Simulizi : Je Haya Ni Mapenzi!! Sehemu Ya Kwanza (1)

Mimba yake ndio iliyosumbua wengi sababu alijikuta akimchukia kila mtu aliyemuona mbele yake, hata mume wake alimchukia kasoro binti mmoja mdogo ambaye ni mtoto wa mwenye nyumba anayoishi Sakina.
Alimpenda sana huyu binti aliyekuwa na umri wa miaka kumi kwa kipindi hicho na alijulikana kwa jina la Sabrina.

Kila kitu ambacho Sakina alikitaka alipenda achaguliwe na Sabrina.
Kitendo cha Sakina kuwa karibu sana na Sabrina kilikuwa kinamkera sana mzazi wa Sabrina aliyeitwa Joyce, hakupenda kabisa mwanae awe karibu vile na Sakina kwani alijua wazi kuwa Sakina atamfanya mwanae kama mtumwa wake ila hakutaka kusema sana kwavile alimuhurumia Sakina kwa ule ujauzito aliokuwa nao kwani mimba zingine huwa zinafanya mtu awe vile kama alivyo Sakina.

Mume wa Sakina nae alikerwa sana na tabia ya mkewe kwani kila alichokifanya yeye mkewe hakukitaka, hata kama akimletea kitu alikuwa anakikataa hadi amuite Sabrina na kumuomba amkabidhi hiko kitu kwa niaba yake, kwakweli hii hali ilimkera na kumfanya aombe usiku na mchana mkewe ajifungue mapema ili awewe kuepukana na hiyo hali.
Bwana huyu alijulikana sana kutokana na tabia yake ya ucheshi, mtaa mzima walimjua Juma kwahiyo tabia ya mkewe pia ikajulikana mtaa mzima na kufanya watu wengi kumsema kwa mazuri na mabaya.

Sakina alikuwa na imani kuwa atajifungua mtoto wa kike kutokana na mapenzi yake kwa Sabrina hivyobasi akaahidi kwamba atakapojifungua huyo mtoto atamuita Sabrina ili tu iwe kama kumbukumbu katika maisha yake.
Sabrina nae alifurahi kwani hata yeye alimpenda sana huyu dada.
Wakati Sakina na Sabrina wakizungumza kwa furaha, Joyce ambaye ni mama wa Sabrina alimuita mwanae kwa nguvu sana ikabidi Sabrina aende kwa mama yake
"Hivi siku hizi huna masomo ya ziada ya shule?"
"Ninayo mama ila nishafanya na kumaliza"
"Kwahiyo ukimaliza ndio unapata muda wa kwenda kuongea na wajawazito! Yani wewe mtoto hata sijui una matatizo gani jamani"
Wakati akiongea hayo, simu yake ikaita na kufanya aache kuzungumza tena na Sabrina hivyo kumfanya huyu mtoto nae arudi kule kwa Sakina.

Sakina alimuomba Sabrina waende mahali, naye Sabrina hakuweza kukataa kwani alikuwa bado mdogo na hakuwa na uelewa wa mambo mengi yanavyokuwa kwahiyo alikubali na kwenda kujiandaa kimya kimya kisha akaondoka bila ya kumuaga mama yake kwani anajua kwa vyovyote vile akimuaga tu lazima atamkataza wakati yeye safari anaitaka.
Kisha yeye na Sakina wakaondoka na kutokomea.

Simu ambayo Joyce aliipokea ilikatika bila mpigaji kuongea chochote kitu hicho kilimfanya Joyce ampigie mumewe na kumuomba amrushie muda wa maongezi ili aweze kuzungumza na huyo mpigaji.
Alipotumiwa, akaipiga ile namba na akapokea mtu ambaye alimfahamu,
"Wifi habari!"
"Kumbe ni wewe! Mbona umetumia namba mpya?"
"Maelezo ni marefu hapo, je Sabrina yuko wapi?"
"Nadhani atakuwa nje, umemkumbuka wajina leo?"
"Nakuomba usimruhusu aende mahali popote wifi"
Kisha akakata simu na kumfanya Joyce amshangae, huyu aliyepiga aliitwa Sabrina na ndiomana alipomuulizia Sabrina mama yake akamuuliza kama amemkumbuka wajina wake.
Huyu alikuwa ni wifi wa Joyce yani ni dada wa mumewe.
Kutokana na ile siku kakatwa bila ya kumaliza maongezi ikabidi Joy atoke kwanza na kwenda kumtafuta mwanae ili ajue kama yupo au vipi ingawa mwanzo aliamini kuwa yupo.

Alipofika nje alimuita bila ya kuitikiwa ikabidi amfata jirani yake mmoja na kumuuliza
"Umemuona Sabrina?"
"Ndio nimemuona, kapita hapa muda sio mrefu na yule mpangaji wako"
"Wameelekea wapi?"
"Nadhani wameelekea stand"
"Jamani huyu mtoto ataniua mimi mwaka huu, mbona amekuwa wa ajabu kiasi hiki jamani! Yani aondoke bila kuaga! Ameanza lini hiyo tabia jamani!"
"Labda hawajaenda mbali sana, usiwe na mawazo sana jirani atarudi tu si yupo na mtu mzima"
"Mtu mzima gani? Yule Sakina hajielewi kabisa na ile mimba yake, asije akamuacha mwanangu njiani sijui nitamueleza nini baba yake"
Joyce alirudi ndani huku akiwa na mawazo sana kuhusu binti yake, akaamua kuchukua tena simu na kumpigia wifi yake ila safari hii akampigia kwa simu yake tofauti na ile namba ya mwanzo.
Ile simu ilipokelewa na mume wa Sabrina, moja kwa moja Joyce alimueleza mume wa Sabrina alivyoambiwa na wifi yake huyo kuhusu mwanae na huyo mwanae ameshatoka bila hata ya kuaga.
Mume wa wifi yake akamjibu,
" Usiumizwe akili na ulichoambiwa na wifi yako kwani hata mimi simuelewi sijui akili yake imekuwaje lakini usishangae sana, si unajua huyu wifi yako ni wa mauzauza tangia zamani!"
"Natambua hilo, ila inabidi kumsikiliza mara nyingine kwani huwezi jua kwanini kasema hivyo"
"Asikuumize akili nakwambia, mimi ndio mumewe namjua huyu vizuri najua hata wewe wamjua sijui umeshasahau mauzauza yake? Ana mwezi mchanga huyu, usijali mwanao atarudi tu tena salama kabisa"
Wakaongea na kuagana ila wazo la kuambiwa kuwa ni mauza uza ya wifi yake bado lilimpa mashaka kwani hakufikiria kama mauza uza hayo yangemfanya apige hadi simu na kumueleza yaliyopo ila bado alikuwa na mashaka na wifi yake huyo kwani kuna kipindi aliwahi kuisumbua sana familia yake kwa mauzauza aliyokuwa nayo kwahiyo alimuamini nusu kwa nusu sababu mengi aliyokuwa akisema kwa kipindi hiko cha nyuma yalikuwa na ya kweli.
Joy alifikiria sana ila hakuwa na jibu la moja kwa moja huku akilalamikia majina ya kurithi
"Ndiyo tabu ya kurithisha watoto majina hii, yani huyu mwanangu akili zake zimekuwa waruwaru kama shangazi yake ila yeye uwaruwaru umemuanza mapema jamani. Mmmh sijui nimbadilishe jina! Ila hawatanielewa hawa, ngoja nitulie nione itakavyokuwa"

Joy alitulia kwa muda ila Sakina hakurejea wala Sabrina na kuzidi kumpa mashaka, akataka kumpigia simu Sakina lakini akakumbuka kwamba Sakina hana simu kwani aliwahi kuivunja kipindi anagombana na mumewe
"Huyu Sakina akili yake sio nzuri kabisa yani sijui kama mwanangu atakuwa salama jamani, mbona ni majanga haya!"
Aliendelea kusubiri na kusubiri lakini hawakurejea na kuzidi kumpa mawazo yasiyo na kikomo.

Mume wa Sakina alirejea nyumbani kwake lakini Sakina hakuwepo na kumfanya huyu bwana apatwe na maswali kuwa mkewe amekwenda wapi. Moja kwa moja alienda kwa mama mwenye nyumba yao kumuuliza,
"Samahani mama James"
"Bila samahani"
"Eti Sakina umeelekea wapi?"
"Hata sijui, tena ameondoka na binti yangu jamani mwanangu akipotea sitakuwa na utu na nyie. Mtoto mwenyewe wa kike ninaye mmoja tu halafu mkeo anaondoka naye tena bila hata ya kuaga, tutaonana wabaya hapa jamani"
Juma alimuangalia tu huyu mama na kubwabwaja kwake kwani alitakiwa kumjibu mara moja ila aliweka maelezo mengi sana, ikabidi Juma aage ili aende kumtafuta mkewe.
"Ndio nishakwambia hivyo, nataka mwanangu arudi akiwa salama kabisa msiniletee mie hayo mabalaa yenu jamani msiniletee kabisa"
Joy aliongea sana kwa uchungu wa mwanae na pia hakujua atamueleza nini mumewe atakaporudi na kumuulizia binti yake huyo maana alimpenda sana na hakuweza kufanya chochote bila kumuulizia binti yake, hilo ndio jambo pekee lililompa mashaka mama wa Sabrina.

Juma hakutaka kupoteza muda, hivyo akajiandaa na kwenda kumtafuta mkewe kwani kwa ndugu zao wote alikupiga simu aliambia kuwa mkewe hajafika hivyobasi akaamua kwenda kumtafuta mwenyewe ingawa hakuwa na uelekeo sahihi wa mahari alipo.
"Yani huyu mwanamke asingekuwa na ujauzito wangu hata nisingejisumbua kumtafuta, bahati yake ana ile mimba sijui mimwanamke mingine ikoje jamani laiti ningejua hii adha ya huyu mwanamke nisingemuoa jamani. Ila dawa yake inakuja, akijifungua tu namuolea mke mwenza ili akili imkae sawa"
Juma alikuwa akiongea kwa hasira sana kwani hakupendezwa na tabia aliyokuwa nayo mkewe kwa hiki kipindi cha mimba yake.
Aliondoka bila uelekeo wa maana kumtafuta mke wake.

Huku Joy naye hakuwa na raha kabisa, akaamua kumpigia tena wifi yake simu kwa ile namba mpya naye akapokea ile simu
"Hebu niambie vizuri kuhusu mwanangu Sabrina"
"Kwani yuko wapi?"
"Ameondoka"
"Ameondoka!!" Akauliza kwa mshangao.
"Ndio ameondoka tena bila hata ya kuniaga jamani"
"Umemuacheje wifi hadi aondoke jamani wakati nilishakupa tahadhari!"
"Jamani wifi yangu hakuniaga jamani"
"Ulitakiwa kuwa makini, unadhani itakuwaje sasa?"
Halafu akakata simu na kumfanya Joy apatwe na mawazo zaidi, wazo likamjia na yeye na kumfanya ajiandae na kwenda kumtafuta mwanae ingawa hakujua pia kama aanzie wapi na aishie wapi kwani hakuelewa kabisa kuwa wameelekea sehemu gani.

Sakina na Sabrina walielekea sehemu moja kulikuwa na miti mingi sana kisha Sakina akamwambia Sabrina dhumuni la yeye kwenda naye huko
"Sikia Sabrina, najua wewe ni mtoto mdogo sana na hujui chochote kuhusu maswala ya uzazi. Umeona hili tumbo lilivyokubwa!"

Huku akilishikashika tumbo lake, Sabrina akaitikia kwa kutingisha kichwa kuwa ameliona.
"Basi hii inaitwa mimba au ujauzito, nimebeba mtoto humu tumboni. Nimekaa kwa muda kidogo nikiwachukia watu wote na kukupenda wewe tu, wengi hawapendezwi na tabia yangu ila mimi nimejikuta tu nikiwachukia"
"Ila mbona zamani kabla ya kuwa na hilo tumbo uliwapenda?"
"Ni kweli, kwamaana hiyo hili tumbo ndio limefanya niwe hivi. Nimekuja huku sababu marehemu bibi yangu alipenda sana kuja huku pindi anapokuwa na tatizo la aina yoyote ile, aliamini akija huku atapata suluhu la tatizo lake. Nami nimekuja huku kujiombea niweze kujifungua mapema ili niepukane na haya mambo ya kuchukizana na majirani na watu wengine. Nahitaji huyu mtoto atoke, awe mtoto mzuri kama wewe na awe na upendo kama mama yake hapa"
Sabrina akacheka kwa furaha baada ya kusikia kuwa mtoto atoke akiwa mzuri kama yeye huku akijipa sifa moyoni mwake kuwa kumbe yeye ni mzuri hadi anasifiwa na watu akatamani hata aletewe kioo ajitazame tena ila ndio hivyo walikuwa kwenye kipori kidogo.
Wakaongea mambo mengi sana wakiwa huko hata kusahau kama wanatakiwa kurudi, kuja kutahamaki muda nao ulikuwa umekwenda sana hivyo ikabidi Sakina amshtue Sabrina na kuanza safari ya kurudi nyumbani.

Wakati wapo njiani gafla wakaona kitu cha kustaajabisha sana na kufanya washtuke.
Kuangalia vizuri kile kitu lilikuwa ni lile joka kubwa ambayo hujulikana kwa jina la chatu.
Uoga ukawajaa wote wawili, Sabrina kukimbia angeweza ila je angeelekea wapi maana walipokuwa wanaenda mbele yake ndio alikuwepo huko chatu. Huyu Sakina ndio kabisa angewezaje kukimbia na lile tumbo lilivyokuwa kubwa, ila wakaamua kukimbia hivyo hivyo.
Kugeuka nyuma yule chatu alikuwa akiwakimbiza, kitendo hicho kilimfanya Sakina aanguke vibaya sana na ubaya zaidi ni kuwa alimuangukia Sabrina

Kugeuka nyuma yule chatu alikuwa akiwakimbiza, kitendo hicho kilimfanya Sakina aanguke vibaya sana na ubaya zaidi ni kuwa alimuangukia Sabrina.

Sabrina alipiga kelele ya maumivu kutokana na uzito aliokuwa nao Sakina, kelele ambazo zilisikika kwa nguvu na kukatika gafla kwani alikuwa amezimia pale pale.
Kitendo kile kilimtoa jasho Sakina na kuzidi kummaliza nguvu, alijisogeza kwa shida na kumuangalia Sabrina ambaye alikuwa hajitambui kabisa.
Sakina akasahau hali yake na kuanza kuwaza kuhusu huyu mtoto wa watu kuwa itakuwaje, alipomtazama yule chatu aliyekuwa akiwafuata hakuonekana tena na kumfanya Sakina ajiulize kuwa ni kitu gani hiki au ni mauzauza tu kati yao bado hakujielewa.

Wakati anajitahidi kuinuka pale chini ili aweze kumuinua na Sabrina, alijikuta amelowa damu na kufanya azidi kuogopa huku mawazo mabaya yakimjia kuhusu kiumbe chake tumboni. Hakuwa na la kufanya zaidi ya kujaribu kujikongoja ili tu yeye na Sabrina watoke eneo lile na waweze kufika eneo ambalo watapata msaada ila atambebaje Sabrina aliyezimia huku na yeye ana mimba kubwa ya kujifungua! Hapo ndio ikawa kazi kubwa sana kwa Sakina huku akiomba Mungu awapatie msaada wowote ule pale walipo ili waweze kupona.
Joyce alitafuta hadi kuchoka na kuamua kurudi nyumbani huku akiwa na mawazo mengi sana kuhusu binti yake na kujisemea
"Yani wakirudi tu nawapa notes wahame kwenye nyumba yangu siwezi kuvumilia huu upuuzi kwakweli. Sijui nitamueleza nini baba yake mimi jamani mmh!"
Wakati akiyawaza hayo, mumewe nae alirudi muda huo huo na kumkuta mkewe akiwa kajiinamia tu.
Alimuulizia kilichomsibu ila Joyce hakutoa jibu la maana lakini mumewe hakusumbuliwa na jibu la mkewe kwani alikuwa na nia ya kumuona binti yake kwakuwa haikuwa kawaida kwa yeye kurudi na kukuta nyumba kimya kiasi kile ikabidi aulize kwanza
"Yuko wapi Sabrina?"
Hapo ndio palimfanya bi.Joyce ajiume vizuri zaidi kwani hakujua hata amjibu nini ila mwisho wa siku aliamua kumueleza tu mumewe ukweli.
"Unasemaje wewe?"
"Sabrina hayupo"
"Unajua ni saa ngapi saizi?"
Joyce akainua macho na kutazama mida, ilikuwa ni saa mbili usiku. Akashindwa hata kumjibu mumewe kuhusu muda
"Hivi unaakili kweli wewe mwanamke? Yani mwanangu hayupo nyumbani na usiku ushaingia halafu wewe umekaa umejiinamia bila kufanya chochote!"
Joy alijaribu kumueleza hali halisi mume wake lakini huyu mwanaume aliyeitwa Deo hakutaka kabisa kumsikiliza mkewe kwa chochote alichokisema badala yake alimpa kauli moja tu
"Naomba upotee kwenye nyumba yangu hadi pale utakapomrejesha binti yangu, usitake kufanya nikatenda dhambi bure. Tafadhari sana potea kwenye macho yangu"
Aliongea kwa ukali sana na kufanya Joy atetemeke na kuondoka kwenda kumtafuta Sabrina ambaye hata hakujua aanzie wapi na aishie wapi.

Joyce alikuwa na mawazo sana ya binti yake na jinsi mumewe alivyompenda mtoto huyo kwa vyovyote vile kama asipopatikana basi ndoa yake itakuwa imefika mwisho kwani mumewe alimuona kamavile ni mwanamke mzembe asiyejua kuitunza familia yake.
Joyce alitembea tu huku mawazo mengi yakiichanganya akili yake na kujihisi kamavile akili yake imetoweka kwani haikuwa sawa kabisa.
Akitembea huku na kule bila ya kujielewa, akamuona mtu mmoja upande wa pili wa barabara na kujihisi kuwa anamfahamu mtu huyo, akajaribu kuvuka barabara ili kumuwahi mtu huyo ila kabla hajamaliza kuvuke ile barabara alijikuta akipitiwa na pikipiki kisha akaanguka na kupoteza fahamu.
Wasamalia wema wakamuwahi na kumkimbiza hospitali.

Deo alitulia nyumbani kwake huku akilaumu akili za mke wake kwa kumuacha mwanae aende mahali pasipoeleweka
"Na akirudi hapa bila mwanangu ajue talaka itamfata kwao"
Kwakweli hali haikuwa shwari kabisa.

Muda nao ulizidi kwenda na kumfanya Deo azidi kupatwa na mawazo dhidi ya mwanae ingawa alikuwa na watoto wengine ila huyu alimpenda zaidi, labda kwavile mtoto huyu alifanana na mdogo wake aliyempenda pia hata jina la mtoto huyu lilikuwa ni jina la mdogo wake mpendwa na kumfanya Deo azidi kumpenda binti yake huyu.
Swala la binti yake kutokujulikana alipo lilimpa mashaka sana na kumfanya apate maswali bila ya majibu, alitamani binti yake arudi ili apate furaha ya moyo ila hakurejea binti yake wala mke wake na muda nao ulizidi kuyoyoma bila ya taarifa yoyote.
Akaamua kumpigia mkewe simu lakini hakupatikana na kumfanya Deo wasiwasi umdhidi kwa kumfikiria binti yake mpendwa.
Alitulia akitafakari cha kufanya kwa muda huo maana naye alihisi kuchanganyikiwa.

Juma naye aliendelea na swala la kumsaka mke wake bila ya tumaini lolote la kumpata.
Aliendelea kumsaka mkewe kila mahari huku akiwaza usalama wa kiumbe chake kwenye tumbo la mke wake.
"Najuta kuoa mwanamke mwenye akili fupi kama Sakina, ona ambavyo ninapata shida hapa"
Alimsaka kila mahali bila ya mafanikio ya kumpata wala ya kujua mahali alipo.
Wakati alipokuwa akikatisha barabarani ndipo aliposhangazwa na lile tukio la ajali, aliposogea karibu akagundua kuwa ni mama mwenye nyumba wake kagongwa na pikipiki, ni hapo aliposaidiana na wasamalia wema wengine kumpeleka hospitali kwani hali yake ilikuwa mbaya sana.

Juma naye hakujielewa kabisa kwani ile hali ilizidi kumchanganya akili yake, mambo ambayo yalikuwa yakimtokea sasa alikuwa akiyahisi kamavile ni ndoto na hakujua kwanini imekuwa kama ilivyokuwa.
Hakupata jibu kwa mawazo yake yote aliyoyawaza ikabidi ampigie simu baba mwenye nyumba wake ambaye ni mume wa Joyce yani yule mwanamke aliyepata ajali.

Deo akiwa bado na mawazo, alishtuliwa na simu aliyopigiwa na Juma na kumfanya azidi kuchanganyikiwa kwa ule ujumbe kuwa mkewe kapata ajali.
Alijilaumu sana kwa kitendo chake cha kumtimua mke wake kuwa akamtafute mtoto wao, alihisi kuchanganyikiwa sasa ikabidi aende huko hospitali ili kujua hali ya mkewe kuwa anaendeleaje.

Bado hali ilikuwa tete kwa upande wa Sabrina na Sakina kwani Sabrina alikuwa bado hajitambui kutokana na kuangukiwa na Sakina aliyekuwa na uzito mkubwa hata msaada nao haukupatikana na kumfanya Sakina azidi kuchanganyikiwa kwani giza lilitawala kila mahari, kwakweli Sakina alihisi kuwa anaenda kufa yeye na Sabrina wake.
Ingawa alijitahidi kujikongoja ila bado alishindwa kutoka kwenye kile kichaka kutokana na maumivu aliyokuwa nayo na vilevile hakuweza kumuacha Sabrina, aliamua kukaa chini huku akimuomba Mungu tu amsaidie yani alijitoa kwa jambo lolote lile kwa muda huo.
Alitulia huku machozi yakimtoka, lakini sala zake zilimsaidia kwani walitokea wawili na kupita njia hiyo kwakweli halikuwa jambo la kawaida ila ndio hivyo wakapata msaada na safari ikawa ni moja tu yani kukimbizwa hospitali.

Walipofika hospitali moja kwa moja Sakina alikimbizwa kwenye wodi ya wazazi kwani ilionyesha kuwa angejifungua muda sio mrefu.
Sabrina naye akafanyiwa huduma na kuzinduka huku akijishangaa tu kwani hakujielewa kabisa.
Manesi walitafuta mawasiliano ya watu wa karibu na hawa na moja kwa moja wakampata Juma na kumpa taarifa kuhusu mkewe na huyu binti mdogo Sabrina.
Juma alishukuru kwa taarifa na moja kwa moja akazifikisha kwa Deo pia yani baba mwenye nyumba yake ili ajue alipo binti yake Sabrina, kwahiyo wakamuacha Joyce pale hospitali akiendelea kuhudumiwa na kwenda kuwaona hawa wengine ambao hawakuelewa hali zao.

Sabrina alifurahi sana kumuona baba yake, ikabidi akae nae pale hadi alipomalizwa kuhudumiwa ila muda nao ulikuwa umekwenda sana na haikuwa rahisi kurudi kwenye ile hospitali ya mwanzo ambako Joy alilazwa kwahiyo wakangoja iwe alfajiri kidogo ndio waondoke ili kuepusha majanga mengine.

Hali ya Sakina kwenye chumba cha uzazi haikuwa nzuri kabisa kwani hakujifungua muda ule waliofikiria wala nini na aliendelea kutokwa na damu tu.
Hali ile iliwapa mashaka manesi wa pale kwani muda nao ulipita hadi pakakucha bila Sakina kujifungua, na kila wakipima wanaona mtoto yupo mlangoni huku mama mtu akizidi kuvuja damu tu.

Madaktari wakakaa na kushauriana kuwa ili kuokoa maisha ya mama na mtoto itabidi operesheni ihusike mahali hapo kwani imeshashindikana kwa mwanamke huyu kujifungua kwa njia ya kawaida.
Wakamuita Juma na kumuelezea hali halisi ambapo alikubali tu mkewe afanyiwe operesheni kwani hata yeye aliweza kushuhudia jinsi hali ya mke wake ilivyokuwa mbaya.

Inaendeleaah.....



USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.