Simukizi: Je Haya Ni Mapenzi? Sehemu Ya Nne (4)
Siku hiyo Joy akiwa ametulia ndani kwake akapigiwa simu na wifi yake na hiyo ni baada ya muda mrefu kupita bila ya mawasiliano yoyote kati yao.
Wakasalimiana vizuri sana na kufurahiana
"Ila wifi kuna jambo moja ningependa ulifahamu"
"Jambo gani hilo?"
"Bado hamjafika mwisho na yule mtu kwahiyo kuweni makini sana"
"Mtu gani huyo?"
Ni yule niliyewahi kukwambia kuwa anaifatilia familia yako, kuwa makini sana wifi yangu"
Joy alishaelewa moja kwa moja kuwa ni mtu gani anayezungumziwa hapo kwahiyo haikumpa shida sana, tofauti na pale mwanzoni wakati haelewi chochote.
Likizo ilifika na wakina Sabrina wakarudi, safari hii Sabrina alifurahi sana kumkuta Sakina nae amerudi na kufanya wawe marafiki kamavile wapo rika moja.
Ila mapenzi ya Sabrina yalihamia kwa mtoto wa Sakina sasa kwani likizo yote Sabrina alikuwa karibu na huyu mtoto, kila alichofanya alipenda kufanya na huyu mtoto.
Huyu mtoto nae alifurahia sana uwepo wa Sabrina hadi kipindi likizo ikiisha huyu mtoto Jeff alikuwa ananyong'onyea sana kwa kukosa uwepo wa Sabrina.
Kitu kimoja kilichomsononesha Sabrina ni kumkuta Sakina hakuwa na raha na ile furaha kama zamani na alipokuja kuchunguza akagundua kwamba mume wa Sakina alikuwa na nyumba ndogo yani alikuwa na mwanamke mwingine.
Sabrina na udogo wake lakini aliumia sana kamavile ni yeye aliyefanyiwa yale na kumfanya azidi kujiapia moyoni mwake kuwa hatokuja kuolewa kamwe katika maisha yake kwani alichokiona kwa watu kilitosha kabisa kumuonyesha kuwa ndoa ni mbaya.
Maisha nayo yaliendelea kama kawaida.
Sabrina akakua sasa na kuwa binti mkubwa kabisa ila hakutaka kujihusisha na mahusiano huku akiamini kuwa ni kitu kibaya na kisichofaa katika maisha yake kwahiyo wote waliokuwa wakimfata na kumtongoza aliwakataa kwamadai kuwa watakuwa sio waaminifu.
Sakina akagundua kuwa Sabrina ameathirika kisaikolojia kutokana na mambo ambayo yalikuwa yakimtokea wakati akiwa binti mdogo, akajaribu kukaa nae ili kumuweka sawa lakini Sabrina hakukubaliana na hali halisi.
Kuna siku Sakina alipewa ujumbe na kaka yake, moja kwa moja aliufikisha ule ujumbe kwa mama wa Sabrina.
"Kaka yangu anahitaji kumuoa binti yako"
"Unajua ulipokuja hapa na kusema kuwa una khabari njema nilijua ni njema kweli kumbe ni upuuzi tu"
"Upuuzi kwa habari ya kuolewa binti yako!!"
"Mwanangu ndio kwanza ana miaka ishirini, subirini akue kwanza msitake kuniharibia mtoto"
"Laiti ungeyajua hayo mawazo ya mtoto wako hata ungetamani kujaribu hili ili kidogo uone ingekusaidiaje"
"Tafadhari, usiniletee khabari kama hizo Sakina"
Ikabidi Sakina atulie na Khabari zake ingawa mdogo wake alimsumbua sana kuhusu Sabrina.
Muda mwingi Sabrina alikuwa akiutumia kuongea na huyu mtoto mdogo Jeff ambaye alisikia mambo mengi ya kumuhusu Sabrina toka kwa mama yake na kujaribu kuyauliza mengine kwa muhusika kama ni kweli au la,
"Eti Anti Sabrina, nasikia hutaki kuolewa eti ni kwanini?"
"Hayo ni mambo ya kikubwa, subiri ukue utayajua tu"
Hakutaka kumuweka wazi kwani bado aligundua kuwa ni mtoto sana na hakupaswa kujua.
Siku moja Sabrina akiwa njiani ameongozana na Jeff huku wakizungumza wanayoyajua wao, likatokea kundi la vijana watatu na kuwavamia na nia yao kubwa ilikuwa ni kwa Sabrina, na lengo lao lilikuwa ni kumbaka.
Walimshika kwa nguvu sana na kutaka kumuingilia, walipomfunua walikuta ana kitu cha ajabu mwilini mwake na kitu hicho kilikuwa ni tofauti kwa mwanamke wa kawaida.
Hivyo wale wabakaji wakamuacha Sabrina na kukimbia hata Sabrina mwenyewe alishangaa ila alishukuru walivyokimbia bila kumfanya chochote ila hakujua ni kwanini walikimbia.
Jeff alimfata Sabrina pale chini na kumsaidia kuinuka huku akimpa pole kwa yaliyomkuta huku wakiondoka.
Walifuka nyumbani wakiwa wamechoka sana kutokana na ile purukushani waliyokutana nayo kwa wale wabakaji, Sabrina alimsimulia mama yake na kumfanya mama yake aumie sana kwa hao wabakaji kutaka kumbaka mwanae
"Ila afadhari hawajakudhuru mwanangu"
"Yani mama, ni Mungu tu kanisaidia maana sijui ingekuwaje"
Sabrina hakujua ni kitu gani kilichowakimbiza wale wabakaji ila alishukuru kwa kutodhurika na kuwa makini sana katika safari zake zingine.
Sakina akasikia kitu cha tofauti kutoka mtu wake wa karibu kuhusu Sabrina ila hakuamini na alijiuliza kuwa hata kama ni kweli huyo mtu kajuaje kuhusu Sabrina!!
Mwanae alipokuja kumueleza kuhusu kilichowatokea yeye na Sabrina wakati wanarudi kwa siku mbili zilizopita ndipo Sakina alipogundua kuwa huenda yule ndugu yake anahusika.
Yule kaka yake aliyetaka kumuoa Sabrina ndiye aliyetuma vibaka wambake ili kumkomesha kwavile alimkataa, ila hao vibaka ndio waliompa taarifa kuhusu utofauti wa Sabrina na wanawake wengine na kuwafanya waogope kumbaka.
Sakina alichukizwa sana na hiyo tabia ya nduguye aliyoifanya kwa binti aliyempenda na kumuheshimu sana, hata hivyo hakuamini kama yale aliyoambiwa yalikuwa ni ya kweli.
Siku moja Sabrina akiwa kwenye matembezi yake akamuona kijana mmoja aliyemvutia sana, ikawa ni mara ya kwanza katika maisha yake kuvutiwa na mwanaume na hakujua aanze vipi kuongea nae ila uzuri ni kwamba yule kijana alimsogelea mwenyewe Sabrina na kumsalimia
"Mambo dada"
"Poa tu, mambo"
"Safi, samahani kuna kitu nataka kukuuliza"
Ila kabla hajamuuliza, Sabrina alijishtukia akibanwa na haja ndogo ya gafla na kumfanya ashindwe kuendelea kuongea na yule kijana wala kumsikiliza zaidi.
Hivyo basi akaondoka kwa yule kijana na kukimbilia kwenye kakichaka kidogo ili kujisaidia, gafla ikasikika sauti yake ikipiga kelele kwa nguvu.
Yule kijana kwa hofu akakimbilia mahali ambako Sabrina alielekea ili kujua nini kimemtokea.
Akamkuta Sabrina kasimama huku anapiga kelele, yule kaka akamfata na kumshikilia kisha akamuuliza
"Nini kimekupata dada?"
Lile swali likaonekana kama kumshtua Sabrina na kumfanya aone aibu gafla kwa zile kelele alizokuwa anapiga, akajikuta akimuacha yule kijana pale tena bila ya kumjibu na kutoka kwenye kile kichaka.
Yule kaka naye alitoka kwenye kile kichaka na kumfata tena Sabrina ila Sabrina hakutaka kabisa kumuangalia yule kijana, badala yake alikimbilia kwenye kituo cha madaladala na kupanda daladala moja wapo kisha akaondoka zake na kumuacha yule kijana akiwa na maswali mengi sana dhidi ya Sabrina.
Sabrina alipofika kwao alikuwa na mawazo sana dhidi ya yule kijana, kila mara alikuwa akijiuliza swali moja tu
"Sijui ameniona nilivyo!!"
Na kila alipojiuliza swali hilo alijisikia vibaya sana, alitamani wakati urudishwe nyuma kisha yeye akutane na yule kijana kwa namna nyingine lakini isiwe kama ilivyokuwa.
Aliwaza sana Sabrina bila ya kupata jibu ila mwisho wa siku aliamua kufanya kama hajawahi kukutana na yule kijana na wala hajaona alichoona ili aweze kutuliza moyo wake wenye mawazo.
Sabrina akiwa chumbani kwake na mawazo, akaitwa na mama yake na kuambiwa kuwa anahitajika nyumbani kwa Sakina.
Hivyobasi Sabrina akajiandaa na kwenda nyumbani kwa Sakina ambako palikuwa sio mbali sana kutoka kwao, na nyumba hiyo waliuziwa na baba wa Sabrina ambaye ni bwana Deo.
Sakina alishukuru kwa Sabrina kuitikia wito wake,
"Jambo nililokuitia hapa Sabrina ni moja tu kama jingine likiongezeka basi ni ziada"
"Jambo gani hilo?"
"Nakuomba uzungumze na mwanangu Jeff, nahitaji kumpeleka shule ya bweni ili asome vizuri lakini hataki. Nakuomba ujaribu kumshawishi ili akubali, tafadhari Sabrina nakuomba"
Sabrina akacheka kidogo, kisha akamuuliza Sakina
"Ikiwa mama yake mzazi kakukatalia je kwangu atakubali?"
"Mwanangu anapatana sana na wewe Sabrina, halafu anakusikiliza sana najua kwa vyovyote vile atakubali tu kwako"
"Basi ngoja nikajaribu"
Sakina akafurahi sana, kisha Sabrina akamfata Jeff ili aweze kumshawishi juu ya hilo.
Mtoto huyu Jeff alimpenda sana Sabrina na hakuna jambo ambalo aliambiwa na Sabrina halafu akakataa ndiomana mama yake aliona kuwa Sabrina ndio mtu pekee wa kumshawishi mwanae.
Sabrina aliongea na Jeff halafu mwisho wa siku mtoto huyu akakubali kwenda hiyo shule aliyotafutiwa na mama yake.
Sabrina akaenda kumueleza Sakina ambapo naye alifurahi sana, kisha akamuuliza
"Umewezaje kumshawishi?"
"Nimemwambia nitakuwa namtembelea mara kwa mara"
Sakina akacheka na kusema,
"Yani mwanangu huyu mmh! Tena shida yake ni akuone tu ndio aridhike"
"Tena amesema huko shule nimpeleke mie"
"Sasa itakuwaje?"
"Usijali nitampeleka"
Sakina akafurahi zaidi na kumshukuru sana Sabrina kwa kumsaidia kwa hilo.
Siku waliyopanga kumpeleka mtoto huyo shuleni, Sabrina alijiandaa na kumuaga mama yake.
"Unajua Sabrina huwa unanishangaza sana mwanangu, yani huyo mtoto majukumu yote juu yako halafu unajisikia raha tu!"
"Jamani mama!!"
"Jamani nini? Nenda zako huko usije kusema nimekuzuia bure"
"Haya mama nashukuru"
Sabrina akaondoka na kumfata Jeff kisha safari ya kuelekea shule ikaanza.
Siku hiyo Jeff aliongea maneno mengi sana kwa Sabrina na kumfanya Sabrina ashangae yale maneno ya Jeff ila alielewa wazi kuwa mtoto yule aliongea yote yale kutokana na mambo aliyoyaona.
"Anti, mimi nikiwa mkubwa nitaoa mke mzuri sana ila sitathubutu kumpiga mke wangu wala kumtesa. Sitaki alie kama mama"
Sabrina huruma ikamjaa kwa maneno hayo,
"Usemayo yawe ya kweli mtoto mzuri, usije badae ukabadilika"
"Utaniona tu anti, nampenda
sana mama yangu. Sipendi alie na ndiomana nilikuwa sitaki kuja hii shule ya mbali ila kwavile umenihakikishia kuwa mama hatalia tena ndiomana nikakubali, ila uwe unakuja kweli kuniona huko shuleni"
"Usijali Jeff"
Sabrina hakupendezwa pia na tabia aliyokuwa nayo Juma, ilimfanya hata achukie wanaume kwaajili ya tabia hiyo na akajua wazi hata Sakina kuamua kwake kumpeleka mtoto wake shule ya bweni ni kutokana kwamba hakupenda kuona mwanae akiyaona yale mambo ya aibu kila siku.
Sabrina akamuhurumia sana mtoto wao huyu mdogo aliyeonekana kuongea kwa uchungu sana na kuumizwa kwa matendo ya baba yake, hivyo basi Sabrina alijiapia kufanya chochote awezacho ili kudhibiti tabia ya Juma haswa ile tabia ya kumpiga mke wake.
Sabrina alifika shuleni na kumkabidhi Jeff kwa walimu wake kisha akamuaga ili aanze safari ya kurudi
"Bye Anti"
"Bye Jeff"
"Nakupenda Anti"
"Nakupenda Jeff"
Kisha akampungia mkono na kuondoka huku akili yake inawaza kitu cha kufanya ili kuikomesha tabia ya Juma.
Akiwa njiani akamuona mtu mbele yake ambapo mawazo yake yaliwaza kuwa kuna mahali amewahi kuonana na mtu huyo ila hakuweza kukumbuka kuwa ni wapi alionana nae.
Ila wakati anawaza hayo, yule mtu naye alimfata na kuanza kumsalimia
"Habari yako dada!"
"Nzuri tu habari!"
"Nzuri, naitwa Francis. Vipi mwenzangu waitwa nani?"
Sabrina akajiuliza kimoyomoyo, "nimekuuliza kwani!"
Kisha akamjibu,
"Naitwa Sabrina"
"Nashukuru kukufahamu dada yangu, unakumbuka siku ile tuliyoonana kwa mara ya kwanza pale stendi!!"
Kisha yule kijana akatoa kapelo aliyokuwa ameivaa kichwani na kumfanya Sabrina kumbukumbu zimjie kichwani na kukumbuka kuwa ni yule kijana aliyekutana nae siku ile aliyoenda kichakani kujisaidia.
Aibu ikamjaa Sabrina na kumfanya aangalie chini kwani hakutegemea tena kukutana na yule kijana.
Sabrina alikuwa kimya kabisa na kumfanya yule kijana ndio aendeleze maongezi
"Vipi dada unaendeleaje?"
"Naendelea vizuri"
"Basi itakuwa vizuri kama tukipeana mawasiliano"
Sabrina akaona ampatie tu hayo mawasiliano ili aende zake kuliko kuendelea kumpa wasiwasi wa moyo mahali hapo.
Kisha akamuaga na kuendelea na safari ya kurudi kwao, ila mawazo yake sasa yalihama kutoka kitu cha kumfanyia Juma ili amkomeshe kuja kwa huyu kijana alikutana naye tena kwani taswira ya sura yake ilibaki kwenye mawazo ya Sabrina.
Alihisi kabisa kitu tofauti kati yake na yule kijana, kwahiyo akajikuta safari nzima akimuwaza yule kijana hadi wakati anapanda kwenye daladala, bado mawazo yake yalikuwa ni kwa yule kijana tu na si vinginevyo.
Alipokaribia maeneo ya kwao alimuona Juma akitokea kwenye nyumba fulani huku ameongozana na mwanamke ambaye hakumjua ni nani ila kwa mawazo yake ya haraka haraka alihisi kuwa huyo mwanamke ndiye anayempa kiburi Juma na kumfanya asirudi kwake na anaporudi agombane na mke wake.
Sabrina akatulia pembeni ili kuwaona wanapoelekea, ila walifika mahali wakasimama na kukumbatiana kama ishara ya kuagana, mambo yote hayo Sabrina alikuwa akiyashuhudia tu pale alipokuwa.
Kisha Juma akaondoka zake na yule mwanamke akawa anarudi nyumbani kwake .
Sabrina sasa ikawa kama wale watu wanaonunua ugomvi tena ugomvi usiowahusu kabisa kwani alimfata yule mwanamke hadi nyumbani kwake tena bila hodi wala karibu akaingia ndani.
"Kheee mbona umeingia hivyo!! Kuna kheri kweli hapa"
"Hakuna kheri"
"Kheee, umekuja kwa shari?"
"Ndio"
"Haya niambie hiyo shari yako"
"Kwanini unatembea na mume wa mtu?"
"Ni mume wako wewe?"
"Hapana"
"Sasa wewe tatizo lako nini? Pilipili iko shamba wewe inakuwasha huku loh! Tena nitolee balaa mtoto wa kike nisije nikakuharibu bure"
"Thubutuuu! Jaribu uone cha mtemakuni"
Yule mama alimuangalia Sabrina kwa hasira sana kwani alikuwa ni mdogo sana kwake na angeweza kumfanya chochote atakacho ila aliona wazi kuwa atamuumiza binti huyo, wakati huo Sabrina naye kajitunisha mbele ya yule mama kamavile ni binti mwenye nguvu sana tena anayejiamini.
"Ila wewe mtoto dawa yako ni ndogo sana na nitakukomesha nakwambia"
"Unikomeshe kwa lipi!! Huniwezi nakwambia. Tena uachane na huyo mume wa mtu"
Kisha akasogea mezani kwa yule mama na kuchukua glasi iliyokuwepo juu ya meza na kuibwaga chini, yule mama akataka kumfata ila Sabrina akashika moja ya chupa iliyovunjika na kumtishia huku akielekea nje
"Wewe mtoto wewe! Umejifanya mjanja eeeh! Nitakukomesha, najua pa kukupata na cha kukufanya. Utajuta kunifahamu wewe mtoto"
Sabrina hakujali kitu chochote zaidi ya kuondoka, na safari yake ya kwanza haikuwa tena nyumbani kwao bali alienda moja kwa moja kwa Sakina.
Alimkuta Sakina akiwa na mawazo sana kama kawaida yake ila alipomuona Sabrina alifurahi
"Asante Sabrina kwa kunipelekea mwanangu shule"
"Usijali kuhusu hilo dada yangu, nina habari nyingine hapa"
"Ipi hiyo?"
Sabrina akaanza kumsimulia Sakina kile alichokifanya kwa yule mwanamke huku akijua kwamba Sakina atafurahishwa na zile khabari ila ilikuwa kinyume na matarajio yake.
"Nimemkomesha yule mwanamke dada"
"Mungu wangu Sabrina kwanini umefanya hivyo?"
"Basi akawa anajitamba eti atanikomesha mimi, nikamwambia thubutu yake! Nimemchamba hadi amekoma"
Sakina alisikitika sana
"Jamani Sabrina jamani"
"Kwani nini dada?"
"Yule mwanamke ni khatari Sabrina, ninapokwambia khatari ni khatari kweli. Mtaa mzima huu wanamuogopa jamani halafu wewe mmmh!! Hadi naogopa hapa"
"Unaogopa nini sasa?"
"Yule mwanamke ni mshirikina, yani ni mchawi hakuna mfano. Mtaa mzima wanamuogopa, hakuna anayeweza hata kumwambia chochote. Sabrina umeharibu mdogo wangu, nakuomba uende ukamuombe msamaha tafadhari"
Sabrina akanywea muda huo huo na kumfanya akose raha gafla.
"Nitaanzaje kumuomba msamaha sasa?"
"Fanya vyovyote Sabrina ila nenda ukamuombe msamaha tafadhari, sitaki matatizo mie Sabrina. Yale ya zamani yamepita, sitaki kuzua mengine. Usijali kuhusu baba Jeff atarudi mwenyewe kwangu wala yule mwanamke hawezi kunifanya mimi kitu chochote, mie nimeaga kwetu mdogo wangu. Ila wewe umeenda mwenyewe kuyafata, tafadhari rudi ukamuombe msamaha"
Sabrina akajifikiria sana, mwisho wa siku akaamua kuwa mpole na kwenda tena kwa yule mwanamke ili akamuombe msamaha.
Alipofika alimkuta yule mwanamke akifagia vile vipande vya chupa kutokana na zile glasi ambazo Sabrina alivunja.
Kwanza kabisa Sabrina alishangaa kuona anafagia muda huo sababu ni muda umepita tayari tangia azivunje, ila hayo hayakumuhusu sana kwahiyo akaamua kufanya kilichompeleka
"Samahani mama"
"Nilijua tu utarudi"
"Naomba unisamehe"
"Ushachelewa tayari, mdomo wako umekuponza rudi kwenu ukajionee kwa macho"
"Naomba unisamehe tafadhari!"
"Nimekwambia umeshachelewa"
Kisha akaingia ndani kwake na kufunga mlango.
Sabrina aliondoka kwa unyonge sana eneo hilo.
Alielekea moja kwa moja nyumbani kwao huku mawazo mengi yakiwa yamemtawala kichwani.
Akaingia ndani na kumuita mama yake, ambaye alitoka chumbani akiwa amechoka sana na moja kwa moja alimuuliza swali moja tu mtoto wake
"Mwanangu Sabrina kwanini unanifanyia hivi?"
"Nimekufanyia nini mama?"
Muda huo huo mama yake akaanguka na kuanza kutokwa na damu puani na mdomoni.
Inaendelea....
No comments: