Simulizi: Je haya Ni mapenzi? Sehemu ya 52


Wakarudi nyumbani sasa huku Sakina akiwaandalia vizuri mazingira ya chumba ili aweze kukaa humo na mtoto huku akili yake ikijiuliza maswali mengi sana juu ya muonekano wa huyu mtoto kwani hawakufanana nae hata kidogo.
Kuna muda mashaka yalimjaa sana hadi mama wa Sabrina akatambua hilo kwa Sakina na kumuita pembeni,
"Mwanangu, usiwe na mashaka kiasi hicho. Utashindwa kumuhudumia mtoto ipasavyo, ni kweli hamfanani nae lakini huwezi jua. Huenda bado ni damu yenu"
Sakina akaitikia kishingo upande kisha akaendelea kumuhudumia mkwe wake.

Kesho yake baada ya maziko ya Rose, Fredy alipita tena nyumbani kwakina Sabrina na kumkuta Sabrina na mama yake.
Alikaa pale na kuanza kuwasimulia khabari za ule msiba,
"Ule msiba ilikuwa khatari jamani, mvua imetunyeshea makaburini hadi tumekoma. Na yote, nilimuona mumeo Sam. Jamaa ana moyo sana yule, Mungu ambariki"
"Alifanyaje kwani?"
Akaulizwa swali na mama Sabrina ingawa alipenda hilo swali aulizwe na Sabrina mwenyewe,
"Alijitolea kumchukua Neema akiwa amelowa chapachapa, ila alivyoondoka nae tu na mvua ikakatika. Kwakweli ilikuwa khatari jamani, aliyemroga yule dada marehemu na alaaniwe miaka yote"
"Kheee kumbe karogwa?"
"Ndio karogwa, kuna tetesi nimesikia pale msibani eti sijui alitembea na mume wa mtu, sasa mwenye mume ndio kamroga ndiomana amekufa gafla."
Sabrina na mama yake wakasikitika sana juu ya hilo.
Kisha Fredy akaingizia khabari zingine za kwanini Sabrina haishi na mumewe ilihali mumewe yupo.
"Yani mama, ningekuwa mimi ndio nimepata hiyo bahati ya kumuoa huyu binti yako, hata kama angekuwa na tatizo gani bado ningeendelea kuwa nae karibu tu yani mtu kupoteza kumbukumbu tu ndio kuishi nae mbali mbali?"
"Aliyekwambia kuwa wanaishi mbali mbali ni nani?"
"Kuna yule ndugu yangu Francis aliniambia kuwa Sabrina anaumwa, hana kumbukumbu tena. Kuna siku nikakutana na Sam na kumuuliza kuhusu Sabrina naye akaniambia kuwa anaumwa na yupo kwao. Ndiomana jana nikapita kwanza hapa"
"Kwahiyo ulipita kuhakikisha tu?"
"Ndio, kuhakikisha na kumuonyesha Sabrina kuwa mimi ni mwanaume pekee ambaye ningekuwa bora kwake"
Mama Sabrina akatabasamu na kumuuliza,
"Kwa kazi gani unayofanya?"
"Naendesha bodaboda"
"Sasa maisha ya bodaboda kweli ungeweza kumuhudumia mwanangu wewe?"
"Jamani mama usinidharau, mapenzi ya kweli si pesa bali ni upendo uliopo baina ya watu"
"Aah nakutania tu"
Fredy aliamua kuaga na kuondoka zake ila kule kuambiwa kuwa na bodaboda angemlisha nini Sabrina kulimuumiza sana ingawa mama Sabrina alibaki akicheka tu.
Sabrina naye alimtazama mama yake na kumuuliza,
"Mbona umefurahi sana juu ya huyu mtu?"
"Alikupenda sana huyu kijana hadi nilikuwa namsikitikia"
"Na yule wa siku ile je?"
"Naye alikupenda sana mwanangu, yani hawa vijana wamekupenda balaa"
"Na mume wangu je?"
"Naye alikuwa anakupenda sana, yani huyo ndio sijui kapatwa na shetani gani? Mtu kakuoa vizuri ila leo sijui kavamiwa na nini?"
"Kwahiyo sasa hivi hakuna anayenipenda tena?"
"Lazima watakuwepo tu mwanangu, naomba tuachane na khabari hizo"
Mama wa Sabrina akaenda kushughulika na mambo mengine huku akimuacha bintiye akijiuliza maswali mwenyewe na kujijibu mwenyewe.

Ilipita wiki sasa na kumfanya Sakina akimshangaa mjukuu wake kuzidi kufanana na watoto wa kichina.
Ikabidi siku hiyo amuulize vizuri mkwe wake Dorry.
"Dorry mwanangu, mbona huyu mjukuu wangu anafanana na wachina?"
"Kumbe na wewe mama umeshangaa eeh! Basi hata mie nilishangaa hivyo hivyo, juzi nikampigia simu mamdogo na kuongea nae kumbe babu yetu alikuwa hivi hivi"
Sakina akashangaa sana na kuuliza,
"Na huyo babu yuko wapi saivi?"
"Alishakufa, ila mama kaniambia kuwa atabadilika tu huyu mtoto badae eti hadi achangamke"
Sakina akajikuta akichukia sana moyoni ukizingatia anaona kabisa akidanganywa.
Akajisemea moyoni mwake kumpa mwezi huyu Dorry ili arudi kwao kisha atakuja kukubaliana na mwanae akirudi kwani aliona akidanganywa kabisa.

Kipindi hiki ni huyu Aisha pekee aliyekaa na Neema nyumbani kwake kwani hakupenda kumuona na ule upweke alionao kwa kipindi kile kwani muda mwingi Neema alionekana kunyong'onyea kupita maelezo ya kawaida.
Siku hiyo akafika tena Sam kumsalimia Neema na kumkuta pale akiwa amelala sebleni huku Aisha akiwa pembeni kama kumliwaza.
Sam aliwasalimia pale ila Neema hakutaka kuitikia kabisa ila alimwambia neno moja tu,
"Sam, nakuomba uende"
Sam bado alisimama pale pale akimuangalia Neema kwani alikuwa akimpenda sana, ila Neema alikuwa akitokwa na machozi tu ambayo yaliumiza sana moyo wa Sam kwani alijisikia vibaya kila alipotazama chozi la Neema.
Sam akajikuta akiinama pale Neema alipo na kumbusu kwenye paji la uso,
"Sam nakuomba uende"
Neema akawa analia kwa staili ya uchungu sana na kumfanya Aisha aingilie kati kwa kumsihi Sam aondoke hadi akatoka nae nje kabisa ambapo Sam alionekana kuwa na uchungu sana.
Sam akamwambia Aisha,
"Naelewa maumivu ya Neema, najua jinsi gani anateseka"
Kisha akatoa pesa na kumkabidhi Aisha endapo kutakuwa na hitaji lolote kwa Neema.
Aisha aliporudi ndani akamkabidhi zile pesa Neema ambapo zilimtia uchungu zaidi na kumfanya akumbuke mambo yale ya nyuma.

Sakina akiwa nyumbani kwake, akapigiwa simu na mwanae Jeff, kisha wakasalimiana nae ila leo alimueleza akiwa amepooza sana,
"Mkeo kajifungua huku Jeff"
"Mke? Mama sina mke huko mbona huwa hunielewi"
"Kwahiyo huyu Dorry ni nani yako?"
"Mama, nikujibu mara ngapi kama sina utambuzi na huyo Dorry? Mi sio mtu wangu huyo mama, kwani ni mambo gani anakudanganya huyo?"
"Subiri uje ujionee mwenyewe nisije nikasema mengi na kuonekana mbaya bure"
"Mama, huyo Dorry asikudanganye lolote. Hata hivyo narudi, na ole nimkute huyo Dorry hapo nyumbani"
"Ni siku gani unarudi?"
"Sitaweza kusema ni siku gani ila wewe ujue kuwa narudi mama"
Sakina alipomaliza kuongea na mwanae akamuangalia Dorry aliyekuwa ametulia akimnyonyesha mwanae na kumfanya Sakina ajiulize kuwa kwanini Dorry anaonekana kuwa jasiri na kujiamini bila wasiwasi, akahisi kuwa huenda ikawa kweli yule ni mtoto wa Jeff ingawa alikuwa na mashaka sana juu ya swala hilo.

Sakina aliondoka pale kwake na kwenda kwakina Sabrina kwa lengo la kumsalimia Sabrina ila lengo lake kubwa ilikuwa ni kutoa dukuduku lake.
Alifika na kumkuta Sabrina akiwa na mama yake pale nyumbani.
Baada ya maongezi mawili matatu alianza kuwaeleza anavyomuona mjukuu wake,
"Jamani mi nina mashaka kabisa kuwa yule sio mtoto wa mwanangu"
Mama Sabrina akacheka na kuuliza,
"Kwanini uwe na mashaka na mjukuu wako jamani?"
"Kwakweli simuelewi, mjukuu ni mchina kabisa yani macho na kila kitu itakuwaje awe mjukuu wangu?"
"Siri ya mtoto anayo mama, ukiona mwanao kakubali basi na wewe ukubali tu mwanangu"
"Haiwezekani mama, yani nishapanga hapa Jeff akirudi tu lazima wakapime damu ingawa huyo Jeff anakataa kabisa kuhusu kuwa na mahusiano na Dorry ila mimi tu ndio nilikuwa nang'ang'aniza toka mwanzo kuwa Dorry ndio mkwe wangu ukizingatia sijawahi kumfahamu mkwe wangu kwa Jeff."
Sabrina akaanza kucheka na kufanya wamshangae, kisha Sakina akamuuliza,
"Au wewe kuna mkwe wetu mwingine unayemfahamu?"
"Huyo mwanao mwenyewe simfahamu. Sasa huyo mkweo mwingine nitamfahamia wapi?"
"Lakini nakumbuka kama uliwahi kuniambiaga kuwa Jeff alizaa na mtoto wa mwanajeshi, nilikufatilia unionyeshe mjukuu wangu huyo lakini sikufanikiwa sababu ulikuwa ukinipa vitisho tu vya mwanajeshi ila sasa nasubiri upone ili ukanionyeshe yote ya zamani"
Sabrina bado alicheka kwani hakuwa na kumbukumbu wala utambuzi wa chochote kilichokuwa kikizungumziwa pale.

Sam alikuwa akijutia sana kwani kwa hali aliyokuwa nayo Neema aliona wazi kuwa kwa vyovyote vile atakufa tu.
Ingawa Neema ndio alikuwa mwanamke msiri sana kupita wote aliokutana nao hata akashangaa kuwa ule ujasiri na usiri Neema anauwezaje, alitamani ampate mtu wa kuweza kumfanya Neema arudi katika hali yake ya kawaida ila je atampatia wapi mtu huyo kwa ugonjwa wa ajabu kama ule?
Sam aliumiza sana kichwa chake bila matumaini yoyote yale.

Siku hiyo Aisha alitoka pale kwa Neema na kwenda kumtafutia matunda, kwa bahati akakutana na rafiki yake ambaye hawakuonana nae kwa muda mrefu sana.
Alifurahi sana kukutana na rafiki yake huyo,
"Jamani Sia, hata siamini kama nimekuona leo"
Wakaongea mengi sana na kubadilishana namba za simu.
Wakati wanaongea, kuna gari ikasimama mbele yao na aliyeshuka alikuwa ni Sam ambapo alisimama ili aweze kumsalimia Aisha.
Wakasalimiana pale na kisha Aisha kumtambulisha Sam kwa yule rafiki yake Sia.
"Yani huyu ni rafiki yangu sana ila tulipotezana kidogo tu"
Sam akaona ni vyema kama akiwapandisha kwenye gari yake na kuwarudisha, wakati huo Sia nae akajitetea
"Ila mie kwetu ni mbali"
"Hakuna shida nitakupele ka, tutaenda kwanza anapokaa huyu Aisha kwasasa halafu na wewe nitakupeleka"
Wakafurahi pale kwani atakuwa amewapunguzia mambo ya nauli.

Sam aliondoka nao pale na kwenda moja kwa moja kwa Neema ili Aisha amuonyeshe rafiki yake alipo kwasasa.
"Basi haina shida, nitakuja kesho maana leo kama nilivyokwambia inabidi nimuwahi mtu nyumbani"
Sam naye hakutaka kushuka kwavile alishafika kabla na Neema kumfukuza.
Ila alitoa pesa na kumkabidhi Aisha kisha akamwambia,
"Tafadhari utampatia Neema maana hataki nikimpa mimi kabisa"
Kisha wakaagana pale na kuanza safari ya kumpeleka Sia na kujikuta wakiongea mambo mengi sana hadi pale Sia alipofika anapoelekea.
"Nashukuru sana kwa ukarimu wako kaka"
"Usijali kitu"
"Mmh sawa, basi huu ndio mwanzo mzuri wa kufahamiana. Unaweza kunipatia namba zako?"
"Hakuna tatizo"
Kisha Sam akamtajia Sia namba zake pale na kuagana nae kisha yeye kwenda kuendelea na shughuli zake zingine kwa wakati huo.

Sia alijiona wazi kuvutiwa na ule ukarimu wa Sam, ila kikubwa zaidi ni kule kumuona kuwa ni mwanaume mwenye uwezo na pesa zake na kumfanya afikirie swala la kuwa naye karibu ili aweze kumfahamu kwa undani zaidi kwani mawazo yake yalishagota juu ya huyu Sam.

Sakina alikuwa akisubiri kwa hamu ujio wa mwanae kwani muonekano huu wa mjukuu wake haukumuingia akilini kabisa, na kule kujiamini kwa Dorry kulimfanya ashindwe kumuelewa kabisa.
Dorry hakuwa na uoga wowote kwa kipindi hiki, hakuhofia kuwa Jeff anarudi wala nini, hakuwa na mashaka juu ya mtoto ingawa alijua wazi kuwa mama mkwe wake kashagundua mchezo kamili ila yeye hakutaka kujitia wasiwasi wowote na alijiamini kupita maelezo.
Sakina alikuwa akijiongelea tu,
"Yani hata kama watu husema kuwa kitanda hakizai haramu, ila safari hii kimezaa jamani mmh huyu si damu yetu ila navumilia tu"
Dorry alisikia ila akajifanya kamavile hajasikia chochote kwani aliendelea na mambo mengine kama kawaida, kitendo hicho kilimfanya Sakina aombe usiku na mchana kuwa mwanae arudi.

Sabrina akiwa amejichokea na ile mimba yake, alikuwa amekaa kwenye mkeka huku akitafakari mambo yake na kuona kama anaweza kurudisha kumbukumbu zake.
Akamuona mtu akija huku akitabasamu sana, huyu mtu alionyesha kumfahamu vizuri Sabrina ingawa yeye alikuwa akimshangaa tu.
"Unanishangaa jamani, mimi ni Jeff"
Kisha akamkumbatia Sabrina ila Sabrina bado alimshangaa na kufanya Jeff ajaribu kujieleza kwani alikuja kwa kushtukiza tena bila taarifa kamili.
Ila kabla Jeff hajajieleza, akashangaa kumuona Sabrina akianguka na kuanza kutapatapa.


Kisha akamkumbatia Sabrina ila Sabrina bado
alimshangaa na kufanya Jeff ajaribu kujieleza kwani
alikuja kwa kushtukiza tena bila taarifa kamili.
Ila kabla Jeff hajajieleza, akashangaa kumuona
Sabrina akianguka na kuanza kutapatapa.
Ikabidi Jeff aite msaada ambapo mama Sabrina alitoka ndani kisha kuanza kusaidiana na Jeff cha kufanya.
Kwavile gari ya kukodi aliyopanda Jeff ilikuwa bado haijaondoka ikabidi waitumie gari hiyo kumuwaisha Sabrina hospitali.

Walifika hospitali na moja kwa moja Sabrina akapelekwa kwa daktari kwahiyo Jeff na mama Sabrina walitulia wakingoja majibu.
"Na wewe Jeff, kwanini unakuja kwa kushtukiza kiasi hiki? Kwanini hukusema kama unarudi?"
"Nilisema kama narudi ila tu sikusema kama narudi leo"
Ikabidi pale wampigie simu na Sakina na kumtaarifu kuwa wako hospitali.

Sakina alikuwa nyumbani kwake na kushangaa tu hadi kuongea peke yake,
"Yani huyu Jeff, hata kusema kuwa anarudi hakuna. Na huyu Sabrina kapatwa na nini jamani?"
Ikabidi ajiandae na kumuaga Dorry kisha kuelekea kwenye hospitali aliyoelekezwa na mtoto wake.

Dorry pale nyumbani baada ya Sakina kuondoka akaona wazi kuwa hali itakuwa mbaya sana pale ambapo Jeff atakuwa amerudi na mama yake, alichokifanya na yeye ni kuingia chumbani kwa Sakina na kuchukua kiasi fulani cha pesa kisha kupanga mizigo yake na kumuita dereva wa gari za kukodi kisha kuondoka mahali pale.

Sakina alifika hospitali na mtu wa kwanza kumuona alikuwa ni mwanae na kumkumbatia kwa shauku yote kisha kumuuliza kilichotokea.
Jeff akamueleza mama yake kama ilivyokuwa,
"Ila wewe Jeff una matatizo sana mwanangu loh! Yani wewe badala ufike kwenu kwanza ukaona ni vyema upite kwa bibi yako. Unaona sasa majanga uliyosababisha?"
"Mama, hii ni bahati mbaya tu na wala sikuwa na nia mbaya. Sabrina atapona, nilimkumbuka sana na ndiomana nikaanzia pale"
"Ulimkumbuka sana!! Yani ulimkumbuka kushinda mie mama yako? Wewe mtoto akili yako wewe loh!"
Akafika na mama Sabrina ikabidi waanze kuongelea hali ya Sabrina huku wakingoja majibu ya daktari kumuhusu Sabrina.

muda kidogo daktari akatoka na kitanda cha kubebea wagonjwa akiwa amebebwa Sabrina na kufanya wote waanze kufatilia kwa nyumba ambapo Sabrina alipelekwa moja kwa moja kwenye chumba kingine na wao kuzuiwa nje ya chumba hicho.
Kisha daktari akawafata pale nje na kuwauliza,
"Mume wa huyu dada yuko wapi?"
Pale nje wakatazamana kwa zamu na kumfanya mama Sabrina aulize,
"Kwani anaumwa nini jamani na mume wake wa nini?"
"Kwani yuko wapi? Kama mnaweza mpigieni simu aje."
Kisha daktari akaingia tena kwenye kile chumba na kuwafanya pale nje watazamane tu,
"Tutampata wapi Sam?"
Na muda huo akawasili baba wa Sabrina na kuwakuta wakijadiliana kuhusu kumpata Sam,
"Tumpigieni simu jamani, hakuna namna nyingine hapa"
"Mumpie simu nani?"
"Tunataka tumpigie simu Sam maana daktari amesema tumuite mume wa Sabrina"
"Sitaki kusikia huo upuuzi kabisa, mwacheni huyo Sam aendelee na miujinga yake. Msimuite hapa"
Baba wa Sabrina hakutaka kuelewa wala kutambua kuhusu huyo Sam kwani alienda kukaa tu kwenye moja wapo ya mabenchi pale hospitali na kuwaacha Sakina na mama Sabrina wakijadili ambapo nao waliamua kutoka nje ili wajue cha kufanya.

Jeff aliyekuwa kaganda pale pale, aliamua kujitoa muhanga na kumfata daktari kisha akamwambia kuwa yeye ndiye mume.
"Na mbona wakati naulizia hukujitaja? Haya twende"
Daktari akatoka kwenye chumba chake na kumpeleka kwenye chumba alichopelekwa Sabrina.
"Huyu mkeo kashikwa na kifafa cha uzazi ila kuna mengi yameingilia kati, mi ni daktari ila huwa naona mambo mengi sana. Nimemleta huku ili tumfanyie operesheni ili tuokoe maisha yake ila kuna kengele ha hatari imegonga kichwani mwangu kuwa kuna uwezekano wa kumpoteza mama na mtoto kwa muda mmoja. Sasa ninachokuomba ni wewe kuweka mkono wako wa kuume chini ya tumbo lake na uombe kuwa ajifungue vyema"
Jeff alishangaa haya mambo kuyakuta hospitali ila alifanya kile alichoelekezwa na daktari huyo.
Baada ya muda mfupi tu akamuona Sabrina akitulia kule kutapatapa kwani pale hospitali alifungwa mikono na miguu ili asiweze kuanguka na kuumiza kiumbe kilichopo tumboni.
Kisha daktari akamwambia tena Jeff akamshike Sabrina kwenye paji la uso ambapo Jeff akafanya kama alivyoelekezwa.
Muda kidogo Sabrina alirejewa na ufahamu na kuweza kujifungua kawaida kabisa.

Sakina na mama Sabrina walikuwa nje na kukubaliana kumpigia simu Sam ambapo walipiga sana ila simu yao haikupokelewa wala nini na kufanya wajadiliane kitu kingine cha kufanya ukizingatia baba wa Sabrina hakuwa na msaada nao kabisa.
Wakati wako pale nje, kuna manesi wawili wakapita wakizungumza,
"Yani huyu daktari ana mambo ya kishirikina sijapata kuona jamani loh!"
"Huyu ndio alivyo, mi nahisi kachanjiwa huyu"
"Ona sasa, yule mgonjwa mule tumemfunga tu eti hadi mume wake aje loh huyu daktari jamani mmh!"
"Na hapo asipokuja huyo mumewe hali itakuwa mbaya, yani huyu daktari bora angekuwa mganga wa kienyeji tu"
Wakaendelea na safari yao huku wakiongea tu.
Sakina na mama Sabrina wakahisi wazi kuwa anaeongelewa pale ni Sabrina tu.
Wakajikuta wakiangaliana bila ya majibu yoyote.
Kisha wakaulizana tena,
"Sasa tutafanyaje?"
"Hakuna namna hapa ila kwasababu Jeff yupo itabidi atusaidie"
"Atatusaidiaje?"
"Itabidi tumuombe akamuangalie Sam ofisini na nyumbani, akimpata aje nae"
Mama Sabrina akaona kuwa lile ni wazo jema na kuamua kwenda kumuangalia Jeff ili wamwambie wazo lao.
"Mungu atusaidie akubali jamani"
"Jeff hawezi kukataa hilo"
Walifika pale walipomuacha Jeff ila hawakumuona, ikabidi wamfate baba Sabrina na kumuuliza kwani alikuwa amekaa tu pale bila wasiwasi wowote.
"Eti Jeff yuko wapi?"
"Nilimuona anazunguka zunguka na daktari, sijui hata walipoishia"
"Kwahiyo hata hujamuuliza daktari kuhusu maendeleo ya mtoto wetu?"
"Kama kungekuwa na chochote angetuambia tu"
Mama Sabrina alimuangalia mumewe na kumuona kuwa ni mtu asiye na faida hapo.
Wakajaribu kupiga simu ya Jeff ila haikupatikana.

Muda kidogo wakamuona Jeff akitoka na kuwafuata, ila kabla hawajamwambia chochote akawapa taarifa njema ya kujifungua kwa Sabrina.
"Amejifungua mtoto wa kiume, tumepata dume sasa"
Wote walionekana kusahau habari ya kumuhusu Sam huku wakifurahia kujifungua kwa Sabrina.
Ilikuwa ni furaha sana kwao na walikuwa wanangoja sasa hitimisho la daktari kama atawaruhusu kuondoka na Sabrina wao.

Sam alikuwa nyumbani kwake muda huu, alishika simu yake sasa na kukuta ni wengi waliompigia ila aliamua kumpigia mmoja tu kati yao ambaye alikuwa ni Sia.
"Khabari Sam?"
"Nzuri tu, mambo vipi?"
"Poa, si ulisema kuwa unaishi Mbezi? Mi nipo hapa stendi, itakuwa ni vizuri kama ukija kunichukua hapa ili nipafahamu kwako"
Ikabidi Sam amuulize vizuri kisha kwenda kumchukua alipo.

Sam alifika stendi na kumkuta Sia kisha akaenda nae nyumbani kwake ambapo walijikuta wakiongea mambo mengi sana.
"Vipi Sam una mke?"
"Hiyo ni historia ndefu labda tuongelee mengine. Kwani wewe una mume?"
Sia hakujibu hilo swali bali aliweka stori zingine na kusahau hayo kabisa.
Jioni ilipoingia, Sam akaamua kuondoka pale na Sia kisha wakaenda hotelini kula halafu akamrudisha kwenye mitaa yao kisha akampa hela kidogo huku akimwambia kuwa ni ya vocha, kitendo hicho kilimtia ushawishi zaidi Sia na kujikuta akifurahi sana huku akisema,
"Hawa ndio wanaume sasa, sio mwanaume hata hela ya bodaboda hana. Huyu nimeenda kwake, kanipeleka kula hotelini na kanipa pesa, eti elfu hamsini ya vocha mmh akinipa ya nguo je itakuwaje? Uwiii msichana wake anafaidi sana, natamani niwe mimi"
Sia alifikiria sana na kutamani kumjua mwanamke wa Sam kwani aliona wazi kuwa atakuwa anapata raha sana ya kuwa na mwanaume kama Sam.

Sam alirudi nyumbani kwake na kujiuliza kuwa kwanini Sakina na mama Sabrina walikuwa wanampigia, akajipa jibu
"Watakuwa walitaka kuniambia habari za Sabrina tu, hata hakuna jipya hapa"
Ila alijifikiria kwa upande mwingine na kujiona na upweke sana kwa kumkosa huyo Sabrina.
Akafikiria sana hadi alipolala.

Hospitali nako wakawaambia ndugu wa Sabrina kuwa Sabrina ataruhusiwa kesho kwahiyo ikabidi warudi nyumbani kwanza ili wawahi kesho asubuhi.
Hakuna aliyejua kuwa Jeff ndiye aliyejifanya kuwa mume wa Sabrina kwani wote walikuwa wamefurahi juu ya habari ya kujifungua kwa Sabrina.

Kulipokucha, Sam alijikuta akiamka huku akiwa na mawazo sana.
Alijikuta akimfikiria Sabrina, akakumbuka jinsi ambavyo alikuwa akilala nae na kuamka nae, akamkumbuka mtoto wao.
"Cherry mwanangu, lazima atakuwa amenikumbuka sana baba yake."
Akapatwa na wazo la kwenda kumuona Sabrina ila aliamua kwenda ofisini kwake kwanza halafu ndio aende kwakina Sabrina.

Neema katika hali yake ya ugonjwa vilevile alijikuta akikumbuka mambo mengi sana na kumuomba Mungu amsamehe kwa yote aliyokosea.
Aisha alikuwa pembeni kama kawaida akimuhurumia ila leo alimuuliza,
"Dada, kwani yule mkaka anayekujaga hapa ndio shemeji?"
"Alikuwa, ila sio shemeji yako tena. Kwanza ni mume wa mtu yule. Usiku uliona kuna karatasi nachoma?"
"Nilikuona ndio ila sikuelewa ni kwanini ulikuwa unazichoma"
"Nilikuwa najutia mambo niliyoyafanya, ni mimi ndiye niliyemuachanisha yule mkaka na mkewe"
"Kivipi dada?"
"Ni historia ndefu, ila kwa kifupi ni kuwa nilimfanyia dawa kwa mganga amsahau mkewe. Sasa yale makaratasi niliyochoma jana ni baadhi ya masharti tu niliyopewa niyatunze na yule mganga. Sasa mimi nimeamua kuyachoma ili roho yangu ibaki nyeupe. Sitaki maumivu ya zaidi ya haya niliyonayo, hata kama nikifa basi nife kwa amani"
Aisha alimuonea huruma sana Neema kwa maneno yale.
"Pole sana dada yangu, ilimradi umetambua kosa basi jua kwamba Mungu naye atakusamehe dada yangu"
"Nashukuru sana Aisha, ila ipo siku nitakupa siri kubwa sana kuhusu yule mwanaume. Ila sio kwasasa, ngoja kwanza nikamilishe toba zangu"
Neema alihofia sana kusema kwani aliogopa kifo, alijua wazi kuwa akisema basi ataishia kama rafiki yake Rose kwahiyo akawa kimya katika kuitoa siri hiyo.

Sam nae alienda moja kwa moja ofisini kama alivyopanga na kuwakuta wafanyakazi wake pale kama kawaida.
Akaweka mambo sawa, kisha akawaaga na kutoka kwani mawazo yake kwa muda huo yalikuwa juu ya Sabrina na mtoto wao Cherry.
Wakati anatoka ofisini akamuona Sia akikatisha pale na kuamua kumuita, kisha wakasalimiana.
"Ndio unapofanyia kazi hapo?"
Huku akionyesha ile ofisi,
"Yeah, ndio ofisi yangu hiyo"
"Hongera sana, sasa unaenda wapi maana unaonekana kama unatoka!"
"Nataka nikamuone mke wangu kidogo"
"Kheee kumbe una mke? Mbona jana hukuniambia?"
"Nilikwambia ni stori kidogo, hata hivyo sijaonana nae kwa miezi kadhaa nashangaa leo nimejikuta nikimkumbuka sana"
Sia akajikuta akijawa na wivu sana moyoni mwake kwani alitamani Sam asingekuwa na mke yani angekuwa hajaoa ili aweze kumpata kirahisi ila hakuwa na jinsi zaidi ya kumtakia safari njema tu.
"Basi nitakupigia simu badae, nenda salama na umsalimie sana huyo mkeo"
"Nashukuru Sia"
Kisha Sam akaingia kwenye gari yake na kuondoka pale ofisini kwake.

Inaendeleaah



USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.