NI KWA NAMNA GANI UNAYAJUA MAPENZI?
Ukiulizwa kama unajua mapenzi na unajibu unajua, huwa unaamini unajua mapenzi yapi? Kivipi, na kwa namna gani?
Wapo wanaosema wanajua mapenzi, wakimaanisha wana ufundi mkubwa kitandani. Ni vizuri sana, ila maana kamili huwa siyo hiyo. Unaweza kuwa hodari na maridadi sana kitandani na bado ukabaki kuwa hujui mapenzi.
Mapenzi ni jumla ya matendo yote. Namna unavyoongea na mpenzi wako, unavyomjibu, unavyotaka jambo kwake, huko ndiko kujua mapenzi.
Pale kitandani ni sehemu ndogo katika ulingo wa mapenzi.
Na abadani haiwezi kutoa tafsiri ya jumla ya kujua mapenzi.
Ukiwa maridadi sana kitandani na huku kwingine ukawa hovyo, tutakuita unajua sana kufanya ngono.
Ili ujue mapenzi inabidi mpenzi wako ajisikie fahari kuwa na wewe karibu kila dakika.
Ujue kuongea naye vizuri. Ujue kudai haki yako katika namna inavyopaswa na pia ujue namna ya kumfanya akasahau madhila yote ya kimaisha kwa uwepo wako kwake.
Ni utani kusema unajua mapenzi kwa sababu tu, mkiwa kitandani unamtoa jasho.
Kitandani sawa, ila vipi katika kauli zako?
Vipi katika usafi wa mwili na nyumba yako?
Mwanamke anayejua mapenzi ni yule anayejua kupangilia vizuri chumba chake kwa ajili ya mumewe.
Yule ambaye akiwa na mume wake anamfanya asitamani hata kwenda maskani kupiga soga.
Mume wake akiwa na tatizo, anamfanya ajisikie ahueni kwa maneno yake matamu na vitendo vyake vya kichokozi vya kujaza faraja na raha katika nafsi ya mhusika.
Wewe unajisifu unajua mapenzi wakati mumeo anaona zaidi fahari kukaa maskani kuliko nyumbani kwake kwa kero ya maneno yako!
Unasema unajua mapenzi wakati hujui namna bora ya kuongea na mpenzi wako? Mapenzi gani hayo?
Mapenzi si kitendo kimoja. Ni jumla ya kila kitu unachomtendea mwenzako.
Ukiwa msafi sana ila kitandani huna kitu, jua kuna walakini mahali.
Ukiwa msikivu sana ila si msafi inavyopaswa, jua kuna kasoro sehemu.
Wewe unajua mapenzi?
Ni kweli katika chumba chako mumeo anaona fahari kuwa na wewe?
Ni kweli mkeo akikuona unatoka kazini anafurahia uwepo wako?
Au zile kero na shida za ofisini zote unampatia yeye?
Kama umegombana kazini kwako basi nyumba nzima wataipata.
Hapa sio tu utakuwa hujui mapenzi, ila pia hata akili yako itakuwa na tabu.
Ni kwa namna gani mabaya yaliyokutokea kazini yawe fimbo ya kuwaadhibu wasiohusika na bado ujione uko timamu akilini.
Familia ni kitu cha thamani sana, haifai kuwa sehemu ya kuipa mizigo na mateso yasiyowastahili.
ITAENDELEA
No comments: