KISA CHA TAJIRI ALIYEKUFA MASIKINI NA MAGOFU YAKE!

Image may contain: 1 person, standing
“Wanawake wapo wengi hata akiondoka leo kesho naweza kwenda kutafuta na kuoa mwingine!” Juma alimuambia Mama yake kwa hasira, Mama yake alienda kumtembelea na kukuta wanazozana na mpenzi wake ambaye walishakua kwenye mahusiano kwa muda wa miaka mitano, walikua na mtoto mmoja. Juma alidhamiria kumuacha, alimuambia kukusanya vitu vilivyo vyake kuondoka.

Mama yake alitaka kuongeana naye, Juma hakutaka kuongea na Mama yake aliondoka kwa hasira. Kuona hivyo alimfuata Aziza mpenzi wa Juma ambaye kila siku alikua akiwasisitiza wafunge ndoa lakini mwanae alikua anapiga kalenda tu. Alimuuliza ndipo yule binti alimuambia kuwa alikua amechoka, anampenda lakini mwanae hapendeki na mzozo ule ulitokana na ukweli kuwa kafumania meseji za mwanamke mwingine katika simu yake.

Mama yake alikua anaondoka lakini alikaa na kumsubiri mwanae, aliporudi alimuomba kuongea naye, alimtoa pale nyumbani na walipokua wakiongea Juma alikua akirudia kauli kuwa yeye hababaishwi na wanawake kwani anaweza kuoa mwingine wakati wowote. Mama yake alimuangalia na kumpa kisa kimoja cha tajiri aliyekufa masikini. Alianza kwa kumuambia kuwa hapo zamani za kale kulikua na tajiri mmoja ambaye alikua na hela nyingi lakini alishindwa hata kujenga nyumba moja ya kuishi na kufa masikini.

Alikua akiishi barabarani kama vile ombaomba hata alipokufa alikosa mtu wa kumzika. Juma alimuuliza ilikuaje kama alikua na pesa akashindwa kujenga nyumba? Mama yake alimjibu, huyu tajiri tatizo lake alikua na tamaa sana, kwakua alikua na pesa nyingi aliweza kununua viwanja vingi sana. Lakini kila akianza kujenga nyumba kabla hata ya kuezeka bati anachoka, anaona nyumba aliyokua akijenga ni mbaya hivyo kutamani nyumba nyingine.

Anaona nyumba nyingine nzuri na kuitamani, anawaza kuliko kuendelea na hii ngoja nijenge nyumba nyingine katika kiwanja kingine ambayo itakua nzuri zaidi. Lakini alipofanya hivyo kabla ya kumalizia aliona ramani mpya na kuitamani, hapo pia alitaka kujenga tena, hivyo mpaka anazeeka alikua na nyumba nyingi sana ambazo zote hazijamalizika, hakua na sehemu ya kukaa, pesa zilimuishia na nguvu kumuishia.

Mwisho wa siku yule tajiri alikufa masikini. Juma alishangaa lakini hakumuelewa ndipo Mama yake alimfafanulia. Alimuambia “Mwanangu mwanaume ni kama yule tajiri na mwanamke ni kama kiwanja. Kuna viwanja vingi sana huko mjini na kama ni tajiri unaweza kununua viwanja vingi utakavyo, mwanaume unaweza kuwa na wanawake wengi utakavyo. Lakini mwanangu kama hutachagua kiwanja kimoja na kujenga basi hutakuja kupata nyumba.

Hapa namaanisha kua kama hutachagua mwanamke mmoja ukamuoa na kumpenda basi hutakuja kupata familia na utakufa mpweke bila familia. Huyu mwanamke anakupenda, hiki ni kiwanja kizuri, umetumia miaka mingi kujenga nyumba mpaka kufikia hapa ilipo, umetengeneza familia, sasa hivi umebakiza finishing, kwakua unapesa na unaweza kupata kiwanja kingine unaweza kuamua kumuacha huyu mwanamke.

Ataondoka na labda yeye atapata shida kupata mwanaume mwingine lakini wewe ukapata mwanamke kwa haraka, kumbuka huyo mwanamke hatakua nyumba bali ni kiwanja na utahitaji kukijenga. Naye utaishi naye hivi hivi, atakua na mapungufu yake na kama kujenga nyumba kulivyo na changamoto kuna wakati utatamani kumuacha kutafuta mwingine, badala ya kudili na changamoto utamuacha kabla ya kutengeneza familia nyingine.

Maisha yako yatakua hivyo hivyo kila siku mpaka ukizeeka utajikuta unafikia hatua unaamua kutafuta tu Gofu, unatafuta tu mwanamke ilimradi mwanamke ambaye naye kaumizwa huko mnatengeneza familia ambayo kama ni nyumba inakua kama Gofu inavuja vuja tu na utatamani ungemalizia kujenga nyumba yako na kuishi kwa amani.” Mama alimaliza kuongea, alimuangalia mwanae na kuona maneno yamemuingia.

“Nenda kamuombe mpenzi wako msamaha, kamalizie kujenga nyumba yako hata kama una uwezo wa kuanza kujenga nyingine!” Aliondoka na kumuacha, jioni Juma alijifikiria na kumuomba msamaha mpenzi wake. Alimsamehewa na kujirekebisha, aliamua kuvumilia kumalizia nyumba yake kuliko kuanza nyingine kwani kila wakati alikumbuka maneno ya Mama yake kuwa habari ya kujenga na kuacha utajikuta unaishia katika magofu! Aliamua kumuoa Aziza na sasa wanafuraha, alimalizia kujenga nyumba yake!



USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.