Mgogoro wa Ardhi wamtesa mjasiriamali
Na Ferdinand Shayo, Arusha.
Mgogoro wa Ardhi katika mtaa wa Kirika B kata ya Osunyai Wilaya ya Arusha mjini umezua sura mpya na kuleta adha kubwa kwa mjasiriamali Bi.Flora Rona ambaye yuko katika hatua za ujenzi wa Kiwanda kidogo cha kutengeneza dawa za tiba asili ya miti shamba ikiwa ni kuitikia wito wa serikali wa kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa.
Flora Rona akizungumza na Waandishi wa habari nje ya jengo hilo alisema kuwa anakabiliwa na changamoto ya mipaka ya jengo hilo ambalo anatarajia kuanzisha kiwanda ambapo amekua akikwama katika umaliziaji wa jengo hilo kutokana na jirani yake aliyejulikana kwa jina moja la Musa kudaiwa kujenga ukuta ambao umeingilia eneo la mjasiriamali huyo.
Alisema kuwa mafundi walipata shida kuchapia kuta za nyumba hiyo kutokana na ukuta huo kuwabana licha ya kukubaliana kuacha mita kadhaa kwa ajili ya hifadhi ya kumwaga maji ya mvua lakini bado anadai jirani huyo alikaidi agizo hilo la Viongozi wa serikali ya mtaa.
“Namuomba Raisi Magufuli asikie kilio chetu wajasiramali tunaojitaidi kujikwamua kiuchumi lakini tunakwamisha na migogoro kama hii inapaswa ipatiwe ufumbuzi” Alisema Flora.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Osunyai Ashura Yusuph alipohojiwa kwa njia ya simu amekiri kuwepo kwa malalamiko hayo na kudai kuwa walishatatua mgogoro huo na kuamuru ukuta huo uliokua umepinda unyooshwe ili Bi.Flora aweze kufanya ujenzi bila kubughudhiwa na hilo lilifanyika .
Ashura alisema kuwa walishauri kuwa iwapo pande zote mbili hususan Bi.Flora hajaridhika na maamuzi yaliyotolewa anaweza kuandikiwa barua na kuwasilisha suala hilo katika baraza la Ardhi lakini hilo halikufanyika ila Flora amelifikisha jambo hilo katika Kamati ya Maridhiano na Usuluhishi wa migogoro ya ardhi Wilaya ambapo suala hilo lipo kwa sasa na pande zote mbili zimetakiwa kuwasilisha mikata ya umiliki wa ardhi zao” Alisema Ashura
Mkurugenzi wa Shirika lisilokua la kiserikali la Gola Foundation Elisha Maghembe alisema kuwa wamekua karibu na mjasiriamali huyo ambaye kwa sasa yuko katika mpango wa kufungua kiwanda chake ila mgogoro huo umekua ukimuathiri hivyo utatuzi huo utawasaidia kukua kiuchumi.


No comments: