Simulizi: je Haya ni Mapenzi sehemu ya kumi na nne (14)
Siku zilipita na Sabrina akamaliza masomo yake na kuanza kujipanga kurudi nyumbani kwao.
Alitoa taarifa kwao na wote walifurahi na kuona vyema Sabrina arejee kwao, kwahiyo wote walioenda kumuulizia Sabrina waliambiwa siku atakayorudi na kufanya wamngoje kwa hamu.
Siku ilipofika, Sam alijipanga vyema kwenda kumpokea Sabrina uwanja wa ndege.
Alishangaa kuwaona na wengine pale akajua wote walikuwa wakingojea ndugu zao.
Sabrina alitokea mbele ya macho yake na kumfanya Sam ajawe na tabasamu mbele yake huku akitegemea kuwa Sabrina ataenda na kumkumbatia.
Akamshangaa Sabrina akienda kwa kijana mwingine aliyekuwa amesimama peke yake na kumkumbatia kwa furaha.
Akamshangaa Sabrina akienda kwa kijana mwingine aliyekuwa amesimama peke yake na kumkumbatia kwa furaha.
Sabrina alimkumbatia yule kijana kwa shauku sana na kumfanya Sam ahisi kupatwa na wivu juu yao.
Akatamani hata aende kuwatoa pale walipokuwa wamekumbatiana ila alijiona wazi kuwa hatakiwi kufanya vile hata watu watamshangaa.
Sabrina aliendelea kumkumbatia yule kijana bila hata ya kujua kama kumbatio lake kwa yule kijana kuna watu waliumia haswaa Sam ingawa alivumilia.
Sabrina alionekana kumfurahia sana yule kijana,
"Siamini kama umekuwa mkubwa kiasi hiki jamani, yani sura yako haibadiliki mwanangu. Sikutegemea kama ungekuja kunipokea na wewe jamani"
Sabrina aliongea sana kwani alifurahi na hakutegemea, kisha akaenda alipo Sam na kumfanya Sam agundue wazi kuwa Sabrina alimuona sema alimuanza mtu muhimu zaidi kupita yeye.
Akamkumbatia pale Sam na kumsalimia huku akipepesa macho yake kuwatafuta wazazi wake,
"Inamaana hawajaja?"
"Wakina nani?"
"Wazazi wangu"
"Wapo hapo nyuma kidogo wanakungoja"
Kisha Sabrina akaongozana na Sam kuwafata wazazi wake, baada ya hatua chache akasita na kugeuka nyuma kisha akamuita mtu kwa jina.
Muda huo Fredy na Francis nao walikuwa pembeni, na Sabrina aliposita na kugeuka walijua wazi wataitwa wao ila akaitwa yule kijana ambaye Sabrina alimkumbatia mwanzo,
"Jeff twende"
Jeff naye hakusita na kuanza kumfata Sabrina.
Wazazi wa Sabrina walifurahi sana na kumpokea mtoto wao kwa shangwe, kisha safari ya kwenda nyumbani ikaanza.
Sabrina alifurahi sana kurudi tena nyumbani kwao kwani ni miaka mingi ilipita bila ya yeye kuwa kwao, akafurahi kuwaona kaka zake ambao nao walikuwa wakimngoja kwa hamu.
Wakafanya tafrija ndogo ya kumpokea Sabrina na wote walikuwa na furaha siku hiyo.
Sam alitulia kabisa huku akiweka matukio yote kwenye kichwa chake, hakuweza kuacha tukio hata moja kwani yote aliona kuwa na maana kubwa sana katika maisha yake.
Muda huu, Sabrina alienda kukaa karibu na Sam kwani alimuona kama mtu aliyepooza kabisa na hakuwa na raha.
Sabrina alipokaa tu akaulizwa swali na Sam,
"Ushamaliza kupiga picha?"
"Aah na yule mtoto!! Nishamaliza tayari"
"Naona umemzoea sana huyo kijana"
"Tena sana, yani ni mtu muhimu sana maishani mwangu"
Sam alimuangalia tu alivyowahi kujibu bila kujua ni kwa jinsi gani yalimuumiza kwenye moyo wake.
Walifurahi pale mpaka muda ulipokwisha na kuagana.
Siku hiyo ilikuwa ya furaha sana nyumbani kwao hata Sabrina alipokuwa amelala alikuwa akitabasamu na kuonyesha kuwa alikuwa na furaha sana siku hiyo.
Alipopitiwa na usingizi, akajiwa na ndoto, hiyo ndoto ilimuonyesha kuwa anaolewa na watu wengi walijaa ila alipotaka kumgundua mume wake kwenye ile ndoto akajikuta akishtuka sana na kuamka, kisha akakaa na kujisemea,
"Sitaki kuolewa, najua hakuna wa kunipenda mimi kiukweli zaidi ya ndugu zangu wanao nizunguka, ila kwanini niote kuwa naolewa!! Sitaki kuolewa kwakweli"
Sabrina alitulia huku akiilaumu ndoto yake aliyoiota, kisha akaendelea kulala hadi palipokucha.
Sam alijiona vyema kumpenda Sabrina ila Sam alikuwa na tatizo ambalo hakupenda hata mtu mmoja alijue tatizo lake hata wazazi wake hakuwaambia na wala hawakujua kama ana hilo tatizo.
Akawaza sana kama ataweza kumwambia Sabrina tatizo lake na akaeleweka, akawaza kama Sabrina akiamua kumtangaza itakuwaje, akawaza pia swala la kumwambia Sabrina kuwa anampenda wakati alimzoea kama rafiki tu!!
Sam alijikuta akiwaza mambo mengi sana kichwani mwake ila akili yake ilimwambia wazi kuwa anampenda Sabrina tatizo alilokabiliana nalo ni namna ya kumueleza Sabrina huyo.
Francis na Fredy kila mmoja alirudi kwao kwa muda wake na kujikuta wote wawili wakijiuliza,
"Inamaana Sabrina hakutuona au ni dharau?"
"Pale imeonyesha wazi kuwa hatuna umuhimu tena kwake"
"Ila me siwezi kukubali Francis"
"Kama huwezi kukubali inamaana unataka kufanya kitu gani?"
"Najua nitakacho kifanya ila siwezi kukubaliana na hili swala kamwe"
Francis alimuangalia tu Fredy huku akijaribu kusoma mawazo yake kuwa ni kitu gani amepanga kukifanya, kisha akamshauri nduguye,
"Ila kuwa makini usije kufanya mambo ya ajabu sababu ya mapenzi ndugu yangu wakati hata mimi mwenyewe uliyenikuta nimeachia ngazi."
"Ni wewe ila sio mimi"
Francis hakuwa na jinsi, zaidi ya kumuacha nduguye aamue kufanya kile kitu anachotaka mwenyewe.
Baada ya siku mbili tatu kupita, Sakina alienda nyumbani kwa Joy kwa lengo la kuongea na Sabrina kuhusu mtoto wake.
"Unajua simuelewi Jeff mwanangu, sijui hata amekumbwa na nini kwa siku mbili hizi amenyong'onyea sana"
"Kwani umemuuliza mwenyewe anasemaje?"
"Ukimuuliza anasema yupo sawa tu"
"Basi usijali"
"Nisijali nini sasa?"
"Ndio kukuwa huko, usiwe na mashaka naye"
"Kukuwa ndio anyong'onyee vile!!"
"Si unajua kama mwanao yupo kwenye kipindi cha balehe!! Kwahiyo usijali sana"
"Kipindi cha balehe ndio mtu ananyong'onyea?"
"Usikute mapenzi nayo yameanza kumpa mawazo, kwahiyo usijali atakuwa sawa tu"
Sakina ikabidi akubaliane na Sabrina kuwa mtoto wake amenyong'onyea kutokana na kipindi hicho cha ukuaji kwake.
Kisha Sakina akaaga na kurudi nyumbani kwake.
Baada ya wiki kupita, Sabrina akaletewa khabari njema na Sam kuwa anahitajika kwenda kufanya kazi kwenye shirika lao haraka iwezekanavyo.
Sabrina alifurahi sana kwani hapakuwa na mambo ya usahili wala nini, alichotakiwa yeye ni kwenda kazini tu.
Yote hiyo ni kutokana na ukaribu wake na Sam ukizingatia Sam ndiye aliyekuwa na mamlaka makubwa na shirika hilo.
Sabrina alimshukuru sana Mungu kwa kumkutanisha na Sam na kuanza kuamini kuwa kila kitu katika maisha hutokea kwa sababu fulani, kwani mambo yaliyotaka kumpata kipindi kile ndiyo yalimfanya kukimbilia jijini Arusha na kukutana na kijana huyo ambaye amekuwa msaada mkubwa sana katika maisha yake.
Sabrina alijiandaa kwaajili ya kwenda kuripoti kazini kwa siku ya kwanza.
Mama yake akamuita pembeni na kumuuliza,
"Hivi hakuna chochote kinachoendelea kati yako wewe na Sam kweli?"
"Hakuna chochote mama"
"Mmh Sabrina mwanangu, mimi ni mtu mzima usinifiche"
"Huo ndio ukweli mama, yani huwezi amini hata kunitongoza Sam hajawahi mama"
"Mmh makubwa haya jamani, hata siamini tena siamini kabisa. Ila mficha maradhi kifo kitamuumbua"
Huku akionyesha ishara ya kama mwanamke mjamzito na kumfanya Sabrina acheke kwavile aliyokuwa akimwambia mama yake yalikuwa ya kweli ila mama yake hakutaka kuamini kabisa kama kuna ukweli wowote ndani yake. Kisha Sabrina akamuaga mama yake na kuondoka zake.
Alipofika kwenye ofisi alizoelekezwa alipelekwa moja kwa moja kwenye ofisi ya Sam kisha Sam akaenda kumuonyesha Sabrina ofisi atakayokuwa na kumfanya Sabrina afurahi zaidi.
Kwakweli Sabrina alishangaa kuwa na bahati kiasi kile, wakati wenzie wanahangaika mitaani na mavyeti yao kutafuta kazi hadi soli za viatu kuisha yeye kapata kazi kiulaini kabisa tena bila jasho, hapo akaamini ule msemo wa ongea na watu uvae viatu kwani hakutegemea kabisa.
Sam akamwambia Sabrina,
"Usijali Sabrina utakuwa unaelekezwa taratibu hadi utazoea mwenyewe, usiwe na wasiwasi kabisa"
"Asante sana Sam, sijui hata nitakulipa nini"
"Hata usijali, wewe fanya kazi yako tu. Mimi nipo kwaajili yako"
Sabrina alijisikia fahari sana huku akitunza ya kumsimulia mama yake nyumbani.
Baada ya kazi, Sam akamrudisha Sabrina nyumbani kwao kisha akamuaga na yeye kwenda nyumbani kwake.
Moja kwa moja Sabrina alikaa na mama yake kuulizwa habari za kazi aliyoitiwa
"Kwakweli mama ni jambo la kumshukuru Mungu sana, Sam ni kijana mwenye roho nzuri na mkweli."
"Niambie khabari za hiyo kazi mwanangu, na siku hizi umebadirika yani tangu uliporudi kila unachosema lazima uweke kumshukuru Mungu na pia unakumbuka sana kusali"
"Ni mambo ya Sam hayo mama, wakati nipo uingereza alikuwa akinikumbusha sana kusali, pia anapenda sana kumshukuru Mungu ndiomana amebarikiwa kiasi kile. Kwakweli mama, Sam ana hela, kwa kifupi ni tajiri"
Sabrina alianza kumueleza mama yake kuhusu vitu vichache tu ambavyo Sam anamiliki na kumfanya mama yake tamaa imshike na shauku pia.
"Huyo ndio mwanaume mwanangu, mng'ang'anie, mshikilie, usimuache aende kwa wengine usije kula wa chuya kwa uvivu wa kupembua. Mwanangu, mng'ang'anie huyo Sam ng'ang'ani ili uwe mke wake"
"Jamani mama, yote hayo yanakutoka bure tu. Huyo Sam mwenyewe hajawahi kunitongoza hata mara moja, na mimi kumtaka siwezi kwanza nalinda heshima yangu na pili sitaki kuumia kama kipindi kile. Nimekuwa Sabrina mpya mimi, sina mchumba wala mpenzi. Mama, kama Sam ananipenda basi ataniambia na kiukweli sitaweza kusema hapana ingawa sijapanga kuwa na mpenzi"
Joy alimsikiliza mwanae huku akiombea muda wowote Sam aweze kumtongoza mtoto wake, hata yeye mwenyewe alishangaa kuwa kwanini Sam hamwambii Sabrina kuhusu kuwa naye wakati dalili zote za kuwa anamuhitaji zinaonekana,
"Kwanini hakwambii mwanangu?"
"Muda utaamua mama, labda muda wake bado"
Kisha Sabrina akaenda kuendelea na mambo mengine.
Kesho yake asubuhi, Sam alifika kwakina Sabrina kumpitia kisha safari ya kuelekea ofisini ukaanza.
"Usiwe unajisumbua hivi Sam jamani, kunipitia kila siku utaweza!!"
"Jana yenyewe sababu ulikataa tu nisikupitie ila usingekataa ningekuja, kila kitu naweza kufanya kwako wewe Sabrina"
Sabrina alitulia kimya kidogo na kuendelea kuongea,
"Ila mimi naona unasumbuka sana jamani"
"Nimekwambia usijali Sabrina, tena wiki ijayo kuna nyumba nitakupeleka ukaishi huko, huwa tunawapangishia wafanyakazi wetu ili na wewe uache kuwategemea wazazi sasa na uanze maisha yako mwenyewe. Wao wamekusomesha na kazi yao imeishia hapo, kwasasa ni wewe kujiendeleza na maisha yako"
Sabrina akakubaliana na Sam na kuona kuwa amepewa ushauri unaofaa kwenye maisha.
Safari ya ofisini iliendelea na walipofika kazi nayo iliendelea.
Baada ya wiki moja, Sabrina alipelekwa kuangalia nyumba aliyotafutiwa na ikamvutia sana, aliipenda na kuifurahia.
"Asante Sam"
"Usijali Sabrina, hivi vitu ni vya kawaida tu"
"Yani nimefurahi sana hata sijui niseme vipi furaha yangu ilivyo hapa"
Muda wote Sabrina alikuwa akitabasamu tu, alijisikia raha sana na kuona anapendwa na Sam ingawa Sam hakumtamkia kuwa anampenda.
Kesho yake Sabrina alienda kwao na kumpeleka mama yake kwenye nyumba aliyotafutiwa.
"Mmh mwanangu, yani juzi tu ndio umetafutiwa nyumba ya aina hii!! Huyu kijana anakupenda sana mwanangu"
Sabrina alikuwa akitabasamu tu na kufurahi.
"Sina cha kusema mama yangu, ila nina furaha sana"
"Lazima ufurahi mwanangu, na uendelee kuwa na utulivu huo huo ili huyu kijana azidi kukupenda mwanangu"
Sabrina alikuwa akipendezewa tu na maneno ya mama yake, kisha siku hiyo Joy akalala kwenye nyumba ya mwanae ili kuweka baraka kwenye nyumba hiyo.
Maisha yaliendelea kuwa ya furaha kwa upande wa Sabrina, huku akipelekwa ofisini na kurudishwa kila siku na Sam tena bila ya kuambiwa chochote kinachohusu mapenzi na kumfanya Sabrina ahisi kuwa huenda Sam aliamua tu kumsaidia ila sio mapenzi wala nini.
Siku moja wakati Sabrina anarudishwa nyumbani na Sam, simu yake iliita. Kuangalia ilikuwa ni namba ngeni, Sabrina akaipokea na kuongea nayo.
Sam alimsikia Sabrina akimuelekeza yule mtu kuwa afike nyumbani kwake, Sam akajikuta wivu ukimjaa moyoni na kutamani kumjua huyo mtu ambaye Sabrina alikuwa akiongea naye kwenye simu.
Sam alimfikisha Sabrina kwake na kuondoka, ila hakuwa mbali na nyumba ya Sabrina.
Sabrina aliingia ndani, na kuweka mkoba kisha akatoka nje kama dakika tano kumngoja mgeni wake.
Akafika Jeff mahali pale na moja kwa moja alienda kumkumbatia Sabrina kwa nguvu huku machozi yakimtoka.
Sabrina aliingia ndani, na kuweka mkoba kisha
akatoka nje kama dakika tano kumngoja mgeni
wake.
Akafika Jeff mahali pale na moja kwa moja
alienda kumkumbatia Sabrina kwa nguvu huku
machozi yakimtoka.
Sabrina akamshangaa Jeff kuona akitokwa na machozi, moja kwa moja akamshika mkono na kuingia naye ndani, bila kujua kama Sam alikuwa akiwaangalia na moyo kumuuma sana ila hakutaka kufanya chochote kwa siku hiyo zaidi ya kurudi kwenye gari yake na kuondoka zake kwenda nyumbani kwake.
Sabrina alimfikisha Jeff ndani na kumkalisha kwenye kochi ili amueleze matatizo yake na ajue kitu gani kinamliza.
"Una tatizo gani Jeff? Niambie mwanangu"
"Sijui hata nina tatizo gani"
"Kwanini hujui? Na mbona unalia?"
"Najihurumia mamy, sijielewi kwakweli, sijitambui kabisa"
"Nieleze basi tatizo lako"
Muda huu Sabrina alikuwa karibu sana na Jeff huku akimbembeleza, Jeff naye aliinama bila ya kusema chochote kile. Kisha Sabrina akamuuliza Jeff,
"Inamaana unanificha? Hutaki kuniambia ukweli?"
"Nashindwa kusema mamdogo"
"Sasa ukishindwa kusema kwangu utaweza kwa nani? Mimi ndio mtu pekee ninayekuelewa Jeff, tafadhari niambie"
Jeff bado aliendelea na msimamo wake wa kushindwa kusema na kumfanya Sabrina achukie sasa,
"Kama kusema hutaki umekuja kwangu kufanya nini? Haya jilize hapo ukichoka utaniita"
Sabrina akainuka na kwenda chumbani kwake na kumuacha Jeff akiwa pale sebleni amejiinamia.
Sabrina alipoingia chumbani kwake, moja kwa moja akachukua simu yake na kumtumia ujumbe mfupi Sakina,
"Toto lako lipo huku linajiliza peke yake, naliuliza tatizo nini halitaki kusema"
Kisha akajilaza kwenye kitanda chake, muda kidogo ule ujumbe ukajibiwa na kumfanya Sabrina afungue haraka simu yake kuangalia kitu alichojibiwa na Sakina.
"Achana nalo hilo halijielewi"
Sabrina akacheka sana na kuandika,
"Na kweli halijielewi, ndiomana nimeliacha sebleni lijilizee wee hadi lichoke. Mitoto ya siku hizi bhana kama mitahira yani na kukua kote kule eti bado linajiliza"
Kisha akautuma ule ujumbe kwa Sakina na kuendelea kujilaza pale kitandani kwake huku akijishauri kwenda kuoga.
Muda wote Sabrina anamtumia ujumbe Sakina kwenye ile namba bila kujua kuwa simu ya Sakina alikuwa nayo Jeff kwa siku hiyo.
Jeff aliumia sana kwa zile jumbe alizozituma Sabrina kwenye simu ya mama yake, na ndiomana ujumbe wa kwanza akamjibu ili aone kuwa ataendelea kutuma ujumbe gani, ila ujumbe wa pili ukamuuma zaidi na kumfanya ainuke na kuondoka tena bila hata ya kumuaga Sabrina ambaye alikuwa ndani huku akijua amemtumia ujumbe Sakina kumbe simu ipo kwa Jeff.
Sabrina akiwa bado anajishauri, simu yake ikaingia ujumbe. Moja kwa moja akajua utakuwa umetoka kwa Sakina, alipochukua simu kuangalia akakuta ujumbe umetoka kwa Sam
"Naomba ujiandae, nakuja kukupitia twende wote kula chakula cha usiku leo"
Sabrina alisoma ule ujumbe huku akitabasamu na kuinuka pale kitandani na kwenda kuoga, hapakuwa na tatizo sana kwavile chumba chake kilikuwa na choo na bafu pia.
Akaoga na kuanza kuvaa kwaajili ya huo mtoko kwani hata muda nao ulienda kiasi.
Alipomaliza kuvaa akatoka chumbani kwake huku akiongea,
"Wee Jeff bado unajiliza hapo, mi mwenzio nataka ku...."
Akanyamaza baada ya kuona anaongea mwenyewe wakati muhusika hayupo, akajaribu kuangalia na kuita ila hakuitikiwa, ikaonyesha wazi kuwa Jeff alishaondoka muda mfupi uliopita.
"Khee huyu mtoto kweli ni mwehu, yani kaondoka bila hata ya kuniaga mmh!"
Akaamua kukaa na kumngoja Sam, muda mfupi ukapita na Sam akawasili mahali pale kwa lengo la kumchukua Sabrina na kwenda naye kwenye chakula cha usiku.
Wakaondoka pale huku Sabrina akiwa na wazo kwamba leo ataambiwa na Sam kama anampenda na kumuhitaji kimapenzi.
Walifika hotelini na kwenda kukaa eneo moja zuri sana kisha wakaagiza vitu wanavyotaka na maongezi ya hapa na pale yakaendelea.
Sam alitamani kumuuliza Sabrina kuhusu Jeff ila alisita na kuona kama vile Sabrina ataona kuwa anamfatilia mambo yake, akatamani pia kumwambia kama anampenda ila akasita pia na kuona kuwa Sabrina atahisi kufanyiwa yote yale sababu ya mapenzi tu na si vinginevyo.
Wakati yeye akifikiria hayo, Sabrina naye alikuwa akijiuliza kuwa kwanini Sam hamwambii ukweli kama anampenda huku wakiendelea na maongezi mengine.
Sam akajitahidi kuziba hisia zake kwa Sabrina ila mwisho wa siku alianza kumwambia kimafumbo,
"Nikwambie kitu Sabrina!"
"Niambie Sam"
Muda huu Sabrina alijawa na tabasamu usoni kwani aliamini kuwa kitu anachotaka kuambiwa na Sam ni kuwa anapendwa tu.
Sam akaanza kwa kumuuliza Sabrina swali
"Hivi kama mtu unampenda, utafanyaje ili ajue unampenda na asiweze kuwafikiria wengine?"
Sabrina akapumua kidogo na kujibu,
"Inatakiwa umwambie kuwa unampenda ili ajue"
"Kwani vitendo haviwezi kumuonyesha kuwa unampenda?"
"Vitendo vinamuonyesha ndio, ila unapomwambia ndio inakuwa vizuri kwake na atafurahi kufahamu hilo"
"Sawa basi nitamwambia"
Sabrina akashtuka na kumuuliza Sam,
"Kwani kuna mtu unampenda?"
"Ndio, tena nampenda sana. Natamani siku moja awe mke wangu"
Sabrina akajibu kwa kunyong'onyea,
"Basi mwambie"
"Nitamwambia tu siku ikifika, nikipata muda nitamwambia ukweli wote ulivyo ili ajue"
Sabrina akatulia kwa muda na kuamua kubadilisha mada kwani aliona mada ile kutompendeza tena.
Walipomaliza kula, Sabrina akadai kuwa amechoka sana, ikabidi Sam amrudishe Sabrina nyumbani kwake.
Sabrina alitulia nyumbani kwake na kuyatafakari maneno ya Sam aliyokuwa akiyaongea,
"Inamaana yupo mwingine anayempenda na sio mimi? Kwanini isingekuwa mimi jamani! Yani huyu Sam na kunifanyia mambo yote haya kumbe kuna mwingine anayempenda!"
Aliwaza sana Sabrina na kujikuta furaha yake ikitoweka kwani alidhani kuwa ni yeye anayependwa na Sam ila maneno ya Sam ya kumueleza kuwa kuna mtu anampenda yalimkosesha raha kabisa.
Akawaza na mwisho wa siku akaamua kulala ili awahi kazini.
Inaendeleeah
No comments: