoka na kutokomea halafu hajarudi tena, sijui na yeye vipi. Au hataki kaka yangu amuoe mwanae? Hata sijamuelewa kwakweli"
"Haya sasa, na wewe ulipotoka pale ndio ukaamua kuja hapa?"
"Nilivyotoka nikarudi nyumbani ila kuna mambo ambayo nimeyafikiria na ndio yamenileta hapa"
Sam akajiuliza kwa haraka haraka kuwa ni mambo gani ila hakupata jibu, na alipojaribu kumuuliza Sabrina naye hukumjibu zaidi ya kumwambia kuwa hayo mambo atayaona tu bila papara.
"Una maana gani Sabrina?"
"Usiwe na mashaka Sam, utaona tu"
Usiku ukaingia kabisa huku Sabrina akiwa hapo hapo nyumbani kwa Sam ambapo kila Sam alipombembeleza kuwa amrudishe nyumbani kwao, bado Sabrina aligoma kuondoka na kuendelea kuwepo mahali hapo.

James ambaye ni baba wa Joyce, alishindwa kuelewa kwani alitafakari sana bila ya kupata majibu ila upande mwingine wa moyo wake ulikuwa unamwambia kuwa ukweli wote ataupata kwa mama mzazi wa mtoto huyo, hivyobasi akapendekeza kuwa aweze kuonana nae na waweze kuzungumza juu ya hali halisi.

Usiku uliingia vizuri, na moja kwa moja Sabrina alienda kulala chumbani kwa Sam ambapo Sam akataka kulala sebleni ili kumpisha Sabrina kitandani.
Ila kabla hajaenda Sabrina akamshika mkono na kumzuia kisha akamuuliza,
"Utanikimbia hadi lini Sam?"
"Sikukimbii Sabrina kama unavyofikiria, ila napenda kutunza kiapo changu"
"Sawa, hata kama unatunza kiapo iweje ushindwe kulala na mimi kitanda kimoja? Kwani tukilala tu nini kinaharibika?"
Sabrina akajaribu pale kumshawishi Sam, na mwisho wa siku Sam akakubali na wakalala kitandani pamoja.

Usiku ulipofika, Sabrina akashtuka na kuamka ila alipomtazama Sam pembeni hakuwepo na kumfanya Sabrina apatwe na hasira sasa kuwa kwanini Sam anamkimbia kiasi hicho?
Akaamua kuinuka na kwenda kumchungulia sebleni, akamkuta amelala kwenye kochi na kumfanya Sabrina asikitike sana huku akizidi kujiuliza na kujiambia kuwa huenda anataka kuolewa na mwanaume ambaye si mzima ndiomana anamfanyia mambo hayo.
Hakutaka kumkurupusha pale zaidi ya kurudi chumbani na kulala.

Asubuhi kulipokucha, Sabrina alipoamka, alimkuta Sam akiwa amelala pale pembeni kisha na yeye akamkurupusha,
"Hivi wewe, kunikimbia usiku na kwenda kulala sebleni ndio nini?"
"Jamani Sabrina, sijakukimbia wala nini. Tena leo ndio hata kutoka hapa kitandani sijatoka"
"Sam, wakati nimekuona kwa macho yangu mwenyewe!"
"Labda uliota Sabrina ila kiukweli leo sijachomoka hapa kitandani"
"Haya bhana nikatalie, ila siandikii mate wakati wino upo"
"Una maana gani?"
"Najua nitakapo kukamata, tulia tu"
Sam akacheka, kisha akainuka na kwenda kuoga kwaajili ya kujiandaa na majukumu ya siku hiyo.
Sam alipomaliza kujiandaa, ikabidi amuage Sabrina kwavile Sabrina alisema hataki kutoka siku hiyo na anataka kushinda hapo hapo nyumbani kwa Sam.

James ambaye ni baba wa Joyce, siku hiyo aliamua kufunga safari na kwenda nyumbani kwakina Sabrina kwa lengo la kuwaomba msamaha kwa kitendo chake cha kuondoka na bila ya kurudi tena ila lengo lake kuu lilikuwa ni kumuuliza mama wa Sabrina kuhusu maneno ambayo ameyasikia kwa siku ile.
Na alifika na kupokelewa vizuri tu na kijana mmoja aliyekuwa kaka wa Sabrina hadi ndani.
Alimkuta mama wa Sabrina akiwa sebleni huku akiendelea na mambo mbalimbali, ila alishtuka kumuona James mahali pale ingawa alimkaribisha,
"Karibu James, naona unamshangaa huyo ni mwanangu anaitwa Sam"
James akacheka na kumwambia,
"Watoto wako wote nilikuwa nawajua kwa sura na kwa majina. Ila mwanao mmoja tu ambaye nilikuwa namjua kwa jina tu, huyo mkubwa James. Sikuwahi kubahatika kukutana nae ingawa nilitamani sana kumuona, na kumbe ndio huyo mkwe wangu"
Mama Sabrina akaamua kujichekelesha hapo ili kuendelea kuukata mzizi wa mawazo kwa James, kisha yule Sam ambaye ni kaka wa Sabrina akainuka na kuwaacha waongee vizuri kwani aliona wazi kuwa wanafahamiana na itakuwa vyema kwao kama watakumbuka ya zamani kwani aliwasikia hata wakitaja khabari za kwaya.
"Kuna mambo mawili yaliyonileta hapa ila hili moja naomba kama utapata nafasi basi tupange siku tuonane na kuweza kuzungumza"
Mama Sabrina aliweza kuhisi kuwa ni jambo gani ila hakutaka Deo akirudi hapo amkute mtu huyo, hivyobasi akamuaga na kukubali kupanda siku ya kuzungumza.
James alipoondoka, akampa nafasi mama Sabrina kufikiria uongo wa kumwambia James ili akubali na aamini,
"Hata hivyo kuna mwingine wa ziada anayejua ukweli huu? Hata kama yupo basi atakuwa anakisia tu. Akisema kuhusu kufanana na mwanangu, nami nitamjibu kuwa duniani wawili wawili, nisipofanya kuongopa zaidi basi lazima nitaharibu tu"
Kwahiyo mama Sabrina akajipanga kwa mambo ya kuongea na James siku atakayo kutana naye.

Jeff alikuwa mpweke sana siku hiyo hadi mama yake alitambua hali ya mwanae,

Inaendeleeah


USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.