Simulizi: Je haya Ni mapenzi Sehemu ya 43
Sam alienda hadi mahali alipoweza kuonana tena na yule mdada ambapo yule mdada alijawa na tabasamu tu usoni.
Wakatafuta eneo la karibu na kukaa kwaajili ya maongezi,
"Kwanza kabisa Sam samahani sana kwa kukuita hapa"
"Hata usijali, sina tatizo ndiomana nimeitikia wito "
"Sawa basi nashukuru kwa hilo, kwanza kabisa napenda ujue kuwa mimi nakufahamu wewe vizuri kabisa ila namfahamu zaidi mkeo"
Sam akashtuka baada ya kusikia kuwa mkewe anafahamika zaidi na kumfanya aanze kumsikiliza kwa makini.
"Niambie mke wangu unamfahamu vipi na mimi umenifahamu vipi?"
Kabla huyu dada hajamueleza chochote Sam, akaona ishara kama ya mtu kumuita na kumuomba samahani Sam,
"Naomba nikamsikilize kidogo, narudi muda sio mrefu"
Sam akamuitikia na yule dada akaondoka, huku Sam akitamani kujua kitu ambacho yule dada anajua kuhusu mke wake.
Dorry aliamua leo kuyachoma yale makaratasi ili kupoteza ushahidi wote ambao ulikuwepo.
Ila kabla ya kuchoma, akakifunua tena kile kitabu kidogo na kukutana na maneno mwishoni,
"Sabrina roho yangu, Sabrina mwanamke wa maisha yangu. Nakupenda na sitakuja kumpenda yeyote kama nikupendavyo wewe. Haya maneno ningependa kuyatamka mbele yako ila siwezi kwavile utaona nakukosea adabu, ila ukweli upo kwenye moyo wangu na matendo yangu. Nitakupenda milele yote"
Dorry akapata jibu la Sabrina anayeongelewa pale, alielewa wazi kuwa ni Sabrina yule yule ila bado hakuelewa kwanini Jeff awe na upendo wa namna ile kwa mama yake mdogo?
Makaratasi yake ya mimba na barua akayachoma moto ila kale kakitabu kadogo akakahifadhi kwenye mkoba wake.
Sabrina akiwa nyumbani huku mawazo yakifurika kwenye kichwa chake, akaamua kuchukua simu yake na kuingia kwenye mtandao wa kijamii.
Alikuta akiwa na ujumbe mwingi kwenye sehemu ya ujumbe iliyopo kwenye akaunti yake ya facebook.
Akaamua kufungua ujumbe alioona umebeba picha, na alipofungua tu akaona picha kubwa ikiwa imetangulia.
Sabrina akashtushwa na ile picha, kwani alijiona yeye na Jeff wakiwa kitandani, kisha ujumbe ukafata chini.
Mapigo yake ya moyo yalienda kwa kasi ya ajabu kupita ilivyo kawaida yake.
Sabrina akashtushwa na ile picha, kwani alijiona
yeye na Jeff wakiwa kitandani, kisha ujumbe ukafata
chini.
Mapigo yake ya moyo yalienda kwa kasi ya ajabu
kupita ilivyo kawaida yake.
Sabrina akausoma ule ujumbe kwa mashaka sana,
"Kamwe sitaisahau siku hii katika maisha yangu"
Akamuangalia mtumaji, alikuwa ni Prince J.
Sasa Sabrina akatambua kwa uwazi kabisa kuwa mwanaume aliyekuwa akisumbua akili yake kwenye facebook siku zote alikuwa ni Jeff.
Ila swali lililomjia kwenye akili yake ni kuwa ile picha ilipigwa na nani, wakati inaonyesha kuwa wote wawili wapo kitandani.
"Hivi huyu Jeff ananitakia nini mimi? Sikapendi haka katoto tena"
Kengele ya hatari ikalia kwenye akili yake kuwa hata mimba aliyonayo ni ya Jeff, muda kidogo ukaingia ujumbe kwenye ile akaunti yake kutoka kwa Prince J.
"Wow mamy, leo umeingia hewani. Nimekukumbuka sana, natamani niwe karibu yako. Sitajali chochote, hata ukiamua kutembea na wanaume wa ulimwengu mzima ila mimi bado nitakupenda na nitazidi kukupenda hadi mwisho wangu"
Sabrina aliamua kumuuliza,
"Wewe ni Jeff?"
"Ndio, mimi ni Jeff, mwanaume pekee ninayekupenda kuliko wote duniani"
Sabrina akatulia kidogo na kuwa kama mtu anayefikiria, ujumbe mwingine ukaingia,
"Nilitamani kusema yote haya mbele yako, mbele ya macho yako ila ulikuwa ukinikatisha. Nashukuru kwa barua yako, nitaitunza kama ambavyo natunza moyo wangu"
Swala la barua likamshtua kidogo Sabrina kwani alishasahau kama kuna barua alimuandikia Jeff, akajifikiria tena kuwa alikuwa na akili gani wakati anaandika barua ile kwani baadhi ya maneno yalimjia na kujiona kamavile ni mpumbavu.
Ujumbe mwingine ukaingia,
"Najua Sam anakupenda ila kamwe hawezi kufikia upendo ule ninaokupenda mimi. Sabrina nakupenda sana, mwambie Sam nipo huku nasoma ila najipanga pia ili nije kuishi na wewe"
Sabrina akamshangaa Jeff na kujiuliza,
"Hivi huyu mtoto ana kichaa au? Ila mimi mwenyewe je nina kichaa au? Mbona na mimi sijielewi? Kuna wakati nampenda Sam, wakati mwingine najiona kama nampenda Jeff lazima nina matatizo kama sio kurogwa"
Sabrina alijifikiria sana ila hakutaka kuendelea kusoma jumbe za Jeff na kuamua kufunga simu yake.
Sam alimngoja yule dada mpaka pale aliporejea na kukaa kwaajili ya kumueleza.
"Eeh niambie vile unavyomfahamu mke wangu"
"Sabrina ni rafiki yangu, nimesoma nae. Ingawa urafiki wetu uliishia kwenye salamu tu kwani Sabrina alikuwa na kitu ambacho kilimfanya atufiche na kuogopa kuwa na marafiki kabisa. Ila namfahamu pia kwa namna nyingine"
"Namna gani hiyo, napenda nijue"
"Ila kitu kingine ni kuwa, mi sijakufahamu wewe kupitia huyo mkeo ila kuna mdada mwingine aliyefanya nikufahamu"
"Nani huyo?"
Sam alikuwa makini sana katika kumsikiliza kwani alihitaji kujua sana kitu ambacho huyu dada anakifahamu.
"Nimekufahamu kupitia dada mmoja anaitwa Neema, ila alikataa kunipa namba yako ndiomana nikakuomba wewe mwenyewe moja kwa moja, nina mengi sana ninayoyafahamu "
"Niambie basi hayo mengi unayoyafahamu, mbona unaishia njiani kwenye maelezo?"
"Kwavile tumefahamiana Sam, jua kwamba nitakwambia mambo mengi sana"
"Basi ndio uniambie"
"Usijali Sam nitakwambia tu"
Sam akaanza kukerwa na huyu mdada sasa kwani hakuna alichomweleza zaidi ya kusema kuwa anafahamu mambo mengi sana.
Sam alimuangalia kwa hasira sasa na kwavile huyu dada alivyozidi kuzungusha habari, ikabidi ainuke na kumuaga.
"Kwaheri, mi nahitaji kurudi nyumbani kwangu"
"Jamani, ila bado nina mengi ya kuzungumza na wewe"
"Tutazungumza siku nyingine"https://ift.tt/2TR5Sxj
Sam akainuka na kuanza kuondoka, yule mdada akatambua wazi kuwa Sam amenuna.
Akainuka na kwenda kumfata kwa nyuma, kisha akamshika bega na kumwambia,
"Nisamehe kama nimekukosea"
Sam akasimama, akageuka nyuma kisha akamkumbatia yule dada.
Muda kidogo akamuachia na kwenda kupanda gari yake akirudi nyumbani kwake sasa.
Yule dada alishangaa na kujiuliza kuwa kwanini Sam alimkumbatia.
Akaangalia pembeni yake, akamuona mtu na kamera kanakwamba alikuwa akiwapiga picha, alipotaka kumfata yule mtu akaondoka na kumfanya yule dada aishiwe na la kusema, huku akijiuliza kuwa kwanini yule mtu ampige picha na kwanini alipoona kuwa anataka kumfata akaondoka.
Akakosa jibu na kujiona kuwa inawezekana wakawa na misheni moja kwa Sam kisha naye akaondoka zake.
Sabrina alitulia ndani akingoja kurudi kwa Sam, na kikubwa aliwaza hatma yake, hatma ya ndoa yake kwa Sam.
Muda mwingi alijutia kitendo chake cha kumuamini Jeff na kuwa naye karibu kwani aliona kuwa ndio kitu pekee kilichomfanya awe vile, kitu pekee kilichompa Jeff nafasi ya kumbaka na hata kumpatia ile mimba.
Alibaki kujisemea tu,
"Najuta mie jamani"
Sam nae ndio alikuwa anaingia ndani kwa muda huo na kumuuliza Sabrina,
"Unajuta nini?"
Sabrina akamtazama Sam bila ya kujibu chochote, kisha Sam akamuuliza tena,
"Kati yangu mimi na wewe, ni nani anayestahili kujuta?"
Sabrina akatulia kimya na kuinamisha macho yake chini, Sam akaenda na kukaa pembeni yake kisha akamuuliza,
"Umewasiliana na Jeff?"
Sabrina akashtuka kwani ni swali ambalo hakujipanga kuulizwa, akajikuta akizidi kukaa kimya na kujipeleleza kama akubali au akatae.
"Mbona kimya Sabrina! Umewasiliana nae?"
Akatikisa kichwa akiashiria kwamba hajawasiliana nae.
"Basi mie nimewasiliana nae jana, kasema nikusalimie sana"
"Sawa nashukuru"
"Hujamkumbuka kwani? Maana ni siku nyingi zimepita tangu aondoke. Eti Sabrina hujamkumbuka Jeff?"
Sabrina akaona maswali ya Sam kukaa kimitego zaidi, akahisi kuwa kuna kitu anahitaji.
Kwa bahati mtoto alianza kulia chumbani na kumfanya Sabrina ainuke na kwenda kumchukua.
Ilikuwa usiku umeingia tayari, na Sabrina hakutaka tena kurudi sebleni kwani aliyaogopa maswali ya Sam.
Ila Sam naye alienda chumbani kwa lengo la kulala muda kidogo simu ya Sam ikaita.
Mpigaji alikuwa ni yule yule dada wa mchana.
Sam akaipokea ile simu,
"Samahani, naomba namba ya mkeo"
"Una shida nae ipi?"
"Kuna jambo nataka nimwambie"
"Niambie mimi nitamjulisha"
Yule dada akakata simu na kumfanya Sam ashangae kwani hakuelewa hata ni kwanini anamfatilia.
Sabrina akamuangalia Sam na kutamani kumuuliza kuwa alikuwa akiongea na nani ila alishindwa kwani tayari ujasiri ulishaondoka katika moyo wake.
Kwahiyo ikabidi awe kimya tu akisikilizia kama Sam atamwambia chochote, ila Sam hakumwambia kitu zaidi ya kulala tu.
Kulipokucha asubuhi na mapema, kama kawaida Sam aliamka na kujiandaa na kwenda kwenye kazi yake.
Sabrina aliinuka na mawazo yake kichwani, wazo la gafla likamjia nalo ni kutoa mimba.
"Ni kheri nikaitoe hii mimba, mfano Sam akigundua badae kuwa sina mimba tena basi nimwambie kuwa daktari alikosea kwa majibu aliyonipa mwanzo"
Wazo hilo la kutoa mimba likajengeka kwenye akili yake vilivyo sasa.
Akawaza tu pa kwenda kumuacha mwanae kabla hajatimiza lengo lake.
Akaona sehemu pekee ni nyumbani kwao.
Sabrina alifunga safari hadi nyumbani kwao, na alipofika alimkuta wifi yake Joy na kaka yake James.
Akawasalimia na kuwaaga kuwa anarudi muda sio mrefu kisha mtoto akamuacha kwa mama yake na yeye kuondoka, hata mama yake akamshangaa kwa zile harakati zake.
Njiani Sabrina akakutana na Sakina,
"Mbona una haraka hivyo unaelekea wapi?"
"Kuna mahari naenda mara moja, na wewe waenda wapi?"
"Kuna msiba hapo kwa jirani ndio naenda"
"Msiba? Wa nani tena?"
"Kuna binti yake amekufa maskini, nasikia alikuwa anatoa mimba. Sasa sijui wamemtoa vibaya amekufa"
Sakina alikuwa akisikitika tu huku akimueleza Sabrina habari hiyo, muda huo Sabrina nae mapigo ya moyo yakamuenda kwa kasi sana na kuwa kama mtu aliyepigwa na shoti ya umeme kwani Sakina alimuaga pale ila yeye aliendelea kuganda pale pale kwa dakika kadhaa kabla hajajipa maamuzi ya mwisho, akajiuliza
"Niende au nisiende!"
Upande mwingine akajishauri kuwa aende tu kwavile tayari ameshapanga na kuamua kisha akaendelea na safari yake.
Alipofika hospitali, alitulia na kumngoja daktari ambaye anajua wazi ndiye atakayeweza kumsaidia.
Daktari alipofika, moja kwa moja akaenda kwenye chumba chake na kumueleza hali halisi,
"Kwani mimba yako ina miezi mingapi?"
"Mwezi mmoja tu"
"Kam ni mwezi unatakiwa uandae laki moja ya kutolea"
"Pesa sio tatizo daktari, cha msingi ni hii mimba itoke tu basi"
"Basi hakuna tatizo, naomba kanisubiri pale kwenye viti vya wagonjwa. Nipe nusu saa tu nitakuita nikuhudumie"
Sabrina akakubali na kutoka kwenye kile chumba cha daktari na kwenda kumsubiri kwenye viti alipoelekezwa.
Joy na James wakiwa pale nyumbani kwa wakina Sabrina na mama yao, muda kidogo akawasili shangazi wa Sabrina ambapo wote wakafurahia ujio wake kasoro mama wa Sabrina kwani alikuwa kila akimuona anahisi kama kuna kitu atamuharibia.
Lakini alimkaribisha tu kwavile ni ndugu yao hakuwa na uwezo wa kumwambia ondoka.
Na moja kwa moja shangazi wa Sabrina alienda kukaa karibu na mama wa Sabrina ambapo alimkabidhi yule mtoto wa Sabrina amshike,
"Yani haka katoto ni baba yake mtupu ila katabadilika kwavile ni kakike"
James naye akadakia na kumuuliza shangazi yao,
"Na wangu je shangazi?"
Shangazi akamkabidhi mtoto wa Sabrina na kumchukua mtoto wa James kisha akasema,
"Huyu sina mashaka nae, damu moja hii"
Mama wa Sabrina aliamua kuingizia habari zingine kwani alihisi kitakachoendelea pale ni kumuumbua yeye tu.
Muda kidogo akawasili Sam pale nyumbani kwakina Sabrina na kuwasalimia.
"Sabrina yuko wapi mama?"
"Sijui, kamuacha mtoto hapa ila kaniambia kuwa atarudi muda sio mrefu"
"Aaah sawa"
Kengele ya hatari ikagonga kwenye kichwa cha Sam na kujikuta akifikiria kitu tofauti toka kwa Sabrina.
Akachukua simu yake na kumtumia Sabrina ujumbe mfupi wa maneno, akatulia dakika kadhaa kungoja majibu ila hakujibiwa.
Akaamua kumpigia simu ila Sabrina hakupokea na mwisho wa siku simu ya Sabrina haikupatikana tena.
Sam akaona ni vyema awaage pale na kuondoka kwani asingeweza kuvumilia hali ya kwamba anahisi kuwa kuna kitu kibaya kikitokea kwa Sabrina.
Kisha akainuka na kuwaaga pale,
"Nitarudi badae mama"
Sam akaondoka na kuwafanya huku nyuma wamjadili, ambapo mada ya ujadili akaianzisha Joy yani yule wifi wa Sabrina.
"Shangazi umesema mtoto wa Sabrina kafanana na baba yake, mbona hata hafanani nae?"
"Nikuulize kitu?"
"Niulize shangazi"
"Wewe unauhakika gani kama baba yako ndio baba yako mzazi?"
Joy akamshangaa kwa lile swali ambapo James akajibu,
"Mi nina uhakika kwa baba yangu, kwanza ananipenda, kanisomesha, ananijali."
"Kwani hivyo vitu ndio vinakuhakikishia kuwa ni mzazi wako?"
"Ndio"
Shangazi akacheka na kusema,
"Siri ya mtoto aijuwae mama"
James akasema tena,
"Na mama ndiye aliyenijulisha"
Shangazi akamuangalia mama wa Sabrina na kumuulize,
"Kheee hujamwambia mtoto ukweli hadi leo?"
Mama wa Sabrina hakujibu, ila akajishika tumbo na kulalamika kuwa anapatwa na maumivu makali sana.
Sabrina akiwa ametulia pale kwenye viti vya wagonjwa, akaona ujumbe umetoka kwa Sam.
Akaufungua na kuusoma,
"Tafadhari mke wangu Sabrina usiende kuitoa hiyo mimba"
Sabrina akashtuka na kujiuliza kuwa Sam kaambiwa na nani kuwa yeye anataka kwenda kutoa mimba.
Wakati akifikiria, akaona simu ya Sam ikiita.
Akaogopa kupokea kwani alijua wazi atamuuliza alipo halafu itakuwa msala zaidi, kwahiyo akaamua kuizima ile simu kabisa.
Muda kidogo, daktari akamuita Sabrina kwenye chumba na kuweka vifaa vyake tayari kwa kazi.
Sabrina akasimama huku akisikilizia maelekezo toka kwa daktari.
"Haya panda kitandani"
Sabrina alipanda kitandani huku mapigo yake ya moyo yakienda kwa kasi sana.
Kabla dokta hajafanya chochote kwani ndio kwanza alikuwa anavaa karatasi za mikononi akasikia mtu akigonga kwa nguvu mlango wa kile chumba.
Naye dokta akashtuka kwani kile chumba alichompeleka Sabrina huwa ni maalumu kwa kazi hiyo na hakutegemea mtu kuja kumgongea vile kwa usumbufu.
Akaenda kufungua, na moja kwa moja akaingia Sam.
Sabrina alipanda kitandani huku mapigo yake ya
moyo yakienda kwa kasi sana.
Kabla dokta hajafanya chochote kwani ndio kwanza
alikuwa anavaa karatasi za mikononi akasikia mtu
akigonga kwa nguvu mlango wa kile chumba.
Naye dokta akashtuka kwani kile chumba
alichompeleka Sabrina huwa ni maalumu kwa kazi
hiyo na hakutegemea mtu kuja kumgongea vile kwa
usumbufu.
Akaenda kufungua, na moja kwa moja akaingia Sam.
Alienda moja kwa moja kwenye kitanda alicholala Sabrina ambapo Sabrina naye akashtuka kwa kumuona Sam kwani hakumtegemea.
Sam akamuangalia Sabrina kisha akamwambia neno moja tu,
"Endelea"
Halafu Sam akatoka na kuondoka.
Sabrina na dokta wakatazamana kwa uoga, kisha dokta akamuuliza Sabrina,
"Ni nani yako huyo jamaa?"
"Ni mume wangu"
"Anajua kama umekuja kutoa mimba?"
"Hajui"
"Sasa nani kamwambia?"
"Hata mimi mwenyewe sijui"
"Mmh! Hii ni kesi dada, naomba uondoke hapa sasa hivi kabla hayajazuka mengine"
Sabrina aliinuka na kutoka kisha akaondoka pale hospitali.
Wakati anatembea ili akachukue daladala aweze kurudi kwao, akashangaa kuna gari imesimama mbele yake na mlango wa gari kufunguliwa.
Ni Sam alikuwepo ndani, akamuuliza Sabrina,
"Umemaliza?"
Sabrina akatulia kimya tu kwa aibu na kuinamisha macho chini.
"Haya panda kwenye gari twende"
Sabrina alijikuta akisita kupanda kwani hakujua ni kitu gani Sam anamuwazia kwa wakati huo.
Sam naye akamkazania kuwa apande ili amrudishe nyumbani.
Sabrina aliamua kupanda huku moyo wake ukiwa umejawa na mashaka ya kutosha kabisa.
Walienda hadi nyumbani kwa Sabrina kisha kabla ya kushuka Sam akamwambia Sabrina,
"Tunaenda kumchukua mtoto kisha tunarudi nyumbani sawa?"
Sabrina akaitikia kwa kutingisha kichwa.
Wakaingia ndani sasa, na moja kwa moja Sabrina akaenda kumsalimia shangazi yake ambaye ni majina wake.
Wakati Sabrina anamsalimia shangazi yake, huyo shangazi akamnong'oneza sikioni
"Mtoto una majanga wewe hadi unatia aibu"
Sabrina akainuka bila kujibu chochote bali alienda chumbani na kumchukua mtoto wake kisha kuwaaga, ambapo mama yake naye akamuuliza,
"Mbona mapema hivyo?"
Sam alidakia na kujibu,
"Kuna daktari alisema tumpeleke mtoto leo ila Sabrina alisahau ndiomana nikamfata"
Mama yao akawaitikia ila shangazi mtu alitikisa kichwa na kutaka kuongea jambo, ila kabla hajaongea Sabrina alishamvuta mkono Sam ili waondoke kwani alishayaelewa maneno ya shangazi yake siku hizi na akajua wazi atakachozungumza kama sio cha kumuharibia yeye basi kitakuwa chochote kibaya.
Kwahiyo Sam na Sabrina wakatoka nje na kuondoka.
Safari ikawa nyumbani moja kwa moja.
Walipofika walishuka na kuingia ndani, Sam alimuangalia Sabrina na kumuona yupo sawa na wasichana wengine ambao yeye aliwaona kuwa hawana akili ingawa mwanzoni alimuona kama mwanamke wa tofauti kabisa.
Akamwambia,
"Kamlaze mtoto Sabrina"
"Huyu ataamka muda sio mrefu sababu amelala sana"
"Una uhakika gani kama amelala sana? Umekaa nae muda wote leo?"
Sabrina akakaa kimya na kwenda kumlaza mtoto huku akijihoji kama arudi sebleni au la, lakini Sam alimuita na kumfanya arudi sebleni.
"Sabrina naomba leo nikuulize tena hili swali, hivi una akili kweli wewe?"
Sabrina akamuangalia Sam na kutikisa kichwa kama ishara ya kuitikia alichoulizwa.
"Umeona sasa, nakuuliza kwa mdomo unanijibu kwa kichwa. Hivi nikisema huna akili nitakuwa nakosea?"
Sabrina hakuweza kujibu na kukaa kimya, akampa Sam nafasi ya kuongea,
"Hivi nikupe nini wewe mwanamke utambue upendo wangu kwako? Nikupe uhai wangu au nikupe kitu gani Sabrina? Kwanini umekuwa ni mtu wa kutesa moyo wangu kiasi hiki?"
Sabrina aliinamisha kichwa chini kwa aibu,
"Niambie Sabrina, nikupe nini uridhike? Haya sasa mimba ya kwanza ulibakwa na hujui ya nani, ya sasa hivi je?"
Sabrina akatokwa na machozi kwani aibu na uoga vilimshika na kumfanya ashindwe kujibu chochote.
Muda kidogo mtoto alianza kulia ndani na kumfanya Sabrina aende kumchukua na kuanza kumnyonyesha.
Inaendeleaaaa
No comments: