Simulizi: Je Haya Ni Mapenzi? Sehemu Ya Ishirini Na Tano (25)
Jeff muda mwingi aliutumia kumfikiria Sabrina tu.
Ukaribu ule wa yeye na Sabrina ndio pekee aliokuwa akiuhitaji bila kujali kitu chochote hata kama Sabrina atamfanyia visa mbali mbali ila kwake aliona kuwa ule ukaribu unamtosha kabisa.
Kulipokucha, Sabrina aliamka kama kawaida na kujiandaa ili kwenda kazini ila akashangaa Sam akikawia kuja kumchukua.
Alitoka sebleni na kukaa, aliinuka na kufungua mlango ili kujaribu kuangaza ila hakuona dalili yoyote ile ya Sam.
Akarudi tena kukaa huku akijiongelesha,
"Sijui niende tu mwenyewe, dah mazoea yana tabu"
Akatokea Jeff na kudakia,
"Mazoea yana tabu kweli"
"Nini na wewe sasa?"
"Bora na mimi ningenunua gari tu ili niwe nakupeleka huko ka....."
Kabla hajamaliza, Sam naye akaingia muda huo huo na kusema,
"Sio kazini tu, bali kila sehemu atakayotaka kwenda"
Kisha akamuangalia Sabrina na kumwambia,
"Haya twende sasa"
Sabrina hakusema chochote cha ziada, zaidi ya kuinuka na kufatana na Sam kwa nyuma.
Walipokuwa ndani ya gari, Sam akayaanzisha maongezi kwa kumuuliza maswali Sabrina,
"Eeh niambie Sabrina, unampenda sana Jeff eeh!"
Sabrina akashtuka na yeye kuuliza,
"Kwanini umeniuliza hivyo?"
"Nimekuuliza sababu kuna kipindi ulimfukuza ila kwasasa umemrudisha tena nyumbani kwako"
"Nimemuonea huruma vile alivyokuwa akitafuta kazi, ndiomana nimemuweka kwangu ili asome"
"Kwani mtu akikaa kwako ndio anapata uwezo wa kusoma?"
Sabrina akakaa kimya na kumfanya Sam aongee tena,
"Nijibu Sabrina"
Simu ya Sabrina ikaita na kumfanya aipokee huku akishukuru kwani aliona ndio njia bora ya kukimbia maswali ya Sam.
Mpigaji alikuwa ni Sakina ambaye alimuulizia Sabrina hali yake kisha akamuomba kuwa badae waonane, Sabrina hakuwa na kinyongo na kukubali wito.
Simu ilipokatika, Sam akamuuliza Sabrina,
"Nani huyo uliyekuwa ukiongea naye?"
"Ni Sakina, anahitaji badae tuonane"
"Sawa hakuna tatizo, mimi nitakupeleka"
"Mmh"
"Sasa unaguna kitu gani?"
"Hamna kitu, nimekubali"
Safari ikaendelea hadi ofisini, na kufika huku kila mmoja akiendelea na shughuli zake za pale.
Kisha Sam akaenda kumuaga kidogo Sabrina kuwa anaenda kufatilia mambo yake huko nje na kumuacha pale ofisini.
Sabrina pale ofisini, akawasikia wale wafanyakazi wenzie wakiongea,
"Jamani, zamani bosi alikuwa hakai kwenye jiji hili, kidogo tu anasafiri. Maskani yake kubwa ilikuwa ni Arusha, sasa siku hizi kulikoni?"
"Mmh jamani, mambo ya Ngoswe hayo mwachieni Ngoswe"
Wote wakacheka, kisha mwingine akasema,
"Funika kombe jamani mwanaharamu apite, mi simo hapo"
Wa kwanza akadakia,https://ift.tt/2TR5Sxj
"Bwana eeh wangapi walikuwa kama yeye na kufanywa kama yeye na wamepita"
Wote wakacheka, Sabrina akachukia na kujua wazi anasemwa yeye.
Akainuka pale kwenye kiti na kutoka nje ya ofisi huku akiwa amejawa na hasira kifuani.
Alitamani hata asingefika ofisini siku hiyo kwani roho ilimuuma sana.
Sam aliporudi alimkuta Sabrina akiwa pale nje.
"Vipi tena, hapo nje"
"Nimeona nipigwe na jua kidogo"
"Halafu wewe Sabrina bado unaumwa ila ni mbishi tu kwenda tena hospitali kupima. Nikupe dereva akupeleke?"
"Hapana, nitakuwa sawa tu."
Kisha akarudi ofisini.
Sam nae hakumuelewa Sabrina kuwa ni kitu gani kinamsumbua zaidi ya kusikiliza anachosema yeye tu kuwa haumwi.
Muda ulipofika, kama kawaida Sam alitoka na Sabrina ila leo safari ilikuwa moja tu nayo ni kwenda nyumbani kwa Sakina.
Walipofika, walimkuta Sakina akiendelea na mambo ya hapa na pale, wakamsalimia kisha Sam akawaaga na kumuacha pale Sabrina na Sakina.
Sakina hakutaka kupoteza muda zaidi ya kuanza maongezi yake na Sabrina, akamuelezea kama jana yake alienda pale kwake na kumkuta akiwa amelala kabisa.
"Ila Sabrina naomba unieleze jambo hili kwanza"
"Jambo gani hilo?"
"Nyie mule ndani mnaishi vipi na Jeff?"
"Tunaishi kawaida tu, kwani vipi?"
Sakina akamueleza jinsi alivyowakuta chumbani na jinsi Jeff alivyomjibu, kisha Sabrina nae akacheka na kumwambia Sakina,
"Mbona ni mambo ya kawaida tu hayo dada, ndio uzungu huo"
"Mmh kuwa makini, mtoto kakua yule"
"Sio tatizo dada, Jeff hawezi kunifanya chochote mamake mdogo mie"
Sabrina aliongea huku akicheka na kuumia kwa lake moyoni kwani alijua wazi kama akisema basi atadharaulika.
Sakina hakuacha kumuuliza Sabrina kuhusu alichoagizwa na Sam,
"Kwani Sabrina una matatizo gani? Niambie mimi, kumbuka mimi ndio mtu wako wa karibu Sabrina"
"Mbona sina matatizo dada"
"Ya kweli hayo Sabrina? Unanificha hadi mimi! Utamwambia nani sasa?"
Sabrina alikaa kimya huku akimuangalia Sakina aliyeonyesha kuwa na hamu kubwa sana ya kujua kinachomsumbua Sabrina.
Alijitahidi kumbembeleza ila Sabrina hakutaka kusema ukweli na kumfanya Sakina akubaliane nae kuwa hana tatizo lolote lile.
Sakina akaongea mambo mengine na Sabrina kisha Sam akaenda kumfata Sabrina na kupita nae kwao kusalimia kidogo kisha wakaondoka.
Sabrina alikaa nyumbani kwake huku akiwa na mawazo sana, aliwaza kuhusu pale kazini na kuhisi kuwa mambo yataharibika endapo akigundulika kuwa ni mjamzito tena ujauzito ambao sio wa Sam.
Alijua wazi itakuwa ni kashfa nzito kwake na anaweza kufukuzwa kazi muda wowote ule na kufanya maneno ya wale wadada kutimia kuwa wengi walikuja na wamepita.
Akaamua kufanya mashauri katika kichwa chake.
Kesho yake alipokuwa ofisini, alienda moja kwa moja kwenye ofisi ya Sam na kumpa barua.
"Vipi tena Sabrina, barua ya nini hii?"
Sabrina akamwambia Sam,
"Isome tu utaona"
Sam akaisoma na kumshangaa Sabrina,
"Unataka kuacha kazi Sabrina? Kwanini?"
"Nimeamua tu"
Sam akamuangalia sana Sabrina, kisha akamwambia
"Mimi najua sababu"
Sabrina akamshangaa Sam na kumuangalia tu, kisha akamuuliza
"Sababu ipi hiyo?"
Sam akainuka na kuzunguka alipo Sabrina, kisha akainama na kushika tumbo la Sabrina kisha akamwambia,
"Hii ndio sababu"
Sabrina akashtuka na kushangaa.
Sam akainuka na kuzunguka alipo Sabrina, kisha
akainama na kushika tumbo la Sabrina kisha
akamwambia,
"Hii ndio sababu"
Sabrina akashtuka na kushangaa.
Sabrina akaogopa hata kumtazama Sam usoni kwa jinsi alivyokuwa akijihisi aibu na uoga, kwahiyo akainamisha kichwa chake chini na kumfanya Sam amuulize,
"Mbona hivyo Sabrina? Mbona umepooza gafla?"
Sabrina akaongea huku akitetemeka,
"Naomba ruhusa nikapumzike nyumbani kidogo"
"Ruhusa nakupa ila kazi huachi hapa, nenda ukapumzike nyumbani na ujifikirie kuhusu hili swala."
Sabrina akainuka na kuondoka, kisha Sam akamwambia dereva wake kuwa ampeleke Sabrina nyumbani.
Sabrina alipofikishwa nyumbani kwake alikuwa na wazo moja tu kwani alijua wazi kwa vyovyote vile Sam kaujua ukweli kuwa ana mimba na anaweza kumfanyia kitu kibaya kwa wakati wowote ule.
Akaingia chumbani kwake na kupakia baadhi ya nguo zake kwenye begi ili aondoke kabisa na asionane na Sam kwa kipindi hiko.
Alipomaliza kupakia nguo zake, akampigia simu dereva wa gari ya kukodi ili aende kumchukua.
Dereva alipofika nyumbani kwa Sabrina akamshtua kwenye simu ili aweze kutoka nje ya nyumba yake.
Wakati Sabrina anatoka ndani, akakutana mlangoni na Jeff,
"Vipi mamdogo unaenda wapi na mabegi?"
"Nitakupigia simu nikwambie"
Sabrina akatoka na kuifata ile gari na kumuacha Jeff akiwa mlangoni anamshangaa.
Sabrina akapanda kwenye gari na kumuacha Jeff akimuangalia tu huku akijiuliza kuwa anaenda wapi, na kwa mawazo ya haraka haraka akahisi kuwa kuna safari anaenda na safi,
"Ila mbona kaondoka na tax?"
Hofu ikamshika Jeff na kumfanya kukariri namba za ile gari.
Sabrina aliamua kwenda mbali ili kuepukana na janga lile, aliona kamavile dunia imemuelemea peke yake.
Aliumia moyoni ila alihisi yupo Sahihi kwa jambo aliloamua siku hiyo.
Kwavile alikuwa na pesa kidogo ya akiba akaamua kwenda kukaa hotelini kwanza.
Sam alipotoka ofisini moja kwa moja alienda nyumbani kwa Sabrina kumuangalia.
Alipofika alimkuta Jeff akiwa peke yake na kumuuliza alipo Sabrina.
"Hata mimi mwenyewe sielewi, nilijua umeondoka naye"
"Halafu wewe dogo usiniletee khabari zako, hebu niambie vizuri Sabrina yuko wapi?"
"Kiukweli sijui alipo"
"Siku ile uliniambia hivyo hivyo halafu kesho yake Sabrina nilimkuta akilia tu hapa, usifikirie sikumbuki ujinga wako na watu wako. Hadi leo Sabrina simuelewi, na unabahati sina hakika na ninachokihisi. Haya niambie upesi alipo Sabrina"
Jeff akamshangaa Sam na kukazia jibu lake kuwa hajui alipo Sabrina.
Gafla Sam akamkunja Jeff na kumpiga ngumi ya sura huku akikazana kuambiwa alipo Sabrina kwani alijua wazi Jeff anajua kila kitu kuhusu Sabrina.
"Unanionea tu brother, mi sijui alipo. Nilimuona tu akiwa amebeba begi lake na kuondoka, mi nikajua anasafiri na wewe"
"Unajua wewe dogo usinichanganye kabisa, yani wewe umuone Sabrina anaondoka na begi halafu asikwambie wewe!! Ni jambo ambalo haliniingii akilini kabis a"
Kisha Sam akiwa vilevile kamkunja Jeff, akachukua simu yake na kumpigia mama yake na Sabrina ili kujua kama yupo nyumbani kwao.
Ila mama wa Sabrina akamwambia kuwa Sabrina hajafika nyumbani kwao tangu walipopita jana kuwasalimia.
Sam akapatwa na mashaka zaidi na kuzidi kuhisi kuwa Jeff lazima anapajua alipo Sabrina.
"Siku ile mambo yalikuwa hivi hivi, wewe dogo lazima unajua alipo Sabrina wewe. Na leo usiponiambia alipo nafumua huo ubongo wako ili unijue vizuri mimi ni nani"
Jeff alikuwa akitetemeka tu kwani Sam alioneka kuwa na hasira na kumaanisha maneno aliyokuwa akiyasema na kumfanya ashindwe hata kujibu,
"Sema alipo alipo Sabrina wewe"
"Sijui"
Sam akazidi kuchukia na kumnasa kofi la nguvu Jeff hadi akajihisi kupepesuka huku akiombea muujiza wa Mungu utokee.
Ikabidi amtajie Sam aina ya gari ya kukodi aliyopanda Sabrina na namba ya ile gari.
"Kumbe ulikuwa unajua, sasa naenda kumtafuta huyo dereva ila na wewe ujipange kwani moyo wangu bado unaniambia kuwa unapajua alipo. Na siku nikigundua kuwa ulikuwa unapajua halafu unanificha, nakuapia siku hiyo utaisalimia ardhi"
Sam akamsukumia Jeff kwa chini na kuondoka zake.
Jeff alipoinuka pale akaona sio mahali sahihi tena kwa yeye kuendelea kuwepo.
Akaenda chumbani kwake, akapakia nguo zake baadhi kwenye begi lake la mgongoni na kuamua kuondoka pale nyumbani kwa Sabrina ili Sam akirudi tena akute tu milango imefungwa na hakuna watu.
Akapata wazo la kwenda nyumbani kwao ila bado akaona kuwa sio sehemu salama kwake kwani Sam anapafahamu mwanzo mwisho.
Akaona ni vyema kwa usiku huo akalale kwa rafiki yake kwanza ili kesho yake ajipange na kitu kingine cha kufanya.
"Dah huyu Sabrina kanipa mtihani mkubwa sana, ila hata hivyo na mimi nahusika kumpa yeye mitihani kwahiyo nijilaumu mwenyewe."
Akaendelea na safari yake.
Sabrina alienda Bagamoyo na kujich imbia mahali palipojificha kidogo ili kuwa huru na mambo yake na pia kuutuliza moyo wake.
Akatamani kumwambia mama yake alipo ila alijua wazi kwa vyovyote vile mama yake atamshauri kuwa arudi nyumbani, akaona ni vyema kutulia huko kwa siku kadhaa ili kupunguza mawazo aliyokuwa nayo.
Aliwaza pia kumwambia Sakina ila alijua wazi Sakina atamwambia ukweli Sam, pia aliogopa kumwambia Jeff kwani alijua wazi kwamba akibanwa lazima atasema ukweli wa mambo.
Sabrina aliamua kukaa pale bila ya mawasiliano na mtu yeyote yule huku akiamini kuwa hiyo ndio njia pekee ya yeye kuepukana na matatizo yanayomsonga kwa kipindi hiko.
Sam alipoona kuwa hata Jeff nae ameondoka akajua wazi ni mchezo wamemfanyia,
"Yani haka kajeff haka nikikashika katanieleza vizuri, haiwezekani nisumbuliwe akili na katoto kadogo kama kale"
Sam aliona kazi haifanyiki na kuamua kwenda tena kumtafuta gari aliyoelekezwa kuwa Sabrina alipanda wakati wa kuondoka.
Jeff aliona vyema asafiri kidogo na kwenda mji wa karibu ili kuepukana na hayo majanga hadi pale atakapowasiliana na Sabrina.
Akampata rafiki yake aliyekuwa Bagamoyo na kuona kuwa ni sehemu salama na isiyo na gharama kwa yeye kwenda.
Kwahiyo akaondoka na kwenda huko.
Sakina alienda nyumbani kwa mama yake na Sabrina kumuulizia vizuri.
"Hivi Sabrina yuko wapi maana nimeulizwa sana na kukosa jibu"
"Mi hata sielewi kwakweli, sijui ni kitu gani hadi mimi mama yake nisijue alipo"
"Khee makubwa, eti hadi Jeff anayekaa naye hajui alipo, jana nimemuuliza"
Wakabaki kushangaa na kumfanya Joy ajaribu kuwauliza baadhi ya ndugu zao kama Sabrina ameenda kwao ila hawakupata jibu lolote kwani kila mmoja hakujua alipo Sabrina.
"Kwakweli nachoka, sijui baba yake nikimwambia atachukua hatua gani."
"Ila ni bora umwambie tu kuliko kukaa kimya"
Joy akachukua simu yake ili ampigie mumewe, ila kabla hajapiga, ujumbe mfupi ukaingia kwenye simu yake kutoka kwenye namba mpya, Joy akaufungua na kuusoma,
"Usiwe na wasiwasi mama, mimi nipo salama na sehemu salama. Nikipata muda wa kutosha nitakupigia ili tuongee vizuri. Sabrina."
Joy akamuangalia Sakina na kubaki kimya kwani hata cha kusema walikosa.
Sam alimtafuta yule dereva hadi akampata na kuamua kumuuliza, akamuelekeza kuhusu Sabrina na mahali alipoenda kumchukua
"Aaah huyo dada ni rafiki yangu sana"
"Eeh niambie ulimpeleka wapi?"
"Mi nilimpeleka stendi tu, aliniambia kuwa kuna mahali anataka kwenda"
"Ndio nataka kujua huko mahali ni wapi?"
"Mi sijui, ila kuna muda nilimsikia kuwa anataka kwenda Bagamoyo"
"Basi sawa, nashukuru kwa ushirikiano wako"
Kisha Sam akaondoka ili akajipange namna ya kumpata Sabrina kwani alihisi akili yake kuchanganyikiwa kabisa.
"Yani huyu Sabrina huyu, sijui hata kwanini ananitesa kiasi hiki"
Sam alikuwa akijisikitikia tu muda wote.
Jeff alifika salama nyumbani kwa rafiki yake ambaye aliamua kuanzisha maisha yake huko na alijulikana kwa jina la Shebby,
"Naona wewe kusoma tena basi"
"Nimeona akili za darasani sina ila za maisha ninazo ndiomana nikaona ni vyema nianzishe maisha tu. Msome nyie Jeff sababu akili hiyo unayo"
Jeff akacheka tu na kufurahia uamuzi wa rafiki yake kwani aliona kuwa ameamua vyema kuliko yeye anayezidi kujipotezea muda.
"Kesho nitaenda kukutembeza kwenye mashamba yangu ili uone jinsi kilimo kwanza kilivyofanya kazi juu yangu"
"Hongera sana"
Wakaongea mengi bila ya Jeff kumwambia rafiki yake kitu ambacho kimemkimbiza mjini.
Joy akiwa nyumbani kwake, akatembelewa na mkwe wake ambaye alikuwa wajina wake kwani na yeye aliitwa Joy.
Walisalimiana pale na kuongea mambo mbali mbali,
"Halafu wewe unaonekana una mimba wewe"
Joy akacheka na kumjibu mkwe wake,
"Ndio nina mimba, ndiomana nimek uja kukutembelea ili nikupe hii taarifa"
"Hongera sana mwanangu, najua utaniletea mtoto wa kike hapo, si unajua huku una wifi mmoja tu"
Joy akafurahi sana,
"Imebaki ndoa tu mama"
"Hilo swala halina tatizo, yani hivi karibuni mambo yote yatatimia na tutacheza chereko hapa"
Wakafurahiana pale kisha akaaga na kuondoka.
Sabrina alikuwa amejichimbia mahali ambako hapakuwa rahisi kwa mtu yoyote yule kupajua.
Alifika sehemu hiyo na kupanga chumba cha kuishi kwa muda mfupi kwani bado alikuwa na malengo yake mengine.
"Maisha yangu yameharibika, nayaona kabisa yakiteketea kwasababu ya kidudu mtu kimoja tu. Yani huyu Jeff huyu, ingekuwa amri yangu ningekapoteza kabisa kwenye macho yangu. Ila ubaya ni kuwa siwezi kumfanyia hivyo, namuhurumia sana. Siwezi kumfanyia vibaya ingawa ameharibu maisha yangu"
Sabrina alikosa raha na alikuwa akisikitika muda wote, aliona wazi kuhangaika na maisha.
Aliona wazi tabu atakazo zipata kwani hana kazi na mtu wa kumweka mjini ndio huyo Sam anayemuogopa.
Kulipopambazuka, Sam kama kawaida akajiandaa na kwenda ofisini ila hakukaa sana na kuwaaga kuwa atakuwa safarini kwa muda wa siku tatu na kuondoka.
Safari yake ilikuwa ni kwenda Bagamoyo ili akamtafute Sabrina kwa gharama yoyote ile,
"Na kama nikijua kuwa kuna mwanaume anayesumbua akili ya Sabrina au aliyemshauri Sabrina kuwa atoroke basi mwanaume huyo atakuwa halali yangu. Haiwezekani mtu mzima kama mimi kusumbuka kila siku usiku na mchana kuitafuta roho yangu halafu nilikute jamaa limetulia nae tu"
Sam alisafiri na gari yake huku kichwa chake kikimuwaza Sabrina tu.
Jeff alichukuliwa na rafiki yake Shebby na kwenda kumtembeza mashambani na kumfanya Jeff kuifurahia mandhari ya Bagamoyo.
"Ila Jeff hujaniambia mwana, ni madili gani yamekuleta huku?"
"Mi nimekuja kutembea tu sina cha madili wala kitu chochote"
Muda wote Jeff alikuwa na mawazo yake ila hakupenda kumuonyesha rafiki yake kama ana mawazo yoyote.
Sam alifika Bagamoyo na kuanza shughuli yake ya kumtafuta Sabrina siku hiyo hiyo ambapo aliwapa watu baadhi picha ya Sabrina ili wamsaidie kumtafuta Sabrina.
Ila siku hiyo ikapita bila ya kupatikana kwa Sabrina na kumfanya Sam kuanza kujipa imani kuwa kesho nayo ni siku.
Inaendeleeaa...
No comments: