Zijue tabia za watu wenye wivu
Mara mtu apatapo mafanikio mambo mengi hutokea au hubadilika. Moja kati ya mambo ambayo hutokea ni mabadiliko kwa watu wanao mzunguka mtu huyo. Wengine humpenda, wengine humheshimu, wengine humchukia au hata kumwonea wivu.
Kwa kuwa wivu hauwaathiri wale walio nao pekee, ni vyema nawe ukafahamu tabia za watu wenye wivu ili uwaepuke wasije wakakuathiri kwa kukurudisha nyuma katika hatua zako za maendeleo.
1. Hawastaajabishwi na mafanikio ya wengine
Moja kati ya tabia kubwa ya watu wenye wivu ni kutostaajabishwa na mafanikio ya wengine. Wao hata wasikie jambo zuri au kubwa kiasi gani la mtu mwingine wao hujifanya kuliona kama la kawaida tu.
Unaweza kusikia hata wakisema kauli kama vile “mbona hayo mambo ya kawaida”, “mbona wapo wengi waliofikia hapo”, “mambo ya kupita hayo, cha muhimu uzima bwana”, “mafanikio ya watu hayanihusu bwana”, n.k. Watu wenye tabia kama hii ni wakuepukwa maishani kwani wivu umewatawala.
2. Huhusianisha mafanikio na bahati
Watu wenye wivu huamini kuwa hakuna mtu mwingine anayestahili au mwenye uwezo wa kufanikiwa. Wao hujiona kuwa wao ndiyo wenye tiketi ya mafanikio na endapo basi yatatokea kwa watu wengine itakuwa ni kwa bahati tu.
Unaweza kusikia wakisema kauli kama vile, “hiyo kazi kaipata kwa bahati tu bwana”, “amepata dili kweli”, n.k.
3. Wanapenda kuiga na kushindana
Kwa kawaida watu wanaopenda kuiga na kushindana ni wale wasiokuwa na malengo wala maono yoyote. Watu hawa wao huangalia wanayoyafanya au wanavyoishi watu wengine na kuiga.
Watu hawa, wengi wao huwa na wivu ndiyo maana hutaka yale yanayotokea kwa wengine yatokee na kwao. Utashangaa kuwaona mara unapofanya hiki nao wameshaiga, unapopanga hiki nao wameshaiga, unapoeleza umefanikisha hiki nao wanaeleza walivyokifanikisha tena hata kwa namna ambayo inaonekana inakuzidi.
Watu wa aina hii ni wenye wivu na watakunyonya nguvu ikiwa utashiriki kwenye mashindano yao.
4. Hupenda kuleta taarifa mbaya
Kuna watu ambao kila mara wao ni kuleta taarifa mbaya hasa juu ya jitihada zako za kimaendeleo au dhidi ya malengo yako.
Unaweza kusikia watu hawa wakisema kauli kama vile, “Aaa! yule jamaa mwenye biashara kama yako amefilisika”, “Inavyoonekana biashara kama hii yako huko tunakoenda haitakuwa na dili”, “ufugaji haulipi”, “biashara hazilipi”, “hakuna maana kuwekeza kwenye kilimo kwa sababu ni pata potea”, n.k.
Tabia hii ni ya watu wenye wivu wakitaka tu kukurudisha nyuma ili ukate tamaa na uwe na hofu ya kutimiza malengo yako.
Sanjari na hilo, watu wenye wivu hupenda kuzungumzia zaidi kushindwa kuliko kushinda. Wao watakueleza zaidi jinsi utakavyoshindwa kwenye kila unalolifanya kuliko utakavyofanikiwa.
5. Hufurahia wengine wanaposhindwa
Ukiona mtu anayefurahia kushindwa au kuanguka kwa mwingine basi ujue kiwango chake cha wivu ni kikubwa sana. Watu wasio na wivu husikitika pale wengine wanapoanguka; pia huwatia moyo ili wainuke tena na si kufurahia.
Kwa kuwa watu wenye wivu huwa hawapendi kuona meli ya mtu mwingine baharini, basi wao hufurahia sana mara wengine waangukapo au wapatapo matatizo.
6. Hawajumuiki pamoja kusherehekea mafanikio
Mtu mwenye wivu hapendi kuona mwingine akifanikiwa kumzidi yeye; hivyo itakuwa ni vigumu sana kwake kushiriki katika tukio lolote ambalo ni lakusheherekea mafanikio ya mtu mwingine.
Watu hawa huishia kutoa udhuru na vijisababu ambavyo vitawafanya wasihudhurie kwenye tukio hilo.
7. Hukusema vibaya kwa wengine
Je umeshaona watu ambao mkiwa pamoja wanakuwa marafiki wakubwa sana lakini ukiwapa tu kisogo wanakuwa nyoka wenye sumu kali? Kama jibu ni ndiyo, basi hawa ni moja kati ya watu wenye wivu.
Kiuhalisia tunao marafiki, ndugu, wafanyakazi wenzetu au hata majirani wengi wa aina hii.
Huja kwako kwa uso wa urafiki na wema lakini wakiondoka tu wanaanza kukusema vibaya ili kuharibu mahusiano yako na watu au kukwamisha kile unachokifanya.
8. Hupenda kujikweza na kujionyesha
Watu wenye wivu hukosa unyenyekevu; wao hupenda kuonyesha kuwa wako juu ya kila mtu na hupenda kutambulika kwa kila mtu.
Wakati wewe ukifikiri kuwa mafanikio ni kitu cha kuwa mnyenyekevu, wao huona ni kitu cha kujitangaza; wakati wewe ukieleza mafanikio yako halisi wao hueleza makubwa zaidi hasa ya uwongo ili tu waonekane bora zaidi.
9. Hutoa ushauri mbaya
Kwa kuwa watu wenye wivu hawapendi watu wengine wafanikiwe, basi wao huwapa wengine ushauri ambao utawakwamisha.
Kwa mfano mtu mwenye wivu anaweza kuona ukiingia kwenye mahusiano na mtu mbaya; lakini akakutia moyo kwa sababu anajua utaangamia.
Pia, mtu mweye wivu naweza kukupa wazo ili ulitekeleze na kukudanganya kuwa ni wazo zuri huku akijua kuwa wazo hilo litakukwamisha ndani ya muda mfupi.
10. Hukupa sifa za uwongo
Kuna msemo usemao “Sifa zinaua”; watu wenye wivu hujifanya wanakukubali na hivyo hukupa sifa za uwongo ili zikuangamize.
Unaweza kulibaini hili kwa kutazama matendo yao kwani utawaona wakikusifia lakini ukiwapa kisogo nao wanaanza kukudharau na kukukejeli kwa wengine.
Ili kulinda malengo yako hakikisha huendeshi maisha yako kwa kutegemea sifa za watu wengine, kwani zinaweza kuwa ni za wenye wivu tu zenye lengo la kukuangusha.
Zilizoelezwa hapa ni tabia 10 za watu wenye wivu ambazo unapaswa kuzifahamu ili uweze kuwaepuka maishani mwako. Bila shaka umeona wazi jinsi tulivyozungukwa na watu wengi wenye wivu na wanavyoweza kuathiri maisha yetu ya kila siku.
No comments: