Simulizi: Je Haya Ni Mapenzi? Sehemu ya kumi na mbili (12)
Sabrina na wazazi wake walifika kwenye nyumba yao, Sakina alitamani kuwaambia kile alichokisikia toka kwa wale wasichana ila akasita na kuona kwamba ni vyema angoje Sabrina awe peke yake ndio amwambie.
Wakaongelea mambo mengine kabisa, hakuthubutu kuongelea chochote kati ya alivyovisikia.
Kesho yake waliporudi pale polisi walishangaa kuambiwa kuwa ile kesi imefutwa.
"Imefutwa!!"
"Ndio imefutwa, kwahiyo hakuna kesi tena labda mfungue kesi nyingine"
Wakapewa maelekezo kuwa yule mdada ambaye mimba ilitoka ameamua kufuta kesi kwani ameamua Kusamehe.
Sakina akaongea kidogo na yeye,
"Sijapata kuona eti kesi ya mauaji inafutwa kirahisi kiasi hiki"
Joy akamuangalia Sakina na kumshangaa,
"Unamaana gani Sakina?"
"Sina maana mbaya, ila nilitaka kujua hatma ya hii kesi eti imefutwa mmh! Na sie tufungue yetu ya usumbufu"
Sabrina akapinga swala hilo na kwenda kusaini karatasi zilizomuhusu kisha akaruhusiwa rasmi na familia yake kurudi nyumbani.
Sabrina alifurahi sana kufika nyumbani kwao na kuwaomba wazazi wake wafanye haraka ili aweze kwenda chuo kwni alishachoshwa na khabari za hapo.
Kwavile Sabrina sasa alikuwa na furaha, Sakina aliamua kutumia muda huo katika kumwambia Sabrina kile ambacho alikisikia kikizungumza.
Sabrina aliishia kushangaa tu,
"Inamaana Sia ndio alikuwa mwanamke wa John?"
"Sasa mbona hakuniambia?"
"Mi sijui ila hapa nimekwambia tu kile ambacho nilisikia."
"Kumbe yote haya ni njama juu yangu! Ila nimejifunza kitu dada"
"Kitu gani hivyo?"
"Sitaki tena kuwa kwenye mahusiano, yaliyonipata yanatosha tayari"
"Usiseme hivyo Sabrina, huwezi jua mambo ya mbele"
"Hata kama siwezi jua, ila ndio hivyo sitaki tena"
Sakina hakuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana na kile ambacho Sabrina mwenyewe alikiamua kwaajili ya maisha yake yanayoendelea.
"Ila kama ungekuwa umemkubali yule kaka yangu haya yote yasingekukuta, maana yule angekuoa tu ila...."
Sakina akakumbuka kitu na kuamua kunyamaza,
"Ila kitu gani?"
"Hapana, nilitaka kuchangany maneno tu hapo"
Hakutaka kumwambia Sabrina ukweli kuwa hata alivyotaka kubakwa ni kaka wa Sakina ndiye aliyepanga mpango ule.
Wakaongea mengi kisha Sakina akaamua kuaga na kuondoka.
Sabrina akiwa ndani kwake ametulia, akaisikia simu yake ikiita kwa mara ya kwanza tangia apatwe na ule msukosuko.
Alipoitazama aliona mpigaji ni Fredy, akaiacha ile simu iite hadi ilipokata na kuchukua simu yake kisha akaizima na kuichomoa ile laini na kuivunja, kisha akajisemea
"Kuanzia leo nataka niwe Sabrina mpya, sitaki rafiki wala kitu gani. Nitakuwa mwenyewe siku zote."
Alitulia na kuyatuliza mawazo yake kisha akamfata mama yake.
"Mama, kumbe marafiki ni wabaya sana eeh!"
"Ulikuwa hujui mwanangu? Urafiki na mwanadamu yataka umakini sana kwakuwa huwezi jua kilichopo moyoni mwake"
"Sasa mama wewe huna marafiki?"
"Wa kazi gani? Rafiki mkweli na wa pekee ni Mungu tu anayetuwazia yaliyo mema siku zote. Wengine hawa salimiana nao tu, cheka nao ila kamwe huwezi jua anakuwazia kitu gani"
Maneno ya mama yake yalimfanya Sabrina kushikilia maamuzi yake ya kutokuwa na rafiki tena.
Kesho yake, Sabrina akaletewa taarifa na baba yake kuwa anatakiwa kusafiri kwaajili ya kwenda kwenye masomo yake.
"Una siku mbili tu hapa mwanangu, unatakiwa kwenda kwenye masomo yako"
Khabari ile ilimfurahisha sana Sabrina kwani alihitaji sana kusahau mambo yote yaliyomtokea katika maisha yake, mambo yote yaliyomfanya aone kwamba maisha ni kitu kibaya.
Sabrina akamfata mama yake na kumwambia,
"Mama, ila kabla sijaenda huko kwenye masomo yangu naomba nikamuage mtu mmoja muhimu sana kwangu"
"Umeanza tena Sabrina, juzi tu hapa umesema kuwa hutaki marafiki, eti leo ukamuage mtu muhimu sana. Ni nani huyo? Kama ndugu zako wote wamesema leo watakuja hapa kukuaga"
"Ndio mama, ila nitapenda nikamuage na huyo mtu pia. Laiti kama nitaondoka bila kumuaga, moyo wangu utaniuma sana"
"Basi kwa huyo mtu tutaenda wote. Kwanza niambie ni nani?"
"Si tutaenda wote mama! Basi usijali, utamjua huko huko"
Joy hakutaka kubishana sana na mwanae kwani anamjua mwanae kama ana tabia ya ubishi.
Badae walifika ndugu baadhi kwaajili ya kumuaga Sabrina ambaye alikuwa anaenda masomoni kwenye nchi ya mbali. Wengi waliumia kwakuwa Sabrina alikuwa ni mtu pekee anayewakumbuka ndugu zake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kaka zake pia walikuwepo, na wote kwa pamoja wakafanya tafrija ya kuagana na Sabrina.
Sakina akamfata Joy na kumwambia,
"Ila hawa ndugu zenu ni kituko, kwenye tafrija wote wamekuja ila kule polisi hakuna hata mmoja aliyekuja"
"Sio hivyo ila hatukuwaambia, kipindi kile nilikuwa nimechanganyikiwa kwakweli"
Sakina akaona Joy anajitetea tu hana lolote la maana.
Tafrija ilipoisha wote wakasambaratika na kuagana.
Kesho yake kabla ya safari, Sabrina akamkumbusha mama yake kuwa waende kwa mtu wake muhimu ambaye anahitaji kumuaga.
Mama yake akajiandaa na kuanza safari yao.
Walienda hadi shuleni, shule ambayo Sabrina alimpeleka Jeff. Nia na madhumuni yake ni kwenda kumuaga Jeff.
"Kumbe mtu muhimu huyo ndio Jeff! Si ungeniambia mapema mwanangu hata nisingesumbuka kuja huku"
Sabrina akacheka, na kuingia lile eneo la shule.
Walipotazama pembeni waliona kuna wanafunzi wengi wamezunguka huku wakipiga kelele, Sabrina akajikuta akikimbilia eneo lile ili kujua kuna tatizo gani.
Alipopita kwenye lile kundi, alimuona mwanafunzi mmoja wa kiume akiwa yupo chini, inaonyesha wazi alikuwa amezirai.
Alipomsogelea na kumuangalia vyema mwanafunzi huyo alikuwa ni Jeff.
Alipopita kwenye lile kundi, alimuona mwanafunzi
mmoja wa kiume akiwa yupo chini, inaonyesha
wazi alikuwa amezirai.
Alipomsogelea na kumuangalia vyema
mwanafunzi huyo alikuwa ni Jeff.
Sabrina akashtuka na kuinama pale chini kumuangalia Jeff, muda huo huo walimu watatu nao wakawasili eneo lile kisha wakawasambaratisha wanafunzi waliokuwa wamemzingira Jeff.
Walimu wale wakasaidiana kumuondoa Jeff eneo lile na kumsogeza katika sehemu nzuri, Sabrina aliamua kuwauliza wale walimu
"Kwani amepatwa na nini?"
"Hata sisi tunamshangaa siku hizi, yani leo ni mara ya tatu ameanguka hivi"
"Mara zote hizo ameanguka leo?"
"Hapana, ila kumuona leo ameanguka ni mara ya tatu. Siku mbili zilizopita nazo alianguka, ila huwa anazinduka mwenyewe. Ila akizinduka huwa hana kumbukumbu "
"Mmewahi kumpigia mzazi wake simu kumjulisha?"
"Tulijaribu ndio ila huwa hapatikani"
Sabrina akakumbuka kuwa pale shuleni aliweka namba zake yeye kwaajili ya lolote lile litakalo muhusu Jeff, na hapo akajua wazi kosa ni lake.
Muda kidogo, Jeff akazinduka. Akamuona Sabrina mbele yake, akainuka na kwenda kumkumbatia Sabrina huku machozi yakimtoka.
Sabrina akamuuliza,
"Nini tatizo Jeff baba?"
"Ulinidanganya wewe"
"Nilikudanganya nini mtoto mzuri?"
"Uliniambia utakuwa unakuja mara kwa mara kuniona ila hujaja hata mara moja tangia uliponileta"
"Ila mama yako si alikuwa anakuja jamani Jeff!!"
"Ndio mama alikuwa anakuja ila nilitaka na wewe uje"
Sabrina alitulia akimsikiliza Jeff huku akitafakari maneno ya mwalimu kuwa Jeff akizinduka huwa kumbukumbu zinapotea, sasa amewezaje kukumbuka ahadi za uongo za Sabrina kwa muda mfupi.
Sabrina akamuangalia mwalimu na kumuuliza,
"Si mmesema huwa anapoteza kumbukumbu, mbona!!"
"Hata sie wenyewe tumemshangaa leo, maana huwa anakaa masaa kama mawili kurejesha kumbukumbu zake"
"Mlimpeleka hospitali?"
"Ndio, na wakampima kila kitu na wakasema ni mzima kabisa hana ugonjwa wowote ule"
"Basi nitawaomba leo niende naye halafu kesho tutamrudisha"
Walimu hawakuwa na pingamizi lolote juu ya swala la Sabrina kuondoka na mtoto Jeff.
Sabrina aliamua kuondoka na Jeff ili kuweza kumuhoji na kumuacha katika hali nzuri.
Joy alimuuliza Sabrina,
"Si unajua kama safari yako ni kesho?"
Nalijua hilo mama"
"Na huyu mtoto sasa utamrudisha muda gani?"
"Nitamrudisha kwanza kabla ya kuondoka, ila hata hivyo mama yake naye yupo"
Walipofika nyumbani, ikabidi Sabrina ampeleke Jeff moja kwa moja kwa mama yake ili waweze kuonana.
Walimkuta Sakina akiendelea na mambo yake, naye alipowaona akashangaa ila alifurahi kumuona mwanae.
"Mbona umemrudisha huyo?"
"Kasema amekumiss mama yake ndiomana nikamleta"
"Na walimu wamekukubalia tu?"
"Ndio wamekubali"
"Mmh mna ajenda zenu nyie, haya mwanangu njoo"
Jeff akamsogelea mama yake, ikabidi Sabrina amueleze Sakina kuhusu hali aliyomkuta nayo Jeff shuleni na jinsi alivyoelezewa na walimu wake.
"Mmh lazima kuna kitu hapa, ngoja nimtafute mtaalamu nimuulize"
"Ushaanza mambo yako ya kishirikina dada"
"Sio ushirikina Sabrina, hili jambo sio la kawaida nakwambia. Lazima kuna kitu hapa, mwanangu hawezi kuanguka hovyo kama mgonjwa wa kifafa"
Sakina akachukua simu yake na kuanza kuwapigia watu wake, Sabrina akamwambia
"Wewe wapigie tu ila hayo mambo usinishirikishe kwakweli"
"Sio tatizo ila lazima nijue"
Sabrina akatulia na Jeff ili kumuhoji maswali mawili matatu na yeye apate kuelewa kilichojificha kwa mtoto huyo.
Ila Jeff naye alijibu kuwa haelewi chochote kile, hata yeye mwenyewe anajishangaa tu kuwa kwanini inamtokea hivyo.
Sabrina hakupata jambo la maana kutoka kwa Jeff zaidi ya kujizidishia maswali yasiyo na majibu.
Sakina akarudi na majibu aliyopewa na watu wake,
"Wewe Sabrina ndio unamtesa mwanangu"
Sabrina akashangaa,
"Namtesa mwanao! Kivipi? Si ile kamba yako ya kipindi kile, ndio inayomtesa"
Jeff naye akashtuka na
kumuuliza mama yake,
"Umesema kamba mama! Kamba nyeusi?"
"Ndio kamba nyeusi, umekumbuka kitu gani hapo?"
"Huwa kabla sijaanguka naona kitu kama kamba nyeusi mbele yangu, huwa kinanizingira usoni na mwisho wa siku nakuja kuambiwa kuwa nilianguka"
Sakina akamuangalia Sabrina na kumwambia,
"Umeona sasa? Umeona mambo yako hayo Sabrina!"
"Huu sio wakati wa kulaumiana dada"
Kisha Sabrina akamuangalia Jeff na kumuuliza,
"Na mbona hukuniambia hayo yote wakati nakuuliza?"
"Nilisahau kukwambia"
Sakina sasa alikuwa anaongea tu tena bila nukta,
"Sijui hata una nini Sabrina kwa huyu mwanangu, yani majanga yako wewe umeenda kumuhamishia mwanangu halafu huku mnajifanya mmepona na mama yako"
"Usinilaumu bure, hata wewe una husika pia hapa sababu yule mtu aliyenifunga kamba sikwenda mwenyewe. Tena ni wewe uliyenishauri kuwa twende hadi leo nimekuwa na matatizo ya milele, tena mimi ndio napaswa kukulaumu wewe ila sio wewe kunilaumu mimi"
Wakajikuta wakibishana muda huo hadi Jeff akawa analia kwa mabishano yao.
Joy akiwa nyumbani kwake aliona kuwa mwanae anakawia sana kurudi nyumbani, na Deo nae alishaanza kumuulizia,
"Umemuacha wapi Sabrina wakati mliondoka wote?"
"Hata kurudi tumerudi wote ila yeye akaenda kwa Sakina mara moja kumpeleka mtoto wa Sakina. Nashangaa hadi sasa hajarudi"
"Hebu nenda kamfate, yule mtoto hatakiwi kukaa mbali na nyumbani kwa muda mrefu kwasasa"
Ikabidi Joy ajihimu kwenda kumfata binti yake.
Alipofika aliukuta ule mzozo baina ya Sakina na Sabrina,
"Kuna nini hapa? Eeh! Mnarumbana nini nyie maswahiba wawili?"
Sabrina akamjibu mama yake,
"Hakuna kitu mama"
Sakina akadakia,
"Hakuna kitu nini? Hebu mwambie ukweli mama yako naye ajue. Si ulikuwa naye katika kuiteketeza ile kamba"
Joy akawashangaa sana,
"Kamba gani mnayoizungumzia hapa?"
"Eti ile uliyoikata"
"Kwahiyo muda wote mnabishania huo upuuzi wa kishetani! Hebu tumieni akili wakati mwingine jamani, haya mambo mengine ni ya kijinga tena hayafai hata kurumbana. Kwani tatizo ni nini?"
Ikabidi Sabrina amueleze mama yake kuwa yale matatizo waliyomkuta naye Jeff, chanzo chake ni ile kamba.
"Sasa hapo ndio hayo mambo yenu ya kishirikina yanaponishangaza, sasa kamba ile ilikuwa kwenye kiuno cha Sabrina mmefungana na waganga wenu wa kitapeli huko, halafu hiyo kamba eti imeruka na kwenda kumtesa mtoto mdogo huyu Jeff asiye na hatia. Inamaana hiyo kamba mliifunga kwaajili ya Jeff au kulikuwa na kitu gani hapo?"
Sakina akataka kusema chanzo kizima cha kufunga ile kamba lakini Sabrina akamzuia hivyobasi wote wawili wakawa kimya tu.
"Kama hamtaki kusema basi. Sabrina nenda nyumbani baba yako anakungoja, nawe Jeff mtoto mzuri twende kwenye maombi."
Kisha Joy akamshika mkono Jeff na kuondoka naye.
Sabrina na Sakina walibaki wakiangaliana, kisha Sakina akamwambia Sabrina
"Nenda kwenu sasa baba yako anakungoja"
"Naenda ila usije ukamwambia mama bhana kile kitu"
"Haya simwambii, ila wewe mtoto mjinga sana huwa unaniona mimi kama rika lako vile wakati nimekupita miaka kibao. Haya nenda kwenu, na huyo mamako kajishauwa kumpeleka mwanangu kwenye maombi sasa ole wake asipone"
Sabrina akaondoka eneo lile na kurudi nyumbani kwao.
Joy alirudi nyumbani kwake kwenye mida ya saa tatu usiku na kuwakuta wote wakiwa pale kwake hata Sakina alikuwepo pale kwa lengo la kumfata mwanae.
"Jamani, mapambano yalikuwa makali sana ila Mungu ni mwaminifu ametusaidia"
Sabrina alikuwa na hamu ya kujua kilichotokea huko, ila kwasababu ya usiku Joy hakuona vyema kuwaelezea na kuamua kumruhusu Sakina amchukue mtoto wake ili akalale, ila Jeff aligoma.
"Kwanini hutaki kwenda nyumbani mwanangu?"
"Nataka kulala na anti Sabrina leo sababu nimesikia kuwa anaondoka kesho"
Sakina akajaribu kumshawishi mwanae ila ikashindikana kumfanya akubali kurudi nyumbani hivyobasi akaamua kumruhusu tu alale pale na Sabrina kisha yeye akaaga na kurudi nyumbani kwake.
Muda wa kulala ulipofika, Sabrina akamchukua Jeff na kwenda kulala nae chumbani kwake ila muda mwingi Jeff alionekana kutokulala kwa haraka ikabidi Sabrina amuulize,
"Mbona hulali toto?"
"Usingizi hauji mama"
"Fumba macho usingizi utakuja"
Jeff akafumba macho yake, naye Sabrina akamkumbatia mtoto yule ili kumfanya alale.
Baada ya masaa mawili, Jeff akashtuka huku jasho jingi likimtoka.
Sabrina nae akainuka na kukaa pale kitandani na kumuuliza Jeff kuwa anatatizo gani,
"Nini tatizo toto?"
"Nimeota ndoto mbaya"
"Ndoto gani hiyo?"
"Nimeota umepata ajari na umekufa"
"Jeff tafadhari usiniotee vibaya toto. Lala tena ila angalia upande wangu ili usiote tena"
Wakalala tena ila baada ya masaa mawili mambo yakawa yale yale, hadi panakucha Jeff alimuelezea Sabrina ndoto moja tu.
Sabrina alijiandaa vizuri, ila kama ambavyo alipanga ni kuwa atampeleka kwanza Jeff shuleni kwao kisha ataelekea uwanja wa ndege kwaajili ya safari yake kimasomo.
Akamwambia mama yake,
"Mi nitawahi kuondoka hapa na Jeff shuleni kwao kisha ndio nitaenda huko uwanja wa ndege"
"Hayo mambo yako ya kuchelewa ndio ambayo baba yako ameyakataa mwanangu. Yeye kasema atatoka moja kwa moja kazini kuelekea uwanja wa ndege kukuaga halafu wewe unaanza mambo yako mengine, Jeff atarudishwa shule na mama yake"
"Nilimuahidi mama, kumbuka ahadi ni deni acha nifanye hivi tafadhari"
"Basi ngoja nimpigie yule dereva aliyesema baba yako ili uwahi, halafu mie nikimaliza kujiandaa nitamshtua baba yako anipitie hapa"
Sabrina alishukuru kuruhusiwa na mama yake.
Dereva alipofika, Sabrina akapikia mizigo yake kisha yeye na Jeff wakaingia kwenye ile gari.
Wakakatisha kidogo kwa Sakina ili Jeff aweze kumuaga mama yake kisha safari ikaendelea hadi walipofika shuleni kwa Jeff.
Sabrina akamuomba Jeff ashuke ili akamkabidhi kwa walimu wake, ila Jeff akagoma na kuanza kulia
"Mbona hivyo Jeff jamani!"
"Sitaki uondoke"
"Naenda masomoni Jeff usijali mtoto mzuri"
"Ndio unaenda masomoni ila sitaki uondoke leo"
"Kwanini jamani Jeff!"
"Sitaki ufe"
"Sitakufa Jeff, niachie tafadhari uende shule na wewe"
Ila bado Jeff hakutaka kumuachia Sabrina, bado alikuwa akilia sana.
Sabrina akajaribu kumpa vishawishi vyote ila mtoto huyu hakutaka kuelewa kabisa, bado alikuwa analia na kumng'ang'ania Sabrina asiondoke.
Ikabidi Sabrina afanye ujasiri tu na kwenda kumuita mwalimu mkali wa Jeff ili Jeff aende darasani kwa wenzie.
Mwalimu yule kama kawaida yake, yeye ni bakora tu kwa mtoto mbishi.
Jeff alipomuona yule mwalimu yeye mwenyewe akashuka kwenye gari na kumwambia mwalimu,
"Tafadhari usinichape, ila niruhusu niongee neno moja tu na anti yangu hapa"
Yule mwalimu akampa dakika mbili za kuongea na Sabrina,
"Nenda salama mama, ila naenda kumuomba Mungu uikute hiyo ndege imeshaondoka"
Sabrina alijua Jeff anasumbuliwa na utoto, kisha akamuaga pale na kuondoka.
Njiani kulikuwa na foleni sana, na kila walipoangalia mida, masaa yalikuwa yameenda sana.
Sabrina akamwambia yule dereva,
"Naona hapa tutazidi kuchelewa, nadhani itakuwa vyema kama nikichukua bodaboda na kuwahi"
Yule dereva alimuhakikishia kuwahi ila Sabrina alihisi kuchelewa na kuamua kushuka kisha akaita bodaboda na kupakia mizigo yake halafu safari ikaendelea hadi uwanja wa ndege.
Akawakuta mama na baba yake wakimngoja,
"Yani wewe mtoto una matatizo sana, haya fanya upesi usije kuchelewa maana imesalia robo saa tu"
Sabrina hakutaka kupoteza muda, moja kwa moja alipeleka mizigo yake kukaguliwa, kisha wakampekua na kuangalia tiketi yake na kuruhusiwa kuingia uwanjani.
Kwavile ilikuwa ni mara yake ya kwanza Sabrina kuingia kwenye uwanja wa ndege, alijikuta akishangaa shangaa tu kisha akaenda kupanda ndani ya ndege.
Wazazi wake walikuwa pale nje wakitaka kushuhudia mtoto wao anapoiacha ardhi ya Tanzania.
Waliondoka eneo lile hadi pale waliposhuhudia ndege ikipaa angani, na kuamua kurudi kwao kwa furaha.
Walipofika nyumbani, waliendelea na mambo mengine kama kawaida.
Mara wakamuona Sakina akiwa amekuja huku jasho jingi likimtoka, Joy akamuuliza
"Una tatizo gani leo?"
Sakina hakujibu, ila alienda moja kwa moja kuwasha luninga iliyokuwepo mule ndani kwao.
Wakakutana na habari iliyoandikwa
"Taarifa zilizotufikia hivi punde"
Habari ile ilihusiana na ndege ile ile aliyopanda Sabrina kuwa imeanguka.
Wakakutana na habari iliyoandikwa
"Taarifa zilizotufikia hivi punde"
Habari ile ilihusiana na ndege ile ile aliyopanda
Sabrina kuwa imeanguka.
Joy alijikuta akiinuka kwenye kiti na kusema,
"Uwiiiii!!! Mungu wangu!"
Na kujikuta akianguka chini na kupoteza fahamu.
Deo nae alihisi kuchanganyikiwa, alijihisi kamavile yupo ndotoni kwani hakuamini kile alichokiona na kukisikia.
Sakina ndiye aliyetakiwa kufanya kazi ya ziada kuwambembeleza ili waweze kuwa katika hali ya kawaida.
"Jamani tusipanic sana, tufatilie kwanza taarifa yenyewe"
Sakina akainama pale alipoanguka Joy na kujaribu kumpa huduma ya kwanza hadi pale Joy alipozinduka.
Deo akawaambia,
"Ngoja mi nijikaze niende huko uwanja wa ndege nikaangalie, yani siamini"
Deo hakutaka tena kupoteza muda pale nyumbani kwake kwani alihisi kuchanganyikiwa tayari, wakati anataka kutoka akakutana mlangoni na dada yake mwenye jina la mwanaye yani Sabrina mkubwa ambapo Sabrina huyo alimzuia kaka na kumuuliza,
"Unaenda wapi sasa?"
"Naenda uwanja wa ndege, kuna khabari mbaya imetokea"
"Ndiomana nimekuja kaka, tafadhari nakuomba urudi ndani"
"Hapana Sabrina, mwanangu yupo kwenye matatizo"
"Sasa wewe ukienda huko uwanja wa ndege utasaidia nini? Au na wewe unajitafutia matatizo tu kaka yangu! Tafadhari nakuomba turudi ndani tukajadili"
Deo alikuwa mbishi kwa hilo kwani muda huo
mawazo yake yalikuwa kwa mtoto Sabrina, ila dada yake alijitahidi kumsihi mpaka akakubali kurudi ndani.
Ila hakuwa na raha kabisa na alihisi kuchanganyikiwa na maisha yale, aliona kama maisha yake yanaonewa kwa wakati huo haswaa maisha ya binti yangu,
"Yani majuzi tu hapo tumetoka kwenye kesi, leo ndio kama haya yaliyotokea. Mwanangu jamani, eeh Mungu baba mnusuru mwanangu na majanga haya"
"Ndiomana nimekuja kaka, ila roho yangu inaniambia kuwa Sabrina ni mzima kabisa. Kwahiyo tungoje kwanza, tungoje miujiza ya Mungu kwakuwa anaweza kufanya chochote kwaajili yetu"
Deo alimsikiliza mdogo wake huyu kwa makini lakini hakuna alichokuwa anaelewa kwani mawazo yake yalikuwa yanampeleka mbali kabisa.
Wakati wanaongea, simu ya Deo ikaanza kuita.
Alipoipokea, habari ilikuwa ni ile ile ya ajari ya ndege huku aliyempigia simu akimpa pole.
Deo alipomaliza kuongea na simu akamwambia dada yake,
"Tafadhari, nakuomba twende uwanja wa ndege ili nikashuhudie kwa macho yangu"
"Hapana kaka, wewe ushachanganyikiwa tayari tunaweza tukasababisha mambo mengine bure"
"Hapana, sitaweza kukaa hapa ilihali sielewi chochote. Sielewi mwanangu mie jamani, sijui amekufa!!"
Deo aliinama kwa muda na kunyanyuka, ikabidi mdogo wake naye ainuke na kumfata kaka yake ili aweze kumsaidia kwa lolote lile litakalo tokea.
Walitoka na kumuacha Joy akiwa hajielewi kabisa pale chini kwahiyo ni Sakina tu aliyebaki naye kumuangalia.
Deo alifika nje na kupanda kwenye gari yake, kisha Sabrina naye akaingia kwenye lile gari la kaka yake na safari ya kwenda uwanja wa ndege ikaanza huku akili ya Deo ikiwa kama mtu aliyechanganyikiwa.
Deo alikuwa anaendesha gari kwa haraka ili aweze kuwahi hadi mdogo wake alikuwa akijaribu kumsihi aweze kupunguza mwendo.
Walipokaribia uwanja wa ndege, palikuwa na watu wengi kiasi kwani wengi walitaka kujua mustakabali wa ile ajali waliyosikia kuwa imetokea.
Sabrina akamshauri kaka yake kuwa aweke gari yake pembeni.
Wakati anaendelea kumshauri kaka yake, mara akashtuka hadi kumfanya kaka yake naye ashtuke kutokakana na ule mshtuko alioufanya mdogo mtu, kisha akamuuliza
"Kuna nini kwani?"
"Kuna kitu nimeona, subiri"
Deo hakumuelewa dada yake huyu kuwa anamaanisha kitu gani na kujikuta akimuangalia tu bila ya kummaliza.
Kisha yule Sabrina akashuka na kuelekea mahali ambapo alisema kuwa kuna kitu amekiona.
Deo naye akajikuta akishuka na kumfatilia dada yake.
Alifika mahali akasita kidogo kwenda mbele, na kumfanya Deo naye asite na kuzidi kumshangaa mdogo wake, kisha akamuuliza tena
"Kwani kuna nini?"
"Angalia pale"
Sabrina akanyooshea kidole mahali ambako alitaka kaka yake apaone, ila ni dhahiri kwamba kaka yake hakuona chochote na kumwambia mdogo wake,
"Sioni kitu, kwani kuna nini?"
"Basi kama huoni, nisubirie hapo hapo hata usiende popote pale"
Kisha akaongoza kwenda mahali alipokuwa anamuonyeshea kaka yake kuwa apaone.
Deo alisimama palepale huku akimuangalia mdogo wake mahali alipokuwa anaelekea na kusahau kabisa kilichowapeleka kule uwanja wa ndege.
Alimuona dada yake akiinama na kuokota kitu kama jiwe, Deo hakuelewa ila alikuwa akimuangalia kila kitu ambacho mdogo wake alikuwa akikifanya.
Mara akamuona akiinuka na kwenda mbele kidogo, kisha akainama tena na kuokota kitu kama jiwe halafu akainuka na kuanza kurudi mahali alipomuacha kaka yake.
No comments: