Simulizi: Je haya ni Mapenzi? Sehemu Ya 02
Madaktari wakamfata muhusika sasa ili akubali na harakati za operesheni zifanyike, lakini Sakina alikataa kabisa kufanyiwa operesheni kwani moyo wake ulimwambia kuwa bado ana nafasi ya kutosha ili ajifungue kwa njia ya kawaida. Madaktari wakamshangaa sana na kujiuliza kuwa labda hapatwi na maumivu
"Sikia dada, tunapenda tukusaidie wewe na hiko kiumbe chako tumboni. Kubali tukufanyie operesheni na utasalimia dada yangu"
Sakina nae aliwajibu kwa maumivu makali sana
"Kama mnapenda kunisaidia basi naomba mnisaidie kitu kimoja tu"
"Kitu gani hicho?"
"Naomba mniitie yule binti niliyeletwa naye hapa usiku wa jana"
"Yule binti mdogo!!"
"Ndio, huyo huyo anaitwa Sabrina"
Madaktari wakaangaliana kwa hamaki na kumuuliza Sakina
"Sasa yule binti atakusaidia nini?"
"Mimi najua atakachonisaidia, nawaomba mniletee tu yule binti"
"Ila hii ni wodi ya wazazi, watoto hawaruhusiwi humu dada yangu"
"Jamani nawaomba jamani, kama kweli mnahitaji kuninusuru nawaomba mniitie huyo Sabrina"
Madaktari hawakutaka kusema zaidi, wakaamua kufanya alivyotaka Sakina ingawa ilikuwa nje ya utaratibu.
Deo alishaagana na Juma kuwa anaondoka na binti yake baada ya hali yake kuwa nzuri ili akamuone mkewe. Ila wakati anataka kuondoka alishangazwa na daktari mmoja aliyemfata na kumwambia kuwa binti yake anahitajika kwenye wodi ya wazazi, kwakweli Deo alikataa sana
"Mtamfanya mwanangu aote jamani, mambo gani hayo!"
Yule daktari akamuomba sana na kumsihi awaruhusu waende na huyo binti yake, mwisho wa siku Deo akakubali na kumuacha Sabrina chini ya uangalizi wa Juma huku yeye akienda hospitali aliyolazwa mkewe.
Sabrina alipelekwa moja kwa moja kwenye chumba cha uzazi, moja kwa moja alipo Sakina kisha akamsogelea Sakina na kumshika mkono.
Muda huo huo Sakina akajifungua, na muda huo huo huyo Sakina akapoteza fahamu.
Deo alienda hadi hospitali aliyolazwa mkewe, akaenda hadi wodi aliyomuacha.
Alipokaribia kitanda alichokuwa amelazwa mkewe alishtushwa kuona pamezungushwa pazia la kijani.
Deo alienda hadi hospitali aliyolazwa mkewe, akaenda hadi wodi aliyomuacha.
Alipokaribia kitanda alichokuwa amelazwa mkewe alishtushwa kuona pamezungushwa pazia la kijani.
Nguvu zilimuisha Bwana Deo na mawazo yake yakavutika mbali kabisa na kuhisi kuwa mkewe amekufa.
Akaanza kusogea taratibu kwenye kile kitanda chenye pazia la kijani kisha akafunua ila hapakuwa na mtu, akamuona nesi akija eneo hilo na kumuuliza kwa masikitiko
"Eti mgonjwa aliyelazwa hapa yuko wapi?"
Yule nesi alimuangalia kwa huruma na kumuuliza tena
"Ni ndugu yako"
Deo alijibu kwa kutikisa kichwa, kisha yule nesi akamsogelea karibu na kumwambia
"Kaza moyo baba, huyu mama wa hapa ametutoka"
Deo alihisi kuchanganyikiwa kwani hata machozi nayo yalishindikana kutoka, ikabidi yule nesi amuombe awasiliane na ndugu zake wengine kwani yeye mwenyewe hataweza kukabiliana na ile hali.
Bwana Deo akatoka nje ya wodi akiwa amechanganyikiwa kabisa, hakujielewa hata kidogo na alijihisi kuwa yeye ndio chanzo cha kifo hiko cha mkewe.
Sabrina aliogopa sana kumuona mtoto mchanga akiwa kajaa damu, ilibidi manesi wamtoe nje Sabrina ili waweze kuendelea na taratibu zingine za pale kwenye chumba cha wazazi.
Juma alimchukua Sabrina na kumuweka mahali ili kumfanya akili imkae sawa.
Manesi nao walimfata Juma na kumpongeza kwa kupata mtoto.
"Hongera sana kaka"
"Hivi ni mtoto gani?"
"Umepata dume kaka yangu, hongera sana"
Juma akafurahi sana kwani ndio kitu alichokuwa anakihitaji siku zote na kusahau hata kuuliza hali ya mke wake, hadi nesi aliyemletea habari akamuuliza kwa mshangao
"Inamaana hata hali ya mke wako hutaki kuijua?"
"Aaah furaha ilipitiliza, eeh anaendeleaje na mwanangu je yupoje?"
"Utamuona tu ila mkeo amepoteza fahamu, ila usijali atazinduka tu"
Swala la mke wake kupoteza fahamu halikumpa wasiwasi sana kwani alichotaka yeye ni kumuona mtoto wake tu na si vinginevyo.
Sakina alipozinduka alikabidhiwa mtoto wake naye pia akafurahi sana.
Kisha yeye na Juma pamoja na Sabrina na mtoto wao wakaruhusiwa kurudi nyumbani na moja kwa moja walifika ndani kwao huku wakisemezana hili na lile.
Sakina akamuomba jambo moja tu mumewe kuwa aruhusu yule mtoto apewe jina na Sabrina, Juma naye hakuwa na pingamizi dhidi ya hilo na kuruhusu tu Sabrina ampe jina mtoto.
Sakina akamwambia Sabrina,
"Kwavile nilikuahidi kwamba nikipata mtoto wa kike basi ataitwa jina lako, sasa nimepata mtoto wa kiume basi ningependa wewe umpe jina. Sawa Sabrina!"
Sabrina akatingisha kichwa akiashiria kuwa amemuelewa, kisha akaulizwa tena
"Nitajie basi jina utakalompa mtoto"
"Aitwe Jeff"
"Jeff!!"
Juma na Sakina walijikuta wakisema pamoja kwa hamaki kisha wakaangaliana, wala Sabrina hakujua kuwa kwanini wameshangaa kwa kiasi kile. Ikabidi awaulize,
"Mbona mmeshangaa au hamjalipenda?"
"Hapana, ila kwanini umechagua hilo jina?"
"Mi nalipenda tu na ningependa huyu mtoto aitwe hivyo"
Basi Juma alimwambia Sabrina kuwa watajadili kuhusu hilo jina na kuona kama linafaa au halifai kwa mtoto wao.
Hali ya Deo haikuwa sawa kabisa kwani alihisi kuwa chini, akatafuta mahali na kukaa kisha akitafakari cha kufanya kwani hakujielewa kabisa, hakujua aanzie wapi na aishie wapi. Hakuweza kupata majibu kwa yote aliyoyawaza, ikabidi aamue kurudi tu nyumbani ili awaambie ndugu wote mambo ambayo yametokea kuhusu mke wake na taratibu za mazishi ziweze kuendelea hata akasahau kama kuna hospitali nyingine aliacha watu wanaomuhusu.
Alipokaribia kwake hakutaka kuingia ndani na badala yake ni moja kwa moja akaenda kwa mpangaji wake ambaye alikuwa ni Juma kwani aliona uwepo wa watu kwenye nyumba hiyo.
Juma alimkaribisha Bwana Deo kwa uzuri sana ila akamshangaa Bwana Deo alivyokuwa amenyong'onyea na hapo hapo akaelezwa habari za msiba uliowafanya wote wakose raha pale ndani kwani ilikuwa kamavile wamemwagiwa pilipili.
Sabrina ndiye aliyetia huruma zaidi kwani hakuamini kuwa mama yake kamtoka kwa mtindo huo ukizingatia aliondoka kwao bila kuaga kwahiyo ikawa simanzi kubwa sana kwake.
Deo akawapigia simu ndugu zake na kuwapa habari za msiba huo, akapiga simu na shuleni kwa watoto zake ili warudishwe kwakweli Deo alikuwa kapatwa na pigo kubwa sana kwenye maisha yake.
Haikuchukua muda sana kwa ndugu na majirani kuanza kukusanyika katika nyumba ya Deo huku kila mmoja akisema lake
"Yani ni jana tu nilikuwa nikitaniana nae eti leo katutoka jamani!"
Wengi waliingiwa na simanzi na walikuwa na majonzi sana kwa msiba huo ambao haukutarajiwa wala kutegemewa.
Sabrina mkubwa alifika kwa kaka yake na kuwapita wale ndugu kisha akamfata kaka yake na kumuuliza
"Huyo marehemu yuko wapi?"
"Maswali gani hayo Sabrina bila hata ya salamu?"
Sabrina akacheka na kumuuliza tena kaka yake
"Marehemu yuko wapi?"
"Hospitali, amepelekwa monchwari"
"Sawa kaka yangu"
Kisha akacheka tena na kuondoka pale msibani na kufanya baadhi ya ndugu waamini kwamba huyu mdada anamatatizo kwenye akili yake au anamambo ya kishirikina kwani kwenye swala la msiba kwa mtu mwenye akili timamu hawezi akacheka.
Deo akazidi kupatwa na mawazo kwa akili fupi za mdogo wake ingawa anampenda sana mdogo wake huyo.
Ndugu waliokuwepo hapo kwenye msiba wakaanza mipango kwaajili ya huyo marehemu kuwa wengine wataenda hospitali kushughulika na mwili wa marehemu huku wengine wakibaki nyumbani kwa mipango na shughuli zingine za mazishi.
Binti mdogo Sabrina hakutaka kuamini ukweli kuwa mama yake amekufa, akaenda kwa baba yake na kumuomba kuwa ampeleke hospitali akamuone mwenyewe mama yake kabla hata hajaletwa nyumbani
"Hawaruhusiwi watoto kule mwanangu"
"Naomba waniruhusu mimi tu baba kwani siamini kama amekufa kweli"
"Akiletwa utamuona mwanangu"
Deo alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa kwani kila alipoitazama familia yake hakuweza kuamini kama mkewe ndio kashamuachia watoto wale tayari, alitamani hata siku zirudishwe nyuma ili mambo yaweze kubadilika na mkasa huu uweze kupotea pia ila hali haikubadilika kwake.
Yule dada wa Deo aliyeitwa Sabrina ilikuwa kamavile kuna kitu anakijua kuhusu huyu wifi yake ambaye inasemekana kwamba amekufa.
Na alipotoka pale huku akicheka alikuwa na nia ya kwenda moja kwa moja hospitali ili akahakikishe kama ni kweli au la kwani mawazo yake yalimtuma kwamba sio kweli na ndiomana akacheka na kuondoka.
Ila wakati anaondoka hakuweza kugundua kitu kimoja kuwa kuna mtu kutoka pale msibani alikuwa akimfatilia kwa nyuma na baada ya dakika chache yule mtu aliyekuwa akimfatilia Sabrina kwa nyuma alionekana akiwa kwenye nyumba yake iliyokuwa njiani na ni njia hiyo hiyo ambayo Sabrina alitakiwa kupita.
Sabrina alipokaribia kwenye hiyo nyumba alishangaa kuona ukungu mbele yake na gafla macho yakamuwasha kamavile mtu aliyemwagiwa pilipili, muda huo huo akahisi kizunguzungu na kuanguka.
Watu wakajaa eneo hilo huku wakimshangaa kuwa amepatwa na kitu cha aina gani.
Yule mtu ambaye alikuwa akimfatilia naye alitoka kwenye nyumba yake huku akionekana kama mtu aliyestaajabishwa na alichokiona kisha akawaomba wamuingize ndani kwake ili ampatie huduma ya kwanza.
Watu waliomzunguka Sabrina hawakusita bali walifanya kama walivyoshauriwa na huyo mwenye nyumba kisha wakaondoka bila hata ya kuhoji kitu chochote.
Sabrina alipobaki na yule mtu akazinduka ila hakuweza kuona kitu chochote kwani alikuwa kama kipofu kisha yule mtu akamuuliza
"Kilichokuwa kinakuchekesha kwenye msiba?"
Sabrina akashangaa na kuuliza pia
"Kwani wewe ni nani?"
"Huna mamlaka ya kunijua ila unatakiwa kujibu unachoulizwa"
"Kwasababu siamini kama kweli amekufa"
"Kwanini huamini? Kuna kitu chochote unajua?"
"Sijui chochote"
"Kama hujui chochote kwanini ulicheka? Na kwanini huamini?"
"Nilijikuta nikicheka tu ila ukweli ni kwamba siamini kama alikufa"
"Basi unatakiwa uamini na usipende kufanya masikhara kwenye mambo kama haya"
Kisha yule mtu akamshika macho Sabrina, naye akaona kilichotokea hospitali.
Kuwa Deo alipoenda hospitali kumuangalia Joyce alikuwa akifatwa na mtu nyuma bila kujua na walipofika hospitali kisha kuhamia hospitali nyingine kwaajili ya kumuona Sabrina mdogo, yule mtu aliyekuwa akimfatilia naye aliondoka, na muda kidogo likatumwa jeshi la watu watatu na kummaliza yule mgonjwa pale kitandani.
Sabrina akatokwa na chozi moja la uchungu kwani alitamani afanye kitu kisha akajisemea
"Nilijua yote haya ndiomana nikamkataza mwanae asitoke"
"Ulijua nini?"
Ila Sabrina hakujibu na wala hakujielewa kuwa ajibu kitu gani kwani aliona ni mambo ya ajabu na kujiambia kimoyomoyo kuwa akipona moja linakuja la pili.
Muda huo huo alijiona yupo pale njiani tena, kwakweli hakuweza kuendelea na safari badala yake alijikuta akikimbia na kurudi nyumbani kwa kaka yake huku amenyong'onyea sana hadi kaka yake akashtuka kuwa mtu aliyeondoka huku anacheka ndio huyo amerudi huku kanywea, kisha akamuuliza
"Ni nini tena muda huu mdogo wangu"
"Sijui"
"Hujui nini?"
"Nitakwambia"
Alikuwa ni mtu mwenye mawazo sana kwa muda huo na hakuna ambaye alimuelewa kuwa alikuwa anamawazo gani.
Ndugu nao waliongezeka pale nyumbani kwa Deo huku wakilia na kuomboleza kuwa wamempotea Joyce aliyekuwa mtu wa watu, kipenzi cha watu yani sifa zote alizipata hapo hata sifa ambazo hakuwahi kuambiwa kuwa anazo ila hapo walizisema huku wakilia na kuomboleza.
Kama ambavyo ilipangwa, ndugu wengine wakajiandaa na kwenda hospitali kwaajili ya kuandaa mwili wa marehemu na wengine walibaki pale nyumbani huku ratiba ya mazishi ikipangwa.
Deo alikuwa bado hajielewi kwakweli, dada yake mdogo akamfata tena na kumwambia
"Nikwambie kitu kaka!"
"Niambie tu"
"Wifi hajafa"
"Mmh Sabrina mdogo wangu umechanganyikiwa au?"
"Sijachanganyikiwa, ila huo ndio ukweli"
Deo alimuangalia Sabrina kwa makini sana bila ya kumuelewa, kisha Sabrina akamwambia tena
"Utaamini maneno yangu wakirudi hao wa hospitali"
Wakati wakiongea hayo wakasikia watu wakipiga kelele nje na kuwa kama wakikimbizana.
Ikabidi watoke ndani na kwenda kushuhudia kuwa kuna nini, walishangaa kumuona Joyce akitembea huku anachechemea akiwa anarudi pale nyumbani.
Ikabidi watoke ndani na kwenda kushuhudia kuwa kuna nini, walishangaa kumuona Joyce akitembea huku anachechemea akiwa anarudi pale nyumbani.
Watu pale nje walitawanyika wote, Deo aliganda mlangoni kama barafu huku macho yamemtoka kwani hakuamini kitu ambacho alikiona mbele yake.
Ilikuwa kama mauzauza tu.
Kati ya wote waliokuwemo mule ndani ni Sabrina pekee aliyepata ujasiri wa kwenda na kumsogelea Joy kisha akamshika mkono na kumsaidia kuingia ndani.
Deo hakuwa na ujasiri zaidi ya kumtazama tu mkewe, hata watoto wa Joy nao hawakuwa na ujasiri zaidi ya kumkodolea macho tu mama yao.
Baada ya Joyce kukaa, naye alikuwa akiwashangaa kuwa kwanini wanamkwepa, akaanza kwa kuwaita majina watoto wake na kuwauliza
"Mbona mpo mbali na mimi wanangu? Inamaana hamjafurahi kuniona?"
Watoto wake wote walikuwa kimya na ilionyesha dhahiri walimuogopa mama yao baada ya kusikia kuwa amekufa.
Ni Sabrina mdogo tu aliyeweza kumsogelea tena mama yake na kumwambia kwa upole
"Tumeambiwa kuwa umekufa mama"
Joyce naye akauliza kwa mshangao,
"Nimekufa!!"
"Ndio"
"Nani kasema kuwa nimekufa?"
"Baba ndio katuambia hivyo"
Joyce akasikitika sana na kumuangalia mumewe, kisha akamwambia
"Hata kama hunipendi tena, si vizuri kuwatangazia watu nimekufa Deo! Kufa wewe uone kama kufa ni kuzuri"
Muda huo huo Deo akaanguka chini na kufanya wote washtuke, watoto wake walikuwa ni wa kwanza kumfata baba yao pale chini huku wakimtingisha na kulaumu maneno ya mama yao kuwa ndio yamesababisha.
Joy nae aliinama kumuangalia mume wake aliyekuwa hajitambui kwa muda huo ila na yeye hakuelewa kwanini imekuwa hivyo.
Sabrina mkubwa alitulia pembeni huku amesimama, kisha akawaacha pale wakimtingisha Deo na kutoka nje.
Alipofika nje akamuona mtu mmoja aliyekuwa amemgeuzia mgongo, mawazo ya Sabrina yakamtuma kuwa yule mtu ndio yuleyule aliyempa kizunguzungu muda ambao na yeye alianguka njini alipokuwa anaenda hospitali kushuhudia.
Kengele ya hatari ikagonga kwenye kichwa chake, kwa haraka akarudi ndani na kuwazui wote waliomzunguka kaka yake kuwa waende pembeni nao wakatii na kusogea halafu Deo akabaki mwenyewe pale katikati alipoanguka.
Joy akauliza,
"Mbona sielewi mambo ya hapa?"
Sabrina mkubwa akamfanyia ishara ya kidole kuwa anyamaza kimya, naye akatii na kunyamaza kama ilivyotakiwa.
Kimya kile kilitanda kwa dakika kama tano hivi kisha Deo mwenyewe akazinduka alipokuwa ameanguka na kuinuka, kisha akajisogeza kwenye kiti kwani hakuelewa hata ni kitu gani kilichotokea kwake.
Ila bado wote waliendelea kuwa kimya mpaka pale ambapo walisikia kuna mtu akigonga mlango wa pale ndani kisha Sabrina mkubwa akainuka na kwenda kufungua mlango, walikuwa ni watu waliotoka hospitali nao wakashtuka kumuona Joy pale nyumbani
"Mambo gani haya jamani?"
Sabrina akawatuliza na kuwaingiza ndani ili waweze kuzungumza vizuri zaidi.
"Mmetutuma hospitali, mmefanya tuzunguke kila jokofu kumtafuta huyo marehemu. Mambo gani haya kumbe mtu mwenyewe ni mzima kabisa"
Sabrina akajaribu kumtetea kaka yake kwa ndugu hawa
"Jamani naomba mtuwie radhi kidogo kwani kaka yangu alichanganyikiwa tayari ndiomana ikawa kama ilivyokuwa, naomba mtusamehe"
Wengi waliongea sana ila mwisho wa siku wakaelewana na kuondoka.
Sabrina mkubwa alitamani sana kujua kilichomtokea wifi yake kwani hata yeye hakuelewa kitu, moja kwa moja akiwa na kaka yake waliamua kukaa na Joyce na kumuhoji imekuwaje kuwaje hadi kufikia hatua ya kudhaniwa kuwa amekufa. Naye Joy akawaelezea ilivyokuwa,
"Nilitoka hapa nyumbani nikiwa na mawazo sana baada ya Deo kunitimua kuwa nikamtafute mtoto, njiani nikamuona Juma. Sasa ile kuvuka ili nimfate si ndio nikagongwa na pikipiki.
Waliniwaisha hospitali kwakweli na kuanza kupewa huduma vizuri tu ila tatizo likawa nilipozinduka sikumuona ndugu hata mmoja, nikamuuliza nesi akaniambia kuwa mume wangu alikuwepo ila ameondoka kwakweli roho iliniuma sana.
Yule nesi alipoondoka aliletwa mgonjwa mwingine, naye alikuwa kagongwa na pikipiki ila kwavile kitanda nilichokuwa mimi ilikuwa ni sehemu nzuri kwa yule mgonjwa ni hapo nilipoamua kumpisha kisha ndugu zake wakaanza kumtafutia huduma.
Ni muda huo nikapigiwa simu na rafiki yangu ambapo nilishangaa kuona vitu vyangu vyote nilikuwa navyo pembeni ingawa nilikuwa nimepata ajali.
Yule rafiki yangu nilipomwambia nilipo na hali halisi ilivyo aliamua kuja kunifuata, kwavile ana zahanati, moja kwa moja akanipeleka kwenye zahanati yake ili nikaendelee kutibiwa huko.
Hata nilivyorudi hapa ni baada ya kuona kuwa hali yangu ina unafuu sasa."
Sabrina akamuangalia kaka yake Deo kama naye yupo makini katika kusikiliza maelezo ya Joyce, hawakuwa na la kufanya zaidi ya kukubaliana na huo ukweli. Deo akajiuliza kwa mshangao
"Inamaana aliyekufa ni yule uliyemuacha mwanzoni"
Sasa akapata picha kwa kilichotokea kwa mkewe bila kujua kama kule kuondoka kwa mkewe pale hospitali palimsaidia sana kwani kifo chote kilikuwa juu yake kwahiyo yule aliyekufa ilikuwa ni badili yake lakini hakuna hata mmoja aliyejua hilo zaidi ni kushukuru tu kwa kurudi kwa Joy.
Siku hiyo ikapita kwa mtindo huo huku kila mmoja akiwa na mawazo sana.
Sabrina mkubwa aliondoka ila alihitaji sana kumjua yule mtu ambaye alikuwa akiwafatilia na akasema kuwa lazima atamjua na akishamjua ndio ataamua ni kitu gani afanye.
Nyumba yao ilirudi katika hali ya kawaida baada ya mambo yote kupita na kufanya wajisikie amani kidogo bila kujua kama adui bado hajajulikana kuwa ni nani na analengo gani kwao.
Sabrina mtoto wa Joyce kuna mambo yaliyomchanganya sana na kuhisi kuwa kuna kitu anakijua ila haelewi kuwa hicho kitu ni kitu gani na kina mpango gani katika maisha yake.
Baada ya hali kuwa shwari kabisa hata wale watoto wao wawili kurudi shuleni ambao walikuwa wakisoma shule ya bweni.
Sasa ndio Joyce alipoamua kwenda kumtazama Sakina kwani hakuweza kuonana nae tangia siku amejifungua.
Alimkuta Sakina akiendelea kupata huduma ya uzazi kama kawaida ya wanaojifungua na huduma wanazopatiwa.
Joy alitamani sana kujua ni kitu gani kilitokea wakati ambao aliondoka na Sabrina, aliona ni vizuri akielezwa muda huo kwani mtoto wa Sakina alikuwa amelala
"Kwani Sabrina hajakueleza?"
"Kwakweli sijui hata nikwambie nini kuhusu huyu mwanangu ila kwa kifupi ni kama amechanganyikiwa hivi maana hata mimi simuelewi na kila ninapomuuliza huwa hasemi chochote"
Ikabidi Sakina amsimulie kwa kifupi ilivyokuwa na kumfanya Joyce ashtuke sana
"Mmmh mbona hayo mambo ni kama ushirikina?"
"Hata mimi nahisi hivyo kuwa kuna ushirikina unaendelea hapa kati yetu ila nitajua tu hata usijali mama James"
Ila kilichomsikitisha zaidi Joyce ni kile kitendo cha kumpeleka mwanae kwenye chumba cha uzazi kwani alijua lazima mwanae kaenda kuona mambo makubwa ambayo hakupaswa kuyaona ila ndio hivyo ilivyotokea.
Joy aliondoka pale akiwa na maswali mengi sana dhidi ya mwanae ambaye alionekana dhahiri kutokuwa sawa.
Joy alipofika ndani kwake alijaribu tena kumuuliza Sabrina maswali mawili matatu ambayo yote hakupata majibu yanayoeleweka toka kwa mwanae
"Ni kitu gani ulikiona wakati Sakina anajifungua?"
"Sikuona chochote"
Alijaribu hata kumbembeleza ila mtoto hakusema kitu chochote kile na kumfanya Joy azidi kupatwa na mawazo kwani alihitaji kujua kuwa mwanae anajua nini ili ajue jinsi ya kumsaidia ila tatizo la mwanae hakutaka kusema ukweli wowote na kila alichoulizwa alidai kuwa hajui kitu wakati hata mama yake alihisi kuwa kuna kitu mwanae anakijua ila hataki kukisema kuwa ni kitu gani.
Joy akajisemea kuwa atakijua tu kinachomsumbua mtoto wake.
Kuna siku Joy alikaa tena na mwanae akamsikia akisema
"Mimi sitaki kuolewa wala kuzaa"
Joy akamshangaa sana mwanae na kumuuliza kwa makini ila hakujibu chochote kuwa amesema kitu gani
"Ila nimekusikia Sabrina, hebu niambie kwanini unasema hivyo"
Sabrina aliendelea kuwa kimya.
"Hivi umemuona tena mtoto wa Sakina alivyopendeza?"
"Anaitwa Jeff"
"Kumbe anaitwa Jeff!! Sikujua jina lake mwanangu. Umemuona tena alivyokuwa mzuri?"
Sabrina akatingisha kichwa kuwa hajamuona tena
"Basi badae tutaenda pamoja kumuangalia mwanangu. Sawa mama!"
"Sawa"
Joy alitamani sana kujua anachojua mtoto wake ila hakuweza kukijua kabisa kwani mtoto wake hakuwa muwazi kwa anachokifikiria muda wote.
Inaendelea.....
Mwandishi ni
ATUGANILE MWAKALILE
No comments: