Simulizi : Penzi Chungu Sehemu Ya Tatu (3)


Usiku wa siku ile ulivyoingia ulikuja na janbo. Saa sita ya usiku, Suto akiwa amelala usingizi mzito. Mlango wa geti lake ulikuwa unafunguliwa taratibu.

Aliyekuwa anafungua mlango ni Zura akishirikiana na yule kijana aliwaibia bahasha kina Inspekta Jasmine mchana uliopita, alikuwa anaitwa Ndula wa Ndulani.



Lakini Zura na Ndula walikuwa hawajui. Suto hakuwa Suto yule, sasa alikuwa Suto mpya, Suto mwenye hisia. Akiwa usingizini alisikia kwa mbali ukelele wa mlango ukifunguliwa.

Aliamka kimyakimya.

Taratibu Suto alijisogeza mpaka nyuma ya mlango. Kulikuwa Giza la kutisha. Akiwa pale nyuma ya mlango Suto alimuona vizuri mtu akiingia kwa mwendo wa kunyata na kisu chake mkononi. Alikuwa anakifata kirago alicholalia Suto muda mfupi uliopita.

Ndula ananyata na kisu chake bila kujua kuwa nyuma nae alikuwa ananyatiwa na mtu, Suto Sutani aliyebadirika !



Kwa mara ya pili Suto anataka kuuwawa, je Ndula wa Ndulani atafanikiwa?



Zura alikuwa amerudi kule getini. Akisubiri Ndula amalize kazi kule ndani, kazi ya kumuua Suto. Ni yeye aliyewabadirishia lindo askari wenzie ili apate nafasi ya kumuingiza Ndula gerezani, na alifanikiwa.



Akiwa kwa nyuma akisaidiwa na giza, Suto alimrukia yule jamaa, kwa nguvu zake zote Suto alimkaba Ndula shingoni. Kutokana na hofu na nguvu ya ile kabali, kisu cha Ndula kilidondoka chini. Suto akazidisha kubana mikono yake. Ndula alijaribu kujitoa bila mafanikio.

Suto alikuwa na nguvu mithili ya mwanamme. Ndula macho yalimtoka, kabari ile ilinasa barabara shingoni mwake.

Ndula hakufurukuta. Mara alianza kuishiwa nguvu, alidondoka chini taratibu.

Alikuwa amezimia.

Suto alimwangalia usoni yule mtu. Alikuwa amevaa soksi kubwa iliyoziba kabisa sura yake. Aliivuta ile soksi na kuivua. Alimwangalia yule mtu usoni. Lakini hakumtambua. Hakuwahi kukutana na yule mtu kabla.

Suto alimvua yule mtu ile fulana nyeusi na suruali nyeusi alizovaa. Alizivaa yeye. Kichwani alivaa ile soksi nyeusi nayo. Alifanana kabisa na Ndula wa Ndulani.

Alitoka nje kwa mwendo wa kunyata, mlangoni alimkuta Zura, alimfungulia mlango Suto bila kumhoji chochote. Akidhani yule ni yule jamaa waliyemtuma, kashafanya walichomtuma.



Suto Sutani sasa akawa huru tena.

Lakini Suto alijua utapita msako mkali juu yake, na labda atakamatwa, lakini alidhamiria kulipa kisasi kwanza kwa watu waliomsababishia madhila yale, kabla hajakamatwa.

Alipofika mbele kidogo, alivua ile soksi usoni na kuitupa. Aliipekuwa mifuko ya ile nguo aliyovaa, katika mfuko wa mbele wa kulia wa suruali ile, alikutana na kitu akichokihitaji sana muda ule.

pesa. Zilikuwa shilingi laki mbili taslimu ndani ya mfuko wa suruali ile. Katika mfuko mwingine alikutana na kisu kirefu.

Sasa alifikiria aende wapi, akajifiche mkoani, ama abakie jijini Dar es salaam.

Mwishowe aliamua kubaki Dar es salaam, Mbagala ndio lilikuwa chaguo lake la kujihifadhi kwa muda, akisubiri sakata la kutafutwa litulie. Alijua kutokana na Mbagala kuwa na mchanganyiko wa watu wengi sana, itakuwa ngumu sana kukamatwa. Usiku wa manane alipanda daladala na kuelekea Mbagala.



**************



Mzee Sutani, alikuwa ni mfanya biashara maarufu wa viatu, katika soko la Karume.

Miaka 22 ilikuwa imepita tangu amtelekeze mama Suto kule Tabata, na mwanae kichanga.

Hadi sasa alikuwa hajui habari za mama Suto, wala mtoto wake Suto. Sasa alikuwa ameoa mke mwengine, na kuzaa nae watoto watatu.



Siku ya ijumaa, ilikuwa siku yenye pilikapilika nyingi sana kwa Mzee Sutani.

Jana yake siku ya alhamisi, alikuwa ametoka jijini Mbeya, kununua mzigo mkubwa wa viatu. Siku ile ya ijumaa asubuhi alikuwa na kazi ya kuusafirisha mzigo ule toka Mbagala Charambe hadi sokoni Karume. Kwa kuwa alikuwa na mzigo mpya, alifanya biashara nzuri sana siku ile.

Kutokana na kupanga vizuri mzigo wake, ili kesho yake aanze kuuza tu, alijikuta anarudi nyumbani kwake usiku wa manane, alipanda daladala iliyokuwa inaelekea Mbagala. Wakati anapanda daladala ile kuna mfanyabiashara mmoja alimwita kwa sauti kubwa

"Mzee Sutani, naona Leo biashara imefanyika kweli"

"Hamna Mzee Ngonyani.........."

Maneno mengine waliyoendelea kuongea wazee wale. Hayakusikiwa vizuri na abiria mmoja wa kike, aliyekaa siti moja na Mzee aliyeitwa kwa jina la Sutani. Neno Mzee Sutani lilirindima katika kichwa chake.

"Baba" alijisemea kimoyomoyo.

Suto Sutani, alikuwa katika daladala ile aliyopanda mtu aliyeamini kuwa ni baba yake, Mzee Sutani.

Hasira zikampanda Suto, aliamini baba yake ndio chanzo cha madhila yote yaliyomkuta. Suto alidhamiria kumuua baba yake usiku ule.



***********



Kule jela ilikuwa patashika, alfajiri iligundulika kwamba Mfungwa mmoja ametoroka, huku mwili wa mtu asiyetambulika, lakini amefariki ukikutwa katika selo ya Mfungwa aliyetoroka, Suto Sutani. Wakati Suto aliamini yule mvamizi alikuwa amezimia, kumbe la, Ndula alifariki kwa ile kabali ya nguvu aliyompiga usiku.

Lakini hakuna aliyeweza kukitegua kitendawili kile, Suto ametorokaje, na yule mtu ameingiaje, kitendawi walikuwa wanaweza kukitegua Beji na Zura. Lakini nao walijifanya hawaelewi kitu. Patashika ikawakumba askari wote waliokuwa zamu usiku wa siku ile. Mkuu wa Gereza la Segerea alikuwa mkali mithili ya mbogo. Lakini haikusaidia kitu, ukweli ulibaki palepale, Suto Sutani alikuwa ametoroka, na yule kijana alikuwa ameuwawa.



Asubuhi ya siku ile msako maalum ulianza, viliwekwa vizuizi katika njia zote kuu za kutoka nje ya Jiji la Dar es salaam, huku askari wote waliokuwepo katika vizuizi hivyo walikuwa na picha ya Suto mkononi. Kuhakikisha Suto hatoki nje ya mkoa wa Dar es salaam, lengo ni kumkamata akiwa hai au amekufa.



Beji na Zura, wao walikuwa hawaelewi kabisa nini kilitokea usiku ule, Zura ndio alibaki katika mshangao mkuu, hakuamini kabisa kama yule mtu aliyemruhusu kutoka ndani ya Gereza alikuwa Suto. Vibarua vyao sasa vilikuwa mashakani, pamoja na msako wa Polisi, nao waliweka msako wao wa siri wa kumsaka Suto, waliapa lazima wamkamate Suto na kumuua !



Wakati Polisi na kina Beji wakipanga hayo, Suto Sutani, sasa alikuwa katika gari pamoja na mtu aliyeamini ni baba yake wakielekea Mbagala. Mahali alipopachagua Suto kuweka maficho yake ya muda.

Bila Mzee Sutani kujua kama binti aliyekaa nae siti moja ni mwanae wa kumzaa mwenyewe, lakini sasa alikuwa ni kama mtoa roho kwake...

https://ift.tt/2TR5Sxj



Gari ilipofika Mbagala rangi tatu, Mzee Sutani alishuka kwenye gari, kwa nyuma akifuatwa na Suto Sutani. Alikuwa sasa akielekea stendi yanakopaki magari ya Mbagala Charambe.

Hakukuwa na gari hata moja, wala abiria pale stendi. Ulikuwa ni usiku mwingi sana. Magari yanayoelekea Charambe, ni tofauti na magari yanayofika katikati ya Jiji, yanayotembea saa ishirini na nne.



Suto alimfata baba yake kimya kimya. Akisubiri wafike sehemu muafaka ili atekeleze alichotaka kutekeleza.

Walipofika stendi, Suto akaona pale ndio mahali muafaka kwake. Mzee Sutani aligeuka nyuma, alishangaa kumuona mtu. Alijua yupo peke yake mahali pale. Kwa usiri mkubwa, Suto alikichomoa kile kisu toka katika zile nguo nyeusi alizovaa, na kumfata Mzee Sutani kwa mwendo wa taratibu, bila wasiwasi wowote.

Alimkaribia kabisa, Suto alimshika mkono yule Mzee kwa nguvu na kumgeuza kwa nyuma. Maana Mzee Sutani alikuwa amegeuza kichwa tu, kiwiliwili kilikuwa bado kinaangalia mbele.



"Naitwa Suto "

"Suto !"

"Unanikumbuka kumbe"

"Suto mwanangu, Suto Sutani ?"

"Nilikuwa mwanao, sasa siyo mwanao tena, ni adui yako, tusiongee sana kwa kifupi nimekuja kuitoa roho yako mbaya !"



Mzee Sutani alifadhaika sana, hakutegemea wala hakuamini kilichotokea. Ilikuwa ni kama yuko ndotoni, kukutana na mwanae usiku kama ule. Tena akiwa anatisha, na anatoa vitisho.

Mzee Sutani alikiona kile kisu kirefu alichokishika Suto. Mzee wa watu alianza kutetemeka.



"Kwanini ulimkataa mama yangu ?, kwanini ulinitelekeza nikiwa mdogo sana?"

Suto aliporomosha maswali mfululzo, lakini Mzee Sutani hakujibu hata swali moja.



"Baba"

"Nisamehe sana Suto" Alisema huku machozi yakimtoka.

"Nimekusamehe baba"



Suto alisema kwa kejeri.

Maana alisema maneno hayo huku akichomeka kile kisu kwa nguvu sana katika kifua cha baba yake mzazi, Mzee Sutani. Alimwacha yule Mzee akigaragara pale chini stendi, huku akiwa ameushikilia mpini wa kisu, kilichozama vizuri sana kifuani kwake.

Kwa haraka Suto alitokomea anakokujua yeye.



Asubuhi, Tanzania iliamka na habari kubwa mbili. Habari ya kwanza ni kutoroka kwa mahabusu hatari sana, na mtuhumiwa wa mauaji gerezani, na habari ya pili ni kuuwawa kwa Mzee mmoja kwa kisu huko Mbagala rangi tatu. Hakuna aliyehusianisha matukio hayo mawili, wote walihisi ni matukio mawili yasiyo na uhusiano wowote. Jeshi la Polisi, chini ya Inspekta Jasmine, likaingia katika michakamichaka mengine mipya.

Mchakamchaka wa kumsaka Suto Sutani, na mchakachaka wa kumsaka muuaji wa mzee huko Mbagala rangi tatu.



Asubuhi ya siku hiyo ilimkuta Veronica Baro, mwandishi mahiri wa gazeti pendwa la Dumizi, Mbagala. Alienda kupeleleza undani wa kifo cha yule Mzee Mbagala. Ili aandike habari yenye uhakika au hata kupata picha mnato za kuweka katika gazeti lake, ili kuwepo na uhalisia na kuvutia wasomaji.

Ni mwandishi Veronica Baro, ndiye aliyeitambulisha jamii ya Tanzania kwamba yule Mzee aliyeuwawa Mbagala rangi tatu alikuwa ni baba mzazi wa mahabusu aliyetoroka usiku wa siku ile. Huku akiweka wazi maoni yake kuwa kifo cha yule Mzee kinahusiana na mahabusu huyo moja kwa moja.

Akimaanisha Suto ndio muuaji !. Msako wa Suto sasa ulipamba moto maradufu....



 Suto Sutani alikuwa Gongo la mboto. Alishaona Mbagala siyo sehemu salama tena. Alirudi tena stendi na kupanda gari linaloelekea Mbagala usiku uleule, na sasa alikuwa kwenye nyumba ya kulala wageni huko Gongo la mboto.

Akiwaza jinsi maisha yake yaliyobadirika ghafla, toka Suto mwema, Suto mstaarabu, Suto mwenye tabia njema mpaka kuwa Suto katili, Suto asiyeogopa chochote, Suto muuaji !

Aliiumalizia usiku ule wenye kumbukumbu mbaya kwake akiwa pale, usiku wa kwanza uliofanya aue mtu, tena baba yake mzazi. Alilala huku masikio yake yakiwa nje, Alikuwa makini sana. Hakutaka kabisa kukamatwa na Polisi kabla hajalipa kisasi kwa watu waliomkosea na kumletea matatizo makubwa hapa duniani.



************



Kwa upande wa Polisi ilikuwa shughuri pevu. Walisaka sana, walipekua sana lakini walikuwa hawajagundua kabisa Suto kaelekea wapi, walitafuta hasa huko Mbagala, Wananchi wa Mbagala waliteseka sana kutokana na msako huo, kila nyumba ilipekuliwa kumsaka Suto Sutani lakini hawakufanikiwa kumwona Suto. Ilikuwa kama wanamtafuta mtu ambayo hakuwahi kuwepo kabisa katika sura ya dunia.



Inspekta Jasmine kichwa kilikuwa kinamuuma. Sasa hakujua kabisa nani mwema na nani mbaya katika mkasa huu. Mkasa alioupa jina la 'Mkasa wa. Suto'.

Mkasa ambao ulisababishwa na penzi, penzi kati ya Suto Sutani na Bruno. Penzi lililoanza kama mas'hara, likashamiri ghafla kama uyoga, sasa penzi hilo lililokuwa na ndoto nyingi sana, ndoto za kuishi pamoja kama mke na mme. Penzi lililopigwa sana vita na wazazi wa Bruno siku ya kwanza tu lilipoanza, na sasa penzi hilo limegeuka kuwa chungu. Penzi Chungu kwa Suto Sutani.



Inspekta Jasmine alikubari, alikubari kushindwa kutatua utata wa mkasa huu, mkasa uliosababishwa na penzi. Aliamua asubuhi aende kwa mkuu wake wa kazi kuomba atolewe katika kuipeleleza kesi hii, na apewe mtu mwengine. kwa mara ya kwanza Inspekta Jasmine alishindwa kumtia mikononi mhalifu, kwa mara ya kwanza Inspekta Jasmine alikubari kushindwa. Maana aliona tangu kapewa kazi ile, hajapiga hatua yoyote ya kuitatua kesi ile, huku watu wakiendelea kuuwawa. Bila kumjua adui halisi ni nani.

Alijua atakumbana na maswali mengi toka kwa mkuu wake wa kazi, na pengine angedharauliwa sana na kukaripiwa, lakini uamuzi wake ulibaki palepale, aliamini kuwa kesi hii ilikuwa imemshinda!



**************



Asubuhi na mapema Suto Sutani aliamka kule nyumba ya kulala wageni, Gongo la mboto. Alioga vizuri na kutoka nje ya nyumba ile ya kulala wageni iliyokuwepo mtaa wa uswahilini sana. Kama bahati alikutana na kijana mmoja karibu tu na 'guest' ile akiuza visu. Alinunua visu kadhaa, maalum kwa ajili ya kazi iliyokuwa mbele yake.



Baada ya kununua visu, alitembea akielekea ilipo barabara kuu. Alikuwa anatafuta sehemu wanakouza magazeti.

Aliyapata.

Aliwakuta watu wengi sana walikuwa wamejaa kwenye meza moja ndogo ya magazeti iliyokuwa kandokando ya barabara. Alijipenyeza katikati ya kundi lile dogo la wanaume, macho yake yalitua gazetini.



"Suto muuaji auwa tena Mbagala !"



Hayo yalikuwa maneno yaliokozwa kwa wino mwekundu, mbele kabisa katika gazeti pendwa la Dumizi.



Suto alistuka sana kuona kichwa kile katika gazeti la Dumizi, alilinunua gazeti lile na kurudi nalo katika guest yake aliyofikia kwa mwendo wa haraka sana. Huku akiwaacha watu wakimjadiri muuaji hatari Suto Sutani pale katika meza ya magazeti, bila kujua kwamba Suto mwenyewe walikuwa nae pale muda mfupi uliopita.



Suto alifika chumbani kwake, alikuwa amevaa miwani na kofia. Alivua miwani kisha akavua kofia kubwa aliyovaa kichwani. Akakaa kitandani na kuanza kuisoma ile habari iliyoandikwa kwa usanii mkubwa na mwandishi Veronica Baro.https://ift.tt/2TR5Sxj

Aliisoma habari ile mpaka mwisho, alisoma jinsi mwandishi alivyomhusisha katika mauaji yale ya mwanzo, ya watu watatu kule Tabata. Pia mwandishi akimhusisha na mauaji mapya yaliyotokea Mbagala rangi tatu alfajiri. Kwanza suto alishangaa sana uweledi wa mwandishi yule, kuandika habari ya upande mmoja tu kwa uhakika mkubwa bila kutoka kujua ukweli toka upande wa Mtuhumiwa. Pia Suto alishangaa sana uharaka wa kuchapa habari wa gazeti lile. Alifanya mauaji saa kumi alfajiri, saa mbili asubuhi alijisoma katika kurasa ya mbele.



"Eti Veronica Baro, una uhakika mimi niliwauwa wale vijana, una hakika ndugu mwandishi? Nitakutafuta Veronica unijibu maswali yangu, wewe ulikuwepo usiku ule? Ulinishuhudia mimi nikishika lile shoka na kulizamisha kifuani kwa yule kijana? Lazima unijibu hayo maswali Veronica, ukishindwa kujibu nitakuuwa Veronica, mimi umeninadi kama Suto muuaji, nitakuthibitishia sasa uuaji wangu!" Suto alikuwa anaongea na lile gazeti kama linamsikia vile. Au unaweza sema gazeti lile lilikuwa ndiye Veronica Baro mwenyewe.



Suto alilichukua lile gazeti la Dumizi. Akalishika kwa mikono yake yote miwili, na kulichana kwa hasira vipande vidogovidogo sana. Akavitawanya kwa fujo mle chumbani.



"Veronica Baro, umejiongeza mwenyewe katika orodha ya watu wangu niliopanga kuwauwa, orodha ya kifo, nitakuua Veronica !" Suto alikuwa anaongea na vile vipande vya gazeti sasa.



Suto alijiliza kitandani chali, akiliangalia bati chakavu la gesti ile ndogo.



"Maisha yamenibadirikia ghafla sana, leo hii nimekuwa natafutw....." Hakumalizia kauli yake.

Mlango wa chumba chake uligongwa kwa nguvu sana. Suto moyo ulimpiga kwa nguvu. Akainuka pale kitandani.



Ngo...Ngo.. Ngo...

Mlango uligongwa tena kwa nguvu zaidi.



"Askari" alijisemea mwenyewe kimoyomoyo.



Suto alikuwa anatetemeka mle chumbani kama kulikuwa kuna baridi kali. Aliona mwisho wake umefika, umefika bila ya kutimiza kisasi chake kwa watu walimsababishia madhila yale makubwa hapa duniani.



"Siendi kufungua mlango" alijisemea tena kimoyomoyo.

Ngo....Ngo....Ngo !

Mlango uligongwa tena kwa sauti kubwa zaidi.

Suto alilivuta begi lake lililokuwa uvunguni mwa kitanda.

Alitoa kisu !

Alikishika imara kwa mkono wake kushoto, alielekea taratibu kwa tahadhari kubwa sana pale mlangoni !

Kilikuwa ni miongoni mwa vipindi vigumu sana kwa Suto. Aliufikia mlango, alishika funguo kwa mkono wa kulia, akaanza kuuzungusha kuelekea kulia, mlango ulianza kufunguka taratibu, Ghafla ukasukumwa kwa nguvu.



Hamadi! Kumbe alikuwa Mhudumu wa Guest ile.

Mhudumu yule wa kiume wa nyumba ile ya kulala wageni aliingia kwa kasi sana, akiwa na gazeti la Dumizi mkononi. Sasa alikuwa anatazamana na Suto uso kwa uso. Macho ya Suto yalitua katika lile gazeti. Akajua kuna hatari!



"Bila shaka ni Suto Sutani"

Mhudumu alisema kwa dharau kidogo. Suto aliuficha kwa nyuma mkono wake wa kushoto, akificha kile kisu.



"Suto umefanya hapa ndio kichaka wauaji, ufanye mauaji huko na kuja kujificha hapa" Mhudumu alisema huku akibonyazabonyaza simu yake, bila shaka akitafuta namba fulani za kupiga.

Suto alijua licha ya kuvaa kofia na miwani lakini yule Mhudumu alikuwa ameshamgundua. Akamwangalia yule mhudumu huku akisikitika, Akijua Mhudumu kajiongeza mwenyewe kwenye orodha isiyomhusu, orodha ya kifo ! Suto hakujibu, Suto alitenda.

Kwa kasi ya haraka aliutoa ule mkono wenye kisu kule nyuma, na kwa kasi ileile na nguvu zake zote alididimiza kile kisu katika tumbo pana la yule Mhudumu, Mhudumu alishikwa na mshangao sambamba na maumivu, hakutegemea kama Suto ana kisu, hakutegemea kama Suto atafanya kitendo kama kile kwa muda ule na kwa kasi ile. Mhudumu alishikilia tumbo lake lililobaki na jeraha baya sana. Mhudumu yule alikufa akiwa anashangaa uwezo wa Suto katika uuaji.



Suto Sutani aliona pale siyo sehemu salama tena kwake. Alichukua begi lake dogo la visu, alipita mlango wa nyuma wa nyumba ile ya kulala wageni na kutokomea. Akiuacha ndani mwili usio na roho wa Mhudumu yule mbea.



***************



Inspekta Jasmine alikuwa ofisini kwake ndani ya makao makuu ya Polisi, Posta. Mara simu ya mezani iliita.



"Hallo Afande"

"Hallo Afande"

"Yametokea mauaji Gongo la mboto"

" Saa ngapi?"Inspekta Jasmine aliuliza kwa fadhaha.

" Kama masaa matatu yaliyopita"

"Naelekea huko, ramani sahihi ya nyumba yalikofanyika mauaji utanipa njiani"

"Sawa Afande"

Simu ikakatwa.



Inspekta Jasmine alichukua gari na askari watano, walielekea Gongo la mboto.

Waliwasiri Gongo la mboto, na kwa msaada wa yule askari aliyekuwa anakaa jirani na ile Guest, walifika hadi katika nyumba ya wageni yalipotokea mauaji. Nyumba aliyokuwepo Suto Sutani, adui namba moja wa Inspekta Jasmine masaa matatu yaliyopita. Walikuta kundi dogo la watu.



Inspekta Jasmine na wale askari watano waliingia moja kwa moja ndani ya nyumba ile ya kulala wageni. Walimkuta Mhudumu pale kaunta na yule askari aliyepiga simu. Askari aliyeamini kuwa muuaji kwa kadri ya sifa alizopewa na Mhudumu ni Suto, na kuamua kumpigia moja kwa moja Inspekta Jasmine.



"Habari yako"

"Nzuri Afande"

"Meneja yuko wapi"

"Hapana Meneja hapa nipo mimi tu"

"Hebu nielezee mazingira ya tukio"

"Tuliamka asubuhi vizuri na Mhudumu mwenzangu wa kiume anayeitwa Jerry, baada ya kufanya usafi wa nje, Jerry aliniaga kuwa anaenda kununua gazeti, baada ya muda mfupi alirudi anakimbia na kuelekea uwani, mimi nilidhani kashikwa na tumbo la kuhara, kwahiyo anakimbilia chooni. Yalipita masaa kadhaa Jerry sikumuona. Ilivyofika saa nne asubuhi, muda wa wateja kukabidhi vyumba. Nikaanza kupita chumba kimoja baada ya kingine. Nilipofika chumba namba nane niliukuta mlango ukiwa wazi, nilipoingia ndani, ndipo nilikutana na maiti ya Jery sakafuni......Jerry aliuwawa kwa kuchomwa kisuuu oooooh masikini Jery" Mhudumu alisimulia kwa uchungu na simanzi, huku machozi yakimtiririka. Inspekta Jasmine hakujari kabisa kilio cha Mhudumu yule. Pamoja na kilio chake aliendelea kumhoji.



"Uliandika jina la mteja aliyepanga katika chumba namba nane?"

"Ndio afande"

"Anaitwa nani?"

Mhudumu akipekua kitabu harakaharaka.

"Ana...anaitwa Susa Zamani"



https://ift.tt/2TR5Sxj

"Suso Zamani?"

"Ndio afande , hili hapa" Mhudumu alisema huku akimuonesha Inspekta lile jina kwa kidole katika daftari la wateja .

"Susa Zamani" Inspekta Jasmine alijisemea kwa sauti aliyojisikia mwenyewe.

Inspekta Jasmine alilipokea lile daftari, kuliangalia vizuri lile jina.

"Susa Zamani "

"Ni nani aliandika hapa ?" Inspekta Jasmine aliuliza swali huku akimwangalia usoni yuke Mhudumu.

"Niliandika mimi, baada ya kutajiwa jina na mteja mwenyewe" Mhudumu alijibu akiwa na hofu kidogo.

"Alikwambia anaitwa?" Ghafla Inspekta Jasmine aliuliza tena.

"Susa Zamani" Safari hii Mhudumu alijibu kwa uhakika zaidi.

"No ni mwanaharamu huyo, ni Suto Sutani !" Inspekta Jasmine aliropoka.

Yule Mhudumu kusikia jina hilo alistuka sana, na kuanza kutetemeka, nani aliyekuwa hajawahi kulisikia jina la Suto Sutani ? Mwanamke aliyeaminika kuwa muuaji, mwenye roho mbaya. Aliyeweza kutoroka katika kuta nne nene za Gereza imara la Segerea.

"Sutoooo"

"Bila shaka, yupoje?"

"Hata sikumuona vizuri muonekano wake, mara nyingi alikuwa anavaa miwani na kofia. Ila ni maji ya kunde na kwa urefu mnalingana na wewe"

"Huyohuyo, ni Suto, bado anaendelea kuuwa mwanaharamu, ana dhamira gani lakini ?" Inspekta Jasmine aliuliza swali, hakukuwa na wa kumjibu.



Inspekta Jasmine na wale askari wengine walienda katika chumba namba nane, chumba alichokuwa Suto Sutani muda mfupi uliopita. Zaidi ya mwili wa yule Mhudumu uliolala bila uhai pale sakafuni, hawakupata lengine la maana. Suto hakuacha alama yoyote mle chumbani.



Inspekta Jasmine aliomba msaada wa kuongezewa Polisi. Polisi ambao walijitahidi kumsaka Suto katika Guest na Baa zote za Gongo la mboto, lakini Suto Sutani hakuonekana. Gongo la mboto iligeuzwa nje ndani, hawakuambulia kitu. Suto Sutani alifanya mauaji na kutoweka kwa mara nyingine.



Asubuhi ya siku iliyofuata ilimkuta Inspekta Jasmine mbele ya meza ya Mkuu wa upelelezi na makosa ya jinai kanda ya Dar es salaam. Lililompeleka ni moja tu, na la aibu. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya kulitumikia jeshi la Polisi, Inspekta Jasmine alikubali mbele ya Mkuu wake kuwa ameshindwa kazi ya kumkamata muuaji. Ilikuwa aibu kwake, aibu kubwa sana kwa jeshi la Polisi pia.



"Inspekta Jasmine"

"Ndio mkuu"

"Unasema umeshindwa kazi ya kumkamata muuaji ?"

"Ndio Afande"

"Nani ataweza sasa?"

"Naomba uchague askari mwengine Mkuu"

"Hilo linawezekana, ilaa naomba unikabidhi mkanda na kofia, hivyo ni mali ya jeshi la Polisi"

"Sijakuelewa Mkuu"

"Umeshindwa kazi Inspekta, sasa kwanini tulikupeleka CCP Moshi? tulikupeleka Moshi ili uje kushindwa kazi?"

"Sina maana nimeshindwa kazi...."

"Sasa umeshindwa nini, nitajie kazi kuu za askari"

"Lakini Mku...."

"Lakini nini afande! Naomba ukaandike barua ya kuacha kazi leo. Kesho asubuhi niikute mezani kwangu !"

Hali ilikuwa tete kwa Inspekta Jasmine.

"Basi nisamehe Mkuu, nitamsaka Suto !"

"Nakupa wiki moja, Suto awe amekamatwa, la sivyo ombi lako la leo, litakuwa limepita bila kipingamizi"

"Ombi gani Mkuu?"

"Ombi lako la kuacha kazi !"

"Sijaomba kuacha kazi mkuu" Inspekta Jasmine maji sasa yalikuwa yanamzamisha.....



"Ulikuja kufanya nini sasa hapa ofisini?"

"Naomba nisamehe Afande"

"Nakupa wiki moja Suto awe amekamatwa. Nitakupa msaada wowote unaoutaka kwa kipindi hiko, nimemaliza, waweza kwenda "



Inspekta Jasmine alipiga saluti na kutoka nje akiwa na hasira zisizo na kifani.



***********



Beji na Zura walipata kashikashi kubwa kazini kwao, baada ya uchunguzi walionekana wao ndio wazembe kazini. Na wote walifukuzwa kazi. Ilikuwa ni huzuni sana kwao, huzuni hiyo ilizidisha hasira kwa dada wale wawili, sasa walirudi mtaani wakiwa na hasira isiyo na kifani dhidi ya Suto Sutani. Waliapa lazima wamkamate Suto, lazima wamuuwe Suto Sutani.



***********



Wakati Inspekta Jasmine akigomewa na Bosi wake kuhusu Suto Sutani, na Beji na Zura wakifukuzwa kazi baada ya kuzembea kazini na Suto Sutani kutoroka gerezani.

https://ift.tt/2TR5Sxj

Suto Sutani, alikuwa nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam. Alikuwa amejificha katika kibanda kidogo katika kijiji cha Mwanambaya, kilichopo wilaya ya Mkuranga. Alijificha katika kibanda hicho kidogo tangu alivyofanya mauaji kule Gongo la mboto. Alipanda daladala inayoelekea Mbagala tena kutokea kule Gongo la mboto, alipofika Mbagala alipanda gari linaelekea Mkuranga na kushuka Mwanambaya. Hakuna mtu aliyemtambua katika magari aliyopanda. Bahati ilikuwa upande wake, alopofika Mwanambaya alikikuta kibanda dhaifu cha nyasi na kujihifadhi humo. Kibanda kilichohamwa na wenyewe kwa kuwa kipindi hiko hakikuwa kipindi cha kilimo.



Jiji Dar es salaam ilikuwa patashika. Baada ya kumkosa Suto Gongo la mboto, Inspekta Jasmine aliomba msaada kwa Bosi wake. Aliomba kuweka askari wa kutosha barabarani ili magari yote yawe yanakaguliwa kumtafuta Suto, nyumba za wageni zote zipekuliwe Dar es salaam nzima kumtafuta Suto, lakini Suto hakupatikana, Suto hakuwa Dar es salaam, Suto alishafika Mwanambaya kabla ya msako wa katika magari haujaanza.

Kutoonekana kwa Suto kulimuumiza sana Inspekta Jasmine. Aliona kazi yake inakaa rehani, kwa ajili ya Suto Sutani, hakutaka kabisa kukubali kushindwa, lakini alielekea kushindwa.



************



Wakati Suto Sutani akiwa katika kibanda dhaifu huko Mwanambaya, katika hoteli moja huko Mwenge kulikuwa na kikao. Kikao kilichoitishwa na mama Bruno, katika kikao hiko pia walikuwemo Manka, Dungu, Banda, Beji, Zura, Veronica Baro, Banda na wanaume wengine wawili. Kilikuwa kikao cha watu kumi wenye dhamira ya mbaya ya kumuua Suto Sutani.



"Habari zenu jamani" Mama Bruno alisalimia.

"Nzuri" wote waliitikia.

"Hapa tuna agenda kuu moja tu, hakuna kufungua kikao wala kufunga kikao, agenda ni kumuua Suto Sutani kwa njia yoyote ile na haraka iwezekanavyo, kikao hiki ni kwa ajili ya kupanga mipango kujua tunaanza vipi na tunamaliza vipi. Lakini tuhakikishe Suto Sutani anakufa !" Mama Bruno alisema kwa kirefu.

"Mpango siyo kumuua Suto, mpango kwanza ni kujua Suto Sutani yupo wapi kwa sasa, Suto Sutani amekuwa mwiba mkali sana, jeshi la Polisi lenyewe linahaha usiku na mchana kumsaka Suto. Sasa sisi tunapanga kumuua, tutamuonea wapi, hapa tujipange kumtafuta kwanza, ili tujue anaishi wapi" Manka nae alichangia.

"Ni kweli kabisa Manka. Kujua Suto Sutani yuko wapi ni kazi ngumu kuliko tunavyofikiria, jeshi la Polisi lenyewe limeshindwa kuvumbua kitendawili hiko mpaka leo wanahaha kumsaka Suto, mama Bruno kama unadhani kazi ya kumuua Suto ni rahisi, unajidanganya mama, Mimi ndiye naziona nyuso za maaskari zilivyo na woga, Inspekta Jasmine mwenyewe tunayemuamini wananchi wote, huku nchi ikimtegemea, anastuka ukimtajia jina la Suto Sutani, Veronica mimi najuta kujiingiza katika kadhia hii, pesa zenu haramu zimeniponza, kuitumia vibaya kalamu yangu kumeniponza, sijui... ."

"Nyamazaaaaa...huu siyo wakati wa kulaumiana, siyo wakati wa kulalamika, kama pesa ushachukua, kama kalamu yako ushaitumia vibaya, lakini ushukuru bado upo kazini, bado ni mwandishi wa gazeti la Dumizi, sisi tumekosa kazi Veronica, kutokana na Suto, kutokana na pesa unazoziita haramu. Cha muhimu hapa ni kutafuta namna ipi tunampata Suto Sutani na kumuua, basi !" Beji aliyasema maneno hayo kwa hasira. Na wengine wote walitikisa vichwa, ishara ya kukubaliana nae.

"Eeh tunafanyaje sasa" Dungu kwa mara ya kwanza alichangia.

"Naona mnagombana sana, kumkamata Suto na kumuua siyo tatizo kabisa. Suto atamatwa na atauwawa!. Kumkamata Suto ni kazi ndogo sana kwa Kurwa na Doto. Kwakuwa mmetushirikisha katika hili hakuna litakaloshindikana. Mnastaajabu Polisi kushindwa, Polisi hawana akili za kutufikia sisi, Kulwa na Doto" Kurwa kijana mpya katika kikao kile alisema kwa kujigamba.

Sasa kikao kilipata uhai, Kurwa alirejesha hali ya kujiamini kwa wanakikao.

"Tunaanzaje sasa msako wetu?" Dungu aliuliza.

"Mwelekeo wetu unategemea mwelekeo wa Polisi, lazima tujue Polisi wanahisi Suto yuko wapi,nasi tunaelekea huko. Kwa hilo tunategemea sana mchango wako Veronica, ukaribu wako wa Polisi utatusaidia sana. Lazima tuhakikishe Suto anakufa kabla hajaingia mikononi mwa Polisi, Polisi wakimkamata tu, atakutajeni ninyi, nanyi mtaangia matatani. Lazima tuwe makini, na tufanye kazi kwa haraka mara mbili au tatu zaidi ya Polisi. Kulwa alieleza kwa kirefu.

" Tunawategemea sana jamani" Manka alisema kwa sauti yenye uwoga.

"Usijari, tutafanya kazi mliyotutuma kwa haraka sana"



Mama Bruno alifunga kikao, kila mtu akiwa na matumaini mapya, huku wakisuburi taarifa toka kwa mwandishi Veronica Baro, ili Kurwa na Doto wakafanye kazi.....



Usiku ulimkuta Suto Sutani akiwa Mwanambaya porini. Suto alikuwa anajisikia njaa. Hakukuwa na chakula chochote kule porini alikokuwa, ilimlazimu aende kijijini Mwanambaya aone jinsi ya kupata chochote cha kutia tumboni. Lakini kwenda kula kule kijijini ilimaanisha kuukaribia mkono wa adui. Suto alijua sasa sura yake ilikuwa maarufu sana ndani ya Tanzania nzima. Hakutaka kabisa kujidanganya eti kwa kuwa ni kijijini basi watakuwa hawajui lolote kuhusu msako wake, pamoja na yote hayo Suto hakuwa na jinsi. Ilikuwa ni lazima aende kijijini kula.



Alitoka taratibu toka katika kile kibanda, alibeba begi lake dogo lililojaa visu, na kuifuata njia nyembamba iliyokuwa inaelekea kijijini Mwanambaya.

Baada ya mwendo mrefu kidogo, alianza kuona ishara ya mwanga, ishara ya uhai, vilikuwa vibatari. Pamoja na muda kutaradadi, lakini baadhi ya watu wa kijiji kile walikuwa bado hawajalala. Hasa wafanyabiashara ndogondogo.

Suto alisogea taratibu, huku umakini wake ukiongezeka kadri ya anavyopiga hatua kukikaribia kijiji.

Hatimaye alifika kijijini.



Suto alimwona Mzee mmoja akiuza mahindi ya kuchoma pembeni kidogo na wenzie, alimfata kwa mwendo wa taratibu.

https://ift.tt/2TR5Sxj

"Habari Mzee"

"Nzuri, hujambo" Mzee alijibu huku alimwangalia Suto usoni.

"Suto akainama kidogo, ili asiangaliane na yule mzee moja kwa moja.

" Nataka mahindi matatu Mzee" Suto alisema huku akiiweka kofia yake vizuri .

"Mia tisa" Mzee alijibu bila kumwangalia Suto safari hii.

Suto alinunua mahindi, na kuifata ile njia aliyotokea muda mfupi.

Yule Mzee alikuwa ni Mzee maarufu sana Mwanambaya. Umaarufu wake ulitokana na sababu kuu mbili, kwanza ni kuuza mahindi na umaarufu wake wa pili ni kwa ajili ya kusoma magazeti. Pale alivyomtazama tu Suto kwa mara ya kwanza, aligundua ndiye muuaji anayetafutwa. Aliiona sana sura ile kwenye magazeti na sasa alikuwa ameshaizora. Akavuta gunia lake la mahindi. Akatoa kipande cha gazeti la Dumizi.



"Ndiye muuaji !"





ITAENDELEA






USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.