Simulizi: Je Haya Ni mapenzi? Sehemu Ya tano (O5)


Alielekea moja kwa moja nyumbani kwao huku
mawazo mengi yakiwa yamemtawala kichwani.
Akaingia ndani na kumuita mama yake, ambaye
alitoka chumbani akiwa amechoka sana na moja kwa
moja alimuuliza swali moja tu mtoto wake
"Mwanangu Sabrina kwanini unanifanyia hivi?"
"Nimekufanyia nini mama?"
Muda huo huo mama yake akaanguka na kuanza
kutokwa na damu puani na mdomoni.
Uoga ukamshika Sabrina, akatamani kupiga kelele ila moyo wake ukasita kufanya hivyo.
Alijikuta akichanganyikiwa kwakweli ila muda huo huo likamjia wazo la kumpigia simu shangazi yake kwanza na kumueleza kuhusu mama yake
"Kwani umemfanyeje hadi imekuwa hivyo?"
Ikabidi Sabrina amuelezee shangazi yake hali halisi ilivyokuwa
"Nimekuelewa sasa,ila nakuomba utumie ujasiri wako. Usipige kelele wala usifanye chochote, mie nakuja huko. Umenielewa!"
Sabrina alimuitikia shangazi yake na kutulia ndani huku akimngoja aje, wakati huo moyo wake umegubikwa na mawazo ya kila aina.
Alitamani hata akamuite Sakina, ila aliamua kufata ushauri wa shangazi yake na kutulia pale ndani.

Hali ya mama yake ndiyo iliyomfanya azidi kutetemeka, alitamani kufanya kitu chochote cha kumsaidia mama yake ila maneno ya shangazi yake bado yalimrudia kuwa asifanye kitu.
Baada ya muda kidogo akapigiwa simu na shangazi yake,
"Haya toka humo ndani kwenu, rudisha mlango kama ulivyoukuta mwanzo halafu njoo kama unakuja stendi ili tukutane katikati halafu ndio tutarudi wote hapo nyumbani. Fanya kama ninavyokwambia tena upesi"
Sabrina akashangaa kuwa kwanini amfate na wakutane njiani wakati huyo shangazi yake anakuja huku nyumbani kwao? Ila alifanya kama alivyoambiwa na shangazi yake kisha akatoka na kuanza kumfata ili wakutane njiani.

Walikutana njiani kweli, Sabrina akatamani alie mbele ya shangazi yake wajina ila shangazi mtu alikuwa na sura kavu sana.
Kabla hata hawajaongea chochote, alitokea yule mwanamke toka upande mwingine na kujikuta akiwashangaa Sabrina na shangazi yake na kwa bahati mbaya akajikwaa na kuanguka.
Kitendo hicho kilimchekesha shangazi wa Sabrina na kujikuta akicheka sana.
Sabrina akamuangalia shangazi yake na kumwambia
"Usicheke shangazi"
"Usijali wajina, haya turudi nyumbani huko"
Yani muda huo huyu shangazi wa Sabrina alikuwa amechangamka sana na hakuwa na mashaka yoyote, kisha akamwambia Sabrina
"Ondoa hofu yote inayokutawala, uliyoyaona kuwa yalimtokea mama yako fanya kamavile hukuyaona. Usiweke kwenye akili yako, na tukifika utulie usifanye hizo papara zako"
Sabrina alikuwa akishangazwa tu na maneno ya shangazi yake muda wote.

Walipofika waliingia ndani, jambo la kwanza ambalo Sabrina alilifanya ni kumuangalia mama yake ambaye hakumuona tena pale chini na kumfanya uoga uzidi kumtawala sasa kuwa mama yake amepelekwa wapi.
Akataka kumuuliza shangazi yake ila shangazi mtu akamuonyesha ishara ya kimya na badala yake, Sabrina alijikuta akiulizwa maswali mengine kabisa na shangazi yake
"Nipe khabari za chuo"
Sabrina alimuangalia tu shangazi yake bila hata ya kumjibu kitu chochote.
Muda huo huo, bi. Joyce ambaye ni mama wa Sabrina alitokea chumbani huku akiwa anajinyoosha nyoosha na alionekana kuchoka sana.
Na moja kwa moja aliushangaa uwepo wa wifi yake
"Kheee wifi umekuja muda gani? Na wewe Sabrina kumbe umerudi!"
Sabrina alikuwa akimshangaa tu mama yake kwani ile hali hakuielewa kwakweli, shangazi mtu ndiye aliyeweza kujibishana na mama wa Sabrina hata Joy aliushangaa ukimya wa gafla kwa mtoto wake
"Una matatiz o gani leo! Mbona umepooza hivyo mwanangu?"
"Hakuna kitu mama"
"Haya kamletee shangazi yako juisi"
"Hapana hata asihangaike"
Wakaendelea kuongea maongezi mengine, ndipo Joy alipoanza kuwaeleza kuwa ameota ndoto mbaya sana
"Yani hizi ndoto za jioni hazifai jamani, eti nimeota kuwa nimekufa halafu watu wanalia kweli. Basi mkaanza kupanga mipango ya mazishi, eti hapo hapo nikashtuka kutoka usingizini. Basi hapa nimechokaje jamani!"
Sabrina aliendelea tu kumuangalia mama yake kwani yeye bado aliona ni mambo ya ajabu na kuzidi kujiuliza kuwa shangazi yake ana mahusiano yapi na mambo hayo? Alihisi kuwa huenda hata shangazi yake naye akawa mchawi kwamaana hakuelewa kabisa yale mambo ambayo shangazi yake aliyafanya, hivyo kujikuta akiwa na maswali mengi sana bila ya majibu kamili ya maswali yale.
Akajiandaa kumuuliza maswali yake kwavile alikuwa akiongea na mama yake akaamua kumvizia atakapomaliza kuongea na mama yake.

Muda ulifika na Shangazi wa Sabrina akajitoa kumsindikiza huku akitarajia kumuuliza yale maswali lakini mama yake aliambatana naye katika kumsindikiza na kumfanya Sabrina ashindwe tena kumuuliza maswali shangazi yake kwahiyo akajipanga kufanya hivyo atakapoenda kumtembelea.

Waliporudi nyumba ilikuwa kawaida kabisa yani kamavile hakuna kilichotokea mahali hapo na maisha yakaendelea kama kawaida.

Siku zilipita bila Sabrina kupata mawasiliano yoyote toka kwa yule kijana aliyempa namba zake, na alipofikiria vizuri zaidi akagundua kuwa kuna namba moja alikosea wakati anampa yule kijana namba
"Ila ndio basi tena sababu sitaweza kuonana nae tena"
Aliishia kujisemea hayo huku akijiandaa kwenda nyumbani kwa shangazi yake kwaajili ya maswali yake ambayo alishindwa kumuuliza siku ile alipokuwa kwao.

Sabrina aliianza safari hadi kwa shangazi yake, na alimkuta akiendelea na shughuli zake zingine
"Nimekuja shangazi, nina maswali yangu nataka unijibu"
"Niulize tu hayo maswali"
"Unajuaje hayo mambo ya kichawi?"
"Ni historia ndefu sana, ipo siku nitakuelezea kwahiyo usijali sana."
Sabrina akakosa majibu aliyoyatarajia hivyobasi akajiandaa kuondoka ili aweze kurudi kwao.

Akiwa njiani alimsikia mtu akimuita kwa jina lake, akageuka nyuma na kumuona yule kijana na hapa ndipo aliposhangaa kwani anajikuta akikutana na huyu katika maeneo ambayo hakuyatarajia.
"Vipi dada yangu za tangu siku ile"
"Nzuri tu, mambo"
"Poa, mbona ukanipa namba ambayo haipatikani!!"
Sabrina akaanza kujitetea pale kwa yule kijana ili asionekane kama ana mambo ya kiswahili, kisha akampa tena namba yake ambayo alikuwa na uhakika nayo sasa
"Nina ujumbe wako Sabrina, nitakutumia"
Sabrina alijiuliza kuwa ni ujumbe gani! Wakati mwingine mawazo yake yalimrudisha siku ile ya kwanza aliyokutana na yule kijana na kujikuta akijiuliza
"Au aliniona nilivyo!!"
Yule kijana alimsikia na kumuuliza kwa makini
"Ulivyo nini?"
"Hamna kitu, kuna jambo nimekumbuka tu hapa"
"Basi hakuna tatizo, nitakutafuta Sabrina"
Kisha wakaagana na kuondoka.

Alipofika nyumbani kwao akajikuta akijiuliza kuhusu yule kijana tu kama alimuona alivyo au la.
Ila kila alipoyawaza hayo alikosa raha.

Kuna kitu kilimsumbua Sabrina kwenye maumbile yake, kitu hicho huwa kinamtokea na kupotea na ndiomana alipiga kelele kule porini kwavile ilikuwa ndio mara yake ya kwanza kukiona ingawa hakujua kama wale wabakaji walikiona na ndiomana wakakimbia ile siku waliyotaka kumfanyia vibaya.
Alijiuliza sana kuwa kinatokana na nini ila hakujua chochote na hakujua kuwa ni kwanini kipo kwenye mwili wake yeye.
Alitamani kumwambia mama yake kuhusu jambo hilo ila aliogopa huku akihisi kuwa pengine mama yake atamfikiria vibaya.
Kwakweli hakuona wa kumwambia kuhusu hilo tatizo lake na ndioma na alijisikia vibaya kila alipohisi kuwa yule kijana alimuona alivyo.
Wakati anawaza hayo, simu yake ikaita
"Hallow, nani mwenzangu!"
"Francis anaongea hapa"
"Francis!! Francis yupi?"
Ikabidi aanze kumueleza walipokutana,
"Ooh nimekukumbuka tayari, eeh nipe huo ujumbe wangu"
"Nakupenda Sabrina"
Sabrina alijihisi kama amepigwa shoti ya umeme kwa lile neno moja tu aliloambiwa na yule kijana na kujikuta akikata ile simu na kuanza kujiuliza
"Atanipendaje mimi wakati kaniona nilivyo!! Au ananitania ila mimi nimechukulia kwa maana nyingine?"
Ile simu yake ikaita tena,
"Mbona umenikatia simu Sabrina?"
Sabrina hakuwa na jibu zaidi ya kukaa kimya tu kwani hakuelewa amjibu kitu gani.
"Nakupenda Sabrina, tena nakupenda sana"
"Uliniona nilivyo?"
"Haijalishi Sabrina, mimi nakupenda kwa vyovyote vile ulivyo"
Sabrina akajipa jibu la moja kwa moja kuwa ameonekana jinsi alivyo na kumfanya ajisikie vibaya zaidi, akamuaga yule kijana kwenye simu na kujikalia kitandani kwake huku machozi yakimtoka kuwa kwanini ameonekana vile alivyo wakati hakutaka kuonekana vile kwa mtu yoyote yule. Akajisikia vibaya sana ila hakuweza kufanya chochote kwani tayari alijua kuwa ameshaonekana na mtu mwingine.

Akiwa nyumbani kwao ametulia, alikuja Sakina kuwatembelea pale nyumbani na nia yake ilikuwa ni moja tu nayo ni kuzungumza na Sabrina.
"Eti mdogo wangu Sabrina una matatizo gani kwenye maumbile yako?"
Leo Sakina alijitoa muhanga na kuamua kumuuliza Sabrina ila Sabrina alishangazwa zaidi kuona kuwa hata Sakina anajua kasoro alizokuwa nazo, na kumfanya azidi kujisikia vibaya zaidi.
"Sina tatizo lolote"
"Niambie ukweli Sabrina, nipo tayari kukusaidia"
"Utanisaidia kweli?"
"Ndio nitakusaidia, ukweli wako ndio utakaokuweka huru"
"Ni kweli nina matatizo dada tena makubwa tu"
"Pole sana na usijali kitu nitakusaidia. Ngoja niongee na mtu halaf u nitakupa majibu yanayoeleweka mdogo wangu hata usijali"
"Ila usimwambie mama"
"Usijali sitamwambia chochote"
Sabrina akakubaliana na huyu Sakina jinsi atakavyoweza kusaidika kutokana na tatizo alilokuwa nalo kwenye maumbile yake.

Wakapanga siku ya kupelekana mahali ambako ataenda kupata msaada wa tatizo alilokuwa nalo.
Siku hiyo wakajiandaa kisha Sakina akamfata Sabrina na kuelekea kwa huyo mtu waliyekubaliana nae.
Ilikuwa ni safari ya mbali kiasi, ambayo ilichukua takribani masaa matano kufika huko.

Walipofika walikaribishwa na bibi mmoja aliyekuwa mzee sana ila alisifika kwa kujua dawa za kila aina na kila mtu aliyemtibia ilikuwa lazima apone kutokana na dawa zake kuwa kali na zenye nguvu.
Wakamueleza yule bibi tatizo la Sabrina, naye akawapa imani kuwa lile tatizo ni dogo tena ni la kawaida tu wala haliwezi kuwa kikwazo kwake na lazima atamsaidia hadi atapona kabisa.
Kwakweli hilo lilikuwa wazo la matumaini kwa Sabrina.

Yule bibi alichuma dawa na kumchanja Sabrina kwenye kiuno, halafu nyingine alimfunga kiunoni ikawa kama shanga kisha akamwambia.
"Kesho mje ili nikutoe hiyo kamba hapo kiunoni, msisahau kuja kwakuwa hiyo kamba natakiwa nikutoe mimi mwenyewe. Tena mje mapema"
"Sawa tumekuelewa"
Sakina naye akauliza,
"Kwahiyo baada ya hapo atakuwa amepona?"
"Ndio, atakuwa amepona. Yani hiyo kamba ndio itabeba huo ugonjwa wake, na itatakiwa itolewe kesho saa saba mchana tena itolewe na mimi mwenyewe niliyoifunga ndiomana nawaambia kuwa muwahi kwamaana isipotolewa madhara yake ni makubwa sana"
Wakakubaliana na yule bibi kisha wakamshukuru na kuanza safari ya kurudi nyumbani.

Wakiwa kwenye daladala, Sabrina akasikia wimbo ukiimba kwenye redio ya mule kwenye daladala na maneno yake yakamchoma kwakweli. Akausikiliza kwa makini, ulisema
"Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu na kumfanya kuwa ni kinga yake....."
Sabrina alijiuliza kuwa kwanini yale maneno yamemchoma sana! Ila aliamua kuyapuuzia na kujifanya kamavile hakuyasikia.

Walifika nyumbani na giza kabisa huku wakijiandaa kwaajili ya safari ya kesho yake.
Ila leo Sabrina hakuulizwa chochote na mama yake kuhusu alipokuwa, ila aliona ni vyema kutokuulizwa kwakuwa mama yake ana asili ya mdomo sana.

Kesho yake ilipofika, asubuhi na mapema akapitiwa na Sakina na kuianza safari yao ya kuelekea kwa yule bibi wa kuwatibia huku wakiwa na imani kuwa lile tatizo linaenda kuisha leo.
Wakiwa njiani lile basi walilopanda likapata pancha, ikabidi wasubiri ila Sabrina alichukia sana kwani aliona wanacheleshwa tu, ingawa konda aligoma kuwarudishia nauli zao ili wasiondoke ila wao hawakujali na wakaenda kupanda gari jingine.
Walipokaribia kufika ile gari nayo ikapata pancha na kufanya wajiulize
"Kuna tatizo gani huko?"
"Hadi nimeanza kuingiwa na uoga dada"
"Ngoja tuchukue bodaboda basi"
Wakaamua kuchukua bodaboda ili iwapeleke kwa haraka.

Walipofika kwenye nyumba ya bibi walishangaa kukuta kimetawala kilio kwenye eneo lile.


Walipofika kwenye nyumba ya bibi, walishangaa kukuta kimetawala kilio kwenye eneo lile.
Wote wawili wakajikuta wakitazamana kwa mshangao, ikabidi Sakina aende kuulizia vizuri ili wajue kuna nini.
Alimfata binti mmoja na kumuuliza,
"Eti kuna nini hapa?"
"Bibi ametutoka"
"Eti nini!!"
Sakina alijihisi kuchanganyikiwa kwakweli,
"Hebu niambie vizuri, bibi madawa ndio amekufa?"
"Ndio amekufa leo saa nne asubuhi yani kila mmoja umuonaye hapa amechanganyikiwa na wala hatujui itakuwaje"
Sakina alinywea sana na kujikuta akifikiria mambo mengi bila ya majibu yanayojitosheleza.
Alihisi ni mkosi wa kujitakia wenyewe.

Akamuita Sabrina pembeni ili wajaribu kujadili cha kufanya kutokana na ile hali.
Sabrina akawa analia tu,
"Usilie Sabrina, ngoja tufikirie kitu cha kufanya kwa sasa"
"Tutafanya kitu gani wakati anayejua amekufa tayari"
Machozi hayakuacha kumtoka Sabrina huku akiwaza kuwa ataishije na atafanyaje ili aeleweke kwenye jamii.
"Usijali Sabrina, tutapata utatuzi tu wa swala hili kwahiyo usijali sana."
Wakakaa chini huku wakitafakari cha kufanya.
Wakamuona mwanamke flani akija pale kwa yule bibi ila baada ya kupewa taarifa za msiba alijitupa chini akijigalagaza huku akilia kilio kikubwa.
Wakaamua kumfata yule mwanamke na kuanza kumpooza
"Niacheni nilie jamani labda itapunguza uchungu nilionao, hata sijui nitafanya kitu gani mimi"
Yule mwanamke aliendelea kulia kwa uchungu sana huku akiendelea kusema
"Kuna dawa hapa ilitakiwa itolewe leo na huyu bibi na ikifika saa kumi na mbili kama haijatolewa basi nakuwa kichaa. Uwiiii jamani ukichaa unanikaribia jamani, nani atanisaidia mimi!"
Sabrina alimuangalia huyu mwanamke kwa huruma sana huku akijiuliza na yeye kuwa atapatwa na tatizo gani? Maana yeye hakuelezwa moja kwa moja kuwa ile dawa isipotolewa au ikitolewa na mtu mwingine, atapata matatizo gani?
Alitamani siku zirudi nyuma ili asikubali ushauri wa Sakina wa kuja kwa huyo bibi.
Sabrina alikuwa na mawazo sana na eneo lile watu walizidi kuongezeka huku wakilia na kujitupa tupa kwani kila mmoja alikuwa na tatizo lake na mtu pekee wa kuwasaidia ni huyo bibi aliyekufa.
Kwakweli kila mmoja ile hali ilimuwia vigumu sana kwani hakuna aliyejua cha kufanya kwa wakati huo kila mmoja alikuwa njiapanda na mawazo yake.
Sakina akamuomba Sabrina kuwa warudi nyumbani ili wakafikirie cha kufanya.
Sabrina akagoma kwani alitamani hata alale hapo hapo ili ajue mbivu na mbichi, ila Sakina akatumi a uwezo wake wote wa kushawishi hadi Sabrina alipokubali kuwa warudi nyumbani.
Nao wakaianza safari ya kurudi nyumbani.

Sabrina alipofika kwao alikimbilia chumbani kwake huku akijiangalia ile kamba kiunoni na kujikuta akilia sana na kujiona kuwa ni mjinga na mpumbavu kwa kufanya vitu bila kufikiria.
Wakati analia, mama yake akamuita ila Sabrina hakuitika na kumfanya mama yake amfate kule alipo ili ajue kuwa mwanae ana matatizo gani
"Ulikuwa wapi Sabrina? Na huo mchezo wa kuondoka bila kuaga umeuanza lini?"
Sabrina alikuwa akilia tu na kumfanya mama yake atake kujua kitu kinachomliza mwanae.
"Niambie una tatizo gani kwani?"
"Sijui mama"
"Hujui nini? Niambie mwanangu, mimi ndio mama yako ninayeweza kukusaidia"
Lakini Sabrina hakuweza kumwambia chochote mama yake na badala yake akadai kuwa kichwa kinamuuma kwahiyo anahitaji muda wa kupumzika.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mama yake hakuwa na tatizo, kisha akamruhusu mwanae apumzike halafu yeye akaenda kuendelea na shughuli zake zingine.

Sabrina hakupata usingizi hadi panakucha na palivyokucha tu akajihimu tena na kuanza safari ya kwenda kwa yule bibi tena bila ya kumwambia Sakina wala nani.
Alifika mapema sana kwa yule bibi na kukuta msiba ndio umenoga vizuri siku hiyo kwani mikeka ilitandikwa na maturubai ya kutosha yaliwekwa.
Sabrina akaamini vizuri sasa kuwa ni kweli yule bibi amekufa ila je hitimisho la yeye na ile kamba kiunoni ni nini?
Akajaribu kufatilia wagonjwa baadhi waliokuwa wakihudumiwa na yule bibi, akawaona wengine wakiwa wamezimia, wengine hawajitambui yani kila mmoja alikuwa na hali yake ya kusikitisha.
Akamkuta yule mwanamke wa jana akiwa anaongea peke yake kwamaana kwamba kichaa ndio kimeshampata tayari.
Sabrina alihisi kuchanganyikiwa kwani hapakuwa na msaada wowote wa kusaidiwa wagonjwa wale wa bibi.

Mpaka muda wa mazishi unafika bado Sabrina alikuwa eneo lile lile hadi walipoenda kuzika, akatazama kwa makini sana kaburi alilozikwa bibi yule huku mawazo yakimtawala kichwa chake.
Ila hakuwa na la kufanya zaidi ya kuamua kurudi kwao ingawa bado alikuwa akisita kwani hakuelewa kuwa ni kwa jinsi gani angeweza kumueleza mama yake na akamuelewa juu ya hayo mambo ambayo mama yake huwa anapingana nayo kila siku.

Wakati anarudi kwao alifika mahali na kukaa chini ya mti huku akitafakari cha kufanya.
Akiwa kwenye mawazo mazito, akatokea yule kijana ambaye huwa wanaonana mara kwa mara.
Akafika hadi pale alipo Sabrina na kumuuliza,
"Sabrina, mbona upo hivyo! Una matatizo gani mama? Niambie, pengine naweza nikakusaidia"
Sabrina akawaza sana kuwa je amwambie ukweli? Na je atamsaidia au atamtangaza? Akasita kumwambia ukweli, ila yule kijana alimuomba na kumsihi sana kuwa amwambie ukweli ulivyo.
Kwavile Sabrina maji yalishamfika shingoni aliamua kumueleza ukweli ili apate kupumua kidogo.
"Pole sana Sabrina, ila usijali kwani nitakuwa nawe bega kwa bega hadi pale tutakapopata ufumbuzi wa tatizo lako"
Kwavile muda ulikuwa umekwenda, yule kijana akaona kuwa ni vyema kama atamrudisha kwanza nyumbani halafu ndio harakati za kushughulika na hilo swala zianze.
Sabrina akakubali kurudi kwao, kisha yule kijana akamsindikiza Sabrina hadi kwao.

Akamkuta mama yake akiwa kavimba kwa hasira, tena bila hata ya salamu wala kuitikia salamu zao moja kwa moja alimuuliza swali Sabrina
"Unaweza kuniambia kuwa huyo kijana ni nani?"
"Ni rafiki yangu mama, anaitwa Francis"
"Haya wewe kijana nenda zako, na wewe Sabrina ingia ndani"
Yule kijana akaondoka kisha Sabrina akaingia ndani kwao, na kufuatwa na maswali kutoka kwa mama yake
"Unaweza kuniambia ulipokuwa?"
Sabrina alikaa kimya tu
"Hivi unatambua kwamba unatakiwa kuwa chuoni wiki ijayo?"
Sabrina akaitikia kwa kutikisha kichwa
"Kwanini unape nda kunivuruga wewe mtoto jamani! Kwanini lakini?"
"Nisamehe mama"
"Kwakweli sipendezwi na tabia yako, nakwambia tena huo uchizi wako peleka huko kwa shangazi yako mwenye jina lako. Sipendi matatizo mtoto wa kike, usinivuruge kabisa. Kaka zako wametulia zao huko ila wewe kichwa maji, sitaki ujinga"
Aliong ea kwa hasira sana na kuondoka zake.
Sabrina alitulia kimya kwani bado mambo yake yalimsumbua.




USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.