Simulizi: Je Haya Ni Mapenzi Sehemu Ya Kumi na Tano (15)
Kulipokucha kama kawaida, Sam alienda kumpitia Sabrina na kwenda naye kazini. Ila Sabrina alipotoka kazini siku hiyo alipotoka saluni hakutaka kwenda nyumbani kwake na wala hakutaka kupelekwa na Sam.
Alichukua usafiri na kwenda moja kwa moja nyumbani kwao ili kumueleza mama yake yaliyojiri kwa jana yake,
"Basi ndio akaniambia hivyo mama, yani roho iliniuma kweli yani"
"Huwezi jua mwanangu, labda huyo ampendae anamaanisha ni wewe""
"Hapana mama, ingekuwa ni mimi lazima angeniambia tu. Yani ndio nishamkosa tayari"
"Usijali sana mwanangu, huwezi jua Mungu amekupangia nini"
"Ni kweli mama, ila sitaki mwanaume mie niliyopitia yanatosha tayari"
Joy akampa moyo pale mwanae na kuanza maongezi mengine.
"Hivi wale watu wa ajabu wameishia wapi kutufatilia mama?"
Joy akacheka sana na kumjibu mwanae,
"Wale walikuwa wakikufatilia wewe mwanangu, sasa ulipoondoka nao wakaacha na vile hawakujua ulipo ndio kabisa. Ila sielewi walikuwa na lengo gani kwakweli"
"Ila bora yalipita mama, leo nitalala hapa hapa"
Kwahiyo siku hiyo Sabrina akalala nyumbani kwao na kesho yake asubuhi akaenda moja kwa moja kazini.
Sam aliumia sana na kuhisi kuwa Sabrina kuna mahali alikuwa na mtu mwingine.
Aliingia ofisini kisha akatoka nje ili kumuona Sabrina atakavyokuja ofisini.
Sabrina naye wakati yupo njiani akielekea ofisini, akakutana na foleni.
Akaamua kushuka kwenye ile daladala na kujaribu kutafuta usafiri wa bodaboda ili aweze kuwahi.
Wakati anang'aa ng'aa macho kutafuta usafiri wa haraka, kuna pikipiki ilifika na kusimama mbele yake.
Kumuangalia vizuri alikuwa ni Fredy.
Sabrina alifurahi kuona kuwa usafiri umepatikana kirahisi vile, akamsalimia na kumwambia ilivyo kisha Fredy akamwambia Sabrina apande kwenye ile pikipiki ampeleke.
Sabrina akapanda na safari ikaanza.
Alipofika karibu na mlango wa ofisi, Fredy akasimama kisha Sabrina akashuka na kumuaga pale Fredy.
"Asante sana Fredy kwa msaada wako"
"Usijali Sabrina, ila naomba nikuombe kitu"
"Niombe tu Fredy"
"Naomba badae nije kukupitia, nina maongezi na wewe kidogo Sabrina"
Sabrina hakuwa na pingamizi sana kwani alishika lile neno la kata neno sio wito, kwahiyo akamwambia muda wa kutoka na kuingia ofisini.
Mambo yote hayo yalikuwa yakishuhudiwa na Sam na kumuumiza sana, na kutambua kuwa Sabrina hisia zake zipo kwa mtu mwingine na sio kwake.
Kisha naye akarudi ofisini kwake kuendelea na kazi zake za kawaida.
Jioni ilipofika alijua itakuwa kama kawaida, yani yeye kumchukua Sabrina na kumrudisha kwake.
Ila akashangaa kumuona Sabrina akiondoka bila hata ya kwenda kumuaga kama ilivyokuwa kawaida yake.
Ikabidi aangalie kwenye camera zao kuwa Sabrina anawahi kitu gani nje, akamuma Sabrina akitoka na kupanda ile pikipiki iliyomleta asubuhi.
Sam akazidi kupatwa na wivu na kuumia moyoni mwake, akaamua afanye kitu cha kumkomesha Sabrina.
Fredy akampeleka Sabrina hadi mahali alipotaka kufanya naye mazungumzo kwanza.
"Kwanza kabisa naomba msamaha kwa kukupotezea muda Sabrina"
"Bila samahani Fredy"
"Nina ujumbe mzito sana juu yako"
"Ujumbe gani huo, hebu niambie"
"Yani huwezi amini Sabrina, nimeonyeshwa kuwa....."
Kabla hajasema, simu ya Sabrina ikaita. Alipoiangalia, mpigaji alikuwa ni Sam.
Sabrina akaipokea ili kusikiliza alichokuwa akipigiwa simu,
"Mbona umeondoka bila kuaga?"
"Nilimuaga secretary jamani Sam"
"Mie ni bosi wako unatakiwa uwe na heshima, kuzoeana isiwe tabu. Huyo secretry sio muajiri wako na hajui majukumu yako, sasa unatakiwa urudi upesi kuna nyaraka zinatakiwa hapa"
Kisha akakata simu na kumfanya Sabrina astaajabu na kushangaa kwani hakutegemea kama ipo siku Sam ataongea kwa ukali kiasi kile.
Sabrina akamuangalia Fredy kwa unyonge na kumwambia
"Natakiwa nirudi tena ofisini Fredy"
"Kheee si ushatoka tayari!!"
"Ndio nishatoka, ila nimeambiwa eti kuna kazi sijaimalizia"
Fredy hakuwa na jinsi zaidi ya kumrudisha Sabrina tena ofisini na kumuaga,
"Nije kukuchukua ukitoka tena au?"
"Muda utakuwa umeenda Fredy kwahiyo usijali"
"Hapana Sabrina, nipo tayari kufanya chochote kwaajili yako"
"Usijali Fredy, tafadhari nit aenda mwenyewe"
"Basi naomba kesho tuonane ili nikupe ujumbe ambao nilitakiwa kukupa leo"
"Hakuna tatizo tutaonana tu Fredy"
Kisha Sabrina akaenda ofisini kwa Sam moja kwa moja.
"Nimekuja bosi"
"Kaa hapo kwenye kiti"
Sabrina akakaa na kuanza kumsikiliza Sam kuwa amemuitia nyaraka zipi.
"Una bahati nyaraka zimeonekana, ila siku nyingine usifanye ujinga kama wa leo. Uwe unaaga kwanza kabla ya kuondoka"
Sabrina alichukia kimoyo moyo ila tu hakuweza kuonyesha jinsi gani amechukia muda huo.
"Basi naomba ruhusa niende nyumbani bosi"
"Usijali, tutaondoka pamoja na nitakupeleka"
Sabrina akatulia kimya kwani hakuweza kubishana na bosi wake.
Fredy alipotoka pale ofisini kwakina Sabrina aliongoza moja kwa moja mpaka nyumbani kwakina Sabrina.
Alimkuta Joy akiwa na shughuli zake.
"Khee Fredy karibu, za siku nyingi! Umepotea sana"
Fredy alimsalimia mama wa Sabrina na kuanza kumwambia kilichompeleka mahali pale.
"Nina shida mama"
"Shida gani hiyo? Niambie"
"Shida yangu ni moja tu, mwambie Sabrina awe makini sana"
"Kivipi Fredy?"
"Kuna mtu anamfatilia Sabrina, na asipokuwa makini atampeleka mahali pabaya. Mwambie awe makini"
"Mbona unanitisha Fredy, mtu gani huyo?"
"Mi simjui mama ila ndio hivyo, kwaheri"
Fredy akaaga na kumuacha Joy na viulizo vingi kichwani bila hata ya majibu.
Sabrina alimngoja Sam na kisha wakaianza safari ya kurudi nyumbani kwa Sabrina kwanza.
Walipofika pale nyumbani kwa Sabrina walishangaa kuona kuna mtu amelala kwenye mlango wa Sabrina.
Wakashtuka kwani hawakumuelewa mtu yule, Sabrina akataka amsogelee ili amjue kuwa ni nani ila Sam akamzuia Sabrina kuwa asisogee.
Wakati wakibishana, simu ya Sabrina ikaanza kuita, ikabidi aichukue na kuipokea.
Mpigaji alikuwa ni mama yake,
"Sabrina mwanangu, nina ujumbe wako"
"Ujumbe gani mama wakati huku mwenzio nimekutwa na makubwa"
"Makubwa!! Makubwa gani hayo?"
"Yani ndio kwanza nimerudi nyumbani, hapa nashangaa kwani nimemkuta mtu amelala kwenye mlango wangu"
"Kheee mwanangu, isije ikawa ndio mtu niliyeambiwa huku"
"Mtu gani tena? Mbona unanitisha mama?"
"Kuwa makini mwanangu, nasikia kuna mtu anakufatilia na mtu mwenyewe si mzuri kwako kwahiyo kuwa makini"
"Sawa mama"
"Lolote litakalotokea unijulishe Sabrina, sawa eeeh!!"
"Usijali mama angu"
Ile simu ilipokatika ikabidi Sabrina amueleze Sam alichoambiwa na mama yake ili aweze kuona ni jinsi gani atamsaidia.
"Basi tutoe taarifa polisi Sabrina, au unaonaje?"
"Hapana Sam, ngoja tumuone kwanza kuwa ni mtu gani yule ndio tutoe taarifa"
Sam akamuangalia Sabrina na kumkubalia wazo lake, wakaanza kusogea karibu ili wajue ni nani.
Yule mtu akajigeuza pale mlangoni na kufanya sura yake igeukie upande wao, hapo Sabrina akashtuka na kumuangalia Sam kisha akamwambia,
"Si Jeff yule!!"
Sam akamuangalia tu Sabrina bila ya kumjibu chochote, Sabrina akamuacha Sam akiwa amesimama na kumkimbilia Jeff pale mlangoni, akainama na kuanza kumtikisha
"Jeff, wee Jeff wewe!!"
Jeff akashtuka na kumuangalia Sabrina,
"Mbona umelala hapa mlangoni, una matatizo gani?"
Jeff alikuwa kimya tu, ikabidi Sabrina afungue mlango wake na kumwambia Jeff aingie ndani kisha yeye akatoka nje na kumfata Sam mahali alipokuwa amesimama ili amuage.
"Sam, yani umesimama hapo hapo tu!! Asante kwa kunileta nyumbani"
"Aah usijali kwa hilo, ila yule kijana huwa ana matatizo gani?"
"Akili za kitoto huwa zinamsumbua yule, ila nitakwambia vizuri kesho"
Sam akaamua kumuaga Sabrina na kuondoka zake.
Sabrina akarudi ndani ili kuyajua matatizo ya Jeff,
"Eeh Jeff niambie una matatizo gani?"
"Sina matatizo"
"Unamaana gani kusema hivyo?"
"Muulize mama"
Ikabidi Sabrina ampigie simu Sakina ili amuulize,
"Dada, Jeff yupo huku kwani ana matatizo gani?"
"Mwache huyo, njoo kesho nyumbani nikuelezee vizuri"
"Kheee makubwa haya, basi sawa dada"
Kisha akamgeukia Jeff na kumwambia,
"Siku nyingine ukiwa unakuja kwangu uwe unasema Jeff sio kulala kwenye mlango, na kama una usingizi sana, chumba kile pale nenda ukalale."
Jeff hakumjibu chochote Sabrina zaidi ya kuinuka na kwenda kwenye chumba ambacho alionyeshwa na Sabrina.
Alipofika kwenye kile chumba akajilaza, Sabrina akainuka na kumchungulia akamuona amelala.
Sabrina akatikisa kichwa kama ishara ya kusikitika na kuanza kuongoza kwenda chumbani kwake,
"Yani watoto hawa akili zao loh!"
Alipofika chumbani akapigiwa tena simu na mama yake,
"Vipi huyo mtu uliyesema yupo mlangoni kwako ametoka?"
Sabrina akacheka na kumjibu mama yake,
"Yani mama ni kichekesho tu, eti mtu mwenyewe alikuwa ni Jeff huyo mtoto wa Sakina"
Joy naye akacheka na kumjibu mwanaye,
"Saivi ndio umenikumbusha kitu hapa, huyo Jeff kabla hajaondoka kuja huko alikuja kwangu na kuniaga kuwa anakuja huko, nimesahau kukwambia kutokana na yale maneno niliyoambiwa"
"Hebu mama nieleze vizuri kuhusu yale maneno"
Joy akamueleza Sabrina vile ambavyo aliambiwa na Francis,
"Sasa mwanangu, inabidi uwe makini. Bora urudi ukae hapa nyumbani au huko kwako utafute mtu wa kukaa naye"
"Kweli mama, ila kuna wazo nimelipata hapa"
"Wazo gani hilo?"
"Kwanini nisimuombe Sakina kuwa nikae na mwanae kwa siku mbili tatu ili niangalie mambo yatakavyokuwa!"
"Wazo lako ni zuri mwanangu, hebu lifanyie kazi hilo wazo kwakweli"
Sabrina akaendelea kuongea na mama yake mawili matatu, kisha wakaagana na kukata simu.
Sabrina akafikiria sana kuwa ni mtu gani anayemfatilia ila hakupata jibu kabisa.
Sabrina alipolala akajiwa na njozi tena kuwa ana mtoto na ameolewa, akashtuka na kujiuliza
"Huyo baba watoto na mume wangu ni nani? Mbona napata maswali bila ya majibu? Ila inawezekana akawa Sam, lakini mbona haniambii chochote? Na vipi na hali yangu nitaweza kweli kuzaa? Mwanaume nitakayelala naye atapona kweli? Mmmh naogopa, hapa dawa ni moja tu kama ikatokea mtu akanitongoza nitamwambia sitaki kufanya naye chochote hadi ndoa. Nadhani hiyo itasaidia"
Sabrina alijiuliza maswali na kujijibu mwenyewe huku akiendelea kujipa matumaini ya aina tofauti tofauti, na moyo wake ukimwambia wazi kuwa Sam ndiye mwanaume pekee ambaye ni sahihi kwake.
Kulipokucha, kama kawaida. Sabrina alijiandaa kwaajili ya kwenda kazini.
Akaenda kumgongea Sam na kumuaga,
"Kama utatoka basi funguo zangu nizikute kule kwa mama"
Na alipotoka tu nje akamkuta Sam na gari yake akimsubiri kwaajili ya kwenda naye kazini.
Wakasalimiana na kuendelea na safari hadi walipofika ofisini na kila mmoja kuendelea na majukumu yake ya kila siku.
Kwasababu siku hiyo ilikuwa ni siku za mwisho wa wiki, ilikuwa ni Jumamosi Sabrina akaona itakuwa vyema kama ataenda kumuaga mapema Sam ili awahi kwenda kuzungumza na Sakina.
Akafika kwa utaratibu kabisa kwa Sam,
"Samahani bosi, naomba uniruhusu niende nina dharula kidogo"
"Dharula gani hiyo?"
"Mama ameniita nyumbani, anataka kuzungumza na mimi"
"Kwasababu ni mama yako basi nakuruhusu uende, ila nakuomba badae nije mimi kukuchukua hapo kwenu na kukurudisha kwako"
Sabrina hakuwa na pingamizi juu ya hilo, ikabidi tu amkubalie Sam na kuianza safari yake.
Alipokuwa njiani kurudi kwao, kuna baba alikuja karibu yake na kumsalimia,
"Hujambo Sabrina!"
"Sijambo, shikamoo"
Sabrina alimtolea macho yule baba sababu sura ilikuwa ngeni kwenye macho yake, yule baba akaitikia na kumwambia Sabrina
"Marhaba, najua ni vigumu sana kwa wewe kunifahamu mimi ila mimi nafahamiana sana na mama yako. Ukifika nyumbani mwambie, anko James yule mwalimu wa kwaya anakusalimia sana"
Sabrina akauliza,
"Mwalimu wa kwaya? Kwaya gani?"
"Wewe mwambie tu mama yako hivyo atakuelewa"
Kisha yule baba akaondoka na kumfanya Sabrina apate maswali juu ya taswira ya huyu mwalimu wa kwaya na kama mama yake amewahi kuimba kwaya.
Sabrina aliendelea na safari yake hadi kwao, na hapo akamkuta mama yake akiendelea na shughuli zake.
Akamsalimia na kuendelea na maongezi mengine,
"Kilichonileta huku leo ilikuwa ni kukusalimia tu ila nia yangu kubwa ilikuwa ni kuongea na Sakina, ila kwa mtu niliyekutana naye njiani amefanya nipate maswali ya kukuuliza leo mama"
"Maswali gani hayo?"
"Kwanza kabisa, je umewahi kuimba kwaya mama?"
"Ndio, ila ni zamani sana. Kwanini umeniuliza?"
"Mbona hujawahi kutuambia mama? Leo nimekutana na mwalimu wako wa kwaya"
Joy akashtuka na kumuuliza mwanaye,
"Umekutana naye wapi? Na je amekufahamu vipi?"
Sabrina akamueleza mama yake jinsi alivyokutana na mwalimu huyo wa kwaya.
"Tena kasema nikusalimie sana"
"Haya nashukuru mwanangu kwa salamu"
"Kwani mama, una undugu na yule mwalimu wa kwaya?"
"Kwanini?"
"Kafanana sana na kaka James, halafu naye kasema kuwa anaitwa James"
Joy akacheka na kumbadilishia mada binti yake,
"Hebu nenda kwa Sakina huko mkajadiliane mambo yenu, duniani wawili wawili bwana"
Ikabidi Sabrina acheke naye na kumuaga kidogo mama yake na kuelekea kwa Sakina.
Alimkuta Sakina akiwa ametulia ndani kwake na kumsalimia,
"Nimekuja sasa uniambie matatizo ya mtoto wetu Jeff"
"Bora umekuja, kuna siku Jeff aliondoka na simu yangu halafu mi mwenyewe hata sikujua, aliporudi hapa alikuwa na hasira sana. Nilipomuuliza akaniambia kuwa nitajisikiaje kuona mwanangu akiitwa litoto litahira, mi nikamwambia kuwa nitajisikia vibaya. Jeff akasema kuwa kuna mtu amemuita hivyo na ananitaka mimi nimpe adhabu kama kweli ningejisikia vibaya, nilipomuuliza ni nani. Akanipa simu na kunionyesha ujumbe, nikaona kuwa wewe umetuma. Hata cha kusema sikuwa nacho ila Jeff akasema nikupe adhabu, kwavile ndio amemaliza kidato cha sita anangoja matokeo nimeona adhabu yake ni aje kukaa kwako"
Sabrina akacheka sana,
"Kweli mwanao hamnazo dada, sasa yeye kaona hiyo ndio adhabu kubwa kwangu?"
Sakina naye akacheka,
"Ndio ni adhabu hiyo ili akusumbue kama anavyonisumbua mimi hapa. Anatoka haagi, mida ya kurudi anajua mwenyewe. Ndio ukome kumuita litoto"
"Ndiomana siku ile aliondoka bila ya kuniaga, kumbe simu yako ilikuwa kwake mmh! Nitamuomba msamaha basi"
Kwa upande wa Sabrina ilikuwa ni kheri kwani hata yeye alitaka kumuomba Sakina ili akakae na Jeff kwa muda kwahiyo akaona wamemrahisishia kazi.
"Ngoja nimpigie aje achukue na baadhi ya nguo zake"
"Hapana usihangaike, wee zifunge tu baadhi kisha nipe nimpelekee tu hakuna tatizo"
Sakina akaandaa nguo za Jeff na kumpa Sabrina aende nazo kisha Sabrina akaaga na kuondoka.
Alipofika tu kwao, alikuta gari ya Sam ikiwa nje ya nyumba yao na kugundua kuwa Sam ameshakuja kumfata.
Akaingia ndani kwao na kumkuta Sam akiongea na mama yake, moja kwa moja Joy alimuuliza mwanae
"Na huo mzigo vipi?"
"Nguo za Jeff hizi mama"
"Aaah sawa, mwenzio amekufata"
Kisha Sabrina akasalimiana tena na Sam na kuongea kidogo kisha wakaaga na kuondoka.
Wakiwa ndani ya gari, Sam akaanza kumwambia Sabrina
"Unajua mimi nikimpenda mtu nampenda kweli"
"Mmh basi mwanamke unayempenda atakuwa na furaha sana duniani"
"Ila, mwanamke ninayempenda mimi sitaki awe na mwanaume mwingine yoyote na laiti kama nikigundua basi naweza kumfanyia kitu kibaya sana"
Sabrina akaguna na kujiuliza kimoyo moyo, "kwanini asinipende mimi huyu kijana jamani?"
Sam akamuuliza Sabrina,
"Mbona umeguna halafu umekaa kimya?"
"Aah! Hamna kitu, natafakari tu huyo mwanamke unayempenda wewe ni wa aina gani!"
"Inamaana haiwezekani nikawa na mwanamke wa kwangu peke yangu?"
"Inawezekana, na wala sikuwa na maana mbaya na kutafakari kwangu"
"Yani mimi nikigundua kuwa kuna mwanaume anamnyemelea mwanamke ninayempenda, basi niko radhi kummaliza mwanaume huyo"
"Upo sahihi Sam, mapenzi yanaumiza sana"
Sabrina akajikuta akikumbuka matukio ambayo yaliwahi kumpata hapo zamani na kumfanya hata afungwe, alijiona akitokwa na machozi hadi Sam akamuuliza
"Mbona unalia?"
"Hapana, macho yananiwasha tu"
Kwa muda huo alitamani afike nyumbani kwake haraka na kujifungia chumbani ili alie kwa uhuru zaidi.
Walipofika, alimshukuru Sam na kumuaga kisha akaingia ndani kwake.
Alimkuta Jeff ametulia huku akitazama video, alimkabidhi ule mzigo wa nguo zake na kuingia chumbani kwake.
Jeff aligundua wazi kuwa Sabrina hakuwa sawa kwa wakati huo.
Sabrina alikaa kitandani kwake na kujikuta machozi yakimtoka na kuanza kujiuliza
"Hivi ni nani mimi atanipenda kwa dhati? Ni nani atanipenda kiukweli? Natamani kupendwa na mimi jamani, eeh moyo wangu tafadhari nakuomba uache kumpenda Sam kwani ana mtu wake tayari anayempenda, yasije kunipata kama yaliyonipata kipindi kile. Ni mwanaume gani yuko pekee? Wote wana wao tayari, rafiki zangu karibia wote wameolewa na wengine wana wachumba zao kasoro mimi tu. Kwani nina kasoro gani mimi?"
Sabrina alijikuta akiumia na kulia sana, alilia hadi usingizi ukampitia.
Alipoamka ilikuwa ni saa tano usiku, alienda sebleni na kumkuta Jeff akiwa macho bado na kumuuliza,
"Jeff huendi kulala?"
"Sina usingizi"
"Huna usingizi kwanini?"
"Na mbona wewe macho yako yamevimba?"
"Sababu nililala"
"Mmh! Nahisi ulikuwa unalia wewe, au hutaki mi nikae hapa kwako mamy?"
"Hapana, sio hivyo usinielewe vibaya"
Jeff akakaa kimya na kumuangalia Sabrina,
"Khee mbona unaniangalia sana?"
"Yani mamdogo, licha ya macho yako kuvimba ila bado u mzuri, kwakweli Mungu alikupendelea sana"
Sabrina akacheka sana,
"Haya, asante toto yangu. Ila ni wewe tu unayeuona huo uzuri"
Sabrina akainuka ili arudi chumbani kwake kulala, ila Jeff akamshika mkono Sabrina na kumfanya Sabrina amshangae.
Sabrina akainuka ili arudi chumbani kwake kulala,
ila Jeff akamshika mkono Sabrina na kumfanya
Sabrina amshangae.
Sabrina akamuangalia Jeff na kumuuliza,
"Nini tatizo Jeff?"
Jeff akamuangalia tu Sabrina bila kusema chochote,
"Hebu niache nikalale mie"
"Nataka tukae wote hapa"
"Kheee! Una wazimu nini, mie nikae hapa kuangalia hayo mapicha yako!! Naenda kulala mie"
Jeff akamuachia mkono Sabrina na kumfanya aende chumbani kwake.
Jeff naye hakuchukua muda pale sebleni na kwenda chumbani pia.
Kuna hisia kali ambazo zilikuwa zikimsumbua Jeff, hisia ambazo hakupenda mtu yeyote azijue.
Zilikuwa zikimsumbua sana na kumpa mawazo muda wote, hisia hizo ndio zilizomfanya Jeff aonekane kama mwehu wakati ana akili zake timamu.
Hakuweza kuzitoa hisia zake na ndiomana alikuwa akiumia muda wote.
Kitendo cha Sabrina kumfokea na kumwambia kuwa ana wazimu kilimuuma ila hakuwa na la kufanya ndiomana akaamua kwenda kulala tu, ila hakulala kwavile hakuwa na usingizi na kuamua kuchezea simu tu.
Sabrina hakupatwa na usingizi kwavile alishalala kabla, akatamani hata angepata mtu wa kuwasiliana nae kwa usiku ule
"Sijui nizame kwenye mitandao ya kijamii ili nipate watu wa kupoteza nao muda usiku huu!"
Wazo hilo likamkaa na kumfanya achukue simu yake na kuzama kwenye mtandao wa facebook, huku akijisemea
"Ila humu wanajaaga watoto tu, basi nitakutana na ujinga mtupu ila kwavile nahitaji kupoteza muda basi si mbaya sana"
Akaanza kuperuzi ule mtandao, akaona kunamtu kamtumia ombi la urafiki muda ule. Alipoangalia jina hakulifahamu kwani liliandikwa 'Prince J'
Pia hapakuwa na picha yoyote, ila kwavile alitaka mtu wa kupoteza naye muda, akaamua kukubali lile ombi la urafiki na kuanza kuzungumza na yule mtu kwa njia ya maandishi.
Sabrina alikuwa akiandika huku akitabasamu sana, kisha akajisemea
"Kweli facebook kuna watu wa ajabu, yani mtu hata hanifahamu ndio kwanza kaiona picha yangu leo eti ananisifia mi mzuri na kunitongoza eti ananipenda. Kheee, kweli watu wengine ni vichaa humu"
Sabrina alipochoka akamuaga yule mtu na kulala.
Kulipokucha, akachukua simu yake kuangalia kwenye mtandao, moja kwa moja akakutana na ujumbe kutoka kwa Prince J
"Umeamkaje mpenzi"
Sabrina akacheka na kujisemea tena,
"Eti mara hii nishakuwa mpenzi wake, khee makubwa haya jamani"
Hakujibu ule ujumbe bali aliinuka na kwenda kuoga ili ajiandae kufanya mambo mengine.
Alipotoka kuoga, akaangalia tena simu yake na kukutana na ujumbe
"Ungeniambia kama unaenda kuoga ili nije nikuogeshe mpenzi"
Sabrina akashtuka na kumuuliza,
"Umejuaje kama nilienda kuoga?"
"Kwasababu nakupenda, najikuta nikijua vitu vingi kuhusu wewe"
Sabrina akaona analetewa mauzauza sasa, ikabidi akae kimya na kuendelea na mambo mengine.
Alipotoka sebleni, alimkuta Jeff akiwa tayari ameandaa chai na vitafunio mezani
"Mamdogo, karibu chai mezani"
"Khee kweli umekuwa mwanaume wa shoka toto yangu, yani umeandaa mwenyewe duh!"
Sabrina akaenda kunywa chai aliyoandaliwa na Jeff.
Alipomaliza alirudi kukaa huku akijiongelesha
"Naona uvivu, sijui leo mchana kama nitaweza kupika"
Jeff akamwambia,
"Usijali madogo, leo kila kitu nitafanya mimi"
"Kheee kweli mtoto nimepata jamani"
Jeff akacheka tu na kwenda kuendelea na mambo yake mengine.
Huku Sabrina akiendelea kuperuzi simu yake kwenye mitandao ya kijamii, ujumbe ukaingia kwenye simu yake
"Unaonaje kama nikiwa karibu yako hapo mpenzi"
Sabrina akatabasamu na kumjibu,
"Itakuwa vizuri sana"
Yule kijana naye akaandika,
"Napenda nikutoe upweke ulionao na kukufanya uwe mwanamke mwenye furaha duniani"
Sabrina akatabasamu tena, na kumjibu
"Una maneno ya ushawishi sana wewe, ila asante"
"Niruhusu nije mpenzi, niwe karibu yako nikuliwaze"
Sabrina akapumua kidogo na kujisemea, "Yani huyu mtu loh! Kuja aje wapi ananijua mie mmh kweli facebook ina mambo jamani"
Muda anajiongelesha mwenyewe, Jeff alikuja na kukaa karibu yake huku akimuangalia na kumuuliza,
"Mbona unacheka mwenyewe?"
"Mambo ya mitandao haya mwanangu loh ni vituko"
Jeff naye akacheka na kumuuliza,
"Kwani unatumia mtandao gani hapo?"
"Facebook hiyo mwanangu"
"Kumbe huwa unaingia huko na wewe duh!"
"Kwani tatizo nini? Huku sio kwa watoto peke yao, hata watu wazima kama mimi wapo"
"Sina maana hiyo mamy, umenielewa vibaya"
Kisha Jeff akainuka na kumuacha Sabrina akiendelea na simu yake pale.
Alipoangalia tena kwenye ule mtandao akakuta ujumbe kutoka kwa yule mtu,
"Mbona kimya mpenzi? Au ombi langu kwako limekukera?"
"Hapana, sio hivyo"
"Mi napenda niwe karibu na wewe, nikuliwaze, nikubembeleze na kukufanyia kitu chochote unachokitaka. Tafadhari nakuomba unikubalie ombi langu mpenzi"
Wakati akifikiria kujibu, simu yake ikaita na mpigaji alikuwa ni Sam
"Naomba nije nikuchukue leo tukatembee Sabrina"
"Hakuna tatizo Sam"
Wakapanga muda wao utakaowafaa kutoka.
Alipomaliza kuongea na simu ikabidi aende kujiandaa kwaajili ya hiyo safari.
Muda ulipofika, Sabrina akapigiwa simu na Sam kuwa atoke nje kwani yeye yupo nje anamngoja.
Sabrina akamuita Jeff na kumuaga,
"Mi natoka Jeff , nadhani nitarudi badae sana kwahiyo kuwa makini tu hapa ndani"
Jeff hakuwa na pingamizi zaidi ya kukubaliana na mwenye nyumba.
Sabrina akatoka nje, Jeff naye akasogea kumchungulia Sabrina, hadi alipopanda gari na ile gari kuondoka kabisa.
Akajikuta akijiuliza,
"Sijui ndio mchumba ake!! Silipendi lile likaka basi tu sina la kufanya"
Sabrina alipokuwa kwenye gari ya Sam akamuuliza,
"Mbona leo hukutaka hata kuingia ndani kwangu?"
"Si kapo kale katoto kako! "
"Nani? Jeff au?"
"Ndio huyo huyo bhana"
"Kafanyaje kwani?"
"Simpendi tu, nadhani damu yake na yangu haziendani"
"Jamani Sam usiseme hivyo, Jeff ni mtoto mpole sana tena asiye na makuu, usimseme hivyo bhana"
"Haya tubadilishe mada, usije ukalia bure hapa maana unavyokapenda ni balaa"
Safari yao ikaendelea na kukomea kwenye nyumba moja kwa nje.
"Vipi Sam, mbona tumekuja hapa?"
"Nataka nikutambulishe kwa mjomba wangu, jana alikuja ofisini ila hakukukuta"
"Sawa, hakuna tatizo"
Wakaingia kwenye ile nyumba na kukaribishwa vizuri sana.
"Sabrina, huyu ni Shangazi yangu. Anaitwa Betty ni mke wa mjomba"
Sabrina akatabasamu na kusalimiana vizuri na huyo shangazi mtu.
Kisha Sam akamuuliza shangazi yake,
"Mjomba yuko wapi?"
"Bado hajarudi kutoka kanisani ila msijali, atarudi muda sio mrefu"
Wakaendelea kuongea mawili matatu huku wakimngoja mjomba huyo arudi na Sabrina apate kumfahamu.
Kwenye mida ya jioni, huyo mjomba aliwasili na kuwakuta Sabrina na Sam wakiwa ndani kwake.
Akafurahi sana na kuwasalimia kwa shangwe, kisha Sam akaanza utambulisho
"Mjomba, huyu anaitwa Sabrina ni....."
Kabla hajamaliza mjomba akadakia,
"Namjua huyu, ni mtoto wa Joyce hata jana nilikutana naye"
Sabrina akacheka na wote wakacheka na kuendelea na mazungumzo mengine, ila Sabrina alijisikia kumuuliza maswali yule mjomba haswaa kuhusu mama yake na uimbaji wa kwaya.
"Eti mjomba, mama yangu alikuwa anaimba kwaya vizuri eeeh!!"
"Tena alikuwa anaimba vizuri sana, sijui ni kitu gani kilimpelekea mama yako kuacha kuimba kwaya wakati alikuwa ni muimbaji mzuri sana. Yani angeendelea hadi leo basi angekuwa ni kati ya waimbaji wakubwa nchini"
"Unajua nini mjomba, mi kila nikimuuliza mama kuhusu kuimba kwaya huwa hanijibu vizuri. Hebu nieleze kwa kifupi, na kwanini hamkumfatilia tena baada ya kuacha kuimba kwaya ili arudi?"
Mjomba akaamua kumueleza Sabrina kwa kifupi kama ambavyo yeye alikuwa akielewa.
"Hakuna anayejua sababu halisi ya Joyce kuacha kuimba kwaya, ila tetesi za watu wengi ni kuwa mumewe alimkataza kuimba sababu haijulikani. Ila Joy alikuwa ni muimbaji mzuri sana, alijua kuipangilia vizuri sauti yake, aliweza kuimba hata alipokuwa mjamzito tena mimba kubwa kabisa lakini Joy bado alimudu kuimba vizuri kwa sauti yenye mvuto. Mambo yalibadilika alipojifungua tu, kwani aliacha kuja kwenye kwaya kabisa"
"Mlijaribu kumfatilia ili kujua nini tatizo?"
"Tumemfatilia sana, kama mimi ndio sikuchoka kumfatilia hata nikawajua nyie watoto wake wote . Ila mwisho wa siku Joy na mumewe wakahama kule walipokuwa wanakaa hadi leo"
"Kumbe!! Mama alikuwa anaimba na mimba ya mtoto gani huyo?"
"Mtoto wake wa kwanza, yule kaka yenu James"
"Aaah ndiomana kaka James naye anapenda sana kuimba, leo umenijulisha kitu mjomba"
"Ndio hivyo, mama yako alikuwa muimbaji mzuri sana, ndiomana hata mimi mtoto wangu wa kwanza nimemuita Joyce kwa ukumbusho wa uimbaji wa mama yako"
Kisha mjomba akamuita huyo Joy ili wapate kumsalimia vizuri.
Joy akasalimiana na wakina Sabrina pale na kufurahi nao.
Wakaongea mengi sana na mwisho wa siku, Sam na Sabrina wakaaga na kuondoka.
Wakiwa ndani ya gari, Sabrina alikuwa akijiuliza maswali mengi kuwa Sam alikuwa na maana gani kwenda kumtambulisha kwa mjomba wake, na je alikuwa akitaka kumtambulisha kama nani yake? Lakini hakupata jibu na kuendelea kujiwazia moyoni tu.
Sam naye alikuwa na mawazo yake ambayo hakupenda kumshirikisha Sabrina kwa muda huo kwani yeye aliona bado muda, alihitaji muda muafaka kuweza kulifikisha wazo lake hilo.
Kwahiyo wote wawili walijikuta wakiwa kimya tu ndani ya lile gari.
Kufika mbele, Sam akaamua kuuvunja ukimya ule
"Unaonaje kama tukienda kula kwanza chakula cha usiku halafu ndio nikupeleke nyumbani?"
"Hakuna tatizo Sam"
Wakaenda mahali palipotulia kiasi na kuagiza chakula na vinywaji, baada ya muda kidogo Sam akainuka na kwenda msalani.
Sabrina akiwa amekaa kwenye eneo lile, mara akafatwa na muhudumu mmoja wa kike kwa karibu kisha muhudumu huyo akamwambia Sabrina,
"Hongera dada, umempata huyu jamaa ana hela sana. Mng'ang'anie leo hadi asubuhi ila hakikisha....."
Kabla hajamaliza kuongea, Sam alikuwa amerudi kwenye ile meza yake na yule muhudumu kuondoka.
Kisha Sam akamuuliza Sabrina,
"Mlikuwa mnaongea nini na yule?"
"Aaah aaah aaa alikuwa anauliza kama naongeza vinywaji"
"Hayo maneno umetunga ndiomana ulikuwa unasita kuongea, kwakweli hii ndio sababu ya mimi kuchukia vibaa vya uswahilini yani ni umbea mtupu"
Sabrina akagundua wazi kuwa Sam amechukia na kubadilisha mada muda ule.
Walipomaliza kula, Sam akamrudisha Sabrina nyumbani kwake na kumuaga kisha naye akaondoka zake.
Sabrina akaingia ndani na kumkuta Jeff amekaa ila alipomuona tu Sabrina mlangoni, akainuka na kwenda kumkumbatia kwa nguvu.
Sabrina akajaribu kumtoa Jeff mikono ila bado Jeff hakutaka kuacha na kuendelea kumkumbatia tu.
Sabrina akaingia ndani na kumkuta Jeff amekaa
ila alipomuona tu Sabrina mlangoni, akainuka na
kwenda kumkumbatia kwa nguvu.
Sabrina akajaribu kumtoa Jeff mikono ila bado
Jeff hakutaka kuacha na kuendelea kumkumbatia
tu.
Sabrina akachukizwa na kile kitendo na kumwambia Jeff kwa ukari,
"Wee mtoto hebu niache huko"
Jeff akamuachia Sabrina, wakati huo Sabrina aliendelea kufoka
"Kunikumbatia gani huko?"
"Nisamehe mamy"
"Wewe umeshakuwa mkubwa saivi Jeff, mambo ya kitoto uache sasa"
"Inamaana hunipendi siku hizi mamy?"
"Hapana, kukupenda nakupenda tena sana tu ila michezo ya kitoto uache. Si vizuri kunikumbatia kiasi kile"
"Sawa mamy nimekuelewa"
Kisha Sabrina akaenda chumbani kwake akiwa amejichokea kutokana na mizunguko ya siku hiyo.
Moja kwa moja akaenda kulala na kupitiwa na usingizi pale pale.
Aliposhtuka ilikuwa tayari ni usiku sana, akakumbuka kuwa alilala bila hata ya kuoga na kuinuka kwenda kuoga.
Alipotoka kuoga, akajihisi usingizi umekatika na kichwa chake kutawaliwa na mawazo tena, akajikuta akiwaza kuwa yule muhudumu wa pale baa alitaka kumueleza kitu gani kuhusu Sam. Akakosa jibu kabisa, kwavile kichwa chake kilizungukwa na mawazo, akaamua kuchukua simu yake tena na kuzama kwenye mtandao wa kijamii ili kupoteza mawazo yake.
Alipoingia tu kwenye mtandao wa facebook, akakutana na jumbe tano kutoka kwa Prince J na tena akamuma huyo Prince J hewani, ikabidi amuulize,
"Hulali wewe?"
Prince J naye akawa haraka sana kumjibu Sabrina,
"Nalala vipi wakati nakuwaza wewe"
"Kheee! Unaniwaza mimi? Kwanini?"
"Kwasababu nakupenda tena nakupenda sana"
"Unawezaje kumpenda mtu ambaye hujawahi kumuona?"
"Hisia ndio zinazoniongoza Sabrina, nipe nafasi tafadhari. Niruhusu nije nikukumbatie na kukubusu, niwe shuka lako unapolala. Niwe joto lako unapohisi baridi, tafadhari Sabrina sikia kilio changu"
"Khee una mashairi wewe!"
"Sio mashairi Sabrina, ni hisia zangu juu yako"
"Ila mimi ninaye wangu tayari"
"Sabrina, hilo sio tatizo kwangu sababu nakupenda. Nipo tayari kupanga foleni kwaajili yako malkia wa moyo
wangu"
Sabrina alikuwa akitabasamu tu kwani maneno ya Prince J yalimvutia sana, kisha akamuandikia tena,
"Ila mimi sikufahamu, sitaweza kukupenda kwakweli"
"Hakuna tatizo Sabrina, nitasubiri tu sababu nakupenda sana na sitaki nikukose malkia wa maisha yangu"
Sabrina hakuishiwa na tabasamu usoni na kusahau hata kama ule ni usiku tayari.
Alijikuta akijisemea tu,
"Yani huyu mtu ningekuwa namjua ningefurahi sana, ila tatizo simjui mmh! Anavyoongea kwa hisia hadi raha"
Akaendelea kuwasiliana nae na mwisho wa siku usingizi ukampitia na kulala.
Asubuhi aliamshwa na hodi ya Jeff kwenye chumba chake,
alipotahamaki, muda ulikuwa umekwenda sana.
Akainuka haraka pale kitandani na kufungua mlango wake,
"Vipi mamdogo, leo huendi kazini?"
"Hata me mwenyewe najishangaa nilivyochelewa kiasi hiki"
Muda huo huo Sam naye alikuwa akibisha hodi kwenye nyumba ya Sabrina kisha Jeff akaenda kumfungulia na kumkaribisha,
"Sabrina mbona nakupigia simu hupokei?"
"Sikuisikia Sam nisamehe, hata hivyo nimechelewa kuamka. Ngoja nijiandae upesi, ila wewe ungetangulia tu"
"Hapana, nakungoja"
Sabrina akaingia chumbani kujiandaa haraka haraka halafu Sam akakaa kwenye kochi kumngoja.
Jeff akamwambia Sam,
"Si umeambiwa utangulie, huoni kama na wewe unachelewa?"
"Kwani wewe shida yako ni nini?"
"Sio shida yangu ni nini, nilikuwa najaribu kukushauri tu"
"Asante, lakini sihitaji ushauri wako"
Jeff akainuka na kwenda kwenye mambo yake.
Baada ya muda kidogo Sabrina akatoka akiwa tayari amejiandaa na kuondoka na Sam kuelekea ofisini.
Jeff alitulia pale kidogo kisha naye akatoka kwenda kwenye matembezi kidogo kupoteza muda.
Alipokuwa njiani kwenye matembezi yake akakutana na mwalimu wake aliyekuwa akipatana naye sana,
"Jeff huji kututembelea siku hizi!"
"Mambo mengi madam ila nitakuja tu"
"Uje bhana"
"Nitakuja madam"
Jeff akaagana na mwalimu wake huyo kisha kila mmoja kuendelea na safari yake.
Sabrina akiwa kazini kwake akapigiwa simu na namba mpya, akapokea ile simu na kuongea nayo.
Ilikuwa ni sauti ya kiume,
"Sabrina, nakuomba hapa nje mara moja"
"Kwani wewe ni nani?"
Ile simu ikakatika na kumshangaza Sabrina, akainuka na kutoka nje ya ofisi.
Alishangaa kumuona Japhet akiwa mbele yake,
"Khee Japhet! Una shida gani?"
"Mmh jamani Sabrina! Hata salamu mama!"
Japhet akasogea na kutaka kumpa mkono Sabrina, ila Sabrina akaukwepa mkono ule,
"Tafadhari Japhet, nakuomba uende"
"Kwani tatizo ni nini Sabrina jamani? Sioni kosa langu"
Sabrina hakutaka kuendelea kumsikiliza Japhet, badala yake alirudi zake ofisini na kumuacha Japhet pale nje.
Sabrina alikaa pale ofisini na kujikuta akiongea peke yake,
"Mijitu mingine kuharibiana siku tu, sijui hata limetokea wapi na ushetani wake"
Alichukia sana muda huo huku akiendelea na mambo yake mengine.
Muda kidogo, simu ya mezani kwake pale ofisini ikaita na mpigaji alikuwa ni Sam
"Njoo ofisini kwangu"
Sabrina akainuka na kwenda ofisini kwa Sam ili kumsikiliza kuwa Sam anataka nini.
Sam akaanza kuongea,
"Unajua huwa sipendi masikhara katika kazi Sabrina"
"Masikhara gani nimefanya tena bosi?"
"Ulienda kuongea na nani pale nje?"
"Aaah mmh ni mtu aah mi simjui"
"Unaona unavyojiuma uma eeh! Haya nenda ukaendelee na kazi yako"
Sabrina akarudi kwenye ofisi yake na kujiuliza,
"Kwanini Sam anapenda sana kunifatilia? Yani nisijambe loh!"
Muda wa kuondoka ulipofika, Sam alimshtua Sabrina na kuondoka naye.
Wakiwa ndani ya gari, Sam akaanza kumwambia Sabrina,
"Yani mimi nikimpenda mwanamke huwa namfatilia sana hadi ataona kero ila ni kwavile nampenda"
Sabrina akajiuliza kuwa ni mwanamke gani huyo, na hapo akaamua kuuvunja ukimya na kumuuliza Sam,
"Ni mwanamke gani huyo umpendaye?"
"Unataka kumjua?"
"Ndio nataka kumjua, kwani kila siku nakusikia tu ukisema, nami nataka kumfahamu huyo mwanamke mwenye bahati"
Sam akatabasamu na kumwambia Sabrina,
"Usijari, utamfahamu hivi karibuni"
"Kwanini unanificha huyo mwanamke jamani?"
"Nakuahidi Sabrina, siku ya Jumamosi ya wiki hii utamjua mwanamke ninayempenda kwani nitakufanyia Surprise"
Sabrina akakaa kimya kwani hakuweza kuyasoma vizuri mawazo ya Sam, hadi pale alipofika nyumbani kwake na kushuka.
"Asante Sam"
"Usijali Sabrina"
Sabrina akaingia ndani kwake na kumkuta Jeff akiwa ametulia huku akichezea simu yake.
Sabrina akamsalimia Jeff na kuingia chumbani kwake.
Ila alipokuwa chumbani alimfikiria Jeff na kugundua kuwa hajachangamka kama siku zote anavyokuwaga, ikabidi atoke sebleni ili akamuulize kuwa tatizo ni nini.
Inaendeleaaah
No comments: