Simulizi : Upendo Kutoka Sayari Nyingine Sehemu Ya Tatu (3)

Matlida yeye alisimamia upande wa afrika na Asia. Na Mark alisimamia upande wa ulaya na Amerika. Kwa ujumla kazi ilienda vizuri sana ikisimamiwa vema na wasaidizi waliobobea katika kazi yao hiyo.
***
Taarifa ya hospitali hii ilimshawishi Mzee Martin kuona kama binti yake angeweza kwenda mahali hapo. Kikao kizima waliamua kuwa wamwite Seba na kumweleza uzuri na sifa ya hospitali hiyo. Ubora wa hospitali hii ulichukuliwa kwa uzito uliostahili kusudi kumshawishi Sebastian akubali Judith apelekwe katika Hospitali hiyo. Kukosekana matokeo ya uponyaji kwa kipindi kirefu kulimfanya kila mmoja kati ya ndugu wa pande zote wakiongozwa na Mzee Martin afikirie namna ya kufanya kwa ajili ya kuleta jawabu la matatizo hayo.

Siku ya pili baada ya kumpata Seba mzee Martini na baadhi ya wajumbe waliokuwepo kwenye kikao hicho walikaa na kumweleza kwa utaratibu. “Ni Hosptali pekee itakayomsaidia kwa haraka mchumba wako kurudia katika hali yake ya kawaida, Japo gharama yake ni kubwa sana.” Alisema Adella mama yake mdogo Judith baada ya kueleza sifa ya Hospitali hiyo maarufu duniani. “Nashukuru kusikia hivyo na niko tayari kwa kubeba gharama yote baada ya kwenda na kujionea utaratibu wao kama maelezo hayajatiwa chumvi.” Alisema hivyo Sebastian. “Ni vizuri zaidi kwenda kujionea wenyewe ili kujiridhisha kabla hatujampeleka Judith. Sasa ninataka kujua kama safari itaanza lini?

Kwangu mimi sina sababu ya kwenda ikiwa ninyi mtaenda.” Alisema Mzee Martin akimaanisha wale walioko kwenye kikao kile ambao ni Adela na Alen pamoja na Seba. “Ni kweli kaka wewe huna sababu ya kwenda inabidi tujipange sisi ili tufike hapo tukiridhika nayo tutakuja kumpelea Judith.” Alisema Alen. “Kusafiri kwetu kutategemea na kupata kwetu tiketi kama zitakuwa hazijaisha. Ikiwa tutapata ndege ya kesho mchana kesho kutwa tutarudi tukiwa na jibu la kila kitu.” Alisema Seba huku akiinua simu yake na kutafuta namba fulani kisha akaweka sikioni.
Aliongea na watu wa Airport kama anaweza kupata Tiketi na baadaye alijibiwa kuwa ipo ndege ya mchana kama akiwahi kutuma majina ya wasafiri mapema angeandaliwa tiketi kwa ajili ya kusafiri mchana wa siku iliyofuata. Walikubaliana wale watu watatu kuwa watasafiri kwenda kuitembelea hospital hiyo siku ya pili yake. Matayarisho ya tiketi yalifanyika nao walisafiri.

Mandhari
Yalikuwa ni mazingira mazuri ajabu! Kila mahali kulikuwa kumesheheni vifaa vya kisasa kabisa. Mazingira yote pamoja na wodi za wagonjwa kulikuwa katika hali ya usafi. Ukaribisho waliopatiwa akina Seba hawajawahi kuupata katika hospitali yoyote ndani na nje ya Afrika. Walitembezwa katika mazingira yote ya hospitali mbapo iliwachukuwa siku mbili kuweza kumaliza mazingira hayo.

Mahali pa kulala palikuwepo ndani ya Hospitali hiyo tena pazuri sana zaidi ya hoteli za nyota tatu. Ukubwa wa eneo la Hospitali hiyo ulitosha kabisa kumweka kila mgonjwa na chumba chake. Kwa ujumla kulikuwa na vyumba vya wagonjwa vipatavyo mia nne na vyumba vya Madaktari mia tatu ambapo ni pamoja na wana Chuo waliokuja kujifunza udaktari katika chuo hicho.

Kwa ujumla kulikuwa na pande mbili yaani Hospitali na chuo na sehemu hizo mbili zilitengwa na ukuta uliofuatwa na bustani ya miti ya matunda iliyopita kama uchochoro wenye upana wa mita mia moja na urefu wa nusu kilomita. Katika bustani hii kulikuwa na matunda ya kila aina yaliyokuwa yanapishana misimu ya kuzaa.
Katika eneo lililobaki la Hospitali hii pamoja na chuo ilikuwa na Bwawa kubwa sana la samaki ambao walitumika kama chakula kwa wagonjwa na wahudumu wao. Mabwawa ya kuogelea yalizungushiwa Seng’enge maalumu ambapo waliruhusiwa wanachuo peke yake kuogelea katika mabwawa haya. Wageni walikuwa wakifikia kwenye Hostel ambazo hazina tofauti na Hotel kubwa ya nyota tano na huko kulikuwa na bwawa kubwa la kuogelea pia. Hospitali hii na Chuo havikuhusu kuuguza au kujifunza kutibu magonjwa mengine yoyote zaidi ya magonjwa ya akili. Hili ndilo agizo aliloacha mwasisi wa Hospitali hii Matlyer Ardorph.

Baada ya kumaliza matembezi hayo ya muda mrefu kwa eneo la Hospitali Sebastiani na wenzake walitembezwa eneo la Chuo cha utabibu wa magonjwa wa akili. Kwanza kabla hawajafika mapokezi eneo la uwanja wa Chuo hiki ulipambwa na sanamu kubwa sana la mwanamke ambaye ni muanzilishi wa Asasi hiyo kubwa duniani Dr. Matlyer Ardorph.

Ndani ya chuo kulikuwa na vifaa vya kufundishia vikiwepo Computer na vifaa vinginevyo. Ambapo eneo la Maktaba kulisheheni vitabu vingi sana na maktaba ilikuwa ni kubwa ya kutosha kila mwanafunzi kujisomea kwa uhuru. Baadhi ya vitabu vya kitabibu viliandikwa na Dr. Matlyer mwenyewe kikiwepo kile kitabu cha historia yake. Mwisho wa mizunguko hiyo ya kiutalii kulifanyika kikao katika usiku wa mwisho wa kuwepo hapo. Kikao hicho kilichofanywa na Seba na wenzake kilizaa matunda ya kukubaliana na hali iliyopo hapo na hivyo ilikuwa ni Ruksa kwa Judith kuletwa hapo kwa matibabu. Mwafaka huo ulipofikiwa ndipo walipotawanyika na kwenda kulala. Asubuhi na mapema walikwenda kuwaaga wenyeji wao ikiwa ni sambamba na Sebastian kuchukuwa fom ya kujiunga na Chuo hicho. “Naona umependezewa kweli na mambo yanayofanyika hapa mpaka umechukuwa Fomu ya kujiunga na chuo!”

Alisema Della mama mdogo wa Judith kishambenga. “Nimeona nijitendee haki kwa tamaa niliyoipata kwa kuwepo ndani ya mazingira haya kwa siku hizi mbili nimejifunza mambo mengi sana ambayo nahitaji kuyakalia kwenye dawati kwa muda wa kutosha nijifunze zaidi.” Alisema Seba huku akibeba begi lake na kulifuata gari linalowapeleka Uwanja wa ndege. “Nakupongeza sana Seba kwa utashi wako wa kutaka kupata kila kilicho chema.”

Alisema Alen baba mdogo wa Judith kwa shauku. “Asante mkwe pia msisahau kuwa hii ni njia nyingine ya kuwa karibu na mchumba wangu. Nisingependa tuwe mbali si unajua kuwa sisi ni mapacha?” Alisema Seba huku akiingia ndani ya gari na kuacha wenzake wakiangua kicheko. Baada ya kufunga mkanda kila mtu gari iliondolewa taratibu kuwapeleka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa jijini Nairobi tayari kwa safari ya kurudi nyumbani Tanzania.

***
Waandishi wa habari walitaharuki mara baada ya kuwakosa vijana wale wawili. Mitaani hawakuonekana wala hakukuwa na majibu ya kuritdhisha pale walipokwenda kuulizia nyumbani kwa mzee Martn. Kwa shingo upande wakageukia habari nyingine huku wakijilazimisha kusahau mambo ya Seba na Judith. Pamoja na kwamba walikuwa wakiandika habari nyingine, lakini macho na masikio yao yalikuwa wazi ili kuona ama kusikia lolote linalomhusu Sebastian na Judith. Kutokujua kuwa wako wapi kwa kipindi kile kuliwachanganya sana kiasi cha kuwafanya wengine waonekane kuwa wamekata tamaa. Kati ya waandishi walioonekana kukaa kimya katika suala la Sebastian walikuwa ni waandishi wa gazeti la UWARIDI.

Walionekana kama ambao hawakuona lolote katika habari hizo walinyamaza kimya bila kuchangia lolote katika habari hizo. Japo wengine wanapokutana katika viwanja vya kazi vikiwepo mikutano wa viongozi wa wa serikali, Bungeni na penginepo waliongelea suala la Seba na Judith kuliko habari nyingine. Ila kwa waandishi wa UWARIDI hawakuwa na neno lolote la kuchangia juu ya habari hizo.
Lakini kwa upande mwingine waandishi hawa walikuwa wakifanya msako wa chini kwa chini na kwa mbinu za kila aina. Kama wapo watu wasiojua nini maana ya kukata tamaa ni pamoja na akina Beka, Gama, Mwalongo na Kulindwa wakiwa na Komredi Hussein Kadabra. Kitu kinachowafanya wapate habari nyeti kila wakati ni umoja wao na makubaliano ya pamoja katika kukabiliana na changamoto za kazi zao za kila siku. Uzuri wa timu yao ni kwamba walikuwa wakiandikia gazeti moja, hivyo yeyote anayepata habari ilikuwa kwa faida yao wote, kutokana na mafanikio ya gazeti lao katika kutoa habari sahihi.

Maajabu ya mguso!

Hakujua kile alichoitiwa katika ofisi ile. Yalikuwa ni moja ya mawazo yaliyobebana katika kichwa chake. Masomo yake yalikuwa yanaendelea vizuri sana huku akielewa kila kipengele alichojifunza. Maisha yake yalibadilika ghafla kutoka kuwa mkurugenzi wa kampuni na mfanyabiashara mkubwa na kuja kuwa mwanafunzi mwaminifu katika masomo ya udaktari. Ndani ya masomo yake alijifunza vitu vingi sana na hakutaka apoteze kitu chochote katika yote aliyoyapata mahali pale. Ingawa kazi zake ziliendelea lakini hakuwekea maanani kazi hizo zaidi ya kile alichokuwa akijifunza mahali hapo. Alimkumbuka yule mtu katika Biblia aliyekuwa akilima shamba la kukodi na kugundua hazina katika shamba hilo.

Baada ya kugundua hazina hiyo alikwenda kwa mwenye shamba na kumwomba amuuzie shamba lile. Makubaliano ya bei yalimgharimu mtu yule kuuza kila kitu alichokuwa nacho ili tu alinunue shamba lile. Hata alipofaulu kuuza vitu vyote alibakia mtupu kabisa lakini hakujali kwani alijua katika shamba lile kutainuka heshima ya kipekee kwake. Kwa ujasiri alikwenda kwa mwenye shamba na kumkabidhi fedha zote zilizo sawa na makubaliano yao katika kuuziana shamba lile.
Mwenye shamba alipokea fedha ile na kuandikiana mbele ya mashahidi kuwa kuanzia siku ile lile shamba litakuwa chini ya umiliki wa yule jamaa. Baada ya makabidhiano nafikiri alikimbilia shambani ili akavune ile hazina aliyoiona. Mabadiliko yaliyotokea katika maisha yake hayakuwa ya kawaida.
Hayo yalikuwa ni moja ya mawazo aliyokuwa nayo Sebastian Changawe juu ya kile alichokuwa anakipata katika Chuo kile cha Udaktari. Mbele yake aliona hazina ya thamani sana inayoweza kumpelekea heshima yake ikapanda juu sana kuliko neno lenyewe lilivyo. Mara katikati ya mawazo yake alishtuliwa na simu yake ya mkononi.


“Halo Dr. Niko njiani nakuja, nilikuwa namalizia kazi ya mwalimu wa Psychology. Baada ya dakika saba kuanzia sasa natakiwa kuwakilisha. Ndani ya dakika kumi nitakuwa hapo Bosi.” Alisema Sebastian huku akiendelea kufanya kazi aliyoachiwa kama Home work huku kichwani akiwa anawaza baadhi ya mambo ya maisha yake. “Okay nakusubiri.” Alijibu Dr. Matlda ambaye pia alikuwa ni Mkurugenzi mkuu wa Asasi hiyo ya Kimataifa. Baada ya kukata simu Seba aliendelea kufanya Home work yake kwa somo la sayansi ya ubongo wa mwanadamu.

Kwa muda wa dakika tano alikuwa amemaliza kipande alichokuwa amebakisha kisha aliprint majibu ya maswali yake na kuyapeleka kwa Mwalimu wake wa somo hilo. Baada ya kukabidhi kazi yake alikwenda kwa Doctor Matlda Ambapo alimkuta akiwa anamsubiri Ofisini kwake. “Hey guy! Mambo vipi? Uko Smat sana katika muda.”

Alisema Doctor Matlda huku akisimama kwenye kiti kwa ajili ya ukaribisho ule. “Nashukuru Doctor kama nimefika kwa muda mwafaka. Pole kwa kusubiri nilikuwa nafanya kazi ya somo langu ninalolipenda sana.” Alisema Seba huku akikaa usoni akiwa amejaa tabasamu pana. “Nimekuita ili nikupe taarifa ya mgonjwa wako.” Alisema Doctor Matlda huku akijiweka sawa katika kiti chake, kisha akaendelea:

“Nakupongeza kwa kuonyesha uvumilivu mkubwa kwa ajili yake na pia kumwonyesha jinsi unavyomthamini na kumpenda. Tiba yetu katika Hospitali hii inahusiana kwa karibu sana na kumjali mgonjwa na kumgusa kwa upendo. Mguso wa upendo huleta matumaini mapya katika maisha ya mwanadamu. Miili tuliyopewa imewekewa hisia za kuhisi kupendwa au kuchukiwa.

Uzima au ugonjwa hutokana na moja ya mambo mema au mabaya anayoyapata mwanadamu kwa njia ya kazi mbaya za shetani au utendaji wa Mungu ndani ya mwanadamu huyohuyo. Kwa sehemu nyingine ni kwamba mwanadamu ana nguvu nyingi san a ndani yake ambapo kwa namna moja au nyingine humtoka na kusababisha uponyaji kwa mtu mwingine. Nguvu hizi hufuatana na Upendo. Unapomwambia mtu kuwa nakupenda ni jambo jingine lakini unaposema nakupenda kisha ukamsogelea mtu huyo na kumgusa mwilini kwa mkono wako ule upendo unapenya ndani yake kupitia hisia.

Mguso ule unafanya kazi ikiwa mtu yule alikuwa ni mgonjwa na kusababisha tumaini jipya ndani yake.” Matlda alisema kisha akanyamaza kidogo kisha akaendelea: “Hayo yote ninayoyaeleza hapa umekuwa ukiyafanya kila wakati kwa mgonjwa wako jambo ambalo limekuwa likileta uponyaji bila wewe kujua.”
Alisema Doctor Matlda kisha akatoa bahasha ya ukubwa wa A4 na kutoa picha ya Exray kisha akamwonyesha Seba. “Mpaka hapa tumempiga picha hii ili kukagua maendeleo ya mchubuko wake katika ubongo tunaona kuwa hakuna kitu kinachoonekana katika picha hii, hii ikimaanisha kuwa tayari Judithi amepona jeraha lake kabisa.”

“Woow! Doctor Judith amepona kabisa?!” Alisema Seba kwa furaha isiyo kifani.
“Ninaweza kusema hivyo Seba kutokana na vipimo pamoja na picha unayoiona hapa ila kuna mambo machache ambayo kwake hayajakaa sawa. Baada ya kumpima tumemjaribisha kumuuliza maswali kadhaa na kumchanganyia habari mbalimbali ili kuona kama atazifumbua lakini amekuwa mgumu kidogo katika mitihani yetu.

Kwa hiyo bado unahitajika muda mwingine wa kuwepo hapa mpaka afaulu majaribio yetu.” Alisema Doctor Matlda. “Unafikiri itachukuwa muda gani tena ili akili zake zikae sawa?” aliuliza Seba kwa umakini mkubwa. “Kiasi cha muda bado sijajua kuwa utatumika muda gani. Lakini kwa muda wa mwaka mmoja aliokuwa hapa Hospitali matokeo yake yamekuwa haya. Juu ya kurudiwa na akili zake timamu ni wakati wowote tu na wala hilo sio tatizo kubwa.” Alisema Doctor Matlda kwa ufafanuzi. “Nashukuru sana Doctor kwa bidii yenu iliyofikisha hali ya Judith mpaka hapa. Naamini mpaka nikimaliza masomo yangu atakuwa amepona kabisa na tutarudi wote nyumbani kwenda kuendeleza majukumu yetu.” Alisema Seba kwa furaha sana huku akimpa Doctor Matlda mkono wa shukrani.

“Nafikiri hii shukrani iende moja kwa moja kwa Mungu aliyemsaidia mama yangu Dr. Matlyer kupitia mambo kama aliyopitia Judith, hatimaye kupata ufumbuzi wa kuanzisha Asasi hii ambayo imekuwa msaada duniani kote.” Sisi wengine tupo hapa kuendeleza kile Dr. Matlyer alichopata na kukianzisha.” Alisema Doctor Matlda akiwa bado kashikilia mkono wa Seba.

Tangu Seba aingie katika chuo hicho ikiwa ni sambamba na kumwingiza Judith kwenye Tiba maalumu Doctor Matlda amekuwa karibu naye sana kila wakati. Maendeleo yake kimasomo yalimfurahisha sana na pia aliona kuwa ndoto yake ya kuanzisha tawi la hospitali hiyo nchini Tanzania imetimia. Uelewa katika masomo pamoja na shauku yake ya kuwa Daktari wa watu wasio na akili timamu vilimfanya Doctor Matlda aone kile alichokitarajia kikiwa mbele yake. Tangu wakati huo alikuwa akimwita Seba na kumfundisha mambo ya ziada nje ya masomo ya kawaida na pia alimhudumia Judith kwa namna ya tofauti kidogo na wagonjwa wengine.
Kwa ujumla Doctor Matlda alimwona Seba kama sehemu ya familia yake japo alikuwa akipokea ada kama kawaida ambayo ilikuwa ni kiasi kikubwa sana cha dola za kimarekani. Tiba kwa ajili ya Judith iligharimu Dola 20000 kwa mwaka hali kadhalika ada ya Seba ya masomo ni kiasi hicho hicho. Fedha yote ilikuwa inalipwa kupitia account za chuo na Hospitali.

Kuhusu Hayo yote hayakuwa tatizo kwa Seba. Shida yake kubwa ilikuwa ni Judith apone na kurudiwa na afya yake. Lakini pia alipata wazo jipya la kufungua tawi la Hospitali ile ili aweze kuwahudumia watanzania walio wengi kutokana na shida za ugonjwa wa akili. Mawazo aliyokuwa nayo yaliwiana na mawazo ya Doctor Matlda japo hakuna aliyemwambia mwenzake juu ya jambo hilo.

Seba alifurahia sana kuona Matlda akiwa rafiki yake na kumpatia elimu ya ziada juu ya masomo yake. Kwake alihifadhi siri ya kutaka kuwa wakala wa Psychological Mental Hospital nchini Tanzania, ili iwe mshitukizo mara tu baada ya kuhitimu masomo yake. Alipanga kumfurahisha Doctor Matlda mara tu baada ya mahafali yake kwa kuwa alisikika mara kwa mara akisema kwa ajili ya kumpata Mtanzania mwenye moyo wa kuanzisha Tawi katika nchi hiyo.

Wakenya wawili na Mmalawi mmoja walimwendea Doctor Matlda kwa wakati tofauti wakimwomba awape kibali cha kuanzisha Tawi Tanzania lakini Matlda alikataa kabisa. “Ninanataka tawi la Tanzania lianzishwe na Mtanzania halisi ambaye atakuwa ana uchungu kwa ajili ya watu wake. Sioni kwamba mtu kutoka katika taifa tofauti atakuwa na uchungu mkubwa kuliko Mtanzania mwenyewe. Sitaki kuona maswala ya Asasi hii yakichukuliwa kwa sura ya kibiashara zaidi ya huduma. Japo watu hulipa fedha zao kwa huduma hii lakini si zaidi ya kile kitu cha thamani kinachotoka katika mioyo ya dhati wanachokipata kutoka kwetu.”

Hiyo ndiyo kauli ya Matlda kwa watu waliomjia na kutaka kuanzisha matawi katika nchi tofauti na nchi za kwao walikotoka. Kwa upande wa Tanzania hakupatikana mtu wa kujiunga na chuo hicho kwa zaidi nusu karne tangu chuo hicho kianzishwe. Pamoja na shauku ya Matlda katika kuanzisha Tawi Tanzania lakini isingewezekana kabisa kutokana na kukosekana kwa Mtanzania aliyepata mafunzo kutoka katika chuo hicho.

Ziara ya Seba na akina Della na Alen iliibua furaha ya aina yake kutoka kwa Matlda na yeye mwenyewe aliona fahari kubwa kuchukuwa nafasi ya kuwatembeza katika Hospitali ile pamoja na chuo na kuwaeleza kila kitu kuhusiana na Hospitali hiyo. Ziara hiyo ya watu kutoka Tanzania ilikuwa ni ya kwanza kabisa tangu chuo hicho kianzishwe. Tangu hapo Mkurugenzi huyo wa chuo akaanza kuona nuru ya kile alichokuwa akikitamani ikianza kutokea.

Hali hiyo ilizidishwa na ujio wa Seba akiwa na mchumba wake kwa ajili ya matibabu. Lakini matumaini makubwa zaidi yalitokea pale Seba mwenyewe alipojiunga kabisa na chuo hicho japo ilikuwa ni kwa nia ya kukaa karibu na Mchumba wake. Sababu iwayo yoyote kwa Matlda haikuwa na uzito wa kumuondolea matumaini ya kuwa Seba anaweza kuwa mtu sahihi aliyemngoja kwa miaka yote kwa ajili ya Tanzania. Kwake alikuwa na shauku ya kulipa fadhili katika nchi hiyo, kutokana na asili ya utajiri wa familia yake kwa vile vipande vya madini vilivyosababisha mafanikio makubwa.
8
Kombolela
Waandishi wengi wa magazeti pamoja na wana habari wa redio na Televisheni waliendelea kushangaa namna walivyowapoteza ghafla Seba na Mchumba wake mitaani. Waandishi walienda kila mahali kutafuta habari za wapenzi wale wawili huku wakitumia kila aina ya mbinu ili wapate habari kamili. Lakini walionekana kugonga mwamba. Kila mmoja alikuwa akipania kupata habari sahihi cha nini kilichokuwa nyuma ya uigizaji ule?
Waandishi wengi hawakuwa na taarifa kamili kuwa yaliyokuwa yanafanywa na vijana wale ni maigizo ama ni shida gani iliyowapata. Kuandika kwao kwa kubuni buni hakukuwapa amani mpaka waupate ukweli. Walifika nyumbani kwa mzee Martin lakini hawakuambulia lolote kutokana na baadhi ya magazeti kutoa habari za kudhalilisha juu ya Judith.

Mara tu baada ya Mzee Martin kusoma habari juu ya binti yake kuandikwa vibaya na kutangazwa wazi kuwa ni kichaa kilimuuma sana. Tangu siku hiyo mzee huyo alijiapiza kuwa hatathubu tena kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari juu ya taarifa yoyote ile. Hata walipokuja baada ya Akina Seba kwenda Nairobi hakuwapa ushirikiano wowote na hivyo habari hiyo ikawa kama giza kwao kwani hawakujua kuwa walielekea wapi watu hao. Upelelezi wa aina yake ulifanywa na waandishi wa habari kusudi wajipatie sifa kwa kufumbua mahali walipokwenda watu hao na kujua habari zao kiundani. Vyombo vya Habari nchini Tanzania vilisubiri kwa hamu sana kupata habari sahihi za sehemu aliko Seba na mchumba wake na maendeleo ya maisha yao.


Kupotea kwa Seba na mpenzi wake kuliyafanya magazeti yawe kimya bila habari zao. Isipokuwa gazeti la kimbea zaidi lililowahi kutoa habari zisizo na uthibitisho sahihi. Gazeti moja linalotoka mara tatu kwa wiki lilitoka na habari isemayo Seba na Mchumba wake waonekana wakisafiri kuelekea Afrika ya kusini. Maelezo yaliyofuata hayakuwa na ushahidi wa kutosha japo gazetii hilo liligombaniwa sana na wasomaji.

Baada ya habari hii ya uongo kutolewa kwenye gazeti hili wananchi walikosa imani na vyombo hivyo vya habari. Jumbe nyingi kutoka kwa wasomaji makini zilielekezwa kwa magazeti mbalimbali kuyashutumu kwa kutokueleza habari kwa umakini. Pamoja na wamiliki wa magazeti mengine kukana kutohusika na habari iliyotoka ya uongo lakini pia wao walikosa habari sahihi ya kueleza ni wapi Seba na Judith walipo na wanafanya nini.

Hiyo ilikuwa ndiyo habari iliyohitajika kuliko zote kwa wakati huo. Hii ilimaanisha kuwa gazeti litakalotoa habari hiyo kwa usahihi litakuwa na wateja wengi kwa zaidi ya asilimia 85. Wamiliki wengi wa vyombo hivyo vya habari waliwatuma waandishi wa habari kila kona wakiwaahidi donge nono pindi watakapokuja na habari za ukweli za Kijana tajiri Seba na mchumba wake Judith Martin. Umaarufu wa watu hao ndio hasa chachu ya vyombo vya habari kutaka kupata habari zao kwa udi na uvumba. Jopo la waandishi wa habari chini ya Waziri wa habari na utangazaji lilikaa na waziri akawataka kupekuwa na kuhakikisha kuwa habari za vijana hao zinapatikana bila kuongeza wala kuzusha uongo juu yake.

“Swala la habari ni kutafuta ukweli wa habari yenyewe na kuitoa kama ilivyo. Bila ushahidi wa kutosha habari inakuwa haijakamilika kuwa habari. Ukiitoa habari ambayo haina ushahidi ni kosa kisheria kwa hiyo itakulazimu kupata adhabu husika kulingana na kosa hilo.” Hayo ni baadhi ya maneno aliyoyasema Mheshimiwa Waziri wa habari. Baada ya maneno hayo alisisitiza kuwa hodari sana katika kutafuta habari za Seba na Judith. “Vijana hawa ni wa muhimu sana katika Taifa letu.

Wote ni watu maarufu na wenye majina makubwa kwa hiyo jambo lolote linaweza kuwapata kama kisasi kwa maadui zao. Zingatieni umakini katika kutafuta habari hizi na kuleta mbele za watu ukweli mtupu juu ya upelelezi wenu.” Aliongeza Mheshimiwa Waziri. Mwisho wa yote alifunga kikao hicho na kila mmoja akatawanyika kwenda kwenye majukumu yake. Baada ya kikao hiki vilifuata vikao vilivyofanywa na kila kampuni ya magazeti na waandishi wao. Wale waandishi wasio na wizara maalumu nao walikuwepo wakijaribu kutaka kuhudhuria vikao viwili ama vitatu kwa mara moja! Lakini walijikuta wakiambulia kikao kimoja kwa wakati mmoja kama wengine.
*** *
Mkurugenzi mkuu msaidizi wa kampuni ya Seba & Elly Changawe Interprises alikuwa nyuma ya meza yake akiwa ametulia juu ya mafaili kadhaa yaliyoko pale mezani. Faili moja lilikuwa la vocha za malipo ya watu wa kampuni ya Usafirishaji na uingizaji wa mizigo kutoka nje ya nchi. Faili hili lilikuwa na hundi kadhaa zilizojazwa na katibu wa kampuni hiyo na yeye alikuwa na kazi ya kuzisaini ili kupeleka katika kampuni hiyo. Faili jingine lilikuwa la wafanyakazi baadhi waliokuwa na barua zao za madai kuhusu kuongezewa mishahara kulingana na nafasi zao mpya kicheo walizowekwa tangu miezi mitatu iliyopita. Wakati akilipitia faili hili mara simu ya mezani ikaita. Mkurugenzi yule akainyanyua simu yake kiuvivu na kuiweka sikioni.

“Hallo.” Aliitika simu ile kwa sauti nzito.
“Hello bosi kuna mgeni wako anataka kukuona, amesema anaitwa Gadna ni mwandishi wa habari.” Alisema Lucy katibu muhtasi wa ofisi ya mkurugenzi mkuu msaidizi bwana Ibrahimu Minya. “Mwambie aingie.” Alisema Mkurugenzi Minya.
Baada ya muda Mlango wa ofisi ya mkurugenzi msaidizi ulifunguliwa na akaingia kijana wa miaka kati ya ishirini na nane na thelasini, mrefu wa futi tano na robo mwenye mwili wa wastani lakini uliojazia kimazoezi na rangi ya mwili wake ilikuwa ya maji ya kunde. Akiwa na mfuko wa ngozi mkononi mwake.

“Karibu Mr. Gadna. Keti kwenye kiti na niko tayari kukusikiliza..” Alisema hivyo Mr. Ibrahimu huku akijiweka vizuri kwenye kiti chake.

“Kwanza pole kwa kazi mkurugenzi. Na pia asante kwa kunipa nafasi angalau ya kukutana na wewe.” Alisema Gadna kwa heshima na nidhamu ya hali ya juu.
“Ndio Gadna karibu nakusikiliza” Alijibu mkurugenzi kwa kifupi.
“Mimi ni mwandishi wa kujitegemea, ambaye habari zangu ninayapelekea magazeti mbalimbali; Kampuni yangu inaitwa Gad News hot Company. Jambo la lililonifanya nije hapa kukutana na wewe ni kupata habari juu ya mkurugenzi mkuu Sebastian Changawe. Nia hasa ni kuujulisha umma wa Watanzania ambao baadhi yao ni viongozi wa kiserikali mahali hasa alipo na kama atakuwa katika hali gani yeye na Mpenzi wake Judith Martin.” Alisema Gadna kwa utulivu mkubwa.”

“Gadna wewe ni mmoja wa waandishi wa habari mashuhuri hapa nchini. Habari zako ninazisoma sana hata makala zako ni nzuri unazoyaandikia magazeti mbalimbali likiwepo gazeti la Kwikwi linalotoka kila jumamosi.” Alisema Mkurugenzi kisha akakohoa ili kusafisha koo na baadaye akaendelea: “Lakini Gadna una bahati mbaya kwamba mimi kwa habari hizo sina haki ya kuzielezea.
Msemaji mkuu wa Sebastian Changawe ni Mheshimiwa Mbunge Mzee Matias Changawe, maana mambo hayo ni ya kifamilia zaidi. Hii hapa ni Kampuni kama kuna swali la kuuliza kuhusu kampuni na kazi zake zote mimi naweza kutoa ushirikiano mkubwa. Lakini Sebastian na habari zake anapaswa aulizwe Mzazi wake kama msemaji mkuu wa familia. Najua utakapopata habari za Sebastian Utakuwa umeshapata habari za Judith pia. Nafikiri umenielewa vizuri.” Alisema Ibrahimu kwa kirefu.

“Sawa Mkurugenzi nimekuelewa lakini imekuwa ni vigumu sana kwa mheshimiwa Changawe kulizungumzia swala la Sebastian na kwa taarifa tu ni kwamba jana nikikuwa Dodoma kwenye Bunge la Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania. Nilionana naye na kumuuliza maswali nikiwa na jopo la waandishi wengine wa habari lakini aligoma kabisa kuelezea swala hilo.

Wakati anaondoka kuingia kipindi cha pili cha Bunge alisema: “Habari hizi mwaweza kuzipata kwa mkurugenzi mkuu msaidizi wa kampuni yake.” Majibu hayo ndiyo yaliyonifanya niwahi kufika hapa mapema nikijua nitakuwa aidha wa kwanza au wa pili kuzipata habari hizi ili kuwafanya watanzania waupate ukweli kuhusu alipo Sebastian na Judith.” Alisema Gadna huku akimtazama Mkurugenzi Ibrahimu kama anayeomba upendeleo wa kupewa habari hiyo japo kwa kidokezo tu.

“Pole sana Gadna! Najua Sebastian na Mpenzi wake wamewachezesha kombolela la aina yake. Ukiona mpaka baba yake mzazi anakataa kutoa habari za mwanae ujue kuwa habari hizi zimefungwa kabisa. Haiwezekani watu walio chini ya Seba kimadaraka wakawa wasemaji wake wakuu. Hukushtukia jambo hilo?!” Aliuliza Ibrahimu kwa tabasamu la mshangao.

“Basi sawa Mkurugenzi inabidi niende kuendelea na mambo mengine nakutakia kazi njema.” Alisema Gadna kwa kukata tamaa. “Asante na kwako pia Gadna. Ila kumbuka hili ni kombolela na mchezo wa aina hiyo unahitaji ujanja wa hali ya juu sana kuweza kumfumbua aliyejificha kuwa kajificha wapi. Usitegemee kupata ushindi kiulaini kijana wangu.”

Alisema Mzee Ibrahimu huku akiwa amemshika mkono Gadna wakati wanaagana. Gadna alitoka mahali pale akiwa hajui namna ya kufanya ili kupata ufumbuzi wa suala lile muhimu. Moyo wake ulikuwa umevunjika kwa kutokufanikiwa kupata majibu ya maswali yake. “Kama hapa sijapata hata fununu ya namna ya kupata habari za Seba ni wapi naweza kupata habari sahihi?” Gadna alijiuliza swali hili kwa sauti wakati akifungua mlango wa gari yake, lakini wakati ule ikajirudia sauti ya Mkurugenzi Ibrahimu ikisema:
Ila kumbuka hili ni kombolela na mchezo wa aina hiyo unahitaji ujanja wa hali ya juu sana kuweza kumfumbua aliyejificha kuwa kajificha wapi. Na usitegemee kupata ushindi kiulaini kijana wangu.

Gadna aliunga mkono maneno ya Mkurugenzi yule kuwa ule ulikuwa ni mchezo wa Kombolela kweli. Ushindi wa kupata habari sahihi zinazotokana na kugundua mahali alipo Sebastian na Judith unategemea juhudi na mbinu za kipekee sana. Tangu wakati huo alipata changamoto ya tofauti kutokana na maneno ya yule mkurugenzi.


Mafunzo ya kijeshi aliyoyachukua nchini China yalimfanya kuwa katika viwango vya juu sana katika fani ya upelelezi. Hii ni moja ya tamaa yake tangu alipokuwa kijana mdogo alipenda sana kazi ya upelelezi. alipofika katika nchi ya china kwa ajili ya biashara zake alilazimika kuingia katika mafunzo ya kung fu, judo na mazoezi mengineyo kwa ajili ya kujiimarisha mwili wake. Hii ni ili kujihami kutokana na ubabe wa Wachina. Maeneo aliyokuwa anafanyia biashara zake yalikuwa na vijana wakorofi sana. Mafunzo hayo alikuwa anayachukuwa katika muda wake wa ziada baada ya kumaliza kazi zake.

Viwango vyake vya mafunzo hayo vilipanda juu sana pale alipofanikiwa kupata mikanda kadhaa ikiwepo mkanda mwekundu na hatimaye mkanda mweusi kulingana na uwezo aliouonyesha. Furaha yake ilikuwa kubwa pale alipoonekana amefaulu baadhi ya mafunzo ya msingi. Mafunzo hayo yalimfanya awe na nyongeza ya mafunzo ya J.K.T. aliyoyapata mara tu baada ya kuhitimu Kidato cha sita kabla ya kuingia chuo kikuu. Matokeo ya ufaulu wa kwenda chuo kikuu yalikuwa mabaya kwa upande wake. Kutokuchaguliwa kwake kulimfanya aingie katika biashara za aina mbalimbali ikiwepo ya maduka ya jumla ya vipodozi na nguo za kike na za kiume.

Biashara zake zilimpandisha sana kimafanikio hata ikawa aliweza kusafiri mwenyewe kwenda nchini china kukusanya bidhaa za maduka yake. Huko ndiko alipoanza utundu wake wa kujifunza mbinu za upiganaji. Baada ya kufaulu katika kupata mbinu mbalimbali alirudi nchini akiwa na ari ya kipekee katika kujaribu kuanzisha kampuni yake ya upelelezi binafsi dhidi ya Majambazi na mauaji ya Albino.

Vizingiti alivyokutana navyo vilimfanya aamue kusomea uandishi wa habari kusudi apambane na wahalifu hao kwa kuwafichua akitumia kamera na kalamu badala ya mtutu wa bastola. Kupata vizuizi hakukumvunja moyo badala yake aliamua kutumia fursa nyingine. Mwisho wa mafunzo hayo ulimfikisha katika shirika la habari la UWARIDI na baadaye akakubaliwa kuwa mmoja wa waandishi wa habari wa Gazeti hilo.
Pamoja na kuwa mfanya biashara jijini Dar es Salaam lakini pia alikuwa na shauku ya kuwa mwanahabari kutokana namsukumo wa kuwasaidia walemavu wa ngozi pamoja na kupambana na uhalifu hususani genge la majambazi. Suala la kupotea ghafla kwa Seba na Judith katika uso wa vyombo vya habari ni habari ambayo yeye haikuwa ikimhusu sana

Mara zote alikuwa katika harakati za kufichua habari za watu wabaya waliokuwa wakikata viungo vya walemavu wa ngozi, pamoja na magenge sugu ya majambazi. Habari za Seba ambaye hakuwa na shutuma za kijambazi wala uhalifu wa aina yoyote kwake hakuwa na sababu ya kumfuatilia. Siku moja katika kikao cha waandishi hao kilichoitishwa na mkurugenzi wa shirika hilo hapo ndipo alipopata ufumbuzi juu ya upana wa habari na faida zake kwa jamii. Somo hilo analikumbuka sana hasa alipokuwa chuo cha habari lakini hakuchukulia uzito zaidi ya kujikita katika mkondo wake wa kusaka habari juu ya wahalifu. Siku hiyo ya kikao mbele ya Mkurugenzi ndipo alipofunguka kutokana na hotuba fupi aliyoitoa mbele za waandishi hao. “Mwanahabari ni kama juya. Kazi ya juya ni kubeba kila kitu kilichoingia ndani yake baada ya hapo ndipo huchaguliwa vinavyofaa na vile vingine hurudishwa baharini.” Alisema Mkurugenzi, kisha akanyanyua gilasi ya maji iliyokuwa katika meza yake, kisha akaendelea.

“Ndugu zangu kazi hii ya habari ina mambo mengi sana yanayohitajiwa na jamii. Na kila habari ni muhimu kwa wakati wake bila kubagua ni aina gani ya habari. Kama mwanahabari akichagua aina ya habari ujue huo ni udhaifu mkubwa sana katika tasnia nzima inayohusu habari. Ukomavu wa mwanahabari ni kutafuta habari yoyote inayoweza kuigusa jamii na kuiwakilisha katika vyombo husika vya habari.

Jamii haiko katika mlengo mmoja wa habari ila kila jambo linalogusa hisia za wanajamii ni habari pia. Ndio maana kuna habari za michezo lakini michezo nayo iko katika vipengele vingi. Kuna mchezo wa mpira wa miguu, mpira wa kikapu, kuna ngoma, muziki sarakasi, mieleka, ngumi na mingineyo mingi. Tunaporudi katika suala la habari zinazohitajiwa na jamii basi ziko habari nyingi mno! Alisisitiza kabla ya kuendelea.

“Mbele yetu kuna suala moja ambalo ninataka katika shirika letu tulifanyie kazi. Pamoja na migawanyo yetu ya majukumu ya kazi bado tusisahau habari kuhusu Seba na Judith. Kitu kilichofanywa na watu wale kuhusu upendo wao hakikuwa maigizo ya sinema bali lilikuwa ni jambo halisi linalouonyesha upendo wa hali ya juu sana katika dunia hii. Kumbuka Seba ni mtu maarufu nchini kwetu kutokana na kuwa mfanya biashara mkubwa.

Mbali na hayo pia alikuwa katika shirika la kimataifa nchini la kuingiza magari yenye ubora wa hali ya juu pamoja na mashine za viwandani. Mambo aliyoyafanya ya kuacha kazi katika shirika lake likiambatana na kukatiza masomo yake nchini marekani kwa ajili ya mchumba wake ni vitu vya kushangaza sana. Mengine ni mambo mnayoyajua kwa sababu yaliandikwa katika Gazeti letu na mengine.

Mguso huo wa upendo ni lulu kwa jamii na ni funzo kubwa sana. Hii ndiyo sababu iliyopelekea gazeti letu kujinyakulia tunzo kwa uandishi wa habari zilizodhibitishwa na zenye ushahidi. Waandishi baadhi yenu mlijipatia zawadi kutokana na uhodari wenu. Sasa kwa wakati huu Seba na Judith wamekuwa bidhaa adimu sana kwenye makaratasi ya magazeti yetu. Ni lazima tuibuke tena washindi katika kinyang’anyiro hiki cha kuwatafuta watu hao na habari zao sahihi kuhusu maisha yao halisi na ni wapi walipo kwa wakati huu.

Watu hawa wamejificha wapi jamii inataka kujua. Kwa namna gani habari sahihi kuhusu wao zitapatikana si kazi ya jamii bali ni kazi ya waandishi wa habari. Mafunzo mliyoyapata na vyeti vyenu vitakuwa na maana ikiwa mtaweza kufumbua fumbo hili kwa jamii. Ninaamini kutakuwa na nyongeza ya mambo ya muhimu ya kujifunza ikiwa watu hawa watapatikana na habari kuhusu wao.

Najua mnatambua kuwa hii ni biashara. Biashara bila bidhaa sio biashara. Bidhaa za biashara ya habari ni habari zenyewe. Nawatambua kuwa ninyi ni hodari na wazuri sana katika kufukunyua mambo yaliyojificha. Sasa kazi kwenu. Nendeni mtafute habari lakini habari kuhusu Seba ni bidhaa adimu sana inayosubiriwa sokoni.” Alisema Mkurugenzi huyo kwa msisitizo mkubwa. Hii ndiyo hotuba iliyomwamsha Andrew katika kuujua upana wa habari. Na hapo ndipo alipoamua kwa namna yoyote ile alifanyie kazi suala lile mpaka apate ufumbuzi wake.

Ndoto ya matumaini
Ilikuwa ni ndoto kweli lakini yale aliyoyaona katika ndoto hiyo aliona kama ndoto nyingine. Ndoto iliyobeba ujumbe wa kufurahisha kuliko kitu chochote katika maisha yake. Aliota yuko na mpenzi wake wakiwa kwenye bustani nzuri ya maua. Maua yaliyopandwa kandokando ya bwawa la kuogelea. Haikuwa mahali pengine zaidi ya eneo la Chuo cha udaktari. Michezo ya kukimbia waliyokuwa wanaifanya iliibua furaha ya aina yake hasa pale upepo mwanana na sauti za ndege ziliposikika.

Mizaha na makimbizano hayo yaliishia katika jabali moja ambalo walilitumia kwa kukaa kikao chao na kupanga mambo yao ya maisha. Kando ya jabali hili kulikuwa na mto mdogo uliokuwa unateremka katika mawe huku maji yake yakitoa sauti ya kuburudisha. Upande wa kulia wa jabali lile lililotambaa eneo kubwa kulikuwa na msitu mdogo wa miti ambao umepakana na shamba la migomba. Kwa mbele ya jabali kulikuwa na bonde ambalo lilikusanya maji ya mto huo mdogo.

Mkusanyiko wa maji ya mto huo ulitengeneza bwawa kubwa, bwawa ambalo lilitumiwa na uongozi wa chuo na hospitali hiyo kufugia samaki wa kila aina. Vilevile bwawa hilo lilikuwa sehemu ya mabata bukini na mabata mzinga kutembelea huku bata bukini wakiogelea kwa furaha na kutengeneza sura ya kupendeza sana ya eneo hilo. Mahali hapa kwenye jabali kubwa na lenye mandhari nzuri ndipo walipokuwa wamekaa wakijadili mambo mbalimbali ya maisha yao. Sura ya msichana huyu ilikuwa nzuri yenye kuvutia kuliko siku nyingine za nyuma. Maneno yake pia yamejaa hekima na maarifa ya hali ya juu sana.

Akiwa ndani ya ndoto alijiwa na wazo kuwa mpenzi wake huyo si alikuwa na matatizo ya akili? Sio hivyo tu pia ilimjia picha kuwa hata hapo walikuwa kwa ajili ya matibabu ya mrembo huyo. Haikuishia hapo tu alikumbuka mengi na dua zake za kila siku kuhusu mchumba wake huyo kuwa apone haraka ili wafunge ndoa yao na kuendelea na utaratibu wa maisha yao.

Lakini wakati anawaza hayo Judith martini akamwambia: “uliteseke sana kwa ajili yangu Seba lakini lile tatizo limekwisha kabisa, Mimi ni mzima sasa inabidi turudi nchini kwetu kwa ajili ya utaratibu wa kufunga ndoa yetu kama tulivyoahidiana.” Alisema Judith na kumfanya Seba afurahie na kumkumbatia kisha kwa pamoja walisimama na kuelekea katika bwawa la kuogelea. Wakiwa wameshikana mikono kwa furaha. Walipolifikia bwawa la kuogelea wote walijitupa ndani yake na kufurahia katika maji hayo wakiwa pamoja. Wakiwa katika hali hiyo ya kuogelea kwa kushindana na kufanya michezo mbalimbali mara waliona kundi la wagonjwa wa hospitali ile wakija nao kutaka kujiunga nao kuogelea wakati watu wale wenye matatizo ya akili walipokuwa wakijiandaa kuingia ndani ya bwawa hilo Seba alimshika mkono Judithi na kumvutia kwenye ngazi za kutokea na mara hiyo wakawa nje ya bwawa huku vichaa wale wakiingia bwawani kwa fujo huku wakipiga makelele.




ITAENDELEA


USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.