Simulizi: Je Haya Ni mapenzi? sehemu ya 50


Dorry hakutaka tena kurudi nyumbani kwakina Jeff huku akikumbukia jinsi alivyopigiwa simu kuwa anatakiwa kumsaidia Sabrina halafu ile namba kupotea.
Wakati akifikiria, akaona tena simu yake ikiita kwa namba ngeni kabisa tena ikionekana kuwa ni ya nchi nyingine.
Akasita kupokea ila badae akapokea na kusikia vile vile sauti kama ya Jeff ila ikiwa katika hali ya upole, huku ikimuelekeza vitu.
"Kwani wewe ni nani?"
"Kwani wewe unahisi mimi ni nani?"
"Nahisi wewe ni Jeff"
"Hapana, mimi sio Jeff"
"Basi wewe ni nani?"
"Fanya nilichokuagiza halafu utajua mimi ni nani"
Kisha ile simu ikakatika na kumfanya Dorry abaki akiduwaa tu huku akijiuliza maswali.
Kisha akajiandaa kwaajili ya safari ya kwenda kwakina Jeff.

Sabrina aliendelea kupata ushawishi wa kumsaidia yule dada aliyeonyeshwa bila ya kujua atamsaidiaje, ila kuna kitu kikamshawishi kuwa akalale kwanza kisha atapata jibu la namna ya kumsaidia.
Sabrina akainuka na kmwenda chumbani kwake kulala pamoja na mwanae.
Na alipolala tu akajiwa na ndoto kuwa kuna mahali anatakiwa kwenda, akaonyeshwa kwenye ile nyumba ya mumewe yani kwa Sam na kumfanya ashtuke.
Akakaa kitandani na kukumbuka ndio mahali alipong'atwa na nyoka,
"Inamaana nikienda huko ndio nitakuwa nimemsaidia? Na je nitakuwa nimemsaidiaje?"
Akajiuliza pale, ila mtu pekee wa kumpeleka kule ni Sakina kwani yeye hakuwa na kumbukumbu nzuri, kwahiyo akapanga kwenda kesho yake kuongea na Sakina kwani siku hiyo gizi lilishaanza kuingia.

Dorry alifika nyumbani kwa Sakina wakati kigiza giza tayari kilishaingia na kumkuta mama mkwe wake akiwa ametulia muda huo akiangalia video tu.
"Karibu Dorry, nimefurahi umekuja"
Dorry nae akafurahi kwani hakutarajia kufurahiwa vile na mkwe wake.
"Usiwe na mpango wa kuondoka tena safari hii, tafadhari sana mwanangu"
Dorry akatabasamu tu kwani kwake ilikuwa ni jambo la kheri na furaha kwa kipindi hiko.
Kisha wakatulia pale ila Dorry hakumwambia Sakina jambo ambalo lilimpeleka pale kwa siku hiyo, mpaka muda wa kulala ulipowadia na wote kwenda kulala.

Kulipokucha, asubuhi na mapema Sabrina akaamka nyumbani kwao huku ile roho ya kumtaka yeye akamsaidie Neema ikimsumbua.
Akaamua kumuaga mama yake kuwa anaenda kwa Sakina kwani mtu pekee wa kumpeleka tena kule kwa mumewe ni huyo Sakina.
"Hakikisha unaenda kweli kwa Sakina"
"Usijali kuhusu mimi mama"
"Lazima nijali, hapo ulipo huna kumbukumbu. Umesahau mambo mengi sana na ukijichanganya tu unapotea, ila je ni muhimu sana wewe kwenda kwa Sakina? Maana naweza kumpigia simu hapa akaja mwenyewe"
"Ila hata mimi naweza kufika kwake mama"
Mama wa Sabrina akaona kama machale yakimcheza na kuamua kumwambia Sabrina arudi ndani.
"Hapana, roho yangu imekataa. Tafadhari subiri nimpigie simu Sakina aje mwenyewe"
Sabrina alirudi ndani huku akiumia moyoni kwani aliona kitendo cha yeye kupoteza kumbukumbu kuwa kama kikwazo katika maisha yake kwani kilimfanya achungwe kama mtoto mdogo.
Kisha muda huo mama wa Sabrina akawasiliana na Sakina na kumuomba afike pale kwake.

Siku ya leo, Neema alijiona akiwa na hali mbaya zaidi licha ya dawa za hospitali ambazo alipewa na kuzitumia.
Lakini kile kiharufu cha kuoza bado alikisikia tena kwa hali ya juu na pia damu bado ziliendelea kumtoka kwa kasi ile ile.
Kama kawaida asubuhi hiyo na mapema, rafiki yake Rose alifika na kuendelea kumshinikiza mambo yale yale.
"Yani Rose, ingawa namuhurumia Sabrina ila kwa hali hii hapana kwakweli, maana naona kifo hicho kikinukia mbele yangu. Twende tu kwa huyo mtaalamu"
"Hapo sawa sasa, ingawa hukuniambia kuwa tatizo ni nini hadi imekuwa hivyo"
"Wee acha tu, ila bora afe yeye kuliko mimi. Watu wengi wananitegemea, familia inanitegemea, ndugu zangu, wazazi wangu yani nife niwaache sababu ya huu ujinga wangu haiwezekani lazima nipambane. Nipiganie uhai wangu, ingawa najuta kumfahamu huyu kiumbe Sam"
"Ila hujaniambia alichokufanya"
"Hayo tuyaache tu rafiki yangu"
Kisha wakaondoka pale na kwenda kwa mtaalamu wao.
Walikaa na mtaalamu wao huku wakifanya dawa za kumvuta Sabrina aende nyumbani kwa Sam ili waweze kumtupia ule ugonjwa wa Neema.

Sakina alifika pale kwakina Sabrina kisha Sabrina akamueleza Sakina ile azma yake ya siku hiyo.
"Hapo ndio naanza kukupenda Sabrina, inatakiwa kutokukata tamaa kabisa. Nipo tayari kukupeleka, yule ni mumeo ni baba wa watoto wako. Unatakiwa kupigania penzi lako mdogo wangu. Twende tu ila leo mtoto tumuache"
Wakakubaliana pale, kisha wakaamua kumuaga mama wa Sabrina na kumuachia mtoto, ingawa mtoto alikuwa akiwalilia ila waliamua kumuacha.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Wakati wanatoka pale, Sakina akamuona Dorry akija mbio huku anawaita.
Wakasimama ili wamsikilize, alipowafikia akawaambia
"Tafadhari msiende"
Sakina akamshangaa Dorry na kumuuliza,
"Unajua tunapoenda?"
"Najua ndio, ila nawaomba msiende"
"Kwanini tusiende?"
"Nawaomba tu msiende"
Sabrina akamuangalia Dorry kwa jicho la chuki sana, kisha akamwambia Sakina,
"Twende bhana, asitake kutuchelewesha huyu"
Hawakumjibu kitu cha zaidi Dorry na kuendelea kwenda.
Dorry alibaki akiwaangalia tu.
Muda kidogo Dorry akiwa ameganda pale pale akasikia sauti kubwa ya mgongano wa magari na watu wengi kukimbilia barabarani, alijikuta nae akikimbilia huko eneo la tukio.
Macho yalimtoka kuona damu zimetapakaa pale, na moja wapo ya watu aliowaona alikuwa ni mmama akionekana kuvuja damu nyingi sana.
Alijishika kichwa kwani rangi ya nguo ilikuwa ni nguo ya mtu anayemfahamu.

Macho yalimtoka kuona damu zimetapakaa pale,
na moja wapo ya watu aliowaona alikuwa ni
mmama akionekana kuvuja damu nyingi sana.
Alijishika kichwa kwani rangi ya nguo ilikuwa ni
nguo ya mtu anayemfahamu.
Dorry alisogea karibu huku mawazo yote yalikuwa kwa Sakina na Sabrina.
Na kweli pale chini kulikuwa na mtu anayemfahamu ila hakuwa Sakina wala Sabrina, Dorry alihisi kuchanganyikiwa kwani Sakina na Sabrina nao walikuwa kati ya watu wanaoshangaa tukio lile, ila Sakina alipomuona Dorry akilia juu ya yule mmama aliamua kumsogelea akiwa na Sabrina huku wakimbembeleza Dorry kisha yule mmama akapakiwa kwenye gari pamoja nao kwa kumuwahisha hospitali.
Sakina na Sabrina walisahau mambo ya safari yao pale na kukazana kumbembeleza Dorry ambapo Dorry alikuwa akilia sana.
"Pole sana mwanangu Dorry, kwani huyu mama ni nani yako?"
"Huyu ni mama yangu mdogo, ni mama aliyenilea mimi. Tangu mama yangu amekufa, huyu ndiye amebaki kuwa mama yangu. Sijui kwanini apate ajali, sijui kama atapona"
Dorry alikuwa akilia sana, kwani moyo wake ulijawa na maumivu yasiyo na mwisho kwa ile damu iliyomvuja mama yake ilimfanya akose matumaini juu ya kupona kwake.
Kwahiyo Sakina na Sabrina wakapata kazi kubwa sana ya kumbembeleza.

Yule mtaalamu wa kina Neema aliamua kuwapa dawa wao wenyewe wakashughulike nayo nyumbani.
"Nendene mkashughulikie nyumbani, mi kuna kazi nyingine nataka kufanya saivi"
Ikabidi Neema na Rose wachukue ile dawa na kuondoka.
Wakiwa njiani wakaanza kujiuliza,
"Ila huyu mganga nae leo sijamuelewa"
"Hata mimi sijamuelewa kwakweli"
"Nakumbuka tulipoingia pale na kuanza kufanya dawa alisema kuwa muda ule ule wa dawa lazima mambo yetu yafanikiwe. Eti mwisho wa siku anasema tukaifanye nyumbani, kama imemshinda yeye mtaalamu sisi tutaiweza kweli?"
"Hapo sasa, ngoja tukajaribu tu"
"Ila naona kama leo katuletea magumashi tu, maana tumeanza vizuri sana. Sasa iweje aishie kati?"
"Siri yake hiyo, wewe twende tukajaribu hiyo dawa nyumbani kama yakitushinda basi tutarudi tena kwake"
"Yani mi nimechoshwa na huu ugonjwa balaa"
"Pole shoga yangu, natambua kuwa unateseka"
Kisha wakaendelea na safari yao hadi nyumbani.

Kule hospitali, mama mdogo wa Dorry aliendelea kupatiwa matibabu kisha wakawajulisha ndugu wa Dorry ambao nao walifika eneo la tukio.
Kisha Sakina akamuomba Dorry kuwa warudi nae nyumbani angalau akabadilishe nguo kwakuwa zile alizovaa zilitapakaa damu.
Mwanzoni Dorry alikuwa akikataa ila badae alikubali kisha wakaianza safari ya kwenda kwa Sakina huku akiambatana nao pamoja na Sabrina.

Walifika nyumbani na kukuta kama walivyopaacha, simu ya Dorry ilikuwa kwenye kiti na walipoingia tu ile simu nayo ikaanza kuita.
Ikabidi Dorry aipokee ile simu,
"Hallow"
Hakuangalia namba ila alishtuliwa na ile sauti ambayo siku zote huwa anaifananisha na sauti ya Jeff kisha akaanza kumsikiliza,
"Pole sana Dorry, ila ungeweza kufanya nilichokuagiza wala hayo yasingekupata"
"Unamaana gani?"
" Nilikutuma nini na umeshindwa kufanya? Hiyo ilikuwa ni namna ya kuwazuia tu"
Dorry akachukia sana na kusema kwa nguvu,
"Sitaki upuuzi wako"
Kisha akaibamiza ile simu chini na kufanya Sakina na Sabrina wamshangae kuwa kwanini ameonekana kuwa na hasira kiasi kile.
Sakina akamsogelea na kumuuliza,
"Nini tatizo mwanangu?"
Dorry alijikuta akikaa chini huku akilia kwa uchungu sana.
Sakina alijitahidi kumbembeleza tu bila ya kujua kuwa ni kitu gani kinamsumbua kwa wakati huo.

Neema na Rose wakiwa nyumbani kwa Neema, wakasikia kuna mtu akibisha kwenye mlango wao, kisha Rose akainuka na kwenda kumfungulia.
Mtu huyo hakuwa mwingine bali ni Sam, kisha Rose akamkaribisha ndani.
Sam aliingia ndani ila alisimama tu na kumuangalia Neema ila Neema alikwepesha macho yake kwani hakutaka kabisa kutazamana na Sam kisha Sam akamwambia Neema,
"Pole kwa matatizo"
Kisha akamuangalia na Rose na kusema,
"Poleni kwa matatizo"
Rose alimtazama tu huku akijiuliza kimoyo moyo kuwa kesi ya John imeishia wapi kwani hawakuwahi kufatwa kwa upelelezi wala kushtakiwa kuhusu chochote. Ila kabla Rose hajauliza kitu tayari Sam alianza kuwajibu,
"Msijali kuhusu yule kijana, mambo yote yanaenda sawa kwasasa ndiomana nimerudi kwahiyo msiwe na shaka"
Kisha akatoa kibunda cha pesa na kumkabidhi Neema, kisha akamwambia
"Endelea kutunza siri ili uendelee kuishi kwa amani. Nakupenda sana"
Kisha akatoka nje na kuondoka.
Hapo ndipo Rose alipoanza kuongea,
"Ulikuwa unalalamika bure tu shoga yangu, ona pesa yote hiyo uliyoipata. Huoni kuwa una bahati shoga yangu!"
"Rose, ni kwavile hujui tu. Ni kheri kufa masikini kuliko kufa na mawazo ya tamaa na hizi hizi pesa ndio zinazonifanya nijute kwa muda huu. Sikuwahi kufikiria kama ipo siku nitakutana na mwanaume wa aina hii kwakweli"
Rose alimuona rafiki yake kuwa kama mjinga kwani kwa muda huo yeye aliwaza pesa tu, na tamaa ya kupata pesa kama zile ikamjaa kwenye moyo wake.
Akatamani sasa awe ni yeye anayepata kiasi kile cha pesa.
Alimshangaa sana rafiki yake kwa kulalamika na kujiapia moyoni kumpindua Neema kwa Sam ili awe yeye anayepewa kiasi kile cha pesa.

Dorry alipotulia, akaenda kuoga na kubadilisha nguo ila hii familia ya kina Jeff aliona ikimpa gundu tu katika maisha yake.
"Kwani lazima niwasaidie mimi tu? Kwanini huyu mtu ananitumia mimi? Najuta kujiingiza kwenye familia ya kishirikina kama hii, ona ninavyoteseka sasa. Yani mama yangu asiye na hatia naye wamemuingiza kwenye mikosi yao. Hivi mama yangu nae alikuwa anatoka wapi na anaenda wapi? Jamani haya mambo sielewi kabisa"
Dorry alilalamika sana kwani aliona ni kitu kidogo alichokifanya yani kusema mimba ni ya Jeff wakati sio yake.
"Lakini mimi sio mwanamke wa kwanza kudanganya bhana, wangapi wanadanganya na bado hawapati matatizo?"
Roho ilimuuma sana na kujikuta akiichukia familia ya Jeff yote wakiwepo ndugu, jamaa, marafiki pamoja na majirani.
Alipomaliza kujiandaa alitoka sebleni na kukuta Sakina alishamuokotea ile simu na kumuunganishia kabisa,
"Yani hii simu yako ni imara sana, kuipigisha chini kote kule halafu bado ni nzima kabisa hata kupasuka haijapasuka"
Kisha akamkabidhi, Dorry aliipokea ile simu ilimradi tu ila kiukweli alitamani kuachana nayo kabisa kisha akawaaga na kwenda tena hospitali pamoja na Sakina huku wakimpitisha kwanza Sabrina nyumbani kwao.

Mama wa Sabrina alimuuliza mwanae kwa makini kilichowapata, kisha Sabrina akamueleza kuhusu ajali waliyoiona,
"Unaona sasa mwanangu, safari zingine sio za kung'ang'aniza sababu ni mikosi mitupi. Mi nilipokuwa nawakataza unaona kama kajinga fulani, haya sasa umeona yaliyowapata? Utulie nyumbani sasa, nishakwambia kuwa usubiri akili yako itengemae. Acha kung'ang'aniza mambo yaliyo nje ya uwezo wako. Sawa mwanangu?"
"Nimekuelewa mama"
"Yani hata Cherry hapa hakuafiki kabisa ndiomana akawa analia, watoto ni malaika mwanangu"
Sabrina aliitikia huku akiangalia tumbo lake ambalo nalo lilizidi kwenda mbele kwa ukubwa.
Muda kidogo wakati anazungumza na mama yake, baba yake naye akafika na kumsalimia pale kisha kuanza kuzungumza mambo ya hapa na pale, ambapo kabla ya muda kupita alifika James yani yule kaka wa Sabrina ambapo alienda kupiga magoti moja kwa moja kwa baba yao.
"Nisamehe baba"
"Nilishakusamehe siku nyingi sana, hata usijali. Haya ni maisha tu, siku zote ni safari ndefu cha msingi ni kukumbuka kuinuka pindi ukianguka sio ukae hapo hapo chini"
"Nisamehe sana, nilichanganyikiwa"
"Usijali James"
Kisha James akasogea kwa mama yake na kumuomba msamaha vilevile,
"Mimi ni mtoto wenu, ni nyie mliofanya niwe hivi nilivyo. Naomba mnisamehe sana"
Mama Sabrina na baba Sabrina wakainuka na kumkumbatia mtoto wao James kwa ishara kwamba walishamsamehe.
James akafurahi sana, kisha kuongea mengi na wazazi wake.
Usiku ulipoingia akawaaga na kuondoka.

James alipokuwa na mkewe Joy, alimsihi jambo moja la kuwasamehe wazazi wake.
"Huwezi kuwachukia wazazi wako kwa maisha yako yote, huna budi kuwasamehe. Na pia narudia tena, kama kuna chochote ulichonificha na mimi tafadhari niambie"
"Hakuna nilichokuficha mume wangu"
"Una uhakika Joy kuwa hakuna ulichonificha?"
"Ndio James, hakuna nilichokuficha"
James akamkumbatia mke wake kisha wakaenda kulala sasa.

Neema alilala kwa usiku ule ila kwa mateso sana, kwani alijisikia harufu vilivyo.
Alitamani arudishe siku nyuma ili aweze kuepukana na yale mambo ila ndio haikuwezekana.
Aliwaza sana hatma yake, akakumbuka walivyokuwa wakifanya dawa mchana ili kumtupia Sabrina ule ugonjwa.
Akakumbuka jinsi ilivyokuwa ngumu na kuwafanya waahirishe tu.
Alilala kwa mang'amu ng'amu hadi kunakucha.
Palipokucha alichukua kioo na kujiangalia.
Akajihurumia sana kwani sura yake ilionekana kudhoofu tofauti na alivyokuwa zamami.
Alijihurumia sana kwa tamaa yake iliyomponza na kumfanya vile alivyo kwasasa.

Rose akiwa nyumbani kwake na yeye alikuwa akiwaza jinsi ya kumteka Sam.
"Niende kwa mganga ili nimpe dawa au nitumie uanamke wangu kumteka? Ila Neema alisema kuwa yule kaka mgumu sana, ila anaweza kuwa mgumu kwangu kweli? Ngoja nitajaribu, na lazima nimpate"
Rose alichokiwaza kwa muda huo ilikuwa ni pesa tu kwani ndiyo iliyomchanganya akili yake.

Sakina akiwa anatoka hospitali siku hiyo kumuangalia mama mdogo wa Dorry, njiani akaona gari ya Sam na kuisimamisha na kweli ile gari ilisimama na Sam kutoka ndani ya ile gari kisha akasalimiana na Sakina pale.
"Sam, kwani umepatwa na tatizo gani?"
"Kwani unadhani nina matatizo dada yangu, sina matatizo. Ila mwanao Jeff karibu atarudi kwahiyo usijali."
Sakina aliposikia kuwa mwanae karibia atarudi akaamua kuachana na mada hizo hapo hapo kisha akaagana nae kwani alishukuru kuona kuwa bado mwanae anakumbukwa kwani alijua kashasahaulika kabisa.

Sakina alienda kwakina Sabrina moja kwa moja ili kumueleza kuwa ameonana na Sam.
"Yani Sam anazidi kupendeza tu, bora tufanye juu chini mrudiane Sabrina tafahari"
"Dada, kama Mungu hajapanga basi haiwezi ikawa tu. Tusilazimishe mambo, hapa ninachoomba ni kurudiwa na kumbukumbu zangu tu"
"Na khabari njema ni kuwa Jeff karibu atarudi"
"Basi itakuwa ni vyema kwani hata mi napenda kumfahamu"
Sakina akacheka tu na kumuona Sabrina kuwa ni kweli akili yake haipo sawa.

Rose alienda nyumbani kwa Neema ambaye alikuwa kitandani tu kwa siku hiyo yote.
"Ila Neema rafiki yangu ni kwanini hutaki kuniambia ukweli juu ya yaliyokupata?"
Neema alitokwa na chozi tu, hata kuzungumza hakutaka kwa siku hiyo.
Kisha Rose akachukua simu ya Neema na kuchukua namba ya Sam kisha kurudisha simu na kumuaga Neema.
Kwa wakati huo mawazo ya Rose yalikuwa juu ya pesa tu za Sam.

Rose alitoka pale nyumbani kwa Neema na kwenda nyumbani kwake huku akiwaza kumpigia simu Sam ili amchombeze kwa maneno, ila akaona kama ni kupoteza muda tu, hivyo akaamua kujiandaa tena kisha kuongoza moja kwa moja hadi nyumbani kwa Sam, na alivyofika pale akamkuta mlinzi kama kawaida.
"Sam nimemkuta?"
"Ndio yupo, je anajua kama unakuja?"
"Anajua ndio"
"Ila mi sikujui vizuri wewe"
"Kheee makubwa, ngoja nimpigie simu yake"
Rose akaona kuwa alitumia jambo la akili sana kuchukua namba ya Sam kwani yule mlinzi alianza kumuwekea kauzibe.
Rose alipoongea na Sam kwenye simu, akampa yule mlinzi ile simu kisha akamruhusu kuingia ndani.
Rose aliingia moja kwa moja na kumkuta Sam akiwa pale sebleni.

Sam hakujua kuwa ni kitu gani haswaa kilichompeleka Rose pale nyumbani kwake, ila hakuacha kumkaribisha.
"Mbona jioni hii shemeji?"
"Upweke shemeji"
"Upweke! Kivipi tena?"
Rose akamsogelea Sam na kuanza kumfanyia mambo ya kumvutia.
"Lakini si unajua kuwa mimi ni shemeji yako?"
"Shemeji kitu gani jamani? Kwani zimewekwa alama hizi kuwa hii ni ya shemeji usiguse? Acha hayo mambo Sam, nimekuja hapa kwaajili yako"
"Umekuja kwa kupenda mwenyewe au umeshawishiwa na mtu?"
"Nimependa mwenyewe Sam, nakupenda sana ni vile tu umewahiwa na rafiki yangu"
Rose akasogea karibu na kumbusu Sam, ambapo akamtia vishawishi vilivyopitiliza na kumfanya Sam atende kile ambacho Rose alikikusudia.
Kwa mara ya kwanza, yule mlinzi wa Sam pale nje alisikia sauti kali ya mtu akilia kwa nguvu na ile sauti kukatika gafla.

Rose akasogea karibu na kumbusu Sam, ambapo
akamtia vishawishi vilivyopitiliza na kumfanya Sam
atende kile ambacho Rose alikikusudia.
Kwa mara ya kwanza, yule mlinzi wa Sam pale nje
alisikia sauti kali ya mtu akilia kwa nguvu na ile
sauti kukatika gafla.
Yule mlinzi alistuka pale nje na kujiuliza kuwa ni kitu gani, alitamani kwenda kuchungulia ila hakuweza kwavile aliogopa pindi bosi wake angemuona basi ingekuwa mwisho wa kibarua chake.

Kitu alichokosea Sam kwa siku hiyo ni yule Rose kumuona maumbile yake kwenye mwanga kwani hupenda kufanyia gizani.
Ingawa Rose alipiga zile kelele na kuzimia, lakini Sam hakuweza kumuachia kwavile tayari alishajawa na tamaa ya mapenzi ambayo alipewa na huyo Rose.
Hata alipomaliza alikaa na kujilaumu kuwa kwanini amemuachia huyo binti kumshawishi yeye kiasi hicho.
Damu zilikuwa zimetapakaa pale sebleni na ndio kitu ambacho kilimfanya Sam asipende kufanya chochote na hawa wadada wa karibu yake, ila ndio basi tena ilishatokea na maji yakimwagika hayazoleki.
Ili kupoteza ile aibu, Sam alimuinua pale chini na kumvalisha nguo zake kisha akambeba na kwenda kumpakia kwenye gari yake.
Akafunga nyumba na yeye kupanda kwenye gari kisha akamuaga mlinzi wake na kuondoka.

Kwavile tayari kulikuwa na giza, Sam akaamua kumpeleka Rose moja kwa moja nyumbani kwake.
Ambapo alipekua kwenye mkoba wake na kupata funguo kisha akafungua na kumuingiza ndani kwake.
Alimuhurumia sana ila tayari alishajazwa na pepo la ngono na Rose mwenyewe kwa vishawishi alivyompa.
Rose alikuwa bado kazimia, ikabidi Sam achukue maji na kujaribu kummwagia wakiwa ndani kwa Rose, na haikuchukua muda Rose akazinduka.
"Pole sana Rose"
Rose alimuangalia kwa kumshangaa tu, kisha Sam akatoa pesa na kumpatia kisha akamwambia,
"Usimwambie yeyote"
Sam akainuka na kutoka mule ndani kwa Rose kisha akaondoka.

Rose alikuwa anajishangaa tu kuwa Sam kafikaje mule ndani kwake na kwanini amempa pesa.
Akajiuliza sana na kujaribu kuvuta kumbukumbu, ndipo alipokumbuka kuwa mara ya mwisho alikuwa nyumbani kwa Sam.
Akaangalia mezani na kuona pesa aliyoachiwa na Sam na kumfanya atabasamu,
"Yes, hiki ndicho nilichokuwa nakitaka. Ila kwanini aseme kuwa nisimwambie mtu? Na kanipa pesa kwa misingi ipi?"
Akakumbuka alivyokuwa akimshawishi Sam kuwa wafanye mapenzi, kumbukumbu ikamjia alichokiona kwa Sam baada ya kuvua nguo.
Akili ikamchemka sasa,
"Mungu wangu, Sam sio mtu wa kawaida. Asante Mungu sijafanya naye chochote"
Akajaribu kusimama sasa na kujihisi kulowa damu huku akihisi maumivu kwenye sehemu zake za siri, hakutaka kuamini kabisa kuwa ni yeye amelala na yule Sam.
Alijikuta akizitupa zile pesa mule chumbani kwake kwa hasira na kuanza kulia.
"Kwanini mimi Rose jamani? Nitapona kweli mimi?"
Alilia sana na kumkumbuka Neema jinsi alivyokuwa akitoa machozi.
Hakuweza kulala kwa usiku wote huku akitamani kurudisha masaa nyuma ili arudishe matukio na yeye asiwe ameenda kwa Sam kama alivyoenda.
Alipata uchungu sana moyoni mwake na kuilaumu tamaa yake kwani ilimponza ipasavyo.

Sam akiwa nyumbani kwake, alitazama jinsi damu zilivyotapakaa mule ndani, alijiuliza kuhusu Neema na Rose,
"Hawa wadada wanamatatizo gani? Kwanini nimelala nao, kwanini wanapenda kunishawishi nifanye nao mapenzi? Na kwanini imekuwa rahisi mimi kufanya nao?"
Sam akamkumbuka na Sabrina pia, mwanamke aliyeweza kulala nae na kuamka nae.
Mwanamke aliyefunga naye ndoa ila hakuthubutu hata siku moja kufanya naye mapenzi, hakutaka kukosea kabisa kwa mwanamke huyu wa pekee aliyempenda kama roho yake.
Akakumbuka maisha yake ya nyuma, akamkumbuka mama yake mzazi ambaye hakuweza hata kuhudhuria harusi yake ila alimpa baraka zote za ndoa, akamkumbuka mama yake mdogo aliyemlea na kumpa taratibu zote za maisha, akawakumbuka nduguze wa kike kama wakina Joy na kujiuliza tena,
"Hivi hawa wote wanatambua kama mimi naua wanawake? Hii ni siri yangu, na siku nikiamua kusema basi nitamwambia msichana mmoja tu ambaye ni Sabrina. Ingawa kwasasa simpendi tena ila huyu ndiye mwanamke pekee wa kuijua siri yangu hii, kwani yeye pia ni miongoni mwa tatizo katika maisha yangu"
Sam aliwaza sana huku akifikiria mwisho wa Neema na Rose, moyo ukamuuma sana kwani alishawazoea watu hawa.

Sam kulipokucha akaamua kwenda kuwatembelea baadhi ya ndugu zake waliopo hapo mjini ili hata aweze kuwasalimia tu.
Na safari yake ya kwanza ilikuwa kwakina Joy ambapo alimkuta Joy nje akiwa amejiinamia.
"Nini tatizo dada?"
Joy hakuweza kumficha Sam na kuamua kumueleza ukweli kuhusu yeye,
"Kwahiyo unaponiona hapa Sam, mi na wewe hatuna undugu kwani huyu mjomba wako sio baba yangu mzazi"
"Joy, wewe ni ndugu yangu haijalishi ni vipi. Jipe moyo haya ni maisha tu, tatizo lako sio kubwa hivyo hadi kukufanya ukate tamaa. Kaa utulie nikwambie kuhusu mimi"
Joy akamtazama Sam na kumsikiliza sasa ambapo Sam akamuuliza swali kwanza,
"Je huyo baba yako mzazi unajua alipo?"
"Sijui, na mama aliniambia kuwa huyo baba alishakufa"
"Sawa, sio mbaya ila mshukuru Mungu kwa hapo ulipofikia. Unaniona mimi nilivyo Joy?"
Joy akatikisha kichwa kuashiria kwamba anasikiliza yale maongezi,
"Basi mimi hapa, nimezaliwa simjui baba na wala sijawahi kumuona. Sijui kama ni mzima au alikufa, hiyo ni siri ya mama. Sitaki kuulizia kwani sijui nitamkumbusha kitu gani."
"Kwahiyo Sam umelelewa na mama pekee?"
"Tena kheri yako wewe uliyeweza kulelewa na mama yako mzazi na baba wa kufikia na wote wakakupenda kwa moyo"
"Ila baba naye hakujua kama mimi sio mwanae"
"Ila amejua sasa? Na amejuaje?"
Ikabidi Joy amsimulie na mkasa mzima wa James na kumfanya Sam azidi kuduwaa na kushangaa jinsi muelekeo mzima wa maisha ulivyo.
"Inamaana Sabrina karithi"
"Unamaana gani Sam?"
"No, tuachane na hayo tuendeleze yetu"
Joy akamaliza kumuelezea na kumsikiliza huku akitamani kujua zaidi kuhusu ya Sabrina ingawa Sam amekataa kuyaelezea.
"Ila Joy bado sio tatizo kwani nina uhakika hata mjomba ameshtuka kusikia hilo ila hawezi kuacha kukupenda kama mwanae kwani amekulea yeye toka udogo wako"
Joy akafikiria na kuona kuwa maneno ya Sam yana ukweli ndani yake,
"Upande wangu mimi sasa, kwanza sijalelewa na mama mzazi unajua ni kwanini?"
"Sijui, niambie kwanini?"
"Mama aliponizaa mimi hapakuwa na baba na sijui alitokomea wapi, ila nilipofikisha miaka mitatu mama akapata mchumba na kuolewa. Baba huyo wa kufikia hakunitaka kabisa mimi kwakifupi hakupenda uwepo wangu, hivyo akajitokeza mamdogo ambaye hakuwa na mume kunichukua mimi na kunilea ili kuokoa ndoa ya dada yake.
Nilipokuwa mkubwa nikayatambua hayo kwani mamdogo hakuwa na mtoto mwingine ila mimi na alinipenda kwa kila hali na ndiye aliyenieleza ukweli juu ya maisha yangu. Nilipata hasira ya maisha na kupambana ipasavyo hadi leo namiliki mali zangu na wote kuomba msaada kwangu. Kwahiyo mamdogo kwangu ndiye mama na ndiye baba, nampenda sana na kama angekuwa na watoto basi ningewapenda sana. Nampenda mama yangu mzazi ila siwapendi watoto aliozaa na yule baba kwani namchukia sana na pia nachukia nikikumbuka walivyowahi kunifukuza siku niliyoenda kumsalimia mama. Ni mengi nimepitia katika maisha yangu, kwahiyo usishangae ukiona napenda kuishi mwenyewe yani haya ndio maisha yangu na nikikueleza yote sitamaliza leo. Cha msingi na muhimu, wapende wazazi wako, wajali hao ndio nguzo yako, ndio waliokufikisha hapo ulipo"
Joy alimshukuru sana Sam kwani moyo wake ulisuuzika sana, akawaza kama angekuwa ni yeye angejisikiaje kwa malezi hayo.
Akatamani kumuuliza alipambanaje na kupata utajiri wote ule ila akaona kuwa anaweza kwenda nje ya mada na kuacha kama ilivyo.
Kisha akainuka na Sam pale na kumkaribisha ndani ambako walikuwepo wazazi wake na muda huo Joy alionekana kuwa na furaha sana na kumfanya hata mama yake kujiuliza kitu ambacho kimemfurahisha bintiye kwa muda huo.
Ila walifurahi tu pamoja naye.

Rose alijitahidi siku ya leo kwenda kwa rafiki yake Neema ili akamueleze kilichompata.
Alimkuta Neema akiwa amejilaza ndani huku harufu ya kuoza nayo ikizidi kutapakaa mule ndani kwake.
Rose alifika na kusogea alipo Neema huku machozi yakimtoka,
"Kweli tamaa ni mbaya rafiki yangu, tamaa haifai. Na mimi leo naumwa, ni mgonjwa kama wewe Neema, najuta mimi"
Neema hakumuelewa rafiki yake kuwa imekuwaje hadi awe vile na kwanini ajute.
Ikabidi amsikilize kwa makini sasa ambapo Rose alikuwa amejawa na aibu huku akianza kumueleza Neema.

Sakina alirudi nyumbani kwake baada ya kuridhishwa na hali ya mama wa Dorry ambaye aliruhusiwa kurudi nyumbani kwa siku hii.
Ila kabla hajafika kwake aliamua kupitia kwakina Sabrina ili kumuhabarisha kuhusu huyu mama na kama kawaida alimkuta Sabrina akiwa na mama yake kama siku zote.
"Jamani Mungu ni mwema, yule mama amepona na leo ameruhusiwa"
"Kheee afadhari jamani maana haya mambo yalikuwa makubwa sana"
Wakati wanaongea ongea pale, Sakina akapigiwa simu na mwanae na kumfanya apokee kwa shauku kwani alipenda pia kumuhabarisha kuhusu khabari ya mama wa Dorry.
"Kheee kumbe alipata ajali?"
"Ndio, yani hali ilikuwa mbaya sana hapa"
Basi Jeff akawapa pole kisha akawahabarisha juu ya swala lake la kurudi,
"Hata jana nimekutana na Sam, amenieleza kuhusu wewe. Nitafurahi sana kukuona mwanangu"
"Usijali mama, narudi"
"Mkeo nae utamkuta mimba kubwa kabisa au utamkuta tayari kajifungua"
"Mama, mbona huwa sikuelewi? Sijaacha mke mie huko jamani mama, hakuna mwenye mimba yangu. Mbona huwa sikuelewi?"
"Mmh haya, ukija utajionea mwenyewe"
Kisha wakaagana na kuikata ile simu.
Sabrina aliyekuwa akiwasikiliza kwa makini, naye akauliza kuhusu mimba inayoongelewa na Sakina siku zote.
"Hivi dada huwa unaisemaga mimba yangu au mimba ya yule binti unayekaaga naye?"
"Kheee na wewe Sabrina sasa umechoka, au ndio wakaribia kujifungua na wewe? Sasa mi niiseme mimba yako kwa lipi? Nimwambie Jeff kuwa mkewe anakaribia kujifungua huku nikimaanisha wewe si nitakuwa nakichaa mimi? Maana hata kiutani haiwezekani, ungekuwa bibi yake labda ungesema natania ila mamdogo na mtoto wapi na wapi? Wewe ngoja mumeo aje tu kukuona basi"
Sabrina akakaa kimya kwa muda kidogo kama anafikiria kitu, kisha akabadilisha mada pale na kuagana na huyo Sakina.

Sabrina alipobaki mwenyewe akafikiria siku ambayo Sakina alimpa simu na kuzungumza na huyo Jeff, akakumbuka maneno aliyoambiwa na huyo Jeff ambapo bado alionekana kuchanganywa na maneno aliyoambiwa na Sakina.
"Ila hakuna tatizo, nitajua kila kitu. Naamini Mungu atanisaidia na nitakumbuka kila kitu ila isiwe kweli hiki ninachofikiria kuhusu huyo Jeff. Mmh isiwe kweli"
Sabrina akatulia kwa muda akifikiria jambo hilo.


Inaendeleaah...


USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON

No comments:

Theme images by pollux. Powered by Blogger.