Simulizi: Je Haya Ni mapenzi? Sehemu ya Kumi Na Tatu (13)


Deo alikuwa ameduwaa tu eneo lile na kumshangaa mdogo wake mpaka alipofika eneo alilosimama.
"Vitu gani hivyo Sabrina?"
"Watu hawa"
Deo akashtuka, na kumuuliza mdogo wake kwa makini
"Watu!! Kivipi?"
"Twende hivi kaka nikakuonyeshe"
Deo aliongozana na mdogo wake mpaka mahali palipoonyesha kuwa ni kiwanja cha
watoto kucheza mpira wa miguu.
Ikabidi Deo amuulize mdogo wake tena,
"Mbona sikuelewi Sabrina?"
"Hata mi mwenyewe sielewi ila tutaelewa tu hapa hapa"
Sabrina akachukua moja wapo ya yale mawe mawili aliyoyaokota kisha akalipuliza na kulituma chini, lile jiwe lilipotua chini tu liligeuka kuwa mtu aliyekuwa amevaa shuka jekundu huku amejipaka masizi usoni na kumfanya Sabrina na kaka yake washtuke na kuogopa ingawa lile jiwe alilitupa mwenyewe.
Deo akamuangalia tena mdogo wake na kumuuliza kwa mshangao
"Mbona maajabu haya Sabrina?"
Sabrina naye akavuta pumzi kwani hakuelewa kama itakuwa vile, akajikuta akipata ujasiri wa gafla na kuanza kumuuliza yule mtu aliyekuwa mbele yao.
"Ni nani wewe na una shida gani?"
Yule mtu alianza kujibu tena bila uoga wa aina yoyote ile,
"Nimetumwa"
"Umetumwa na nani?"
"Na mkubwa wangu, siwezi kumtaja"
"Umetumwa kitu gani?"
"Nimetumwa nisababishe ajari kwaajili ya mtu mmoja tu tunayemuhitaji"
"Mtu gani huyo?"
"Sabrina"
Sabrina akashtuka ila moja kwa moja akajua Sabrina anayetajwa pale ni mtoto wa kaka yake, kisha akamuuliza tena yule mtu,
"Unamuhitaji huyo Sabrina wa kazi gani?"
"Tunataka kumtoa kafara kwakuwa alikiuka masharti yetu na kumuumiza mkubwa wetu"
"Masharti yenu? Masharti gani hayo?"
"Mwenzangu ndio anayajua"
"Mwenzako yupi?"
"Huyo uliyemshika kwenye mikono yako"
Sabrina akajikuta akishtuka na kuliachia lile jiwe chini bila kufanya kama alivyofanya kwenye jiwe la kwanza yani kulipuliza kwanza.
Lile jiwe la pili nalo lilipoanguka tu chini liligeuka kuwa mtu aliyekuwa amevaa shuka yenye rangi nyeusi na kujipaka masizi usoni.
Ila yeye hakuonesha kuganda kama mwenzie bali alishika shuka la mwenzie na wote wawili wakayeyuka kabisa wala yale mawe mawili hayakuwepo tena pale chini, Sabrina alijikuta akishtuka sana na kuanza kukimbia huku kaka yake akimfata kwa nyuma.

Walifika mahali Sabrina akiwa anahema sana utafikiri kakimbia mrefu.
Deo alimuangalia kwa makini tena mdogo wake na kumwambia,
"Yani leo nimeamini maneno yote niliyokuwa naambiwa kuhusu wewe mdogo wangu, kwakweli wewe sio mtu wa kawaida"
Kisha akaanza kuondoka na kumfanya Sabrina amfate nyuma ili ajaribu kumueleza,
"Tafadhari kaka usinifikirie vibaya"
"Unajua siku zote nilijua watu wanatunga maneno kuhusu wewe kumbe ni kweli ndivyo ulivyo"
"Hapana kaka, nisikilize kwanza"
"Nitakusikiliza endapo utaniambia ukweli, wewe wale watu uliwaonaje? Na uliwezaje kuyabeba yale mawe mawili wakati unajua ni watu? Na ujasiri wa kuwahoji watu wa ajabu kiasi kile umeutoa wapi?"
Muda huo Deo alikuwa amesahau kabisa kuhusu ajari ya mtoto wake kwani haya mambo yalimtisha na kumchanganya zaidi.
"Ngoja nikueleze kaka yangu"
"Ndio nieleze tena kwa umakini kabisa"
Ikabidi Sabrina amueleze kaka yake kwa kifupi jinsi alivyowaona wale watu,
"Sikia nikwambie, wakati tunakuja hivi nilikuwa nahisi kuwa kuna kitu si cha kawaida. Pale nilipokwambia uweke gari pembeni nilihisi nywele zikinisimama na kuona kuwa kuna kitu si cha kawaida, ndipo nilipoangalia kule mbele na kuwaona wale watu, nikakuonyesha ukasema huoni kitu hapo ndio nikagundua kuwa wewe huna uwezo wa kuona kile ambacho mie nilikuwa nakiona.
Ikabidi niwafate mwenyewe, ila waliponigundua kuwa nimewaona wakajigeuza kuwa vile vijiwe, hata mimi mwenyewe sijui nilipata ujasiri wapi na kujikuta nikiweza kuviokota vile vijiwe viwili, kuna kipindi niliwahi kupatwa na matatizo na kujikuta nikijua vitu vingi kuhusu wachawi na ndiomana nikakuomba kuwa tuonde kwenye kile kiwanja.
Lile jiwe la kwanza nililitupa kwa ujasiri sababu nililipuliza kwanza yani pale nilipuliza nguvu zake na ndiomana aliweza kusema kila kitu nilichomuuliza, nilichokosea ni kwenye lile jiwe la pili sababu nilipatwa na uoga na kulitupa bila kulipuliza na kufanya wao pia wapate nguvu za kupotea eneo lile, ila kama ningepuliza majiwe yote mawili basi wale wangesema kila kitu"
Deo akamuuliza swali moja mdogo wake,
"Wewe ni mshirikina?"
"Hapana mie hata ushirikina wenyewe siupendi"
"Kwahiyo wewe ni nani?"
"Mimi ni mdogo wako"
Deo akaongoza kwenda mahali alipoacha gari yake.
Alipofika pale akajikuta akijiuliza,
"Hivi huku tumefata nini?"
Hakupata jibu na kupanda kwenye gari yake, Sabrina akamfata nyuma naye akapanda kwenye lile gari na kumuuliza kaka yake
"Inamaana umeshalizika sasa na majibu ya kitu kilichokuleta huku!"
"Hivi ni kitu gani kilichonileta huku?"
Sabrina akatambua kuwa akili ya kaka yake imeshachanganyikana na kuona ni bora warudi tu nyumbani kuliko kuendelea kuwa katika eneo hilo na kusababisha mambo mengine wakati anaona wazi akili ya kaka yake imechanganyikana.

Walipokuwa njiani, Sabrina alimuona mtu ambaye alimstua sana na kumuuliza kaka yake
"Si yule mama aliyekuwaga jirani yenu yule!"
Deo akamuangalia kwa makini na kumjibu mdogo wake,
"Ndio ni yeye, kwani vipi tena?"
"Muangalie vizuri halafu ujijibu mwenyewe"
"Namuona kawaida tu"
"Mie nahisi kitu juu yake"
Wakati Sabrina akiongea hayo, muda huo huo Deo akajiwa na kumbukumbu za binti yake na kujikuta akisema,
"Jamani mwanangu!"
Sabrina akajua kuwa kaka yake amekumbuka kila kitu, na muda huo huo akafunga breki gafla kwani ilibaki kidogo tu asababishe ajari.
Ikabidi Sabrina amuombe kaka yake na kwenda kukaa eneo la kuendeshea na kuanza kuendesha yeye mpaka nyumbani.

Walipofika, Joy alikuwa pale pale chini na alipowaona jambo la kwanza aliwauliza
"Yu wapi mwanangu Sabrina?"
Deo na mdogo wake wakaangaliana bila ya kutoa majibu na kumfanya Joy azidi kuchanganyikiwa na kuwa kamavile mtu mwenye kichaa, kwani akainuka pale chini na kwenda kumuuliza Deo huku akipiga makelele ya kilio
"Yuko wapi mwanangu? Mwanangu mimi yuko wapi jamani? Sina tena mtoto wa kike mimi jamani, namtaka mwanangu, namtaka Sabrina wangu"
Machozi mengi yalikuwa yakimtoka Joy hata Deo hakuwa na jibu la moja kwa moja kumpa mkewe na kujikuta naye akilia na kuwafanya Sabrina na Sakina nao walie.
Joy alikuwa akilia huku akiongea,
"Niitieni Sabrina wangu jamani, Sabrina wangu hayupo tena, muiteni jamani"
Huku akipaza sauti ya kilio na kuita,
"Weee Sabrina weee, Sabrina mwanangu nakuita mama yako jamani...."
Wakati akiendelea kulia huku akitamka maneno akasikia sauti,
"Mimi hapa mama nimekuja"
Kuangalia mlangoni wakamuona Sabrina akiwa amesimama.

Kuangalia mlangoni wakamuona Sabrina akiwa
amesimama.
Wote wakajikuta wakimshangaa Sabrina huku Sabrina naye akiwashangaa wao.
Ikabidi Deo ainuke na kumfata Sabrina pale mlangoni kwavile ni yeye tu aliyekuwa na ujasiri huo, kisha akamshika mkono na kumvutia kwa ndani.
Sabrina hakusita na kuingia ndani kwao.
Joy hakuamini kwakweli, alimfata mtoto wake na kumshika vizuri ili kuweza kugundua kama ni yeye kweli.
"Sabrina mwanangu ni wewe au naota?"
"Ni mimi mama, mbona hivyo mnalia kwani kuna kitu gani?"
Sabrina hakutambua chochote kilichoendelea kwao na kujikut akiwauliza kuwa wanalia nini.
Deo alimuangalia binti yake kwa makini na kuwa kama mtu anayeshangaa na kustaajabu lile tukio la Sabrina.
Deo akamuuliza mwanae,
"Hebu tuambie mwanetu, umeokokaje kwenye ile ajari!"
Sabrina akalishangaa swali la baba yake kisha na yeye akajikuta akiulza
"Ajari gani hiyo?"
Wote ndani wakaangaliana baada ya kugundua kuwa Sabrina hata hajui kama kuna ajari iliyotokea, ikabidi Deo amuulize tena binti yake
"Si tulikuacha unasafiri wewe!!"
Sabrina akawaangalia wazazi wake kwa jicho la uoga kwani alishajua kuwa ana makosa tayari kisha akaanza kuwaomba msamaha,
"Baba na mama naomba mnisamehe sana. Najua nishapoteza pesa zenu tayari, ila sio kosa langu"
"Kivipi Sabrina? Na je ni kosa la nani?"
"Ni kosa la ushamba wangu na kale katoto kadogo Jeff"
Sakina naye akashangaa kusikia kuwa mtoto wake naye anahusika na kuamua kuuliza kwa upana zaidi,
"Jeff!! Jeff kafanyaje tena mtoto wangu?"
Sabrina aliamua kuwaeleza kuhusu Jeff, kwanza kabisa aliwaeleza jinsi Jeff alivyokuwa anashtuka usiku na kumwambia Sabrina kuwa amemuotea kapata ajari na jinsi kesho yake alivyokuwa akimzuia kuwa asiende, na maneno aliyomwambia wakati anataka kusafiri.

Walimsikiliza Sabrina kwa makini, na kujiuliza kuwa mtoto Jeff alijuaje na vipi Sabrina aliweza kupona wakati alikuwa akibishia maneno ya huyo mtoto na hadi akafika uwanja wa ndege kwaajili ya safari yake, Deo akamuuliza mwanae
"Halafu ikawaje mwanangu?"
Sabrina akaendelea kuwaeleza,
"Kwanza kabisa kale katoto kalinichelewesha sana pale uwanja wa ndege yani nilichelewa sababu yake, hadi kuchukua bodaboda chanzo ni yeye. Sasa nilipoingia pale uwanja wa ndege, dah kumbe ni pazuri, si nikajikuta nashangaa ila nikaona watu wanaenda kupanda ndege nami nikawafata na kupanda, nilikaa kama dakika tano hivi kuna mtu akanifata na kuniuliza nilipomwambia ndege ninayotakiwa kupanda akaniambia kuwa nishachelewa na ndege imeshaondoka.
Kwakweli nilijisikia vibaya sana na kushuka, nilitamani kulia lakini nilijua haitasaidia, nikaogopa kurudi nyumbani kwanza kwani najua mngenisema sana.
Nilipotoka pale uwanja wa ndege, moja kwa moja nikaenda shuleni kwakina Jeff kumsema ila na kumsema kote yeye alikuwa akifurahi tu na nimekaambia sitaenda tena kukaona. Jamani wazazi wangu nawaomba mnisamehe sana mtoto wenu kwa kuwatia hasara, hapa hata sijui itakuwaje tena"
Maelezo yale ya Sabrina yalifanya waone kwamba mtoto wao kuna nguvu kubwa inayomzunguka na ndiomana inakuwa vile, kwanza walifurahi zaidi ya mwanzo.
Joy aliwatuliza na kuanza kumshukuru Mungu kwa hayo aliyowatendea.
Baada ya hapo wakamsimulia Sabrina tukio lililotokea kuhusu ile ndege aliyotakiwa kupanda kuwa imelipuka
"Kheee kwahiyo na mimi ningekuwa nimekufa!!"
"Ndio mwanangu, ndiomana ulitukuta tunalia hapa"
"Ooh asante Mungu kwa kumtumia mtoto Jeff kuyakomboa maisha yangu"
Sabrina alijisikia furaha sasa, ikabidi Deo awaambie na mengine,
"Tena kuna mambo mengine ya ajabu tuliyoyakuta huko na huyo shangazi mtu"
"Mambo gani tena?"
"Ngoja awaeleze mwenyewe, mi hata sielewi na kuelezea siwezi"
Ikabidi Sabrina mkubwa awaeleze kila kitu alichokiona uwanja wa ndege akiwa na kaka yake huyo na kuwafanya wote wazidi kushangaa maajabu yale.
Joy akajikuta akitahamaki,
"Mungu wangu, kumbe ile ajari ilipangwa kwaajili ya mwanangu tu! Lakini kwanini wanamuonea mwanangu kiasi hiki! Hivi ni lini mwanangu ataachiwa na hawa watu jamani!! Mwanangu kawakosea nini!"
Joy alijikuta akilalamika kwa uchungu sana kwani moyo ulimuuma kutokana na yale mambo aliyoyasikia juu ya binti yake.

Waliongea mengi sana na kushauriana vitu vingi, ila Sakina akawapa wazo lingine
"Jamani hapa si pa kupoteza muda, kwavile wale watu wanajua kuwa Sabrina amekufa basi asikae hapa kwanza, ikiwezekana hata asafiri na kwenda mkoa hata wa jirani kwanza kubadilisha mazingira yake. Au mnaonaje jamani juu ya hilo?"
"Ni wazo jema kabisa hilo, basi tusipoteze wakati. Mimi shangazi yake nitaenda naye"
Joy akajikuta akiguna kwanza,
"Mmh nyie wote wawili ni majanga tu, bora aende na Sakina halafu sisi tutamfataga tu"
Basi wakakubaliana juu ya hilo, kisha Sakina akaenda nyumbani kwake na kujiandaa kidogo halafu safari ya kwenda kituo cha mabasi ya kwenda mkoani ikaanza.

Walipofika kituoni kwa bahati wakapata basi la kwenda Arusha na kupanda kwavile Sakina aliwaambia kuwa Arusha ana ndugu zake.
Kisha Sakina na Sabrina wakaondoka halafu wengine wakarudi nyumbani huku wakiwa hawaamini amini kitu ambacho kimetokea kwao kwa siku hiyo.

Waliporudi nyumbani sasa wakapumua na kupumzika kwani yale mambo yaliwapa hofu na kuwachanganya tu.
Sabrina mkubwa aliwaambia kuwa siku hiyo hatoondoka hapo kwahiyo atalala hapo hapo kwaajili ya kuangalia mambo yanavyokwenda tu kwenye hiyo familia yao.

Wakiwa wamekaa pale sebleni wakapatwa na mgeni, huyo mgeni alikuwa ni yule mmama ambaye walimuona njiani wakati Deo anarudi nyumbani kwake na mdogo wake.
Wakaamua kumkaribisha yule mmama ili kujua kuwa ni kitu gani kimemleta mahali pale.
Yule mmama alianza kwa kuwapo pole,
"Poleni sana jamani, nimesikia hayo mambo yaliyowapata na kushtuka sana."
Joy akamuuliza huyu mmama,
"Kitu gani hicho kilichokushtua?"
"Si nimesikia kuwa mtoto wenu alikuwa anasafiri kwenda nje na ndege aliyopanda imeanguka"
Joy alijikuta akipatwa na hasira sana moyoni mwake, akamjibu huyu mama kwa dharau
"Sasa kama imeanguka sie tufanyeje!"
"Khee mfanyeje wakati binti yenu naye yumo?"
"Hayo hayakuhusu, nakuomba uende"
Joy aliongea kwa hasira sasa kuonyesha kwamba maswali ya huyu mama yalimchosha tayari na kuhisi kuwa huenda ana husika na kitu kilichokuwa kinataka kumpata binti yake
"Nimekwambia uende zako, unangoja nini sasa?"
Yule mmama akainuka na kuanza kutoka,
"Muone kwanza, mchawi mkubwa wewe"
Ikabidi Deo aanze kumtuliza mke wake, ila yule mama baada ya kusikia kuwa kaitwa mchawi akageuka na kuuliza tena
"Umeniita nani mimi?"
Joy hakuacha kumwambia kwavile alikuwa na hasira sana kwa wakati huo,
"Nimekwambia wewe ni mchawi tena mchawi mkubwa, ondoka nyumbani kwangu"
"Naondoka ndio ila utauona huo uchawi wangu vizuri"
Yule mama akaondoka na kumuacha Joy akiwa amevimba kwa hasira huku mumewe akikazana kumbembeleza pale.

Walipotulia kwa muda, wakajikuta wakimshangaa Sabrina mkubwa aliyekuwa amekaa kimya muda wote tangia yule mmama alipofika pale ndani, Joy akamuuliza
"Wifi, mbona hujaongea chochote?"
"Kuna kitu nakitafakari"
"Kitu gani hicho?"
"Huyu mama si mtu mzuri jamani, kwa ushauri wangu mdogo tu hebu tuondoke hapa kwa muda"
"Twende wapi sasa?"
"Nyie twendeni, halafu nitawaambia pa kwenda, najua kaka una pesa bora ufanye haya mambo sasa kisha tuendelee na vitu vingine"
Deo alikuwa akimshangaa mdogo wake kwa muda mwingi sana kwani alikuwa akimuma kama ni mtu wa ajabu
"Mbona una mambo ya ajabu kiasi hicho mdogo wangu? Unajua huwa sikuelewi kabisa?"
"Ni ngumu kunielewa kwa sasa ila ipo siku utanielewa kaka. Nawaomba tufanye ninavyosema ili tuwe na amani kwa muda na kujua jinsi ya kupambana na haya mambo"
Ikabidi wamsikilize na kuamua kufanya walichopanga kisha wakajiandaa na kuianza safari.
Moja kwa moja wakampeleka Sabrina mkubwa nyumbani kwake na wao kuanza safari ya kwenda Arusha kumfata Sabrina mdogo ili kuweza kuendana na mawazo waliyopewa na Sabrina mkubwa.

Sakina na Sabrina walifika salama kwenye mji wa Arusha na moja kwa moja wakaelekea hotelini kwanza ili waweze kupumzika hapo na kesho yake wafikirie kuianza safari ya kwenda kwa mojawapo za ndugu wa Sakina.
Sabrina alikuwa na mawazo sana na kujiona kuwa binti mwenye mkosi katika maisha yake, alijihisi vibaya sana.
Baada ya muda kidogo akamuomba Sakina kuwa aweze kwenda kukaa nje pale mbele ya hoteli ili apate kidogo upepo wa Arusha.
Sakina hakuna na pingamizi, kisha akatoka naye nje na kumuacha apumzike halafu yeye akarudi ndani kuweza kuendelea kuwasiliana na ndugu zake.

Sabrina alipokuwa amekaa pale na mawazo yake, akatokea kijana wa makamo kiasi na kumsalimia pale kisha akamwambia,
"Samahani dada, naweza kukaa hapa karibu na wewe!"
Sabrina akamuitikia kwa kichwa na kumfanya yule kijana akae mahali pale, kisha akaanza kujitambulisha pale,
"Samahani dada, mi naitwa Sam. Je wewe mwenzangu unaitwa nani?"
"Naitwa Sabrina"
"Nashukuru kukufahamu, mbona umejiinamia hapo una matatizo gani Sabrina?"
"Matatizo ya kimaisha tu"
"Niambie basi hata kidogo tu kama hutojali"
Sabrina alimuangalia huyu kijana kwa makini huku akitamani kumueleza na huku akisita, ila moyo wake ukaamua kumwambia kwa kifupi tu kuwa alitakiwa kwenda masomoni ila ndege ikamuacha ila hakusema kama hiyo ndege ilipata ajari, yule kijana akamuhurumia Sabrina na kumwambia,
"Pole sana Sabrina, ila usiwaze sana hilo sio tatizo kubwa"
"Sio tatizo kubwa !! Unadhani mi nitapata wapi tena pesa ya nauli kwenda huko?"
"Usijali, nitakusaidia"
Sabrina akashangaa na kushtuka
"Utanisaidia kivipi?"
"Si hiyo pesa ya nauli nitakusaidia"
"Khee wewe utaitoa wapi?"
Yule kijana akacheka na kumuangalia tena Sabrina,
"Unanidharau! Hata hii hoteli ni yangu pia"
Sabrina akashangaa sana kumuona yule kijana mdogo kuwa na uwezo kiasi kile.
"Mbona unaonekana bado mdogo?"
"Ni mwili wangu tu ila mimi ni kijana mkubwa tu"
Sabrina akaongea mengi sana na yule kijana na kujikuta akifarijika moyo wake kwani yule kijana alikuwa akimwambia mengi ya kumtia moyo na kumpa amani kwenye ro ho yake.

Deo na mkewe waliwasili Arusha usiku sana na kuamua kutafuta hoteli ya karibu ili wapumzike halafu kesho yake waanze kuwatafuta Sabrina na Sakina hewani kwakuwa muda huo hawakupatikana.
Kulipokucha waliwapata hewani na kujishangaa kuwa wote wapo hoteli ya aina moja.
Ikabidi wakutane pamoja na kujadiliana mawili matatu ya kitu cha kufanya, Deo alienda pembeni na binti yake kuongea
"Nahitaji uende mwanangu ukaendelee na hayo masomo ila kuna mtu nangoja anitumie pesa kiasi nikakate tiketi nyingine"
"Usijali baba, kuna mtu amesema kuwa atanisaidia"
"Mtu gani huyo?"
Sabrina akamueleza baba yake kila kitu kuhusu kijana aliyekutana naye, Deo naye akapenda kuonana na huyo mtu.

Mchana wa siku hiyo, wote wakakutanishwa na huyo kijana naye akakiri mbele ya wazazi wa Sabrina kuwa yupo tayari kumsaidia.
Wote wakafurahi na kukubaliana juu ya hilo.
Joy akamuita pembeni mwanae na kumwambia,
"Kuwa makini mwanangu, hata shangazi yako aliolewa na mtu anaiwa Sam"
"Sio tatizo mama, huyu hata kunitongoza hajanitongoza yani tofauti kabisa na wengine"
Mama yake akakubaliana nae.

Baada ya siku mbili Sabrina alifanikiwa kusafiri na kwenda kwenye nchi aliyotakiwa kusoma kisha wazazi wake na Sakina wote wakarudi mjini kwao huku wakiwa na amani baada ya Sabrina kuwapa majibu kuwa amefika salama.

Walipokuwa nyumbani kwao, Sakina akaamua kumueleza Joy ukweli kuhusu kitu kilichokuwa kinamsumbua binti yake Sabrina.
"Ni kitu gani hicho?"
"Alikuwa na kinyama fulani kimeota huku kwenye sehemu....."
Kabla hajamaliza kuongea, wakashtuka na mshindo mkubwa uliotokea nje ya nyumba ile.

Kabla hajamaliza kuongea, wakashtuka na
mshindo mkubwa uliotokea nje ya nyumba ile.
Ule mshindo uliwafanya wajikute wakiulizana kwa pamoja kuwa,
"Kuna nini?"
Wakatazamana, kisha wote wawili wakainuka ili waweze kwenda kuangalia nje wajue kuna kitu gani kinaendelea.
Ila wakati wanataka kutoka nje Sakina kuna kitu kikamzuia na kujikuta naye akimshika mkono Joy na kumzuia kwenda nje.
"Kwani vipi Sakina?"
"Kuna kitu kimenizuia, nahisi huko nje si kwema hebu tungoje kwanza"
Joy akatulia kimya huku akimtafakari Sakina na ule mshindo.
Kimya kikatawala kabisa hata wao walikuwa kimya kabisa kamavile kuna mtu aliyewakataza kuongea jambo lolote lile.
Muda kidogo ukapita, kisha Joy akauvunja ukimya ule uliokuwa umetawala pale ndani.
"Mbona hivi Sakina!!"
Sakina alikuwa kimya kamavile kuna kitu anakisikilizia, gafla wakasikia mshindo mwingine na muda huo huo ikasikika sauti ya paka kama ambavyo huwa wanali, ile sauti ilikuwa kama inalilia mule ndani kwa Joy na kumfanya Joy ahamaki,
"Ndani kwangu sina paka wala kiumbe chochote chenye umbo la mnyama, sasa hiyo sauti ya paka inatokea wapi? Lazima ni nguvu za giza tu"
Joy akaanza kukemea ile hali na ile sauti ya paka aliyoisikia kuwa ishindwe.
Sakina alikuwa kimya tu huku akimuangalia Joy akiendelea na maombi yake.
Baada ya muda kidogo hali ikawa shwari kabisa na hakikusikika kitu chochote tena.

Wakiwa wametulia mule ndani, wakasikia mtu akibisha hodi.
Ikabidi Joy ainuke ili kuweza kumkaribisha, alikuwa ni Fredy yule rafiki wa Sabrina.
"Karibu sana Fredy, za siku nyingi!"
"Nzuri tu za hapa"
"Nzuri kabisa, mbona leo hujachangamka kama unavyokuwaga siku zingine?"
Joy alimuuliza Fredy kwani hakuwa kawaida kama anavyokuwaga siku zote haswaa kwa kipindi cha nyuma ambacho alikuwa anakuja kuwatembelea, ila Fredy hakujibu swali kuwa kwanini hajachangamka na badala yake akauliza swali jingine
"Kwani Sabrina yuko wapi?"
"Si amesafiri kwani hujui?"
"Amesafiri kwenda wapi?"
Joy akaona anaulizwa maswali kama polisi yani kamavile huyu muulizaji ana haki ya kujua alipo Sabrina.
Ingawa Joy anaelewa wazi kuwa Sabrina hakuwaaga wale rafiki zake ila bado hawakuwa na haki ya kuuliza kwa jazba kiasi kile ambacho yule Fredy alikuwa akiuliza.
Ikabidi Joy ajaribu tena kumkaribisha hata akakae kwanza.
"Karibu basi ukae kwanza"
Yule Fredy alijivuta na kwenda kukaa kwenye mojawapo ya makochi pale ndani, kisha Joy akaenda mlangoni ili aurudishie vizuri.
Alipoona kuwa geti lake nalo lipowazi akaamua kwenda kulifunga kwanza.
Alipofika getini akapata wazo la kuangalia pale nje kwake.
Alipoangalia kwa mbali akamuona mtu kama Fredy na kujiuliza mwenyewe,
"Sio Fredy yule!!"
Akamuangalia kwa makini na kugundua kuwa ni yeye kwavile macho yao yalipogongana alitabasamu na kisha Fredy akaanza kuja pale alipo Joy.
Wakati huo Joy alikuwa ameganda kama sanamu huku akijiuliza kuwa je yule aliyeingia ndani kwake ni nani kama Fredy yupo huku nje.
Yule Fredy alipokaribia tu Joy akamuuliza bila salamu,
"Mpo mapacha?"
"Hapana mama, shikamoo"
Joy hakuitikia kwani akili yake ilianza kuvurugika na kujikuta akimuuliza yule yule Fredy,
"Sasa aliyekuwepo humu ndani kwangu ni nani?"
Fredy naye akashangaa na kumuuliza,
"Kivipi mama?"
"Twende ukaone"
Joy akamshika Fredy mkono na kuanza kumvutia kwenye nyumba yake ili akaone na aseme mwenyewe.

Walipoingia ndani wakapatwa na mshangao kwavile Sakina alikuwa chini amezirai na wala yule Fredy aliyeingia mwanzo hakuwepo mule ndani.
Joy alitahamaki sana na kujiuliza kuwa ni kitu gani kinaendelea, waliinama na kuanza kumpa huduma Sakina ambaye alikuwa ameanguka pale chini.
Sakina naye alipozinduka akashtuka kumuona yule Fredy na kutamani kupiga makelele, ila Joy ndio akajaribu kumtuliza ili awe sawa kwanza.
Baada ya muda kidogo Sakina akatulia na kurudi katika hali ya kawaida kabisa.
Fredy alikuwa pembeni akishangaa kuwa aliambiwa kuna mwingine yupo ndani akamuone ila hakumuona na badala yake ndio kumkuta yule Sakina akiwa amezimia.
Walipotulia ikabidi naye aulize kuwa kuna kitu gani, wakamueleza kuwa kuna mtu alifika pale mwenye muonekano kama wake na kumfanya azidi kushangaa
"Nilipotoka kufunga geti ndio nikashangaa kukuona wewe sasa"
Fredy alishangaa sana na kuuliza,
"Huyo mtu yuko wapi sasa?"
"Ndio hapo cha kushangaza kuwa ndani hatujamkuta tena"
"Mmh mambo ya kutisha hayo jamani"
Walikaa pale ndani ila wote walijawa na uoga kwenye mioyo yao tu.
Muda kidogo Sakina naye akapata ujasiri wa kuzungumza,
"Unajua yule mtu alibadilika na kuwa yule mmama wa siku ile, nikataka kupiga kelele lakini kabla sijapiga kelele akageuka na kuwa paka mweusi kwakweli sijui ni nini kiliendelea baada ya hapo"
"Kheee makubwa haya jamani, mbona mambo ya ajabu kutokea kwenye nyumba yangu mie Joy! Bora nimpigie simu mchungaji aje leo"
Joy hakutaka kupoteza wakati, aliamua kuchukua simu yake na kumpigia mchungaji wao.
Fredy naye aliamua kuaga kwani aliona ile nyumba kuwa na mauzauza tu, kwahiyo aliaga na kuondoka.

Jioni mchungaji na watu wengine wa maombi wakafika pale nyumbani kwa Joy na kufanya ibada kwa pamoja.
Baada ya ibada kila mtu akarudi nyumbani kwake, hata Deo aliporudi na kusimuliwa kilichotokea hakuamini kabisa kama ni kweli yametokea kwenye nyumba yake mwenyewe.

Kesho yake Joy alimfata Sakina ila kumuuliza vizuri kuhusu binti yake.
"Uliniambia mwanangu Sabrina alikuwa na kitu gani?"
"Mmh yasije yakatokea ya jana bure, mie sipo tayari kukabiliana na matatizo dada kwahiyo sitaweza kukwambia tena"
"Sasa mimi nitajuaje ukweli?"
"Utaujua tu, ipo siku binti yako atakueleza kila kitu kinachohusiana naye na kila kitu kinachomsumbua katika mwili wake, kwahiyo usijali chochote"
"Hivi unajua kama Sabrina huwa hasemi?"
"Najua ndio, ila ipo siku atakwambia mwenyewe, yani hakuna hata haja ya mimi kukwambia. Ila uamuzi wenu wa kumpeleka kwenda kusoma mbali mlitumia busara sana kwamaana hapa asingeweza kusoma kamwe"
Joy alielewa vizuri kauli ya Sakina ila aliona ni mbali sana kumngoja mtoto wake mpaka arudi, alitamani sana kuambiwa kila kitu na Sakina ila Skina alikataa kumwambia ukweli huku akisisitiza kwamba anajikwepesha na matatizo ya kujitakia.
Ikabidi Joy aache mambo kama yalivyo na kumuaga Sakina kisha kurudi nyumbani kwake ili kuendelea na mambo mengine ya umuhimu.
Maisha yaliendelea bila ya chochote kile kibaya kuwapata kwa kipindi hicho.

Miaka ilipita na maisha nayo yaliendelea, Sabrina hakuacha kuendelea kuwasiliana na yule kijana Sam aliyemsaidia.
Alimfanya kuwa rafiki yake mkubwa sana na wala Sabrina hakutaka tena kujiingiza kwenye maswala ya kimapenzi kwani kila alipofikiria alikopita alijikuta akiumia sana na kutokutaka tena kuwa na mpenzi.
Kwajinsi alivyokuwa akiwasiliana na Sam tena bila ya kumtaka kimapenzi aliona ndiye mwanaume pekee wa tofauti duniani kwani wengine wote walishamfanyia mambo ya ajabu ambayo yalimfanya alie muda wote, ila sasa anaishi kwa furaha na amani huku akiwasiliana na kijana Sam kama ndugu yake au rafiki yake wa karibu.

Jeff aliporudi kwao alimkuta mama yake kama kawaida, kwa kipindi hiki alikuwa amekua kiasi cha kuweza kwenda mwenyewe shule na kurudi mwenyewe kwenye likizo ikifika.
Kwavile ilikuwa ni kipindi kirefu tangu Sabrina aondoke akajikuta akimkumbuka sana Sabrina na kuamua kumuulizia kwa mama yake,
"Hivi mamdogo Sabrina atarudi lini?"
"Khee! Miaka yote hiyo bado unamkumbuka Sabrina! Kweli ameitawala akili yako"
Jeff akacheka na kumuuliza tena mama yake,
"Niambie bhana mama, atarudi lini?"
"Kwakweli sijui atarudi lini, ila nikisikia kuwa anataka kurudi nitakwambia. Kwani nimemkumbuka sana pia, ila unataka nini?"
"Yeye ndio mshauri wangu"
"Kaone vile, lini umeshauriwa na Sabrina? Au ndio zile story zenu za kudanganyana za sungura na fisi"
Jeff akacheka sana na kuonekana kuwa amekumbuka mambo ya mbali sana. Na kumwambia mama yake,
"Ila nashangaa yeye hata hanikumbuki tangia ameondoka hadi roho inaniuma"
"Usijali mwanangu, atakuwa anatingwa tu si unajua mambo mengi kule alipo"
Akaongea mambo mengi na mama yake pale kisha akamuaga na kurudi shuleni kwao.

Sabrina aliendelea kufurahia maisha ya nchi aliyokuwepo huku akiendelea kuwasiliana na kijana Sam.
"Karibia nitarudi Sam, hata sijui nitapata kazi wapi!"
"Hilo sio tatizo Sabrina, ila bora urudi ni miaka mingi sasa imepita"
"Basi nikutumie cv zangu uanze kusambaza kwenye sehemu tofauti ili nipate kazi Sam"
"Usijali Sabrina, niamini mimi, kazi umeshapata tayari"
Maneno ya Sam yalikuwa yanampa sana moyo Sabrina na kumfanya ajilaumu kwa kuchelewa kwake kufahamiana na mtu kama Sam kwani alikuwa akimpa furaha na faraja kwa muda wote aliokuwa akiwasiliana naye.
Wakaongea mambo mengi na kupanga mambo mbali mbali, hakuna aliyechoka kuongea na mwenzie na hakuna aliyewahi kumtamkia mwenzie kuwa anamuhitaji kimapenzi.

Fredy alimkumbuka sana Sabrina ila hakujua ni jinsi gani ataweza kumpata kwani hakujua hata alipo kwa wakati huo, aliamua kumwambia ukweli nduguye Francis
"Kwakweli miaka yote hii nimejaribu kumsahau Sabrina ila nimeshindwa, nisaidie cha kufanya"
"Sasa mie nitakusaidia kitu gani? Labda uende kwao"
"Itabidi nifanye hivyo ili nijue kuwa atarudi lini, kwakweli nimemkumbuka sana yani hadi nakosa raha nikimfikiria"
Francis alitulia kimya huku akimsikiliza kwa makini nduguye, na muda huo huo yeye mwenyewe alijihisi akimpenda sana Sabrina na kujiona wazi kuwa Sabrina ndio mwanamke anayemuhitaji katika maisha yake ila hakuelewa kuwa ni kwanini yeye na nduguye wamejikuta wakiwa na hisia zinazofanana na kujiuliza kuwa ni nani anayempenda Sabrina kiukweli kati yao kwakuwa alijiona yeye na nduguye wakiwa na upendo unaofanana kwa Sabrina.
Kila mmoja kwa wakati wake akajipanga kwenda kwakina Sabrina ili kuulizia ujio wa Sabrina.



USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.