Simulizi: Je haya ni mapenzi sehemu ya 11


Joy aliporudi alishangaa kumkuta mwanae akiwa analia kiasi kile tena akiwa na alama za kupigwa kwenye mwili wake.
"Sabrina mwanangu nini tatizo?"
Sabrina hakuweza kuelezea kwa wakati huo na kujikuta akizidi kulia tu,
"Nyamaza mwanangu, kichwa kitakuuma jamani. Nyamaza dada"
Joy alijitahidi pale kumtuliza mwanae na kumbembeleza hadi Sabrina akatulia kabisa ila bado alishindwa kuelezea anavyojisikia kwenye moyo wake kwani alihisi kama kuna kitu kimemkaa kooni na kumfanya ashindwe kusema.
Macho yake yalivimba sababu ya kulia sana.
Kisha Joy akamshauri mwanae kwenda kupumzika ili kuweza kupoteza yale mawazo ambayo yanamsumbua na kumtesa kwa wakati huo.
Sabrina akainuka na kwenda kulala.

Kwenye mida ya saa tatu usiku alienda kuamshwa na mama yake ili aweze kwenda kula.
Alitoka ndio na kula kwa kiasi kidogo sana kwani mawazo bado yalimsumbua.
Aliporudi chumbani kwake ili alale, alikuta ujumbe mfupi umetumwa kwenye simu yake kutoka kwa John,
"Kumbe yule mwanamke wa jana alikuwa ni mwanamke wa mpenzi wako, nasikia mimba yake imetoka. Najua utakuwa na mawazo kama hukukusudia ila kama ulikusudia utakuwa na furaha ila hukufanya vyema kwakweli. Kumbuka yule hana kosa lolote, ni mwanamke tu kama wewe. Yakupasa ukamuombe msamaha, yangu ni hayo tu Sabrina. Usiku mwema, ila ulivyo na mambo uliyoyafanya havifanani"
Sabrina aliumia tena kuona kila mtu akimpa lawama kwa jambo ambalo sio kosa lake kabisa, alijisikia vibaya sana.
Hakuweza kulala tena, na alikuwa akijizungusha tu usiku kucha kwani kila upande aliogeuka alijiwa na mawazo yale yale ukizingatia hakutaka mama yake aujue ukweli kuhusu Japhet wala yule mwanamke ambaye mimba ilitoka.

Kulipokucha, Sabrina aliamka na kuoga huku akili yake bado ikiwa na mawazo yasiyo na majibu wala mwisho.
Akapigiwa simu na rafiki yake Sia, akajua wazi kuwa mambo ni yale yale tu. Akatamani asipokee ila aliamua kupokea ili asikie naye atakavyomponda,
"Pole sana Sabrina, nimesikia yaliyotokea. Ila sijaamini kwakweli, na siwezi kuamini kabisa. Sabrina nakufahamu rafiki yangu, najua wazi huwezi kufanya haya niliyoyasikia"
"Ndio hivyo Sia, hata mi mwenyewe sielewi. Kila mtu ananichukia kwa kosa ambalo sio langu"
"Usijali, nitakuja ili tuongee vizuri. Najua wazi huwezi kufanya hivyo Sabrina, utakuwepo kwenu lini ili nije?"
"Nipo Sia, saa yoyote ile ukija utanikuta"
"Sawa nakuja kwenye mida ya saa kumi rafiki yangu"
Huyu akamfanya Sabrina ajisikie vizuri kiasi kwni hali yake ilikuwa mbaya sana mwanzoni,
"Nashukuru Mungu, rafiki yangu Sia ananielewa jamani"
Kidogo muda huu Sabrina akapata nguvu ya kufanya baadhi ya mambo yake huku akimngoja huyo Sia ili aweze kumueleza yote yaliyopo kwenye moyo wake.

Sabrina alikaa na mama yake kuzungumza mawili matatu,
"Nimeongea na baba yako kasema amechelewa kutupa taarifa, ila wiki ijayo unatakiwa kuanza chuo. Kwahiyo mwishoni mwa wiki hii utasafiri mwanangu. Sawa!"
"Sawa mama, hiyo ni khabari njema kwangu na nimefurahi sana mama"
"Usijali mwanangu, kwahiyo hao mashoga zako sijui wakina nani nani huko uwaage kabisa. Sio siku inafika, nawe uanze porojo zako"
"Hakuna tatizo mama"
Mara mlango wao ukagongwa, moja kwa moja Sabrina akajua kuwa ni Sia tu anayegonga mlango na kwenda kumfungulia.
Ni kweli Sia alikuwa mbele, nyuma yake walikuwepo wale wadada wawili waliompiga Sabrina na yule aliyekuwa mjamzito siku mbili zilizopita.
Sabrina akashtuka sana baada ya kumuona mtu mwingine aliyekuja na hao watu akiwa amevalia mavazi ya kipolisi.


Sabrina akashtuka sana baada ya kumuona mtu mwingine aliyekuja na hao watu akiwa amevalia mavazi ya kipolisi.
Sabrina alikuwa kama mtu aliyepigwa na bumbuwazi kwani hakuelewa kabisa kuwa kwanini Sia aje na hao watu, na kwanini aje na polisi!
Wakati Sabrina akistaajabu hayo, Sia akasogea karibu na kuwaambia wale wenzie
"Sabrina ndio huyo hapo"
Yule polisi akamsogelea Sabrina na kumuuliza yule binti ambaye mimba ilitoka
"Msichana mwenyewe ndio huyu?"
Yule binti akajibu huku akiwa kama machozi yanamlenga lenga,
"Ndio huyo huyo"
Yule askari, akamshika Sabrina na kumwambia,
"Upo chini ya ulinzi, unahitajika kituoni"
Sabrina hakuelewa kitu kawani alikuwa anashangaa tu na kuona mambo yale kama ni ndoto tu kwake.
Alijikuta akiuliza,
"Kwani nimefanyaje jamani!"
Yule askari akamjibu kwa ukari,
"Utajua huko huko kituoni"
Joy nae muda wote alikuwa akishangaa tu kwani hakuelewa kabisa kuwa ni kitu gani kinaendelea, akazuia mwanae asipelekwe kituoni lakini ilishindikana.
Alihisi kuchanganyikiwa kwakweli, akamuangalia Sia na kumuuliza
"Yani wewe ndio unamfanyia hivi rafiki yako?"
Ila Sia hakumjibu chochote mama huyu na safari ya kwenda kituoni iliendelea.

Walipofika, moja kwa moja wakampeleka Sabrina rumande na kumfanya Joy azidi kuchanganyikiwa.
Akamfata askari mmoja na kumuuliza,
"Kwani binti yangu amefanya nini jamani?"
"Inamaana hujui kama mwanao ameua!"
"Ameua? Kamuua nani?"
Yule askari akacheka, kisha akanyoosha kidole huku akimuonyesha Joy yule msichana ambaye alikuwa mjamzito,
"Umemuona yule binti pale! Alikuwa na mimba yule, sasa inasemekana mwanao alikuwa na mahusiano na mchumba wa yule binti. Mwanao asivyokuwa na akili sasa, alimuibia mwenzie mwanaume halafu siku hiyo kamkuta mwenzie njiani nasikia akamsukuma na kumponda na kitu kizito tumboni kisha akakimbia. Ndio hapo mimba ya huyo binti ikatoka, je sio uuaji huo?"
Joy alitulia kimya huku machozi yakimlengalenga, alijisikia vibaya sana kusikia hivyo vitu ambavyo ni tofauti kabisa na alivyosimuliwa na mwanae kabla.
Joy akainuka pale na kuomba kuzungumza kidogo na mwanae, kwa bahati wakampa nafasi hiyo.
Sabrina alipoitwa kwa mama yake alikuwa akilia tu na kufanya ashindwe kabisa kuzungumza na mama yake hata pale walipomrudisha tena rumande alikuwa akilia tu.

Joy ilibidi ajikaze na kujipa moyo ili aweze kufanya kitu cha kumsaidia mtoto wake.
Akamfata yule binti inayesemekana kuwa mimba imetoka.
"Mwanangu, unauhakika kweli Sabrina alikusukuma na kukupiga na kitu kizito tumboni?"
"Ndio, Sabrina kaniulia mwanangu"
Huku akijiliza liza pale.
Joy alimuangalia tu huyu binti kisha akamwambia,
"Kama uyasemayo yana uongo ndani yake basi jua kwamba Mungu anatambua hilo naye ndiye atakayetoa hukumu"
Kisha Joy akaondoka eneo lile, akatafuta eneo la utulivu ili aweze kumpigia simu mumewe na kumwambia yaliyojiri.

Sabrina alikuwa akilia tu huku akiwaza yote yaliyotokea nyuma, hakuelewa kwanini rafiki yake Sia amegeuka kiasi kile na kuamini maneno ya watu kuwa rafiki anaweza kugeuka na kuwa adui kwa dakika moja tu.
Sabrina hakuweza kukaukwa na machozi, alikumbuka hadi jinsi Fredy alivyokuwa akimzuia kuwa asiende ila kwa kiburi chake akaenda na kukutana na hayo yaliyomkuta sasa.
Alitamani siku zirudishwe nyuma ili awe Sabrina mpya ila ndio hivyo tena alikuwa rumande tena kwa kosa asilohusika nalo.
Alijikuta akiyachukia mapenzi, na kujiapia kule rumande kuwa hatokuja kupenda tena katika maisha yake yote yaliyobaki.

Khabari ya mwanae kupelekwa rumande ilimsikitisha sana Deo, na vile alivyoambiwa kuwa dhamana imeshindikana kwahiyo mtoto wake atalala rumande kulimfanya aombe likizo ya dharura ili aweze kwenda kumsaidia mtoto wake aliyejua wazi kuwa hana hatia.

Sakina nae alisikitishwa sana na khabari hii, alijua wazi kuwa Sabrina amesingiziwa tu.
Alikuwa akijisemea tu,
"Maskini Sabrina sijui ana damu ya kuchukiwa jamani!! Wachawi wamemfatilia wee hadi basi, saivi kaanza kufatiliwa na watu wa kawaida hadi kufikia hatua ya kumsingizia mmh!"
Kumbe Joy alikuwa akimsikiliza Sakina kwa makini na kujikuta akisema,
"Umeona eeh! Mwanangu anaonewa jamani hata sijui amewakosea nini watu hawa hadi wanafikia kumfanyia hivi mtoto wangu!!"
Wote wakajikuta wakisikitika kwa pamoja kwani jitihada zote walizokuwa wakizifanya kwaajili ya dhamana ziligonga mwamba na kufanya siku hiyo Sabrina alale rumande.
Joy aliumia sana tena sana hata hakutamani kurudi nyumbani kwake, alitaka alale pale pale polisi ila Sakina ndiye aliyefanya kazi ya kumpooza na kumbembeleza.

Sabrina alizidi kuumia kuona vile anakandamizwa kwa kosa ambalo hakulitenda hata kidogo na wakizidi kumwambia kuwa amelitenda.
"Ila ni Mungu pekee anayejua hatma yangu, ni Mungu pekee atakayenihukumu kwa haki juu ya hili"
Moyo ulimuuma zaidi pale alipogundua kwamba siku hiyo atapaswa kulala hapo rumande sababu dhamana yake imekataliwa.
Sabrina alilia muda wote, hakujisikia kunyamaza kwani moyo ulikuwa ukimuuma tu na kujiona kama mtu mwenye mkosi katika maisha yake, ukizingatia kile chumba kilikuwa na mbu na harufu ya mikojo ndiyo ilitawala mule ndani na kumfanya Sabrina ajisikie vibaya zaidi.

Deo hakutaka kupoteza muda na kuamua kuchukua gari yake na kusafiri siku hiyo hiyo ili aweze kuwahi hata kwa kesho na kumsaidia mtoto wake.
Wakati yupo njiani, kuna jamaa mmoja alionekana kupatwa na matatizo kwenye gari yake njiani na kuliweka pembeni, alionekana kusimamisha kila gari inayopita ili kuweza kupata msaada ila gari zote zilimpita kwenye eneo lile, kwahiyo lilipopita gari la Deo nalo akalisimamisha.
Deo alitamani kutokusimama kwani aliona kuwa anacheleweshwa tu, ila huruma ikampata na kusimama, kisha akamuuliza yule mtu
"Nini shida hapo kaka?"
"Nina tatizo bhana na gari yangu hapa, sijui kama utaweza kunisaidia"
"Tatizo ni kitu gani?"
"Tairi langu la mbele limepata pancha, ubaya ni kuwa sina hata tairi la ziada"
Deo akaenda kwenye buti la gari yake na kutoa tairi, kisha akamwambia yule bibi
"Mimi ninalo, chukua hili"
Kwakweli yule baba hakuamini kupata msaada kiurahisi kiasi kile,
"Dah, nashukuru sana na Mungu akubariki. Ngoja nijaribu kuliweka, ila unaweza kwenda sasa usije ukachelewa zaidi"
"Usijali, ngoja tusaidiane kuliweka ili tuondoke kwa pamoja. Eneo sio zuri hili, nisije nikafika mbele na kusikia mengine bure"
Kisha Deo akaanza kumsaidia yule jamaa, yani alijikuta tu akipatwa na moyo wa kumsaidia.

Walipomaliza pale, ikabidi wafahamiane na kupeana mawasiliano yao
"Naitwa Deo"
"Nami naitwa James, itabidi unipe namba zako Deo yani hapa hata simu yangu haipo hewani sababu haina chaji na namba zake sijazishika"
Ikabidi Deo amuandikie yule James namba zake kwaajili ya kufahamiana zaidi.
Kisha kila mmoja akapanda kwenye gari yake na safari kuendelea.

Hali ya Sabrina kwenye kale kachumba haikuwa nzuri kwakweli, bado alikuwa na matatizo mule ndani na kila kilichoendelea hadi palipokucha.
Alimsikia mama yake akizungumza nje ya kile kituo cha polisi na kugundua kwamba mama yake alikuwa mtu wa kwanza kufika pale kushinda hata watu wote.
"Naombeni jamani hata nimuone mtoto wangu"
"Hairuhusiwi mama, subiri muda ufike"
"Msinifanyie hivyo jamani, mwanangu anahitaji uwepo wangu kwasasa. Naomba nimuone tu"
Malalamiko hayo ya mama yake yalimfanya Sabrina azidi kuumia moyo mule kwenye kile kichumba.
Joy alizidi kuwaomba lakini walimkatalia kabisa, yote hayo yalifanywa kwa lengo la kumtesa Sabrina tu ukizingatia ndugu wa yule binti ambaye mimba ilitoka walishafanya mambo yao pale kwenye kituo na Kuhonga baadhi ya askari ili kumfanya Sabrina ateseke na ndiomana Joy hakusikilizwa kabisa.
Joy aliona itakuwa vyema kama ataenda kumtafutia mwanae chakula kwanza, kwa kifupi Joy alikuwa amechanganyikiwa kabisa.

Njiani wakati anaenda kumtafutia mwanae chakula akakutana na Sakina.
"Najua umeshachanganyikiwa dada yangu, ila usijali chakula mie nimekibeba"
"Ni kweli nimechanganyikiwa, tena nimechanganyikiwa kabisa kabisa"
Wakaenda tena pale kwenye kituo cha polisi na kuanza kumuomba askari ili awatolee Sabrina waweze kumpa kile chakula,
"Hairuhusiwi, labda mnipe hiko chakula nimpelekee. Kesi ya mtoto wenu ni kubwa sana. Sitaki kufanya makosa tena"
Wakamuomba sana, ila yule askari alikataa na kuamua kumpa kile chakula ili akampe Sabrina.
Yule askari akachukua kile chakula na kumpelekea Sabrina kwenye kale kachumba ambapo alikuwa na watuhumiwa wengine kama watatu hivi, hao watuhumiwa wengine ndio waliokula kile chakula.

Joy na Sakina wakajaribu kufatilia ili wajue hatma ya ile kesi ya Sabrina,
"Mtoto wenu ana hatia sana, na ushahidi upo wa kutosha. Kwanza kabisa alikimbia eneo la tukio baada ya kulitenda, huo ni ushahidi tosha kuwa alitenda. Halafu kila tukitaka kumuhoji analia tu, inaonyesha wazi anajutia kosa alilolifanya ila tu hataki kukubali ukweli kuwa amelifanya"
Ndivyo walivyojibiwa na yule askari, akaendelea kuongea
"Hapa ni moja kwa moja segerea, tena kesi ya mauaji hiyo ataenda kufungwa huko maisha"
Joy alihisi kama moyo wake ukitaka kupasuka kabisa, ikiwa ameshindwa kukabiliana na hali ya mwanae kulala pale polisi kwa usiku mmoja je ataweza kukabiliana na hiko kifungo cha maisha kwa mwanae!!
Joy alihisi kama hiyo hukumu itatolewa kwa mtoto wake basi na yeye ndio itakuwa mwisho wa maisha yake.
Walishinda pale pale kituo cha polisi huku wakiwangoja ndugu wa yule dada ambaye mimba ilitoka kujua hitimisho la ile kesi inayomkabili Sabrina.

Deo alirudi nyumbani kwake na kushangaa kukuta hakuna mtu ila milango yote iko wazi,
"Kweli huyu mke wangu ameshachanganyikiwa jamani mmh!"
Na yeye hakutaka kupoteza muda, nia yake ilikuwa ni kujiandaa kidogo na kwenda huko kituoni.
Wakati anajiandaa, akapigiwa simu na namba ngeni. Akaipokea,
"James anaongea hapa, yule mtu uleyemsaidia njiani"
"Aah kumbe ni wewe, nipe khabari ndugu yangu"
"Salama tu, nishafika nyumbani kwangu. Najiandaa hapa kwenda kazini kidogo ila naomba jioni nikutafute"
"Sawa hakuna tatizo"
Kisha akakata ile simu na kumalizia mambo yake kisha kuanza safari ya kwenda kwenye kituo cha polisi alichoambiwa na mkewe jana.

Alipofika hakuwakuta, ikabidi aulize.
Akajaribu kumpigia mkewe simu lakini hakupatikana, ikabidi awafate askari wa pale na kuwaeleza kisha wakamwambia,
"Ile kesi imehamishwa na kupelekwa kituo cha kati kule"
Deo, akaondoka eneo lile na kwenda alipoelekezwa.

Alipofika, aliwaona Joy na Sakina wakiwa wamekaa chini ya mti pale kituoni, ikabidi awafate.
Joy alipomuona mume wake, akapata nguvu kiasi huku machozi yakiendelea kumtoka.
"Hebu nielezeni kwanza ili nijue pa kuanzia"
Joy akamuelezea mume wake kila kitu hadi vile alivyoelezewa na mwanae wakati wapo nyumbani.
Deo akawa amepata picha kichwani kuwa ni wapi waanzie na wapi waishie.
"Ngoja nikamuulizie mkubwa wa kituo kwanza"
"Mkubwa wao hayupo, kuna msaidizi tu. Ila huyo naye hataki hata kutusikiliza"
"Na ilikuwaje mkaamishiwa huku?"
"Nahisi ni njama tu Deo, yani kule hata hatukukaa sana ile jana wakatuhamishia huku utafikiri mwanangu ndio muharifu wa kwanza duniani. Hata dhamana wakatukatalia"
Deo kuna kitu kikawa kinajengeka katika akili yake, alijua wazi kuwa mkewe alisahau kumwambia kama walihamishwa kituo ile jana sababu ya kuchanganyikiwa.

Deo akawaacha pale na kuanza kushughulikia kesi ya mwanae, alitaka kuhakikisha kwamba siku hiyo mwanae anapata mdhamana hata kama siku inakaribia kuisha sababu alichelewa kufika.
Alienda kwenye ofisi ya mkuu wa kituo na kuambiwa angoje nje, baada ya muda aliruhusiwa kuingia.
Alishtuka sana kumuona mkuu wa kituo ni mtu waliyeonana naye kabla,
"Kheee bwana Deo, umejuaje kuwa nipo huku? Maana hapa nikakumbuka ile ahadi yangu na kutaka nimalize nikupigie"
"Tatizo mwanangu bhan"
"Kafanyaje!!"
Deo akamuelezea vile alivyoelezewa na mke wake.
"Dah! Vijana wetu hawa wanamatatizo kwakweli, ni ujana tu unawasumbua. Ngoja waniitie hapa huyo binti yako nimuhoji mwenyewe. Sababu maelezo unayonipa na niliyopewa ni tofauti kabisa"
Yule mkuu wa kituo akaamuru Sabrina apelekwe ofisini kwake, kwahiyo askari akaenda kumtoa Sabrina.

Sabrina alikutwa hajitambui kwenye kile kichumba, inaonyesha wazi kuwa alilia sana hadi kupoteza fahamu kwahiyo walimtoa kama mzoga.

Sabrina alikutwa hajitambui kwenye kile
kichumba, inaonyesha wazi kuwa alilia sana hadi
kupoteza fahamu kwahiyo walimtoa kama mzoga.
Deo alishtuka sana kumuona mwanae katika hali ile, ikabidi mkuu wa kituo atoe amri kuwa Sabrina awahishwe kwenye kituo cha afya, nao wakafanya hivyo.
Joy alihisi kuchanganyikiwa zaidi kwa ile hali ya mtoto wake, hata alipopelekwa hospitali bado hakuwa na matumaini juu yake.

Sabrina aliendelea kupewa huduma huku akiwa chini ya uangalizi kwa wafanywavyo watuhumiwa wengine.
Yule mkuu wa kituo akamuita Deo na Joy pembeni ili kuweza kuwahoji vizuri kuhusu mtoto wao.
"Kwani hii kesi imekuwaje hadi kufikia huku?"
"Kwakweli, labda mke wangu ndio anaweza kueleza"
"Sasa, ngoja niwape kazi ndogo ya kufanya"
"Ipi hiyo? Inamaana mwanangu akitoka hospitali mtamrudisha tena rumande?"
"Hapana, siwezi kukufanyia hivyo Deo. Ila ningependa mjaribu kuchunguza kidogo kwa upande ule wa pili, sababu naona kama kuna mchezo unachezeka hapa"
Wakatulia na kumsikiliza kwa makini yule mkuu wa kituo ambaye alimuhurumia sana Deo ingawa walifahamiana kwa siku moja tu.

Kesho yake, hali ya Sabrina ilirejea na kuwa katika hali yake ya kawaida, hata yeye mwenyewe akajishangaa kujikuta pale hospitali.
Wazazi wake waliruhusiwa kurudi naye nyumbani ila kwa masharti ya dhamana iliyopitishwa na yule mkuu wa kituo.

Joy alifurahi sana kurudi na mwanae nyumbani ingawa kesi ilikuwa bado haijaisha.
"Nashukuru Deo mume wangu kwa kujuana na watu"
"Kwani unafikiri mtu mwenyewe nimejuana nae siku nyingi basi!! Nimejuana nae wakati narudi, najua Mungu ndiye aliyepanga yote haya. Hii kesi itaisha tu, hata usiwe na shaka"
"Naamini itaisha kwakweli"
Sabrina alikuwa amenywea sana, tofauti na jinsi anavyokuwaga siku zote. Ile kesi ilionyesha wazi kuichanganya akili ya Sabrina vilivyo.

Siku waliyoambiwa kwenda tena kwaajili ya ile kesi wakajiandaa ili kwenda huko.
Joy alikaa kidogo na mwanae ili kumpa nguvu na hali ya kujiamini pindi atakapokuwa anahojiwa na askari.
"Usiogope mwanangu, haya ni mambo ya kawaida tu. Babako saivi yupo basi hakuna baya litakalo kupata. Umenielewa?"
"Ndio mama, nakuelewa"
"Na ukiulizwa kitu elezea vile kilivyo, hakuna atakayekudhuru mwanangu"
Sabrina akaelewa aliyoambiwa na mama yake na kujiamini, ukizingatia hakuna alichohusika nacho kati ya vyote walivyomsingizia ingawa hakuwa na shahidi.
"Ila mimi sina shahidi mama"
"Usijali mwanangu, shahidi wako ni Mungu peke yake ambaye hana upendeleo"
Kisha wakatoka hapo nyumbani kwao na kuelekea kwenye kituo cha polisi.

Sakina alikuwepo kwenye kile kituo cha polisi tena hata kabla wakina Sabrina hawajawasili.
Hata walipowasili alikuwepo pale pale nje kwani ilimuuma sana kwa rafiki yake kipenzi na mdogo wake kupewa kesi kama ile aliyopewa.
Wakati yupo pale nje alikuwa amekaa nyuma ya mabinti watatu ambao hakuwafahamu kwa muda huo ila aliwasikia wakizungumza,
"Kheee Sia wewe ni noma, hata sikujua kama ungemkomesha hivi Sabrina"
Mwingine akacheka na kujibu,
"Yani nimemkomesha haswaaa na aache tabia ya kutaka bwana za watu, kazidi. Yani nilivyoona meseji zake kwa John wangu, halafu John akaniacha kwaajili yake. Eti na yeye akajileta mwenyewe kwetu, nikasema hapo hapo ndio pa kumkomesha"
"Ila ameyataka mwenyewe, inamaana hakujua kama mwanamke wa John ni wewe!"
"Atajijua mwenyewe, nimemfatilia nyendo zake mwanzo mwisho halafu lenyewe kama zoba hata halikujua. Na nimemkomesha, hadi kaonja tamu ya rumande. Kanywea kawa mdogo kama piritoni"
Wote watatu wakawa wanacheka bila kujua kama kuna mtu wanamuumiza na maneno yao ambayo wanayaongea kumuhusu Sabrina.
Waliendelea kuongea huku wakifurahi na kugongeana viganja vya mikono yao.
"Na pale angejua kama ni mimi nilimsukuma wee angechukia balaa"
"Angejulia wapi? Mi nakuaminia Manka ndiomana nikakupa kazi, huyo Bi. Shoga naye anavyojua kujiliza utadhani mimba imetoka jana kumbe kitambo tu, ila nimewakubali jamani kazi mnaiweza"
Wenyewe walikuwa wakifurahia maneno yao ila Sakina alipata kitu kutoka kwao tena bila hata ya wao kujua chochote kile.

Sabrina alikuwa akihojiwa na kuamua kuelezea kila kitu jinsi kilivyokuwa ila kama watamuamini basi na wamuamini, na kama ikishindikana kumuamini basi wasimuamini lakini ukweli akiwa kashausema wote jinsi ulivyo.
"Inamaana huyo mdada unajuana nae kwa muda mrefu?"
"Sio kwa muda mrefu, ni kama nilivyowaelezea kuwa mara ya kwanza nilikutana nao kwa kaka wa rafiki yangu"
Sabrina hakutaka kuwaficha kitu kwa wakati huo, aliwaelezea mlolongo mzima wa tangia mara ya kwanza alipoonana na yule mdada ambaye mimba imetoka na wenzio hivyobasi akafanya waweze kumuelewa kwa urahisi zaidi tena kushinda hata alivyoelewa yeye.
"Kuna picha fulani naipata kwenye kichwa changu"
Aliongea yule askari ambaye alikuwa akifanya kazi ya kumuhoji Sabrina, kisha Sabrina na wazazi wake wakaruhusiwa kurudi nyumbani na kutakiwa kuja tena kesho kwaajili ya hitimisho la ile kesi.

Sakina aliendelea kuwasikiliza wale mabinti waliokuwa wakibwabwaja bila hata ya kuangalia pembeni,
"Hivi Sia, yule kaka yako Japhet naye yupo katika mlolongo huu wa mchezo?"
Huyo Sia akacheka,
"Awepo wapi? Hata yeye haujui ukweli, na yeye nilimfanyia kusudi sababu kazidi na tabia yake ya kupenda penda"
"Kwahiyo alikuwa anampenda kweli?"
"Ndio, kaka yangu ni penda penda yule"
Wakawa wanacheka, wakamuona Sabrina akitoka na wazazi wake kwenye kile chumba cha mahojiano wakatulia kimya kama wamemwagiwa maji.
Kisha wakamuona yule dada wa nyuma yao akiinuka na kuwafata wakina Sabrina kisha akaondoka nao.
Wakajikuta wakishangaa kwa pamoja,
"Inamaana yule dada anajuana na wakina Sabrina!"
"Na inamaana maongezi yetu yote ameyasikia! "
"Mmh pameshanuka hapa jamani, tuondokeni tu"
Kuna askari alitoka kwenye kile chumba cha mahojiano, kisha Sia akamfata yule askari kuongea nae
"Imekuwaje kwani?"
"Naona hii kesi inataka kuwa kubwa, maana yule mzee wa yule muhalifu kasema anaenda kutafuta mwanasheria"
"Mmh kugumu huko, au tuje tuifute?"
"Ni nyie tu na makubaliano yenu, sie tunafanya kazi yetu tu"
Sia akamuaga yule askari na kwenda kuwafatilia wale wenzie ili wapange cha kufanya kwa wakati huo.
"Nadhani itakuwa vyema tukimwambia Vicky awaambie ndugu zake waje kufuta hii kesi jamani, maana yule dada ameshatusikia kila kitu, yanaweza yakatugeuka haya jamani"
Wakakubaliana na kuondoka eneo lile.

Inaendelea




USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.